Viongozi msiogope kutoa maoni yenu katika katiba mpya

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisoma hotuba yake wakati akifungua rasmi Kongamano la Dini la Waislam na Wakristo lililoanza leo Aprili 18, kwenye Hoteli ya White Sands jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine aliwataka viongozi hao kujizuwia na ushawishib wowote utakaosababisha kuliingiza taifa kwenye machafuko wakati wa uandaaji wa katiba mpya

Na Juma Mohammed
Mara nyingi shuwari ya meleji inashangaza wavuvi na wasafiri wengi wa baharini,ukimya na uvumaji utafautiana sana na pepo nyengine,aghalab kipindi cha mwezi wa Juni ndio kipindi cha upepo huu. Mnasaba wa hilo unakaribiana na kuanza kazi kwa Tume ya Katiba ya Tanzania ambayo yenyewe inaanza mwezi Mei ikiwa shuwari imeingia katika upwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wajumbe wa Tume wameshakula kiapo mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Jakaya Kikwete,kama ni safari basi tayari Nahodha wa chombo ameshaanza kukiondoa gatini.

Kama inavyoeleweka Katiba ya nchi ni mali ya umma,sio ya kikundi,Chama cha siasa,Asasi za Kiraia,Dini au Kiongozi,hivyo inakubalika kwamba Taifa lolote lenye kufuata demokrasia,katiba inasalia kuwa ni mali ya wananchi na hivyo ni wananchi pekee ndiyo wenye haki ya kubadili katiba ya Taifa lao kama ilivyo sasa hapa Tanzania.

Kwa msingi huo,katiba ya Tanzania ni mali ya Watanzania na si vyenginevyo,hatutaraji kujitokeza kikundi cha watu kuhodhi Mamlaka ya umma kwa niaba yao.

Kumekuwa na dhana kwamba jamii fulani tu ndio yenye mamlaka au uwezo wa kutoa maoni au kuamua jambo,hali hii imezoeleka katika jamii yetu kiasi kwamba akijitokeza mtu kutoa maoni tafauti anaonekana msaliti na kituko.

Wiki hii nimebahatika kuzungumza na Waziri Mwandamizi katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar asiyekuwa na Wizara Maalum,Mansoor Yussuf Himid juu ya suala zima la katiba mpya na Muungano wetu uliotimiza miaka 48 tangu kuzaliwa kwake mwaka 1964.

Waziri Mansoor anatoa angalizo kwamba kuelezea kasoro za Muungano au kupendekeza mfumo mpya wa Muungano kunachukuliwa na baadhi ya watu kama usaliti. “Dhana hii sio sahihi lazima tuheshimu mawazo ya kila mtu,hivi sasa hatuna tena Chama Dola(State Party) watu wote wanaoishi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wana haki ya kutoa maoni yao na kupendekeza mfumo unaowafaa”.

Anazungumziaje dhana ya ushirikishwaji wananchi na demokrasia? “Nchi zenye demokrasia kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania maamuzi yapo mikononi mwa wananchi wenyewe hivyo, suala la kuwa na Katiba mpya itakayokidhi mahitaji ya umma ni lazima iridhiwe na watu wote.

Wakati huu wananchi ndio wanaopaswa kuamua ni kitu gani wanahitaji au kiwe na sio kuamuliwa na watawala kama ilivyo zamani watawaliwa waliamuliwa na watawala”

Kwa tafsiri ya haraka ni kwamba Mansoor anajaribu kuelezea demokrasia ya moja kwa moja ambayo inatoa haki kwa umma kushiriki kuamua masuala ya kisiasa, kijamii, kisheria, na kiuchumi bila kutumia chombo cha uwakilishi kama vile bunge.

Wataalam wa sheria wanaona kitendo hicho ni sawa na nguvu za wananchi kutoa uamuzi kama ule wa kimahakama ingawa mara nyingi wananchi hupewa uwezo wa kutunga au kupitisha sheria tu.
Katika hili la katiba hakuna uwakilishi wa mtu wa tatu,kila Mtanzania anayo haki kwenda mbele ya Tume ya Katiba kutoa maoni yake hivyo, hatutaraji kuona watu wakibeza maoni ya wenzao.

Ni miaka 48 sasa imetimia,wanasiasa wanauonaje muundo wa Muungano uliopo wa kuwepo Serikali mbili,ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoshughulikia mambo ya Muungano na yale yasiyokuwa ya Muungano kwa upande wa Tanzania Bara na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayoshughulikia masuala yasiyokuwa ya Muungano kwa upande wa Zanzibar?

“Mimi mtazamo wangu ni huu,mfumo wa muundo wa Muungano wa Serikali mbili umeshindwa na utaendelea kushindwa kuhimili mabadiliko ya nyakati ndo maana kero za Muungano hazitatuliki, nadhani ni jambo la busara kuangalia muundo mpya wenye kukidhi matumaini ya watanzania Anasema Waziri Mansoor.

Akitilia mkazo hoja ya mabadiliko,Waziri huyo anaeleza kushindwa kwa mfumo wa Serikali mbili ni jambo la wazi na ili kujenga Muungano wenye matumaini na tija kwa kila mshiriki lazima tuingia kwenye mfumo mujarab.

“Mimi msimamo wangu nikwamba hapa tulipo fika tunahitaji mabadiliko makubwa katika mfumo wa Muungano wetu ‘radical change’
Aliongeza Waziri huyo.

Waziri Mansoor anajenga hoja kwamba kuelekea mchakato wa Katiba mpya,lazima kupatikana kwa mfumo wa muundo wa Muungano utakaoendelea kulinda maslahi ya Wazanzibari na Mapinduzi yao kwani walifanya Mapinduzi kujitawala na walipoamua kuungana na Jamhuri ya Tanganyika ilikuwa kutafuta nguvu zaidi na maslahi ya kiuchumi nakadhalika .

“Mimi naamini,msingi wa mapinduzi na yale ya mzee wetu bwana Abeid Amani Karume na Afro Shiraz Party na Wazanzibari walio wengi walimpindua Mkoloni na Mfalme ili wajitawale kwa sababu walikataa kutawaliwa na imani yangu pia waliingia katika Muungano kujenga Taifa moja lenye nguvu na matumaini ya aina mbalimbali na ikiwa hayo haya timizwi kwa sasa basi tunahitaji kufikiri upya” anabainisha Waziri Mansoor.

Waziri Mansoor alitoa wito kwa Viongozi wenzake kujitokeza hadharani kueleza misimamo yao badala ya kuzungumza kwenye ‘vibuyu’ ili wananchi wanaowaongoza waweze kujuwa misimamo na maoni yao.

“Viongozi waeleze wazi maoni yao, hawapaswi kuwa watu wa kufuata upepo ilimradi usivunjie sheria na kuchochea vurugu na mgawanyiko miongoni mwa wananchi…mimi msimamo wangu sikupata kuuficha na sitauficha” Anasema Mansoor.

Bila shaka Waziri Mansoor anawakumbusha viongozi wenzake wajibu wao kwa waliowachagua kuwataka kujitokeza hadharani kueleza hisia zao,lakini kwani viongozi wakumbushwe wajibu wao?

Hivi kwanini viongozi Zanzibar kuanzia wa vyama vya siasa, Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi,Madiwani wanakosa ujasiri na kupungukiwa ujabali kusema hadharani wanapendelea muundo upi wa Muungano badala ya kujiegemeza kwenye misimamo ya vyama vyao?

Anataja suala zima la katiba lazima liwe lenye tija kwa wananchi na hivyo kuwepo ulazima wa sharti hilo mwanzo katika nchi zenye kufuata misingi ya demokrasia,lazima katiba iridhiwe na watu wote kwa maana ipatikane consensus kwa lugha yetu maafikiano, na pia katiba iwe na maana yenye kukidhi matakwa yao,iwapo utaratibu huo kama hautakidhi matakwa ya Wazanzibari itakuwa haina maana kwao.

Akivuta taswira iwapo wananchi wataridhia kuwa na mfumo kama wa EU, Waziri huyo anasema kwamba Muungano wa Umoja wa Ulaya licha ya kutumia pasi moja ya kusafiria,sarafu moja,lakini hakuna Taifa lililopoteza Utaifa wake kila Taifa limeendelea kubaki na uanachama wake UN.

Anafafanua zaidi faida na kusema kwanini tunahofia kuwa na Muungano utakao panua wigo wa kiuchumi kwa upana zaidi,ambapo hata katika uwakilishi kwa mfano katika Umoja wa Mataifa, kutakuwa na viti viwili kile cha Tanganyika na Zanzibar.

“Hata ndugu kwa mfano mmoja akiwa ana uwezo kifedha na mwengine hana itakuwa malalamiko kila siku,lakini kama nyote mkiwa na hali sawa au zinazofanana mtaweza kuishi vyema bila mizozo kwa mfano hivi sasa Tanganyika imebarikiwa kuwa na madini mengi na mengine adimu kupatikana duniani wanavuna gesi kwa wingi na kuendelea na kazi ya utafutaji wa mafuta na gesia asilia pia.”

…lakini Zanzibar inapotaka kuvuna maliasili zake tunaambiwa maliasili hizo ni za Muungano na Zanzibar ifuate inavyoelekezwa na si vyenginevyo, sasa najiuliza huu ni Muungano wa Tanganyika pekee au Zanzibar na Tanganyika kwani bila Zanzibar hakuna Muungano hapa utaona tatizo la kuwepo kwa mfumo dhaifu. Anaongeza Waziri Mansoor ambaye pia ni Mweka Hazina wa CCM Zanzibar na Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki.

Anautazama mfumo huu ulioleta utata, kuna mkanganyiko wa mambo,Katika nchi moja yanaweza kuwepo mabunge mawili au hata zaidi,lakini pia kunaweza kuwepo Mawaziri viongozi wawili au watatu; lakini hakuna nchi yo yote kwenye sayari yetu yenye Marais wawili isipokuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wengi wanahoji kuwa ikiwa Zanzibar haikukusudiwa kuwa ni dola na waasisi wa Muungano vipi walikubali kuwepo kwa Mamlaka ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ikiwa na Rais Mtendaji,Waziri Kiongozi, Mahakama na Baraza la Wawakilishi?

Utata mwengine ni kuwa chini ya hati za Muungano ilikubaliwa kuwa kuwepo na Serikali mbili tu na kama nilivyoeleza hapo juu kiongozi wa serikali hiyo asiwe Waziri Kiongozi, Gavana au Waziri Mkuu,bali awe ni Rais na pia awe ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wazee waliofanya kazi na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar wanaweza kujibu swali hili kwamba hivi Bwana Abeid Amani Karume aliamini kuwa yeye ni Rais wa Dola ya Zanzibar au ni Rais wa SMZ bila ya dola?

Katika kesi iliyokuwa ikiwakabili wanachama 18 wa Chama cha CUF kudaiwa kula njama kutaka kuipindua Serikali ya SMZ chini ya Dk Salmin Amour,Mahakama ya Rufaa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitamka Zanzibar sio Dola.

Ijapokuwa Mahakama ya Rufaa, ilitoa hukumu hiyo na huku baadhi ya watu wakiona kuwa wana SMZ na Rais hilo kwao haliwashughulishi.

Lakini siku itakapoamuliwa kuwa kwa sababu Zanzibar si dola, basi hakuna ulazima wa kuwa na serikali wala Rais hapo ndipo watu watakapoacha kuwabeza wenye mawazo tafauti na kujiunga na hoja pendwa ya mfumo mpya wa Muungano

Mfumo huu inawezekana hata Mwalimu Julius Nyerere kama angekuwepo leo,angeweza kukubaliana na hoja hizi kwani Mwalimu hakufungika kwenye misimamo ndio maana wakati fulani aliwahi kusema CCM sio Baba wala Mama yake akiona kimebadili muelekeo ataweza kukiacha.

Kuhusu Muungano na matakwa ya Wazanzibari,Mwalimu Nyerere katika miaka ya mwanzoni ya Muungano huu aliwahi kusema kuwa na matamshi haya na kukaririwa na gazeti maarufu wa Uingereza la Observer mwaka 1968 kwamba; Ikiiwa wananchi wengi wa Zanzibar bila kushawishiwa na nguvu kutoka nje kwa sababu zao wenyewe wakiamua kwamba Muungano wanaona hauwafai ,mimi sitawapiga mabomu…Muungano utasita tu ikiwa Wazanzibari wataaondosha ridhaa yao”
(hii ni tafsiri isiyo rasmi)

Basi wale wanaotoa maoni yao kutaka Serikali tatu na Muungano usiokuwa wa Katiba wasichukiwe na kukejeliwa waonekane ni wazalendo kama walivyo wazalendo wengine wanaotaka ama Serikali mbili,moja au Shirikisho.

Katika mahojiano yangu na Waziri Mansoor anatoa ushauri kwa jamii kuacha kuwachukia watu wenye mtazamo na maoni tofauti “Tusichukiane kwa mawazo yetu kila mmoja ana haki na maoni yake kuheshimiwa.

Na pia hivi sasa wapo Wazanzibari hawautaki kabisa Muungano,wapo wanaotaka mkataba,wapo wachache wanakubaliana na mfumo huu na wapo wachache zaidi wanataka tubaki na Serikali mbili kuelekea moja, haya yote ni maoni ya watu ambao ni wananchi wenye haki sawa na wenziwao na hatimae kwa mfumo wa utawala tulionao maamuzi ya walio wengi ndio yatakayo simama.”

Katika mchakato wa katiba kama hupendi mawazo ya wengine unaweza kuweka hoja zako zenye mawazo mbadala,lakini sio jazba wala kuwachukia wengine kwani hata Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk. Ali Mohammed Shein anasisitiza ulazima wa kujenga hoja wakati wa kutoa maoni ambazo pengine zitawashawishi wengine kuunga mkono.

Lakini pamoja na hoja hizo,jambo la msingi ni kuweka mbele maslahi ya wengi na pia kutazama hatma ya sasa na ya baadaye ya Zanzibar ambayo misingi yake ilitokana na dhamira njema na sahihi za waasisi wa Mapinduzi matukufu ya Januari 12,1964 pale walipoiweka katika hali ya umoja,kuheshimiana na usawa kwa watu wote.

Advertisements

2 responses to “Viongozi msiogope kutoa maoni yenu katika katiba mpya

  1. hata kama wamekwambia mwizi bora wewe kuloko kungi la seif aliy idi na shamuhuna firaunaaa wazanzibar tuko njyuma yakoooo

  2. Ah..! Bilal huna lako tena ukimaliza hapo nenda kafungue makanisa, mzee wa kukata utepe na kufungua matawi ya chama.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s