Serikali yavuliwa nguo

Mansour Yussuf Himid Machano Othman Said ni miongoni mwa mawaziri waliotajwa katika kamati teule ya baraza la wawakilishi ya kuchunguza ubadhirifu uliofanyika katika sekta mbali mbali na kutumia madaraka yao vibaya wakiwemo maafisa wa Ikulu Zanzibar

Kamati imebaini kwamba, Mikataba yote ya mauziano iliyofungwa baina ya Serikali na Ndg. Juma Ali Kidawa na baina yake na Ndg. Amina Aman Abeid Karume ni batili na ya udanganyifu. Aidha, Hati ya Matumizi ya Ardhi aliyopewa Ndg. Amina Aman Abeid Karume na Mhe. Mansour Yussuf Himid, kama tulivyoitolea ufafanuzi wake katika ukurasa wa 182-183, imekiuka taratibu za kisheria na kiutawala.Mhe. Spika: Pia tumegundua kuwa: Mzee Juma Ali Kidawa sio Mmiliki halali kisheria wa Nyumba. iliyokuwa imefuatiliwa na wala hakuhusika na Uuzaji wa Nyumba hiyo kwa mtu yoyote na hakuwahi kufuatilia Utengenezaji wa Warka wa Nyumba hiyo.Mhe. Spika:Hata hivyo, kwa mujibu wa nia njema na mazingira halisi yalivyojitokeza yanaonesha Mzee Juma Ali Kidawa alihusika na kufanya kazi kwa Mhindi aliyeimiliki nyumba hiyo kabla ya kutaifishwa na Serikali.Mhe. Spika:Kamati imejiridhisha kwamba:Ndg. Ramadhan Abdalla Songa na Mama Fatma Karume walishiriki katika Udanganyifu wa Mkataba wa Mauziano uliofungwa baina ya Serikali (Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati) na Ndg. Juma Ali Kidawa. Mhe. Spika:Maelezo haya yanafafanuliwa katika ukurasa wa 178 hadi wa 180 wa ripoti yetu.Mhe. Spika: Mbali na taarifa hizo, lakini pia Kamati imebaini kwamba:Ndg. Mwalimu Ali Mwalimu kama Katibu Mkuu, amechangia kufanyika kwa udanganyifu wa Mkataba wa Mauziano baina ya Wizara yake na Ndg. Juma Ali Kidawa.

HOTUBA YA MWENYEKITI WA KAMATI TEULE YA BARAZA LA WAWAKILISHI-ZANZIBAR.

Mhe. Spika:
Kwanza kabisa, naomba sote kwa pamoja tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuturuzuku uhai na kutujaalia afya njema, inayotuwezesha kuhudhuria katika Mkutano huu wa Saba kwa amani huku tukiwa wazima wa afya, na zaidi kwa kuweza kuhudhuria kikao cha leo, kikao ambacho kinaweka Historia ya miaka 10 iliyopita ya Baraza hili. Hatuna budi tuendelee kumuomba Allah, kwa njia ya kutekeleza mema aliyotuamrisha, ili azidi kuturuzuku uhai na afya njema.

Mhe. Spika:
Nakushukuru wewe kwa kunipa fursa hii kwa niaba ya Kamati Teule, kusimama mbele ya Baraza lako tukufu, kwa lengo la kuwasilisha ripoti ya kazi ya Kamati Teule ya Baraza la Wawakilishi, uliyoiunda chini ya matakwa ya Kanuni za Baraza hili, mwezi wa August, 2011.

Mhe. Spika:
Mamlaka ya Baraza la Wawakilishi ya Kuunda Kamati Teule, kwa madhumuni ya kuchunguza jambo maalum, yanatokana na mamlaka ya Baraza hili kama mmoja ya Mihimili mitatu mikuu ya Nchi, iliyoelezwa na 5A, cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. Mhe. Spika, kumbu kumbu zinaonesha kwamba, mara ya mwisho Baraza hili kuunda Kamati Teule ilikuwa ni mwaka wa 2002, wakati Baraza hili Tukufu lilipounda Kamati Teule kuhusu Magendo ya Karafuu, iliyoundwa katika Kikao cha tarehe 22/04/2002 takriban miaka 10 sasa. Na ndio maana hapo mwanzo tulisema kwamba, leo hii tunaweka historia ya miaka 10 iliyopita.

Mhe. Spika:
Kwa niaba ya Wajumbe wa Kamati Teule, sina budi kukupongeza kwa dhati Mhe. Spika wa Baraza hili la Wawakilishi, Mhe. Pandu Ameir Kificho, kwa namna unavyoliendesha Baraza hili, ambalo ndio chombo cha wananchi. Mhe. Spika, namna unavyoliendesha Baraza hili kwa UWAZI na kwa kufuata SHERIA NA KANUNI za Baraza, kunaonesha wazi kwamba wewe ni namba moja wa kusimamia mageuzi ya kukuza Demokrasia na Utawala Bora nchini bila ya shaka Mhe. Spika, historia itakukumbuka kwa wema.

Mhe. Spika:
Napenda nitumie fursa hii kuipongeza Serikali ya Awamu ya Saba, yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa inayoongezwa na Dr. Ali Moh’d Shein, kwa namna ilivyotayarifu katika kuendeleza misingi ya Utawala Bora kwa maana ya kuheshimu mgawanyo wa madaraka, Uwazi na Uwajibikaji.

Mhe. Spika:
Wananchi wa Zanzibar baada ya muda mrefu kupita, sasa wameanza kuona uhalisia wa utekelezaji wa dhana ya Muasisi wa Baraza hili, Mhe. Rais wa awamu ya Pili wa Zanzibar, Al-haj Aboud Jumbe Mwinyi, kwamba Baraza la Wawakilishi ndio ngome ya wananchi wa Zanzibar, wananchi ambao ndio wenye mamlaka ya kuendesha nchi kwa mujibu wa kifungu cha 9(2) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Mhe. Spika:
Kufuatia Mkutano wa Nne wa Baraza la Wawakilishi ambao ulikuwa maalum kwa ajili ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2011/2012, Baraza liliridhia kuundwa kwa Kamati Teule ya Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya kuchunguza mambo mbali mbali ambayo yaliibuka kwenye majadiliano ya Bajeti, kutokana na kupata majibu ambayo yalionekana kuwa na utata na hivyo Wajumbe kutoridhika nayo.

Kufuatia maamuzi hayo ya Baraza, Mhe. Spika kwa mamlaka uliyonayo, ulifanya uteuzi wa wajumbe hao, siku ya tarehe 09/08/2011 kawa wafuatao:

1. Mheshimiwa Omar Ali Shehe Mwenyekiti.
2. Mheshimiwa Asha Bakari Makame Mjumbe.
3. Mheshimiwa Hamza Hassan Juma Mjumbe.
4. Mheshimiwa Hija Hassan Hija Mjumbe.
5. Mheshimiwa Mbarouk Wadi Mussa (Mtando) Mjumbe.
6. Ndg. Yahya Khamis Hamad Katibu.
7. Ndg. Othman Ali Haji Katibu.
Mhe. Spika:
Naomba niitumie fursa hii kuwasilisha shukrani za Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati hii kwako Mhe. Spika, kwa busara na hekima yako ya kututeua Kuunda Kamati hii ambayo ina changamoto nyingi. Aidha, naomba pia niwasilishe shukurani za Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati, kwa Waheshimiwa Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi, kwa kuridhia kwao kuunda Kamati hii, kwa lengo lile lile la kusimamia utekelezaji bora wa shughuli za Serikali yetu. Naomba niitumie nafasi hii kuwashukuru sana Wajumbe wenzangu wa Kamati Teule, kwa kukubali kwao kuniteua kuwa Mwenyekiti wa Kamati hii muhimu sana.

Mhe. Spika:
Kuteuliwa kwetu kwenye Kamati hii, kunatokana mbali na matakwa ya kanuni, lakini pia imani uliyonayo wewe Mhe. Spika, pamoja na Waheshimiwa Wajumbe wenzetu kwetu. Mhe. Spika; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, aliwahi kusema wakati akikubali uteuzi wa Chama chake cha C.C.M kuwa, “Deni la fedha hulipwa fedha na deni la imani halilipiki ila kwa imani”

Mhe. Spika:
Nasi wajumbe wa Kamati hii, hatuna budi kurejesha deni la imani zetu kwetu kwa kuonyesha imani yenye UADILIFU kwa kazi mliyotutuma kwa niaba ya wananchi wa Zanzíbar, kufanya kazi ambayo ilikuwa na Hadidu rejea (Terms of References) Tisa kama zifuatazo:

1. Kamati ilitakiwa ifanye uchunguzi juu ya zoezi la uhaulishaji wa Kiwanja cha Wizara iliyokuwa ya Mawasiliano na Uchukuzi kilichopo Mtoni kwenye eneo la Karakana ya Wizara hiyo.

2. Kuchunguza suala zima la Uwanja wa Ndege wa Zanzibar kuhusu ulipaji wa fidia kwa watu ambao mali zao zimeathirika kutokana na ujenzi wa uzio wa Uwanja wa Ndege, matatizo ya ununuzi wa jenereta, mikataba ya ukodishwaji wa sehemu za biashara kwenye eneo la Uwanja wa Ndege na utaratibu wa ajira na utoaji wa huduma mbali mbali kwenye maeneo ya Uwanja wa Ndege na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kwa ujumla.

3. Kuchunguza matatizo ya uvamizi wa fukwe na uharibifu wa mazingira kwenye hoteli inayopakana na Chuo cha Maendeleo ya Utalii Zanzibar, Maruhubi, kwenye Hoteli ya Zanzibar Ocean View, Kilimani-Zanzibar, na Hoteli ya Misali iliyopo Wesha, Chake Chake-Pemba.

4. Kuchunguza zoezi la uhaulishwaji wa Kiwanja kinachopakana na jengo la ‘Livingstone House’ Mbuyu Taifa, Mjini, Zanzibar.

5. Kuchunguza uhalali wa Mikataba ya Nyumba ya Serikali iliyopo Kiponda inayodaiwa kwamba alipewa mwananchi na baadae kuiuza kwa mtu mwegine.

6. Kuchunguza sababu na ukweli kuhusu matatizo yaliyotokea kwenye ujenzi wa jengo jipya la Wizara ya Fedha, Pemba.

7. Kuchunguza uhaulishaji wa Majengo ya Mambo Msiige na Starehe Club.

8. Kuchunguza Ukodishwaji wa Kisiwa cha Changuu kilichopo nje kidogo Magharibi ya Mji wa Zanzibar.

9. Kuchunguza hatma ya majenereta yaliyoletwa Zanzibar kusaidia shughuli za Usambazaji wa maji wakati Zanzibar ilipokosa umeme kwa miezi mitatu.

Mhe. Spika:
Hizo ndizo hadidu rejea ambazo Kamati Teule ilikabidhiwa kwa ajili ya kuzifanyia kazi. Naomba kumshuru sana aliyekuwa Katibu wa Baraza la Wawakilishi na hivi sasa ni Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka, Ndg. Ibrahim Mzee Ibrahim, kwa namna alivyotoa msaada na mchango mkubwa uliopelekea Kamati kufika katika hatua hii, licha ya uchache wa muda, rasilimali fedha na vikwazo mbali mbali vilivyojitokeza kwa baadhi ya Watendaji. Kamati inamuombea mafanikio katika majukumu mapya ya kazi yake.

Mhe. Spika:
Kamati yetu ilitumia jumla siku 30 ilizopangiwa na Afisi ya Baraza la Wawakilishi kufanya kazi ya uchunguzi wa hadidu mbali mbali za Kamati, ambapo ripoti kamili juu ya kazi hiyo ni hii tuliokabidhi leo, ikiwa na jumla kurasa 224, na jumla ya Vielelezo 232. Naomba nitumie fursa hii, kuelezea muhtasari wa ripoti katika eneo la matokeo ya uchunguzi wa Kamati kwa kila Hadidu rejea. Na hivyo, naomba nianze na Hadidu Rejea inayohusiana na:
“Uhaulishwaji wa Kiwanja cha Wizara ya Miundombinu na Mawasililiano ambacho kipo kwenye eneo ilipokuwepo Karakana na Wizara hiyo, eneo la Mtoni, Mjini, Zanzibar.

Mhe. Spika:
Katika kufuatilia Hadidu hiyo, Kamati ilichunguza sababu za kuhaulishwa kwa kiwanja hicho, na kugundua kwamba, kuna tofauti kubwa ya majibu yaliyotolewa na Waziri na Naibu wake, walipokuwa wanatoa ufafanuzi wa suala hili hapa Barazani na majibu ambayo Kamati imeyapata katika vikao vya Kamati na Watendaji Wakuu wa Wizara hii. Lakini, Kamati imejiridhisha kwamba, sababu zilizoelezwa hazikuwa za msingi na matokeo yake ni kuiingiza Serikali katika hasara kwa kutojenga Ofisi ya Wizara kama vile ambavyo Serikali ilikwishatoa Tsh. 49,100,000/- kwa kazi hiyo.

Mhe. Spika:
Kabla sijafanya muhtasari wa mambo ambayo Kamati imeyagundua katika Hadidu hii, naomba nitangulie kueleza kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilitoa waraka maalum kwa taasisi zote za Umma, kuzuiya uuzwaji wa mal iza Serikali, waraka ambao katika ripoti yetu tumeuleza katika Ukurasa wa 20 hadi 22 na kuufanya kama Kielelezo Namba 11 na Namba 12.

Mhe. Spika:
Katika agizo hilo, jambo la msingi ni kukatazwa kwa kila Afisa Mhasibu (Accounting Officer) kuuza mali za Serikali, mpaka pale watakapopewa agizo jengine la kuruhusiwa kuuza mali hizo. Lakini jambo la kusikitisha, agizo hilo limekiukwa na Watendaji na Viongozi wa Wizara hizi bila hata ya kujali kwamba, wao wanawajibika kuheshimu maagizo ya Serikali Kuu. Hivyo, kama tulivyoeleza katika ripoti yetu kuanzia ukurasa wa 5 ukurasa wa 24, kwamba Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, ambayo sasa ndio Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, imeuza kiwanja chake ambacho kilipewa kwa ajili ya ujenzi wa Afisi yake, kinyume na kuheshimu maagizo ya Serikali. Mhe. Spika; Jambo hili linahitaji kuchukuliwa hatua kama ambavyo tumependekeza katika ripoti yetu kuanzia ukurasa wa 24 wa ripoti hii.

Mhe. Spika:
Sasa naomba nifanye Muhtasari wa mambo ambayo Kamati yetu imefanikiwa kuyagundua baada ya Uchunguzi iliyoufanya kwa Hadidu rejea kama ifuatavyo:

Muhtasari wa Mambo yaliyobainika na Kamati kufuatia Uchunguzi wake wa
Hadidu hii Rejea:

(i) Kuna ukiukwaji mkubwa wa Sheria na Taratibu za Uuzaji wa Mali za Serikali:

Mhe. Spika:
Kamati imejiridhisha kwamba Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano haikufuata taratibu za uuzaji wa kiwanja ilichokuwa inakimiliki na kuamua kukiuza kwa Kampuni binafsi bila ya kufuata taratibu za Kiutawala na Taratibu za Kisheria, hali inayopelekea wasi wasi mkubwa wa kuwepo kwa harufu ya ubinafsi na harufu ya rushwa, na zaidi ukizingatia thamani ya kiwanja hicho kuwa ni sawa na Tsh. 200,000,000/- bei ambayo ni ndogo kwa mujibu wa bei ya soko na kwa kuzingatia ukubwa wa kiwanja chenyewe na eneo kilipo.

Mhe. Spika:
Mhe. Spika, suala jengine ambalo Kamati yako imeweza kulibaini ilipokuwa inafuatilia Hadidu hii ni kuhusu:

(ii) Upotoshaji mkubwa kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Kamati zake kuhusiana na taarifa wanazopatiwa na Viongozi wa Wizara na Watendaji wao wakuu.
Mhe. Spika:
Itakumbukwa kuwa, suala hili la kama kweli kiwanja hicho kimeuzwa na Wizara ama laa, lilileta mjadala mrefu hapa Barazani, na ilikuwa ni tabia na misimamo ya Mhe. Waziri na Naibu wake, kueleza kwamba Kiwanja hicho hakijauzwa na kipo salama. Aidha, walieleza kwamba, katika uhaulishwaji wake, Wizara ilifuata taratibu zote za sheria na hivyo, hakukuwa na haja ya kwenda kufanya uchunguzi wa suala hili. Pamoja na maelezo haya, Kamati imejiridhisha kwamba, kiwanja hicho kimeuzwa na alieuziwa ni Ndg. Said Salum Bakhressa, kupitia Kampuni yake ya Coastal Fast Ferries Ltd, kwa thamani ya Tsh. 200,000,000/- ingawaje malipo ya fedha hizo sio kulipa kwa ‘cash’ ama kulipa fedha, na badala yake atumie kiasi hicho cha fedha kwa kujenga ‘Ground floor’ ya Afisi ya Wizara inayotarajiwa kujengwa katika Kiwanja cha Wizara hii, kilichopo Mazizini (Kiembe Samaki).

Mhe. Spika:
Kwa mnasaba huu, Kamati imejiridhisha kwamba, majibu ya Mhe. Waziri na Naibu Waziri wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano na majibu yaliyotolewa kwa Kamati katika Kikao cha pamoja na Watendaji Wakuu wa Wizara hii, na kwa mnasaba wa taarifa zilizowasilishwa kwa Kamati ya P.A.C ilipokuwa inafuatilia uuzwaji wa kiwanja hiki, imebaini wazi kwamba, kuna taarifa nyingi zisizo za kweli zinazotolewa kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, bila ya watoaji wa taarifa hizo kuzingatia Haki, Fursa na Uwezo wa Wajumbe katika kupewa taarifa sahihi na zilizo za kweli.

Mhe. Spika:
Jambo la tatu ambalo Kamati yetu imeweza kulibaini ilipokuwa inafuatilia Hadidu hii, katika Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano ni:
(iii) Kuna ukiukwaji mkubwa wa maadili ya kazi na utumiaji mbaya wa madaraka.

Mhe. Spika:
Kamati imegundua kwamba, Viongozi wajuu wa Wizara na watendaji wao wakuu wanatumia vibaya madaraka yao bila ya kujali maadili ya kazi zao ama bila hata ya kujali sheria na kanuni za utumishi wao ama wadhifa wao, hali ambayo kama itaendelea kuachiwa, itaifikisha pabaya nchi hii inayoongozwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria.

Mhe. Spika:
Kama tulivyoeleza katika ripoti yetu, katika ukurasa wa 13, tulipokuwa tunazungumzia Tatizo la Saini katika Mkataba, ni wazi kwamba, Kitendo cha Mhe. Waziri (Mhe. Machano Othman Said) kuingia katika Mkataba wa kuuza kiwanja cha Wizara, kinakiuka maadili yake ya kazi. Jambo baya zaidi, ni kumkuta Mhe. Waziri huyu, akiffanya maamuzi yeye mwenyewe ya kumtafuta Mnunuzi wa kiwanja hicho, kama ambavyo tumeeleza katika ukurasa wa 9 hadi wa 12, tulipokuwa tunazungumzia Utangazaji wa Zabuni na Mamlaka ya Kumtafuta Mnunuzi, ni wazi kwamba, kwa mashirikiano ya pamoja baina ya Mhe. Waziri na Ndg. Abdalla H. Kombo, ndio waliofanikiwa kumpata Mnunuzi, kwa kumtafuta wao. Aidha, wakati Ndg. Bakhressa alivyotoa uhalisia wa hili, alijibu kwamba ni yeye Mhe. Waziri alimpigia simu kumweleza kwamba kuna kiwanja kinauzwa.

Mhe. Spika:
Suala hili, linakiuka taratibu za Maadili ya kazi na sio busara hata kidogo kuendelea kuvumiliwa, kwani tukiliachia leo, litaendelea kuota mizizi kesho na hatimae, ikifikia wakati, kila mtumishi wa Serikali ama Kiongozi wa juu, anatumia madaraka yake kama anavyoona yeye na wala sio kama anavyotakiwa kutekeleza, kwa mujibu wa Sheria za nchi.

Mhe. Spika:
Suala jengine tulilolibaini katika Wizara hii, kuhusiana na Hadidu yetu ni hili:

(iv) Kuna utumiaji mbaya wa Madaraka ya Ofisi ya Rais:
Mhe. Spika:
Suala hili tumelieleza kuanzia ukurasa wa 16 hadi wa 18, tulipokuwa tunaangalia namna gani maamuzi mazito ya kuuza kiwanja cha Serikali, yakaruhusiwe na Mhe. Rais. Mhe. Spika, katika utafiti wetu, tuligundua kuwa, maombi ya ruhusa ya kuuzwa kwa kiwanja hicho, yametoka kwa Katibu wa Rais, Ndg. Haroub S. Mussa, ambae aliandika barua, tuliyoifanya kielelezo Namba. 9 cha Ripoti yetu.

Mhe. Spika:
Hoja yetu kubwa ambayo tumeieleza katika ripoti yetu, ni kwamba, Ndg. Haroub hana mamlaka ya kuruhusu uuzwaji wa kiwanja, wala kusimama katika nafasi ya kupeleka maamuzi ya Mhe. Rais kwa mtu mwengine yeyote, na kazi hii kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, kifungu cha 49(1), ingelifanywa na Katibu Mkuu Kiongozi, na wala sio Katibu wa Rais. Hivyo, inapofika wakati, Mhe. Waziri, anasimamia kwamba amepata ruhusa ya Mhe. Rais ya kuuza kiwanja cha Serikali, hoja yake haina uzito wa kikatiba.

Mhe. Spika:
Suala hili linapaswa litizamwe upya, kwani Kamati inaamini kwamba, nafasi ya Rais na Ofisi yake inatumiwa visivyo.

Mhe. Spika:
Suala jengine ambalo Kamati imeligundua ni:

(v) Kuwepo matumizi mabaya ya fedha za Serikali kinyume na taratibu zake:
Mhe. Spika:
Kamati imegundua kwamba, Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano haikutumia fedha iliyoidhinishwa kwa ajili ya Ujenzi wa Afisi yake ya Kudumu kwa mwaka 2009/2010 badala yake imeamua kuzitumia fedha hizo kwa ukarabati wa jengo la Bohari Kuu na Jengo la Afisi yao ya Makao Makuu ya zamani ambalo linamilikiwa na Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana. Kosa zaidi, ni kufanya matumizi haya bila ya kufuata taratibu za fedha ikiwa ni pamoja na kuhaulisha kisheria na matokeo yake, Serikali imetoa fedha iliyoidhinishwa na Baraza la Wawakilishi huku fedha hizo zikitumika kinyume na malengo yaliyokusudiwa.

Mhe. Spika:
Suala hili pia tumelijadili kwa upana wake katika ukurasa wa 19 hadi wa 20 wa ripoti yetu.

Mhe. Spika:
Suala la Sita, ambalo Kamati yetu imeweza kuligundua linahusu:

(vi) Kukiukwa kwa Ushauri na maelekezo yanayotolewa na Kamati za Baraza la Wawakilishi kunapelekea gharama zisizo za lazima kwa Serikali.

Mhe. Spika:
Kamati imefahamu kwamba, Hoja hii ya kuuzwa kwa kiwanja cha Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, ilianza kwanza kufuatiliwa na Kamati ya Kuchunguza na Kudhibiti Hesabu za Serikali na Mashirika (P.A.C) ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ilipokuwa inafuatilia Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2008/2009, ingawaje hoja hii haijaibuka moja kwa moja katika Ripoti hiyo, lakini kwa mamlaka iliyopewa Kamati hiyo, imeliuliza suala hili na kupewa majibu yasiyoridhisha. Hata hivyo, Kamati ilitoa agizo la kuzuia ujenzi katika kiwanja hicho na Wizara ikajibu kwamba wamefuata taratibu zote za kisheria katika kuhaulisha kiwanja hicho na hivyo kwa kuwa tayari wameshakiuza, hawana mamlaka ya kuwazuia badala yake ni Serikali Kuu yenye Mamlaka ya kuzuia ujenzi huo.

Mhe. Spika:
Kamati hii inaamini kwamba, laiti kama Kamati ya P.A.C ingepatiwa majibu ya kuridhisha, kusingekuwa na haja ya kuundwa kwa Kamati Teule kufuatilia jambo hili, na matokeo yake fedha nyingi zimetumika kuunda na kusimamia Kamati hii Teule.

Mhe. Spika:
Suala la saba ambalo Kamati imelibaini ni kuhusu:
(vii) Mawaziri kuingilia majukumu ya Makatibu Wakuu wa Wizara zao:
Mhe. Spika:
Kamati imegundua kwamba, baadhi ya Mawaziri wa Serikali wanatekeleza majukumu ya Makatibu Wakuu, kitendo ambacho sio tu kutekeleza majukumu yasiyo yao ambayo hawajatumwa kisheria, lakini pia hupelekea kuwepo kwa shaka kubwa juu ya usahihi wa utekelezaji wa majukumu hayo.

Mhe. Spika :
Ukiangalia ripoti yetu, ukurasa wa 13, tumeeleza kwamba, Waziri wailiyokuwa, Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, ametia saini Mkataba wa Mauziano ya Kiwanja hicho, ambacho kilikuwa ni mali ya Wizara. Kitendo hiki kinatofautiana na mazoea (practice), lakini kinakiuka matakwa ya Katiba na Sheria za Fedha, kama tulivyoeleza katika ripoti yetu.

Mhe. Spika, tatizo jengine tulilolibaini ni kuhusu :

(viii) Ukiukwaji wa Maagizo na Maelekezo ya Serikali.
Mhe. Spika:
Kama tulivyosema awali, kwamba Wizara hii haikuheshimu maagizo na maelekezo yanayotolewa na Serikali katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Kamati imejifunza hili kwa mnasaba wa Agizo la kuzuia uuzwaji wa mali za Serikali ambapo Wizara ya Miundombinu haikulifuata maelekezo yake.

Mhe. Spika:
Sasa naomba nieleze Mapendekezo ya Kamati kuhusiana na suala hili. Mhe. Spika, baada ya Kamati kuifanyia kazi hadidu rejea hii na kugundua mambo mengi kama nilivyokwisha yaeleza hapo awali, imependekeza hatua za Kuchukuliwa kutokana na matokeo ya uchunguzi huo. Na kwa ruhusa yako, naomba sasa kuzitaja hatua hizo kama ifuatavyo:

(i) Aliyekuwa Waziri wa Nchi, Afisi ya Raisi, Mawasiliano na Uchukuzi (2008-2010) na watendaji wote waliohusika katika kuingia mikataba na Kampuni ya Coastal Fast Ferries Ltd, wawajibishwe kwa misingi ya sheria.
(ii) Kamati inapendekeza Waziri na Naibu Waziri wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano waliombe radhi Baraza la Wawakilishi kwa kutaka kulipotosha Baraza, juu ya ukweli wa uuzwaji wa Kiwanja tulichokizungumzia katika hoja hii. Aidha Watendaji mbali mbali wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano wachukuliwe hatua kwa msingi wa sheria Namba 4 ya mwaka 2007, kwa kosa la kuzidanganya Kamati za Baraza la Wawakilishi.
(iii) Serikali ichukue hadhari kubwa na matumizi ya jina la Mhe. Rais na Ofisi yake.
(iv) Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano achukuliwe hatua za kinidhamu kwa kutosimamia ipasavyo mali ya Serikali iliyo chini ya Wizara yake ambapo kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Fedha (Sheria Na. 12 ya 2005 na Kanuni zake) yeye ndio msimamizi Mkuu.
(v) Uhaulishwaji huu sio halali kisheria na kiutawala, hivyo Kamati inapendekeza kiwanja hicho kirejeshwe Serikalini mara moja.
Mhe. Spika:
Kamati pia ilipewa Hadidu ya Pili, ambayo ilikuwa kama ifuatavyo:
“Kuchunguza suala zima la Uwanja wa Ndege wa Zanzibar kuhusu ulipaji wa fidia kwa watu ambao mali zao zimeathirika kutokana na ujenzi wa uzio wa Uwanja wa Ndege, matatizo ya ununuzi wa jenereta, mikataba ya ukodishwaji wa sehemu za biashara kwenye eneo la Uwanja wa Ndege na utaratibu wa ajira na utoaji wa huduma mbali mbali kwenye maeneo ya Uwanja wa Ndege na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kwa ujumla.

Mhe. Spika:
Katika ripoti yetu, tumeieleza Hadidu hii rejea kuanzia ukurasa wa 25 hadi ukurasa wa 123, na tuliigawa Hadidu, katika maeneo Matano Makuu kama ifuatavyo:
1. Kuhusu ulipaji wa fidia kwa watu ambao mali zao zimeathirika kutokana na ujenzi wa uzio wa Uwanja wa Ndege.
2. Kuhusu matatizo ya ununuzi wa jenereta;
3. Kuhusu mikataba ya ukodishwaji wa sehemu za biashara kwenye eneo la Uwanja wa Ndege
4. Kuhusu utaratibu wa ajira Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kwa ujumla.; na
5. Suala la utoaji wa huduma mbali mbali kwenye maeneo ya Uwanja wa Ndege.
Mhe. Spika, naomba sasa nianze kutoa muhtasari wa kipengele kimoja baada ya chengine, kama ifuatavyo:

“Kuhusu ulipaji wa fidia kwa watu ambao mali zao zimeathirika kutokana na ujenzi wa uzio wa Uwanja wa Ndege”
Mhe. Spika:
Kuhusu suala hili, Kamati imeweza kufanya uchunguzi wake, kama taarifa ya suala hili inavyoonekana kuanzia ukurasa wa 27 hadi 33 ya ripoti yetu, na kwa muhtasari, Kamati imeweza kupata kugundua mambo yafuatayo:

(i) Utaratibu wa Ulipaji wa Fidia kwa wananchi walioathirika na Ujenzi wa Uzio wa Uwanja wa Ndege, haukufuata taratibu za kisheria.

Mhe. Spika:
Kamati imegundua kwamba, ulipwaji wa fidia kwa wananchi walioathirika na mali zao za kudumu pamoja na mali zao za muda, haukulipwa kwa kufuata maelekezo ya sheria za fedha. Hali hii inaleta wasi wasi kwamba, fedha hizo inawezekana sana hazikutumika ipasavyo.

Mhe. Spika:
Katika ripoti yetu, ukurasa wa 26 hadi uk-30 tulizungumzia namna gani malipo hayo yalivyokosa sifa za kisheria. Aidha,

(ii) Hakuna tathmini ya Kitaalamu iliyofanyika kwa wananchi wenye mazao na vipando mbali mbali na wengi wao wamelipwa bila ya kufanywa kwa tathmini yoyote.
Mhe. Spika:
Kutokana na ushahidi uliowasilishwa na kwa mujibu wa uchunguzi wetu, tumebaini kwamba, wananchi wengi wamelipwa fedha zao kupitia Benki ama kupitia mkononi bila ya kufanyiwa tathmini yoyote ya kitaalamu, juu ya vipando na mazao yao, hali ambayo imepelekea kulipwa fedha kidogo kuliko thamani halisi ya mazao na vipando vyao. Kwa upande wa waliomiliki mali zisizohamishika, Kamati imejiridhisha kwamba tathmini halisi ya mali kwa mnasaba wa soko imefanyika, ingawaje kasoro iliyojitokeza ni kutoshirikishwa ipasavyo kwa wamiliki hao wakafahamu namna gani tathmini hiyo imefanyika.

Mhe. Spika:
Kuhusiana na hoja kwamba wananchi wote wamelipwa fidia ama laa, Kamati imebaini kwamba;
(iii) sio wananchi wote waliolipwa fidia za mali zao huku msisitizo ukiwekwa kwa Ndg. Ali Mwinchande Simba ambae ndie sababu ya Kamati hii kutumwa kwenda kufanya uchunguzi.
Mhe. Spika:
Kama tutafanya marejeo ya ukurasa wa 26 mpaka 31 wa ripoti yetu, tutafahamu kwa nini na kwa utaratibu gani, Kamati imegundua masuala haya.

Mhe. Spika:
Suala jengine ambalo Kamati imeligundua ni hili linalohusu :
(iv) Viongozi wa Wizara, yaani Waziri na Naibu Waziri wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kwa wamefanya kosa la kulipotosha Baraza la Wawakilishi kwa kutoa majibu yasiyo na ukweli wowote.
Mhe. Spika :
Kinyume na Kanuni za Baraza zinavyoelekeza, Kamati imethibitisha kwamba, Waziri na Naibu wake walipokuwa wanatoa ufafanuzi wa suala hili walilipotosha Baraza kwa kutoa taarifa zisizo za kweli, hali inayoonesha ama majibu haya wanayatoa kwa kuongozwa vibaya na watendaji wao ama kwa kutofanya utafiti binafsi wakajiridhisha juu ya usahihi wa taarifa wanazotakiwa wazitoe katika Baraza la Wawakilishi.

Mhe. Spika :
Suala hili liko wazi kwamba, kwa muda wote kabla ya kuundwa kwa Kamati hii, Viongozi wa Wizara hii walisimamia misimamo yao kwamba hakuna mwananchi ambae hajalipwa fidia, katika kupisha ujenzi wa Ukuta wa Uwanja wa Ndege. Hata hivyo, Kamati imejiridhishwa kwamba, Ndg. Ali Mwinchande Simba, mwananchi huyu anamiliki nyumba katika sehemu ya Uwanja wa Ndege, bado hajalipwa fidia wala hakuna uthibitisho wa kwamba wananchi wote wamelipwa fedha zao

Mhe. Spika :
Suala jengine ambalo pia linanasibiana na taarifa sahihi kwa Kamati, Kamati imebaini kwamba,

(v) Imepewa taarifa za Uongo na upotoshaji.

Mhe. Spika:
Mbali na vikao vya Baraza, wakati Kamati ilipofanya kazi na Uongozi wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege, pamoja na Uongozi wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kuhusiana na suala hili, ilipatiwa taarifa zisizo za kweli kuhusiana na fidia hiyo, hivyo, Watendaji Wakuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano pamoja na Mamlaka ya Uwanja wa Ndege walishirikiana katika kutaka kuipotosha Kamati juu ya uchunguzi uliotakiwa ufanywe.

Mhe. Spika:
Kutokana na yote haya, Kamati inapendekeza hatua zifuatazo zichukuliwe:

(i) Hatua za Kinidhamu zichukuliwe dhidi ya watendaji waliohusika na malipo ya fedha za fidia kwa wananchi walioathirika na ujenzi wa uzio, kutokana na watendaji hao kutofuata ipasavyo taratibu za malipo hayo kwa mujibu wa sheria za fedha (Na. 12 ya 2005)
(ii) Mwananchi ambae bado hajalipwa fidia, Ndg. Ali Mwinchande Simba alipwe fidia yake kwa mnasaba wa thamani ya mali zake katika wakati tulionao na sio tena wakati uliopita, kwa sababu tokea muda uliofanywa tathmini hadi leo, maisha yameshabadilika na thamani halisi ya Nyumba imeongezeka.
(iii) Kwa kutumia Kanuni za Baraza la Wawakilishi, Kamati inapendekeza Waziri na Naibu Waziri wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, waliomberadhi Baraza la Wawakilishi kwa kutoa maelekezo yasiyo ya kweli kuhusiana na ulipwaji wa fidia kwa wananchi walioathirika na Ujenzi wa Uzio, Uwanja wa Ndege.
(iv) Hatua zinazofaa kwa mujibu wa Sheria Namba 4 ya mwaka 2007, zichukuliwe kwa Watendaji wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano pamoja na Mamlaka ya Uwanja wa Ndege waliohusika na upotoshaji wa Kamati kwa kutoa taarifa zisizo za kweli.
Mhe. Spika:
Kipengele chengine kinachohusiana na Hadidu hii rejea ni kuhusiana na Ununzi wa Jenereta liliopo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume, Zanzibar.

Mhe. Spika:
Wakati Kamati inafuatilia suala hili, mambo yafuatayo yameweza kujitokeza:

(i) Uzembe wa makusudi umejitokeza katika ununuzi wa Jenereta hilo:
Mhe. Spika:
Kamati imegundua na kujiridhisha kwamba, kumefanyika uzembe wa makusudi na Wizara zote mbili zimehusika katika uzembe huo, yaani Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, na matokeo yake zaidi ya Tsh. 300,000,000/- zinaelekea kupotea huku jenereta lililonunuliwa na kwa fedha zote hizo, limeshindwa kujaribiwa kwa kipindi chote cha muda wake wa majaribio (warrant period). Aidha, kitendo cha jenereta kukaa bila ya matumizi ya muda mrefu pia ni sehemu ya uharibifu wake. Kwa mantiki hii, Kamati inafahamu kwamba, jenereta hilo limetelekezwa.

Mhe. Spika:
Kama tulivyotumwa kuangalia sababu kuu za matatizo ya ununuzi wa jenereta hilo, Kamati imegundua kuwa:

(ii) Kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu za Sheria ya Manunuzi na Ugavi wa Mali za Serikali.
Mhe. Spika:
Kamati imejiridhisha kwamba, ununuzi wa jenereta hilo haujafuata taratibu za Sheria Namba 9 ya mwaka 2005 inayohusiana na ununuzi wa mali za Serikali. Na kama Sheria hiyo ingelifuatwa kwa ukamilifu wake, uzembe huu wa kununua jenereta ungelifanywa kwa umakini mkubwa na ufasaha.

Mhe. Spika:
Jambo jengine ambalo Kamati imelibaini ni kuwepo kwa :

(iii) Utata wa ununuzi wa vifaa baina ya Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo na Wizara ama Taasisi nyengine za Serikali.

Mhe. Spika:
Kamati imegundua kuwepo kwa utata mkubwa katika ununuzi wa mali za Serikali unaofanywa kwa mashirikiano baina ya Wizara ama Taasisi za Serikali na Mnunuzi Mkuu akawa ni Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo. Hali hii hupelekea kutokuwepo kwa mashirikiano ya karibu na kila taasisi ikikwepa lawama pale ununuzi huo unaposhindwa kufikia lengo.

Mhe. Spika:
Kamati inaamini iwapo suala hili la ununuzi wa jenereta hilo lingelifanywa na Wizara moja tu, basi ufanisi wake ungelikuwa mkubwa, kuliko hali iliyojotokeza ya taratibu za kununua zifaywe na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, wakati Mnunuzi ndio awe Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo.

Mhe. Spika:
Suala jengine ambalo Kamati imelibaini ni :
(iv) Matumizi ya Sheria za nje katika masuala ya Ununuzi wa Mali za Serikali, kufanywa kwa kutumia rejea ya Sheria ya Tanzania Bara, na wala sio Sheria za Zanzibar.

Mhe. Spika:
Kamati imegundua kwamba, Taasisi za Serikali zinafanya manunuzi ya mali za Serikali kwa kutumia sheria zisizo za Zanzibar hali ambayo hupelekea utata wa kisheria. Jambo hili linahitaji uangalizi mkubwa, kwa sababu vyombo hivyo vya maamuzi ya ununuzi wa mali hizo (kwa mfano Bodi ya Zabuni ya Wizara husika ama Kamati ya Tathmini) imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria Namba 9 ya mwaka 2005 ya Sheria za Zanzibar na inatakiwa itejeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria za Zanzibar, lakini katika hali ya kusikitisha, hufanya maamuzi yake kwa sheria zisizo za Zanzibar.

Mhe. Spika:
Kamati pia imegundua kuwa:

(v) Kamati imebaini kwamba, hali inayoendelea sasa ya kutokufanya kazi kwa standby jenereta la uhakika ambalo limenunuliwa kwa kazi hiyo katika Kiwanja chetu cha Ndege ni hatari zaidi kwa usalama wa kiwanja chetu na Mashirika ya Ndege za ndani na za Kimataifa. Hali hii pia haitoi picha nzuri ya haiba ya Uwanja huo.

Mhe. Spika:

(vi) Matumizi mabaya ya fedha za Serikali zinazotokana na Msamaha wa Madeni.

Mhe. Spika:
Kamati imegundua kwamba fedha zinazotoka kupitia msamaha wa madeni huwa zinatumika bila ya uangalifu wowote. Kitu ambacho huleta picha mbaya kwa nchi changa kama hii kupata msahama wa madeni lakini fedha hizo zikatumika bila ya uchungu wowote na kujali.

Mhe. Spika:
Itakumbukwa kwamba, fedha zilizotumika kununulia jenereta hili zinatokana na msamaha wa madeni, lakini fedha hizo zimetumika kununulia jenereta, wakati jenereta hilo limetelekezwa. Haiwezekani kwa Serikali inayojali, kuamua kununua jenereta na jenereta hilo likabaki bila ya, angalau kujaribiwa kufanya kazi ndani ya mwaka, huku ‘warrant period’ yake ikimalizika.

Mhe. Spika: kutokana na hali hii, Kamati imependekeza hatua zifuatazo zichukuliwe:

(i) Hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa watendaji wote waliohusika na uzembe wa ununuzi wa jenereta hilo, huku msisitizo ukiwekwa kwa Makatibu Wakuu wa Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano; Mkurugenzi na Meneja wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege.
(ii) Ili kuondosha matatizo kama haya, Kamati inapendekeza matumizi ya fedha kama hizi yabakie katika Wizara moja tu ambayo ndio yenye mahitaji na inayojua upatikanaji wa mahitaji yake.
(iii) Kamati inapendekeza ndani ya mwezi mmoja kuanzia leo, Jenereta hilo lifanyiwe ‘installation’ ili liweze kujuulikana uzima ama ubovu wake, na kama litakuwa bovu, Kamati inaendelea kusisitiza kwamba hatua za kurejeshwa kwa fedha hizo ziwe dhidi ya Makatibu Wakuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano pamoja na Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo.
Mhe. Spika:
Sehemu ya Tatu ya Hadidu hii rejea, ilihusiana na :
Mikataba ya ukodishwaji wa sehemu za biashara kwenye eneo la Uwanja wa Ndege”
Mhe. Spika:
Ripoti ya suala hili inaanzia katika ukurasa wa 42 hadi 82 na Kamati iliipitia Mikataba ya Wakodishwaji iliyokabidhiwa, huku kukiwa na wimbi la Wafanyabiashara wanaendesha biashara zao katika eneo la Uwanja wa Ndege, bila ya kuwa na Mkataba wowote. Hali hii pia inapelekea kutokuwepo kwa kodi yoyote inayolipwa na wafanya biashara hao.

Mhe. Spika:
Wakati Kamati inaaifanyia kazi sehemu hii, imebaini mambo yafuatayo:

(i) Mikataba takriban yote ya Ukodishwaji wa maeneo ya Uwanja wa Ndege tayari imeshapitwa na wakati na kukosa sifa za msingi kisheria.
Mhe. Spika:
Kamati imegundua kwamba, asilimia kubwa ya Mikataba iliyokabidhiwa kwake tayari ilikuwa imeshapitwa na wakati na ina kasoro nyingi za kisheria. Kasoro hizo ikiwa ni pamoja na kusainiwa na Meneja wa Idara ya Anga, Mhasibu Mkuu wa Idara hiyo, kinyume na kutiwa saini na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi; pia Kamati imepewa Mikataba iliyomalizika muda wa kufanya kazi mwaka 2010, wakati Kamati imefika na kufanya kazi, mwezi wa Septemba 2011.

Mhe. Spika:
Kamati pia imebaini kwamba:
(ii) Uongozi wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege umeshindwa kuisimamia Mikataba kwa maslahi ya nchi.
Mhe. Spika:
Kamati imegundua kwamba, Mikataba hii inavunjwa kiholela bila ya kuwa na usimamizi madhubuti wa Idara ya Anga, ambayo leo inaitwa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege, hali ambayo inapelekea kuikosesha Serikali mapato huku kutosimamiwa kwa mikataba hii kunatokana na uzembe na kutowajibika kwa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege katika majukumu yao ya kazi.

Mhe. Spika:
Kamati pia imepata tatizo la
(iii) Kudanganywa sana na kutaka kupotoshwa juu ya ukweli halisi wa Ukodishaji wa maeneo ya Uwanja wa Ndege.
Mhe. Spika :
Katika wakati wote Kamati ilipokuwa inafanya kazi, Kamati haikupatiwa taarifa za kweli wakati inafuatilia orodha kamili ya wakodishwaji na wafanya biashara wote wa eneo husika la Uwanja wa Ndege na wakati huo huo kutopewa taarifa za kweli kuhusiana na masharti ya Mikataba husika.

Mhe. Spika :
Kamati imeambiwa kwamba, mikataba mingi imeanza tarere 1/1/2011 na kumalizika tarehe 31/12/2011, wakati sio kweli. Kamati ilipopatiwa Mikataba husika, imebaini kwamba, Mikataba hiyo imeanza kazi tarehe 1/1/2010 na kumalizika tarehe 31/12/2010. Aidha, Kamati imeambiwa, ni jumla ya maeneo 40 tu ya biashara ndio yaliyokodishwa, wakati ukweli ni zaidi ya hayo. Aidha, Kamati imeambiwa kwamba, Wakodishwaji wote wanalipa kodi, wakati sio kweli na mambo mengine ambayo yanaonekana katika ripoti yetu.

Mhe. Spika :
Kasoro nyengine iliyojitokeza ni kuhusu :
(iv) Kuna uvujaji Mkubwa wa Mapato ya Serikali yanayotokana na Ukodishwaji wa maeneo hayo ya Uwanja wa Ndege.
Mhe. Spika :
Kamati imegundua kwamba, kodi za maeneo yaliyokodishwa hazilipwi kwa wakati na pia hazilipwi kabisa na baadhi ya Taasisi zilizokodi na kufanya biashara khususan zile ambazo Kamati haikupatiwa Mikataba yake, kwamba Mapato yanayolipwa hayakuweza kuthibitishwa, hali inayoifanya Kamati kuamini kwamba mapato hayo yanavuja. Aidha, uvujaji huu pia unahusiana na Matangazo ya Biashara yaliyopo katika Uwanja huo wa Ndege, Zanzibar, na kwamba Kamati haikupatiwa taarifa za za Mabango ya Global Media Outdoor systems na mabango mengine kama tulivyoeleza katika ukurasa wa 74 wa ripoti na Kielelezo Namba 74 cha Ripoti yetu

Mhe. Spika :
Suala jengine ambalo Kamati imelibaini ni
(v) Kuwepo kwa Taasisi nyingi zinazoendesha biashara bila ya kuwa na Mikataba.
Mhe. Spika :
Taasisi hizi kama tulivyozieleza katika ukurasa wa 77 hadi 80, zinafanyabiashara bila ya kuingia Mkataba na Mamlaka ya Uwanja wa Ndege. Hali hii ama inatokana na Taasisi hizo kukodishwa na Wakodishwaji walioingia Mkataba na Mamlaka, bila idhini ya Mamlaka ama kwa njia nyengine.

Mhe. Spika :
Kwa ujumla, Kamati imegundua kwamba, Taasisi nyingi zinafanya biashara bila ya kuwa na Mikataba, huku kukiwa na mtindo unaonekana wa kawaida kwa wanaokodishwa nao kukodisha maeneo hayo kwa wafanya biashara wengine bila ya idhini ya Uongozi wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege, na ni sawa na kusema kwamba, Taasisi hizi zinafanya biashara ya kukodisha maeneo ya biashara ambayo wao wenyewe wamekodishwa na Mamlaka ya Uwanja wa Ndege kinyume na Matakwa ya sheria za Mikataba na masharti ya Mikataba husika.

Mhe. Spika :
Miongoni mwa matatizo makubwa ya Mamlaka ya Uwanja wa Ndege kuhusiana na hoja hii ni kwamba :
(vi) Viongozi Wakuu wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege, wakati huo Idara ya Anga wamehusika sana katika udhaifu Mkubwa wa Mikataba hii.
Mhe. Spika:
Kamati imegundua kwamba, Mikataba mingi ipo kirafiki zaidi kuliko kisheria kwa maana, miongoni mwa kasoro hizo ni kwamba, muda mwingi Mikataba hii imo mikononi mwa wakodishwaji kwa lengo la kutafutwa saini zao, jambo ambalo liko kinyume na masharti ya Mikataba husika. Aidha udhaifu huu unatokana na Viongozi Wakuu wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege, wakiweka mbele maslahi yao binafsi zaidi kuliko maslahi ya Taifa.

Mhe. Spika:
Kama tulivyoripoti katika ripoti yetu, kwamba Mikataba hii mingi inafungwa mwaka hadi mwaka, lakini ndani ya miezi sita ama zaidi, mikataba mingi bado imo mikononi mwa Wakodishwaji wakisubiriwa watie saini zao. Jambo la kushangaza zaidi ni kwamba, Taasisi hizo nyingi zina ofisi zao hapo uwanja wa Ndege.

Mhe. Spika:
Jambo jengine ambalo Kamati imelibaini ni kuhusu Uongozi wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege kujihusisha na biashara wakati huo huo wao ndio wasimamizi wa Kodi na maslahi ya Serikali juu ya Wafanyabiashara husika:

Mhe Spika, kamati imebaini kwamba:
(vii) Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege anahusika na biashara wakati huo huo yeye anawajibika kuwasimamia Wafanyabiashara wenzake watekeleze masharti ya Mikataba, kitu ambacho hakiwezekani.
Mhe. Spika:
Kamati imegundua kwamba, Capt. Said Ndombugani ambae ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege amekodi eneo la Biashara na amekiuka masharti ya Mkataba kwa maslahi binafsi huku akiamini hakuna mtu wa kumchukulia hatua. Mhe. Spika, Mkurugenzi huyu amekodishwa Hanger kwa USD 200 tu kwa mwezi wakati yeye ameamua kuwakodisha ZAN AIR kwa USD 1000 kwa mwezi, ni wazi kwamba anafaidika kwa USD 800 ambazo ni kipato kizuri kwa Kampuni yake mbali ya kasoro hiyo kwa kipindi kirefu hakuweza kulipa deni lake la USD 200.

Mhe. Spika:
Kutokana na hali hiyo, Kamati imependekeza hatua zifuatazo zichukuliweo.
(i) Kwa kuwa sasa Idara ya Anga ni Mamlaka Kamili ya Uwanja wa Ndege, Kamati inapendekeza Mikataba yote inayohusiana na Ukodishwaji wa biashara mbali mbali katika eneo la Uwanja wa Ndege ipitiwe upya ili iendane na mabadiliko ya biashara na msisitizo ukiwekwa katika gharama za kodi husika
(ii) Kamati inapendekeza hatua za kisheria na kinidhamu zichukuliwe kwa Watendaji Wakuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano pamoja na Mamlaka ya Uwanja wa Ndege waliohusika na upotoshaji wa Kamati kwa kutoa taarifa zisizo za kweli.
(iv) Fedha na malipo yote ambayo hayajalipwa na Taasisi/Makampuni zilizokodishwa, ni Lazima zilipwe kabla Mamlaka ya Uwanja wa Ndege haijaingia tena Mkataba na Taasisi ama Kampuni hizo za biashara katika Uwanja wa Ndege wa Zanzibar.

(v) Watendaji wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege, wanaohusika na usimamizi wa ukodishwaji wa maeneo ya uwanja wa Ndege (msisitizo ukiwekwa kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uwanja wa Capt. Said Ndombugani) wachukuliwe hatua za kinidhamu kwa kushindwa kuwajibika kuisimamia Mikataba hiyo huku baadhi yao wakigeuka ni wafanya biashara katika eneo la kazi na matokeo yake kupoteza mapato ya Serikali.

Mhe. Spika:
Suala jengine ambalo Kamati imekabidhiwa kulifanyia kazi, linahusiana na

“Kuhusu utaratibu wa ajira Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kwa ujumla”

Mhe. Spika:
Katika kufuatilia suala zima la ajira za wafanyakazi wapya wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, Kamati imeangalia kuanzia mwezi wa Octoba 2010 hadi Septemba 2011. Lakini kwa bahati njema, ilipewa orodha ya wafanyakazi walioajiriwa tarehe 1/6/2011 na hivyo imewachunguza kama tulivyoeleza katika ripoti yetu kuanzia ukurasa wa 83 hadi 116 kwa Unguja na Pemba. Aidha, kwa upande wa Unguja, Kamati imebaini mambo yafuatayo:
(i) Kiuhalisia Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano ndio iliyohusika na uajiri wa wafanyakazi wake kuliko Mamlaka husika, (Idara ya Utumishi Serikalini, yaani kuliko Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora,) kutokana na wafanyakazi hao kuajiriwa katika nafasi zilizokuwa hazijaelekezwa na Mamlaka husika na hivyo, Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano bila ya utaratibu wowote kwa kuona wao tu inafaa, wameamua kuondosha (kutomuajiri mfanyakazi) katika nafasi zilizoelekezwa na kujaza nafasi walizotaka wao, bila hata ya kuangalia sifa na uwezo wa wafanyakazi hawa.

Mhe. Spika:
Hali hii imejitokeza kwa kuzingatia uhusiano uliopo baina ya Mfanyakazi na Mdhamini wake, ambae ama ni Kiongozi wa Wizara hii ama kwa uhusiano uliopo baina ya mfanyakazi huyo na watendaji wakuu wa Wizara hii. Lakini baya zaidi, wamefanya hivi bila ya kuwajuulisha ama kupata idhini ya Wizara inayohusika na Utumishi.

Mhe. Spika:
Jambo jengine tuliloligundua ni:

(ii) Idara ya Utumishi Serikalini kwa kushirikiana na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano imewaajiri wafanyakazi wengi wasio kuwa na sifa na wengi wao wameambatanisha katika maombi yao taarifa zisizo za kweli na za udanganyifu.
Mhe. Spika:
Kama utafanya rejea ya ripoti yetu kuanzia ukurasa wa 83 hadi wa 104, suala hili liko wazi. Kwa ufupi, wafanyakazi karibu ya wote, wameajiriwa bila ya kuzingatia sifa zilizopendekezwa na Wizara iliyoomba kibali cha wafanyakazi hao. Hali hii pia inaenda sambamba na udanganyifu mkubwa wa taarifa za wafanyakazi hao ambapo Kamati, bila ya kumuonea mtu haya, imebainisha kwa uwazi.

Mhe. Spika:
Tatizo jengine linalohusiana na suala hili ni:
(iii) Kuwepo kwa wafanyakazi wameajiriwa mara mbili katika Taasisi moja, yaani Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano huku Wizara zinazohusika zimekaa kimya bila ya kutoa taarifa husika Serikalini.
Mhe. Spika:
Kama utasoma maelezo ya Ndg. Hanifa Saleh Moh’d, katika ukurasa wa 88 hadi 89 na Ukurasa wa 97 wa ripoti hii, utafahamu kwa uwazi tatizo hili.

Mhe. Spika:
Tatizo jengine ni :
(iv) Kitengo cha G.S.O hakikushirikishwa katika kutoa taarifa za wafanyakazi hawa, kitendo ambacho kimezidi kupelekea udanganyifu mkubwa wa taarfa sahihi za wafanyakazi hawa.
Mhe. Spika:
Katika kuajiriwa kwa wafanyakazi wote hao tuliowaripoti kwa Upande wa Unguja, hakuna hata Mfanyakazi mmoja aliefanyiwa veting na Kitengo cha G.S.O, suala ambalo limezidisha kuwepo kwa udanganyifu.

Mhe. Spika:
Tatizo jengine tulilolieleza kuhusiana na hoja hii ni kwamba:
(v) Hakukuwa na ushahidi wowote wa kufanyiwa usaili wafanyakazi hawa kabla hawajaajiriwa ili kuthibitisha uwezo wao, Kamati imegundua kwamba wengi wao wameajiriwa kwa kuzingatia uenyeji.
Mhe. Spika:
Mbali na wafanyakazi hawa kuajiriwa katika kada mbali mbali, na nyingi zikihitaji kupata wafanyakazi madhubuti, hakuna usaili wowote uliofanywa kwa wafanyakazi hawa, hali iliyoepelekea kushindwa kujua usahihi wa taarifa zao na uwezo wa Mfanyakazi husika.

Mhe. Spika:
Kasoro nyengine ni pamoja na:
(vi) Viongozi na Watendaji Wakuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano pamoja na Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora wamehusika na Upendeleo wa wazi wa watoto na jamaa zao katika utaratibu wa ajira na zaidi katika utekelezaji wa majukumu ya wafanyakazi hao.
Mhe. Spika:
Kama utafanya rejea ya ripoti yetu, unakuta wazi kwamba Waziri wa Wizara Miundombinu na Mawasiliano, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, wakiwaajiri watoto, ndugu ama jamaa zao, huku wakiwapa fursa nyingi za upendeleo kinyume na utaratibu.

Mhe. Spika, naomba kwa makusudi Wajumbe wako wapate taarifa hizi katika Mfanyakazi, Ndg. Aisha Msanif Haji, Mtoto wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, ambae ameajiriwa na vado akiwa katika kipindi cha majaribio, tayari amepewa ruhusa ya kusoma, huku akiwa anaendelea kupokea mshahara kama kawaida.

Mhe. Spika:
Tatizo jengine ni:
(vii) Kwa kupitia mfano huu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, Kamati imegundua kuwepo kwa matatizo makubwa ya ajira katika Utumishi wa Serikali yaliyochangiwa sana na Idara ya Utumishi Serikalini.

Mhe. Spika:
Iwapo ufatanya rejea ya ripoti yetu, unakuta wazi kwamba, matatizo kama haya, yanazikabili taasisi nyingi za Serikali na hivyo, ipo haja ya kuzidi kufanyiwa kazi kwa suala hili.

Mhe. Spika:
Pia Kamati imegundua kuwa:
(viii) Tatizo la Wafanyakazi hewa litaendelea kuisakama Serikali na ni wazi kwamba limeshindwa kudhibitiwa.
Mhe. Spika:
Katika ripoti yetu tumezungumzia Mfanyakazi mmoja kuajiriwa mara mbili na Wizara ya Utumishi, huku ikishindwa kuwa na takwimu sahihi ya taarifa za wafanyakazi wake.

Mhe. Spika:
Pia Kamati imebaini kwamba:
(ix) Uajiri huu wa wafanyakazi hawa umefanywa kinyume na utaratibu kwa mujibu wa sheria za Utumishi.
Mhe. Spika:
Kama tulivyosema katika taarifa yetu. Kwamba wafanyakazi wengi wameajiriwa kinyume na kibali cha Utumishi na bila ya kuangalia usahihi wa taarifa zao.

Mhe. Spika:
Pia Kamati imegundua kuwa:
(x) imepata taarifa kwamba Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano baada ya kazi za Kamati, imewasumbua watendaji wake, ambao ama walitoa mashirikiano mema kwa Kamati au wamegundulika na kasoro mbali mbali za uajiri wao, vitendo vyote vikifanywa kabla hata ya ripoti hii kuwasilishwa Barazani.
Mhe. Spika:
Baada tu ya zoezi la uchunguzi kukamilika, na kabla ya Kamati yetu kutoa ripoti yake hapa Barazani, imegundulika kwamba, baadhi ya wafanyakazi wameanza kusimamishwa kazi, huku wengine wakipata usumbufu kadhaa, ama kwa sababu walitoa mashirikiano na Kamati, ama kwa kugundulika kasoro zao baada ya kupita Kamati, lakini sisi kama Kamati, vado hatujatoa maelezo yaetu hapa Barazani.

Mhe. Spika:
Tukiendelea na mambo tuliyoyabaini kuhusiana na hoja hii ni kwamba:
(xi) Imethibitika kwamba, kuna mfanyakazi analipwa mshahara wa ngazi ya Mtaalamu (msomi wa Degree) wakati bado hajafikia elimu hiyo.
Mhe. Spika:
Huyu si mwengine ispokuwa Mtoto wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, ambae taarifa zake zipo katika ukurasa wa 102 hadi 103.

Mhe. Spika:
Mbali na kukiukwa kwa taratibu za kupewa ruhusa ya kusoma wakati akiwa masomoni, lakini pia ameajiriwa akiwa na Diploma, lakini alilipwa mshahara wa Degree huku vado hajasomea ngazi hiyo ya Degree. Lakini yote haya yamewezekana kwa sababu, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ni baba yake Mzazi.

Mhe. Spika:
Kutokana na hali hiyo, tumependekeza hatua zifuatazo zichukuliwe:

(i) Viongozi na Watendaji Wakuu wa Wizara zote mbili (Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano na Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora) waliohusika na kadhia hii wawajibishwe kwa mujibu wa sheria.
(ii) Fedha zote alizolipwa Ndg. Mwanakombo Vuai Iddi katika ngazi ya Utaalamu ambao hakuufikia, zirejeshwe Serikalini kwa utaratibu wa kukatwa mshahara wake. Na hatua hizi zitumike kwa wafanyakazi wote walioajiriwa mara mbili, ingawaje kwa wafanyakazi hawa, fedha hizo zirudishwe kupitia mishahara ya Watendaji Wakuu wa Wizara hizi mbili zilizohusika (Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano na Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora).
(iii) Uajiri wa wafanyakazi wote ambao Kamati imegundua kwamba hawana sifa za kuajiriwa, ufanyike upya kwa kufuata muongozo wa Sheria zilizopo sasa.
Mhe. Spika:
Kwa upande wa Ajira, kisiwani Pemba, Kamati imegundua matatizo yafuatayo:
(i) Kama ilivyofanyika Unguja, ni wazi pia kwa upande wa Pemba, Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano imehusika zaidi na uajiri wa wafanyakazi wake kuliko Mamlaka husika, yaani Idara ya Utumishi Serikalini.
Hii inatokana na ruhusa za awali za wafanyakazi hao kutoka Idara ya Utumishi zimebadilishwa na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano bila ya taratibu za Uhamisho wala taratibu nyengine za ajira zinazohusika. Hili limefanywa bila ya ruhusa wala taarifa kwa Mamlaka husika.

Mhe. Spika:

(ii) Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano imewaajiri wafanyakazi wengi wasio kuwa na sifa na wengi wao wameambatanisha katika maombi yao taarifa zisizo za kweli na za udanganyifu.
Kama maelezo haya tulivyoyatoa kuanzia ukurasa wa 105 hadi 116 wa ripoti yetu.

Mhe. Spika:
Tatizo jengine ni kuhusu:
(iii) Wafanyakazi wote 37 walioajiriwa, wamepeleka maombi yao ya kazi, baina ya mwezi wa March, April na May 2011 na kuajiriwa mwezi wa June, kuna maombi mengi ambayo yalishaombwa na wananchi wengi wenye sifa zaidi ama sawa na hawa walioajiriwa ambao walioomba zaidi ya miaka miwili nyuma, bila ya kuzingaitiwa maombi yao.
Mhe. Spika :
Kuna wananchi wengi wenye elimu ya Degree, Diploma na Kidato cha Sita wamepeleka maombi yao zaidi ya miaka miwili nyuma, lakini hawakuajiriwa na badala yake wameajiriwa wafanyakazi wengi, takriban wote, waliomaliza Kidato cha Nne na maombi yao ni kuanzia mwezi wa March hadi May 2011, wakati ajira zenyewe zimeanza kuanzia June 2011.

Mhe. Spika:
Tatizo jengine ni kwamba:
(iv) Wafanyakazi wengi walioajiriwa ni watoto wa wakubwa ama jamaa zao wa karibu. Hata Afisa Mdhamini aliieleza Kamati kwamba, aliombwa na aliekuwa Mhe. Ashura Abeid Faraji na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, kuwasaidia watoto ama jamaa zao. Aidha, wafanyakazi wengi waliobakia ni watoto na jamaa wa wafanyakazi wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, hali ambayo imepelekea wepesi wa kuajiriwa kwao huku wananchi wengi wasio na wakubwa wala wazee wenye kazi Wizarani hapo wakiendelea kusota bila ya kuajiriwa kwa muda mrefu sasa.

Mhe. Spika:

(v) Kamati inapongeza hatua za Wizara kuwapeleka waajiriwa hao Kitengo cha G.S.O ili kufanyiwa uchunguzi, kitu ambacho hata Makao Makuu wameshindwa kukitekeleza. Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa walizozitoa kwa wafanyakazi hao, Kamati imegundua vigezo vya kisiasa vimetumika kushawishi ajira za wafanyakazi hao.

Mhe. Spika:
(vi) Viongozi na Watendaji Wakuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano wamehusika na Upendeleo wa wazi wa watoto na jamaa zao katika utaratibu wa ajira na zaidi katika utekelezaji wa majukumu ya wafanyakazi hao.
Mhe. Spika:
Kutokana na hali hiyo, Kamati imependekeza hatua zifuatazo zichukuliwe:
(i) Viongozi na Watendaji Wakuu wa Wizara zote mbili (Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano na Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora) waliohusika na kadhia hii wawajibishwe kisheria.
(ii) Uajiri wa wafanyakazi wote ambao Kamati imeona hawana sifa za kuajiriwa, ufanyike upya kwa kufuata muongozo wa Sheria zilizopo sasa.
Mhe. Spika:
Naomba sasa tuendelee na sehemu ya mwisho ya Hadidu hii rejea inayohusiana na”

“Suala la utoaji wa huduma mbali mbali kwenye maeneo ya Uwanja wa Ndege”.
Mhe. Spika:
Katika kufuatilia suala hili, Kamati imejiridhisha kwamba, suala la utoaji huduma kwenye eneo la Uwanja wa Ndege linakabiliwa na Changoto nyingi, lakini tatizo kubwa zaidi lipo katika migogoro baina ya Kampuni inayosimamia kazi hiyo, ya ZAPS na wanaushirika, ambao kabla ya kuanzishwa kwa Kampuni hiyo, walikuwa ndio wenye kuendesha huduma hiyo. Pia kuna Mwananchi, Ndg. Khamis Mussa Juma ambae nae alifanya maombi ya muda mrefu ya kuanzisha kazi hizo, lakini hakupewa na matokeo yake, migogoro hii haishi.

Mhe. Spika:
Kwa ujumla, wakati Kamati inalipitia suala hili, mambo yafuatayo yamebainika:

(i) Mamlaka ya Uwanja wa Ndege (Wakati huo Idara ya Anga) kwa kiasi kikubwa imehusika katika mgogoro ambao wao wenyewe wameshindwa kuutatua.
Mhe. Spika:
Kama utafanya rejea ya ufafanuzi wetu kuanzia ukurasa wa 117 hadi 123, ni wazi kwamba chanzo cha mgogoro huu kimechangiwa sana na iliyokuwa Idara ya Anga.

Mhe. Spika:
Ni wazi kwamba;
(ii) Chanzo cha mgogoro huo kinahusiana zaidi kimaslahi kwamba kila kikundi pamoja na Ndg Khamis Mussa Juma kinataka kufanya kazi hizo za ubebaji wa mizigo peke yao bila ya kuwashirikisha wengine.

Mhe. Spika:
Vijana hawa hawana wanachogombania zaidi ya kila mtu kutaka kufanya yeyé kazi hiyo ya utoaji wa huduma za mizigo, jambo ambalo linapelekea chuki na kila mtu anatafuta kumfitinisha mwenzake, ili Kampuni, yeyé binafsi ama Kikundi chake kipewe kazi hiyo bila ya kuwashirikisha wengine.

Mhe. Spika:
Pia, Kamati imegundua kuwa:
(iii) Uanzishaji wa Kampuni ya ZAPS bila ya kuwashirikisha viongozi waandamizi Kikundi cha Ushirika wa ZAP wala kumshirikisha Ndg. Khamis Mussa Juma, kumechangia zaidi katika migogoro isiyokwisha.

Aidha, baada ya kufahamu hali hiyo, Kamati imependekeza hatua hizi hapa zifuatwe:
(i) Pamoja na Viongozi waandamizi wa Ushirika wa ZAP na Ndg. Khamis Mussa Juma kushindwa kununua hisa katika Kampuni hiyo kutokana na Umaskini wao (Ingawaje Ndg. Khamis amenunua kwa 5%), Serikali kupitia Mamlaka zinazohusika ziwasaidie kununua share hizo kwa asilimia 50 (50%).

Mhe. Spika:
Baada ya Kamati kupendekeza vikundi hivi vikae kwa pamoja na kukubaliana namna ya uendeshaji bora wa taasisi zao, kwa lengo la kutoa huduma bora, walifanya vikao na Kamati imejuilishwa, lakini maamuzi ya mwisho ni kwamba, wanakikundi cha ZAPS hawakuweza kununua hisa na Ndg. Khamis Mussa Juma kuweza kupata hisa ya 5%. Kwa hivyo, ili kuondosha kasoro hiyo, Kamati imependekeza Serikali kuwasaidia wanakikundi hiki na Mzee Khamis Mussa Juma, ili kuwepo na muwiyano wa umiliki na uendeshaji wa Kampuni hiyo.
Mhe. Spika:
Pia Kamati imependekeza kwamba:
(ii) Mamlaka ya Uwanja wa Ndege isijiingize katika Mgogoro huu na badala yake iwe muangalizi (observer) au msimamizi wa majukumu ya Kampuni hii.

Mhe. Spika:
Hadidu ya Tatu iliyokabidhiwa kwa Kamati inahusiana na:
“Matatizo ya uvamizi wa fukwe na uharibifu wa mazingira kwenye hoteli inayopakana na Chuo cha Maendeleo ya Utalii Zanzibar, Maruhubi, kwenye Hoteli ya Zanzibar Ocean View, Kilimani-Zanzibar, na Hoteli ya Misali iliyopo Wesha, Chake Chake-Pemba.

Mhe. Spika:
Kamati imeifanyia kazi hadidu hii rejea na kutoa maoni yake kwa pamoja kama inavyoonekana kuanzia ukurasa wa 125 hadi wa 164 ya ripoti yetu. Na hivyo, mambo hayo tuliyoyagundua ni kama haya yafuatayo:

(i) Kuna Uvamizi Mkubwa wa Maeneo ya Fukwe na Uharibifu wa Mazingira na Kamati imejiridhisha kwamba, Ujenzi wa Miradi ya Mahoteli Zanzibar hauzingatii matakwa ya Sheria zinazoelekeza juu ya masuala ya ardhi na mazingira.
Mhe. Spika:
Kama tafanya rejea ya ripoti yetu, tumeeleza kwa uwazi kwamba yale tuliyotumwa na Baraza lako tumeweza kuyathibitisha na tumejiridhisha kwa Hoteli zote 3 zilizohusika na Hadidu hii rejea, zimefanya makosa hayo. Kwa hali hii, tumefanya mfano halisi (sampling) kwamba, tatizo hili sio tu kwamba lipo kwa Hoteli zilizohusika, lakini ni kwa Mirado yote ya Mahoteli Zanzibar.

Mhe. Spika:
Pia tumegundua kuwa:

(ii) Idara ya Mazingira imeshindwa kuisimamia ipasavyo Sheria zinazohusiana na Mazingira kwa kutowachukulia hatua za kisheria Wawekezaji hawa na matokeo yake wanaendelea kufanya uharibifu bila ya kujali mamlaka yoyote ama athari kubwa ya kimazingira na kiustawi wa wananchi, inayoweza kutokezea.

Mhe. Spika:
Katika taasisi zote zinazohusika na miradi hii, Idara ya Mazingira wamefanya kazi kubwa sana ya kufuatilia, kutoa maagizo mbali mbali ya kusitisha ujenzi, lakini kosa lao moja tu, kwamba, hawakuitumia sheria Namba 2 ya mwaka 1996 inayowapa Mamlaka ya kuchukua hatua. Kwa hali tumeridhika kwamba, pamoja na juhudi zao kubwa, lakini wanastahiki kubebeshwa lawama hii ya kushindwa kuwa mfano wa kuigwa katika utekelezaji wa majukumu yake.

Mhe. Spika:
Vile vile tumegundua kuwa:

(iii) Kamisheni ya Utalii pamoja na Taasisi nyengine za Serikali zinazohusika na Uwekezaji wa Miradi ya Utalii zimehusika kwa kiasi kikubwa katika uharibifu wa mazingira na uvamizi wa fukwe uliofanywa na Wawekezaji hawa.

Mhe. Spika,
Kwa miradi yote Mitatu ya Hoteli hizi, Taasisi hizi zenye dhima ya kufuatilia suala hili, zimekiuka majukumu yao ya kazi, hali iliyopelekea kuzidi kuvunjwa kwa sheria na wawekezaji hawa.

Mhe. Spika:
Kamati pia imegundua kuwa:

(iv) Aliekuwa Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, Zanzibar, Mhe. Machano Othman Said, kwa kumuliki kwake 10% katika Kampuni iliyomiliki Hoteli ya Misali Sun set Beach ya Wesha, ametumika kusababisha kasoro tulizozizungumzia katika Mradi wa Hoteli ya Misali Sun set Beach, iliyopo Wesha.
Mhe. Spika:
Mhe. Machano Othman Said, anamiliki 10% ya hisa katika Kampuni ya inayomiliki Mradi wa Hoteli ya Misali Sunset Beach, iliyopo Wesha. Na kwa afasi yake wakati huo kama Mhe. Waziri, ametumika kuisaidia kuendeshwa bila ya kibali cha Mazingira wala Leseni ya Utalii kutoka Pemba, ambako ndiko kwenye Mradi huo

Mhe. Spika:
Kamati pia imegundua kuwa:
(v) Watendaji Wakuu wa Serikali (ikiwa ni pamoja na Watendaji Wakuu wa Idara ya Utunzaji na Uhifadhi wa Barabara (UUB)) wameshiriki katika uharibifu wa mazingira kwa kushirikiana na Muwekezaji kwa kufanya ufukiaji wa Bahari katika Hoteli ya Maruhubi Beach Villa, kinyume na utaratibu.
Mhe. Spika:
Wakati Kamati inafuatilia kuhusu Ujenzi wa Hoteli ya Maruhubi Beach Villa, imegundua kuwa, Idara ya UUB imeshiriki katika kupeleka dongo, ama vyovyote tutakavyoliita, lililotoa mchango wa ufukiaji wa Bahari kinyume na utaratibu.

Mhe. Spika:
Pia Kamati imefahamu kwamba:
(vi) Wawekezaji wa Miradi ya Utalii kwa makusudi na kwa jeuri kabisa hawaheshimu sheria zinazohusiana na uwekezaji wa Miradi ya Kitalii huku Serikali inakaa kimya na kuwatizama na bado wanapewa leseni za biashara hali ya kwamba Serikali inafahamu uharibifu unaofanywa na Miradi yao. Hii inaonesha kuwa kuna harufu ya rushwa katika maeneo hayo.

Mhe. Spika: ili kukemea vitendo kama hivyo, Kamati inapendekeza hatua zifuatazo zichukuliwe:
(i) Serikali ndani ya miezi 3 (kuanzia tarehe ya kuwasilishwa ripoti hii) iunde Kamati itakayofuatilia suala la uvamizi na uharibifu wa mazingira katika miradi yote ya hoteli Zanzibar na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kukiukwa na kadhia hiyo, huku pia ikizichukulia hatua za kisheria hoteli zote zitakazobainika kikiuka taratibu za Uwekezaji. Iwapo baada ya kumaliza muda huo wa miezi 3, Serikali imeshindwa kufanya hivyo (kuunda Kamati hiyo), Baraza la Wawakilishi litekeleze jukumu hilo la kuunda Kamati Maalum ya Muda, ya kufuatilia suala hili na ripoti yake iwasilishwe Barazani.
(ii) Aliekuwa Waziri w anchi (AR), Mawasiliano na Uchukuzi, Mhe. Machano Othman Said awajibishwe kutokana na kushiriki kwake kwa kiasi kikubwa katika uharibifu uliofanywa na ujenzi wa Mradi wa Pemba Misali Sunset Beach Hotel, wakati yeye ni kiongozi wa Serikali.
(iii) Kwa kuwa Sheria Namba 2 ya mwaka 1996 imewapa mamlaka yanayofaa Idara ya Mazingira ya kumchukulia mtu anaekengeuka sheria hiyo, hatua za kisheria, jambo ambalo halikufanyika, Kamati inapendekeza Watendaji wakuu wa Idara ya Mazingira wanaohusika na kusimamia mazingira, wachukuliwe hatua za kinidhamu kwa kushindwa kwao kuisimamia sheria.
(iv) Watendaji Wakuu wa Idara ya Ujenzi na Utunzaji wa Barabara (UUB) walioshiriki katika ufukiaji wa ardhi (reclamation) katika hoteli ya Maruhubi Beach Villa wachukuliwe hatua za kinidhamu ili iwe ni funzo kwa watendaji wengine.
(v) Maagizo ya Idara ya Mazingira iliyoyatoa kwa wawekezaji hao kuhusiana na uvamizi wa fukwe na uharibifu wa mazingira walioufanya kufuatia ujenzi wa miradi yao (ikiwa ni pamoja na kuvunja majengo ya Mikahawa iliyojengwa ndani ya fukwe, katika Hoteli ya Zanzibar Ocean View pamoja), yasimamiwe na Serikali Kuu huku ikihakikisha yanatekelezwa ndani ya miezi 2 (tokea tarehe ya kuwasilishwa kwa ripoti hii) na taarifa za utekelezaji wake ziwasilishwe katika Baraza la Wawakilishi.
(vi) Serikali isimamie ndani ya mwezi mmoja (baada ya kuwasilishwa kwa ripoti hii) ikihakikisha kwamba, malipo yote ya leseni za biashara ya Utalii ambazo hazikukatwa na Wawekezaji hao tokea kuanza kwa miradi yao, yalipwe mara moja kama sheria zinavyoelekeza huku ikihakikisha kwamba, Wawekezaji hawa wanafuata ipasavyo matakwa ya sheria zinazohusika na uwekezaji kabla ya kupewa leseni na vibali vyengine vyovyote vinavyohusika na miradi yao.
(vii) Hatua za kisheria zinahohusiana na Mazingira na Uwekezaji wa Miradi ya Utalii kwa ujumla zichukuliwe mara moja dhidi ya Wawekezaji hawa na taarifa ya hatua hizo ziwasilishwe katika Baraza la Wawakilishi katika Mkutano wa Nane wa Baraza, unaotarajiwa kuanza mwezi wa September/Octoba 2012.
Mhe. Spika:
Hadidu nyengine ya Nne iliyokabidhiwa kwa Kamati, ilihusika na:
“Kuchunguza zoezi la uhaulishwaji wa Kiwanja kinachopakana na jengo la ‘Livingstone House’ Mbuyu Taifa, Mjini, Zanzibar.

Mhe. Spika:
Kamati imelichunguza suala hili la uhaulishwaji wa Kiwanja cha Serikali, kinachopakana na jengo la ‘Living Stone’ House katika Mtaa wa Mbuyu Taifa na kugundua kasoro zifuatazo:

(i) Uhaulishwaji wa kiwanja hicho umezingatiwa kibiashara zaidi na sio kwa haja halisi ya matumizi ya ardhi husika.

Mhe. Spika:
Kwa kawaida Serikali inapofanya uhaulishaji wa ardhi kwa wananchi wake hufanya kwa kuzingatia hali halisi ya maisha na haja ya matumizi ya mwananchi huyo, kwa maana, huwasaidia wananchi wake wanyonge. Lakini ardhi hii haikuhaulishwa kwa msingi huo. Misingi ya uhaulishwaji wa ardí hii kwa mujibu wa utafiti wa Kamati, umezingatia zaidi maslahi ya biashara ya Kampuni ama Mtu binafsi na sio malengo yaliyokusudiwa na Sheria.

Mhe. Spika:
Pia Kamati inafahamu kwamba:
(ii) Pamoja na Sheria ya Ardhi kutoa mamlaka makubwa kwa Mhe. Waziri anaehusika na msuala ya ardhi kuweza kuihaulisha ardhi ya Serikali kwa mwananchi, ni wazi kwamba mamlaka hayo yalitumika vibaya kwa kuzingatia zaidi maslahi ya biashara na maslahi binafsi na sio maslahi ya umma.
Mhe. Spika:
Vile vile Kamati imegundua kuwa:
(iii) Uhaulishaji wa ardhi hii umezingatia zaidi maslahi binafsi na wala sio maslahi ya umma.
Mhe. Spika:
Maelezo haya yote ya ufafanuzi wa hoja ama hadidu hii rejea, yanapatikana katika ukurasa wa 164 hadi 175 ya Ripoti yetu ya Kamati.

Mhe. Spika, mbali na hoja hizi, Kamati inapendekeza hatua zifuatazo zichukuliwe:

(i) Kwa kuwa Uhaulishwaji wa kiwanja hicho haukuzingatia masharti ya utolewaji wake kama yalivyokusudiwa na Sheria, hivyo, Kamati inapendekeza kiwanja hicho kirudi Serikalini mara moja.

(ii) Kuna haja ya kuifanyia marekebisho Sheria ya Umiliki wa Ardhi, Namba 12 ya mwaka 1992, ili isitoe mamlaka yasiyo na mipaka ya Mhe. Waziri kuhaulisha Ardhi ya Serikali.

(iii) Kuna haja ya kufanya marekebisho ya Kanuni zinazohusiana na masuala ya ardhi ili zitoe utaratibu wa Maombi ya matumizi ya ardhi kwa mtu yoyote anaehitaji na yawe kwa kupitia Katibu Mkuu wa Wizara inayohusina na masuala ya ardhi.

Mhe. Spika:
Hadidu ya Tano inahusiana na:
“Uhalali wa Mikataba ya Nyumba ya Serikali iliyopo Kiponda inayodaiwa kwamba alipewa mwananchi na baadae kuiuza kwa mtu mwegine.

Mhe. Spika:
Kamati imelifanyia kazi suala hili na kutoa taarifa yake kuanzia ukurasa wa 175 hadi 184 ya ripoti hii.

Mhe. Spika:
Katika kuchunguza suala hili, Kamati imegundua mambo yafuatayo:

(i) Mikataba yote ya Umiliki wa Nyumba hiyo ni batili na haina nguvu za Kisheria.

Mhe. Spika:
Kamati imebaini kwamba, Mikataba yote ya mauziano iliyofungwa baina ya Serikali na Ndg. Juma Ali Kidawa na baina yake na Ndg. Amina Aman Abeid Karume ni batili na ya udanganyifu. Aidha, Hati ya Matumizi ya Ardhi aliyopewa Ndg. Amina Aman Abeid Karume na Mhe. Mansour Yussuf Himid, kama tulivyoitolea ufafanuzi wake katika ukurasa wa 182-183, imekiuka taratibu za kisheria na kiutawala.

Mhe. Spika:
Pia tumegundua kuwa:
(ii) Mzee Juma Ali Kidawa sio Mmiliki halali kisheria wa Nyumba
iliyokuwa imefuatiliwa na wala hakuhusika na Uuzaji wa Nyumba hiyo kwa mtu yoyote na hakuwahi kufuatilia Utengenezaji wa Warka wa Nyumba hiyo.

Mhe. Spika:
Hata hivyo, kwa mujibu wa nia njema na mazingira halisi yalivyojitokeza yanaonesha Mzee Juma Ali Kidawa alihusika na kufanya kazi kwa Mhindi aliyeimiliki nyumba hiyo kabla ya kutaifishwa na Serikali.

Mhe. Spika:
Kamati imejiridhisha kwamba:
(iii) Ndg. Ramadhan Abdalla Songa na Mama Fatma Karume walishiriki
katika Udanganyifu wa Mkataba wa Mauziano uliofungwa baina ya Serikali (Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati) na Ndg. Juma Ali Kidawa.

Mhe. Spika:
Maelezo haya yanafafanuliwa katika ukurasa wa 178 hadi wa 180 wa ripoti yetu.

Mhe. Spika:
Mbali na taarifa hizo, lakini pia Kamati imebaini kwamba:
(iv) Ndg. Mwalimu Ali Mwalimu kama Katibu Mkuu, amechangia
kufanyika kwa udanganyifu wa Mkataba wa Mauziano baina ya Wizara yake na Ndg. Juma Ali Kidawa.

Mhe. Spika, maenelezo kwa undani yanapatikana katika ukurasa wa 177 hadi 180.

Mhe. Spika:
Kamati pia imegundua kuwa:
(v) Afisi ya Mrajis haikutekeleza majukumu yake ipasavyo iliyopelekea kuwepo kwa Mkataba wa Mauziano batili baina ya Ndg. Juma Ali Kidawa na Ndg. Amina Aman Abeid Karume.

Maelezo ya hoja hii yanapatikana katika ukurasa wa 180 hadi 182 ya ripoti yetu.

Mhe. Spika:
Kutokana na hali hiyo, Kamati yetu inapendekeza hatua hizi zichukuliwe:
(i) Nyumba hiyo ambayo sasa imeshajengwa Hoteli ya Ndg. Amina Aman Karume, Kamati inapendekeza hati zote hizo za umiliki wake zifutwe na apatiwe tena hati ya umiliki wa ardhi husika na baadae atakiwe (Ndg. Amina Aman Abeid Karume) amsaidie Ndg. Juma Ali Kidawa kwa kiwango cha fedha kisichopungua Milioni Ishirini (20,000,000/) ili kumsaidia kujinasua na maisha. Kwa sababu kwa mujibu wa ushahidi wa kimazingira, inaonesha wazi kwamba mwananchi huyu alikusudiwa kuimiliki nyumba hiyo kutokana na uhusinao wake na mmiliki wa Nyumba hiyo kabla ya kutaifishwa na Serikali.

(ii) Hatu za Kisheria zichukuliwe dhidi ya Wananchi wote waliohusika katika udanganyifu uliojitokeza katika Upatikanaji wa Mikataba ya Mauziano kutoka katika Mamlaka ya Serikali na kumuuzia Ndg. Juma Ali Kidawa na mauziano baina ya Ndg. Juma Ali Kidawa na Ndg. Amina Aman Abeid Karume.

(iii) Hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa watendaji wakuu wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati waliohusika na upatikanaji wa Mkataba wa Mauziano ya Nyumba Namba 755/56 kwa thamani ya Tsh. 5,000,000/- baina ya Wizara hii na Ndg. Juma Ali Kidawa.
Hatua za nidhamu kama hizi zichukuliwe dhidi ya watendaji wa Afisi ya Mrajis Mkuu wa Serikali walioshiriki katika upatikanaji wa Mkataba wa Mauziano baina ya Ndg. Juma Ali Kidawa na Ndg. Amina Aman Abeid Kaurume.

Mhe. Spika:
Katika Hadidu rejea ya Sita, kama inavyosomeka:
“Kuchunguza sababu ukweli kuhusu matatizo yaliyotokea kwenye ujenzi wa jengo jipya la Wizara ya Fedha, Pemba.
Kamati imegundua mambo yafuatayo:

(i) Taratibu za kumtafuta Mkandarasi wa Ujenzi wa Jengo hili hazikuzingatia muongozo na matakwa ya sheria zinazohusika.

Mhe. Spika:
Kamati imeridhika kwamba Watendaji wa iliyokuwa Wizara ya Fedha, hawafuata taratibu za Sheria ya Manunuzi na Ugavi wa Mali za Serikali , Namba 9 ya mwaka 2005 katika kumtafura Mjenzi wa Jengo la Ofisi ya Wizara, Pemba. Hali hii ndio chanzo cha matatizo yote yaliyotokea.

Mhe. Spika:
Vile vule:
(ii) Mkandarasi wa Ujenzi wa Jengo hili hakuwa na sifa zinazohitajika kisheria za kumfanya achaguliwe kufanya kazi hiyo.
Mhe. Spika:
Imedhihirika wazi kwamba, Mjenzi wa Jengo hilo hakuwa na utaalamu wa Ujenzi, wala hakuwa na Kampuni ya Ujenzi na badala yake amechaguliwa bila ya kuzingatia sifa zake, kinyume na muongozo wa Sheria zinazohusika.

Mhe. Spika:
Aidha, Kamati pia imefahamu kwamba:
(iii) Viongozi Wakuu wa Wizara hii (Mhe. Waziri aliehusika na masuala ya fedha wakati huo) na Watendaji Wakuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi pamoja na Bodi zao za Zabuni hawakausimamia ipasavyo majukumu yao kama wanavyohitajika kisheria.

Mhe. Spika:
Kama ilivyobainika kukiukwa kwa taratibu za Manunuzi na Sheria za Masuala ya Ujenzi, Uongozi wa Wizara hiyo, kama ilivyokuwa, ulishiriki kwa kiasi kikubwa katika uzembe huo na ni sawa na kusema, hawakuwajibika ipasavyo katika kutekeleza majukumu yao:

Mhe. Spika:
Vile vile Kamati imebaini kwamba:
(iv) Kitendo cha kutokuwepo kwa Mshauri Mwelekezi Mkaazi (Local Consultant) kimechangia sana kumfanya Mkandarasi ashindwe kutekeleze majukumu yake kwa usimamizi wa karibu wa Mshauri huyo kama ilivyohitajika.
Mhe. Spika:
Katika ujenzi huo, hakukuwa na Mshauri Mwelezi kutoka Zanzibar ambae muda wote angelikuwepo katika ‘site’. Matokeo yake wametafuta Mshauri Mwelekezi kutoka Tanzania Bara ambae nae hakuwa akikaa muda wote katika ujenzi. Hili nalo limechangia kwa kiasi chake kupelekea hali hiyo.

Mhe. Spika:
Vile vile, Kamati imebaini kwamba:
(v) Hakukuwa na mashirikiano ya karibu baina ya Mshauri Mwelekezi na Mjenzi, hali hii pia imesababishwa na kutoshirikishwa kwa Mshauri Mwelekezi (ambae alikuwa ameshapatikana kabla ya kupatikana Mjenzi) wakati wa kumtafuta Mjenzi.

Mhe. Spika:
Pamoja na kutolazimika kufanya hivyo, kwa kuwa Wizara hapo mwanzo ilimtafuta Mshauri Mwelekezi, ilikuwa vyema pia wamshirikishe wakati wa uteuzi wa Mjenzi. Matokeo yake hawakufanya hivyo, lakini pia Mshauri huyu Mwelekezi, aliwatoa ushauri wake mapema kuhusiana na ujenzi unavyoendelea, lakini hatua za haraka hazikuchukuliwa na matokeo yake ikapelekea suala hili kuharibika zaidi.

Mhe. Spika:
Vile vile:
(vi) Suala la hatua za kuendelea na Ujenzi ama Mkandarasi kwa gharama zake abomoe jego hilo kwa kushindwa kulijenga katika kiwango kinachofaa, linahitaji maamuzi ya haraka iwezekanavyo.
Mhe. Spika:
Sasa baada ya kuharibika ujenzi huo, kumekuwa na mawazo ya kumlazimisha Mjenz abomoe jengo hilo kwa gharama zake na hatimae awalipe fedha zote alizolipwa na Wizara hii, huku Mshauri Mwelekezi nae ana mawzo yanayokinzana, kwamba anashauri, Ujenzi huo hauna tatizo kama utafanyiwa ‘Under pinnig’ (marekebisho ya Kitaalamu).

Mhe. Spika:
Kwa upande wa Kamati inaona suala hili lishachukua muda mrefu, na hatima yake haifahamiki. Kamati inaona ni vyema hatua za haraka zaikachukuliwa kwa umakini mkubwa

Mhe. Spika:
Vile vile
(vii) Wizara ya Fedha na Uchumi (kama ilivyokuwa) ilifanya malipo makubwa kwa Mshauri Mwelekezi na Mjenzi huku ujenzi husika ukiwa katika hatua za awali.
Hali hii inapelekea (iwapo kutatokezea kutorejeshwa kwa fedha hizo na Mkandarasi) ugumu wa kupata uhakika wa kushinda kesi iwapo suala hili watalipeleka katika vyombo vya Sheria kutokana na wao wenyewe hawakuwajibika kisheria katika kumpata Mkandarasi kwa mujibu wa Sheria zinazohusika (contributory negligence).

Mhe. Spika:
Kutokana na kasoro hizo, Kamati inapendekeza hatua zifuatazo zichukuliwe:
(i) Viongozi na Watendaji wote waliohusika na kadhia hii wawajibishwe kisheria, kwa sababu imethibitika kwamba, Wizara hii (Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo) imechangia kutokezea kwa tatizo hili.

(ii) Ujenzi wa Jengo hilo usiendelee tena na Serikali isimamie kurejeshwa kwa fedha
zote zilizotumika kujengea jengo hilo ndani ya miezi 3 tokea tarehe ya kuwasilishwa kwa ripoti hii.
Aidha, taarifa ya hatua iliyochukua Serikali kuhusiana na suala hili ziwasilishwe katika Baraza la Wawakilishi.

Mhe. Spika:
Hadidu rejea ya Saba inahusu:
“Uhaulishwaji wa Majengo ya Mambo Msiige na Starehe Club”

Mhe. Spika:
Katika uchunguzi wetu mambo yafuatayo yamejitokeza:

(i) Ukodishwaji wa Majengo ya Mambo Msiige na Starehe Club haukufuata taratibu za uwekezaji zinazoelekezwa na sheria zinazohusiana na Uwekezaji Zanzibar.

Mhe. Spika:
(ii) Kamati haikupata kumbu kumbu zozote Serikalini zinazoonesha kuombwa kwa majengo hayo ya Mambo Msiige na Starehe Club na Mwekezaji na hivyo, haiwezi kuthbitika kwamba taratibu za kisheria na kiutawala zimefuatwa.

Mhe. Spika:
(iii) Kamati haikupata uthibitisho wowote wa kutoka agizo Ikulu juu ya ukodishwaji wa majengo hayo (kwa mujibu wa taratibu zilizopo) na hivyo ni sawa na kusema kwamba, Ukodishwaji wa Majengo hayo umezingatia zaidi amri ya mdomo ambayo iko kinyume na taratibu.

Mhe. Spika:
(iv) Sio Mamlaka ya Mji Mkongwe wala Idara ya Nyaraka na Kumbu Kumbu za Taifa iliyoshirikishwa ipasavyo katika Ukodishwaji wa majengo hayo wakati vyombo hivi ni sehemu muhimu ya kutoa ushauri unaofaa juu ya suala hili.

Mhe. Spika:
(v) Kulikuwa hakuna haja ya Uharaka wa kuhama kwa Ofisi za Serikali zilizokuwa zinatumia Majengo hayo na hivyo, hoja ya kuvuja kwa majengo hayo haina msingi wowote na ni wazi kwamba sehemu waliyohamia ndio inavuja kabisa.

Mhe. Spika:
(vi) Nyaraka za Serikali zilizopo katika Afisi ya Mrajis wa Serikali, zipo katika hali mbaya zaidi ukilinganisha na awali kutokana na jengo zilikohamishiwa sasa (Jengo la PBZ ya zamani) kuwa katika hali mbaya na linavuja kabisa. Aidha, jengo hilo halina mazingira wala hadhi ya kuhifadhia kumbu kumbu hizi muhimu, hali ambayo inahatarisha kumbu kumbu hizo kupotea.

Mhe. Spika:
(vii) Serikali imetumia nguvu na ubabe katika kuzihamisha Ofisi zilizokuwa zinatumia majengo hayo bila ya kuzingatia athari zitakazopatikana baada ya kuhama kwa Ofisi hizi kwa mnasaba wa utaratibu huo.

Mhe. Spika:
(viii) Ukodishwaji wa Majengo hayo haukuzingatia maslahi ya umma na umefanywa zaidi kwa maslahi binafsi ya Kampuni huku Serikali ikifunga mkataba wa miaka 99 bila ya kujali mabadiliko ya kiuchumi na kihistoria ya Mji wake.

Mhe. Spika:
(ix) Licha ya Majengo hayo kukodishwa kwa USD 1,500,000/, Serikali haijafaidika na fedha hizo kwa kiasi kilichotarajiwa kutokana na fedha nyingi hivi sasa zinatumika kugharamia safari za kwenda na kurudi UNESCO kufuatilia hadhi ya Mji Mkongwe na athari za kukodishwa kwa majengo hayo, ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa michoro husika.

Mhe. Spika:
Kamati yetu imependekeza hatua zifuatazo zichukuliwe:

(i) Mkataba wa Kodi kwa Mwekezaji huyu (ASB Holdings Ltd) aliyekodishwa Majengo hayo usitishwe mara moja kwa Serikali kurejesha Fedha za kodi iliyokwisha zipokea, na Majengo haya yarudi Serikalini huku Serikali ikiona ipo haja ya kuyakodisha, ni Lazima Majengo hayo yakodishwe kwa kufuata taratibu za kisheria kwa maslahi ya Taifa.

(ii) Ofisi ya Mrajis Mkuu wa Serikali itafutiwe eneo jengine kwa matumizi ya Ofisi itakayokidhi haja na hifadhi bora za kumbu kumbu za Taifa, huku jengo hilo la PBZ ya zamani lifanyiwe ukarabati liwe halivuji na kuwepo mahitaji yote muhimu ya Ofisi, ikiwa ni pamoja na matumizi ya maji salama na ya uhakika na zibakie Taasisi zilizopo baada ya kuondoka Ofisi ya Mrajis.

(iii) Mamlaka ya Mji Mkongwe na Idara ya Nyaraka na Kumbu Kumbu za Taifa zishirikishwe ipasavyo katika hatua zote za ushauri na maelekezo juu ya uhifadhi wa Majengo hayo ili yasipoteze haiba na historia yake.

Mhe. Spika:
Hadidu yetu rejea ya Nane inahusika na:
“Ukodishwaji wa Kisiwa cha Changuu”

Mhe. Spika:
Katika hadidu hii rejea, mambo yafuatayo yamejitokeza:

(i) Serikali (kupita kwa Mamalaka ya Uwekezaji Zanzibar na vyombo vyengine vinavyohusika), haina takwimu yoyote inayoonyesha idadi ya wageni wanaingia kwenye kisiwa cha Changuu, si kwa siku, kwa mwezi wala mwaka. Pia haieleweki ni kiasi gani cha mapato ambacho mwekezaji anaingiza kutokana na biashara anazofanya kwenye Kisiwa hicho. Lakini kibaya zaidi, hakuna hatua inayochukuliwa wala taarifa yoyote inayopatikana ya kiulinzi na usalama kwenye Kisiwa cha Changuu.

Mhe. Spika:
(ii) Tathmini ya Ardhi iliyokodishwa kwa Mwekezaji bado haijafanywa na Idara ya Ardhi, kitu ambacho kinakengeuka taratibu zilizopo.

Mhe. Spika:
Kamati pia imegundua:
(iii) Shirika la Utalii halikushirikishwa kwa ukamilifu katika ukodishwaji wa biashara ya utalii ambayo walikuwa wanaifanya kabla ya kisiwa hicho hakijakodishwa kwa Mwekezaji.

Mhe. Spika:
Vile vile Kamati imegundua kuwa:
(iv) Mmiliki wa Hoteli hiyo iliyopo katika kisiwa hicho hafuati ipasavyo sheria zinazongoza masuala ya uwekezaji wa miradi ya kitalii ikiwa ni pamoja na kutoa tarifa za mapato yake, wageni wanaoingia na kutoka Hotelini hapo. Aidha kwa upande wa Serikali, Mamlaka husika haziwajibiki kikamilifu katika kufuatilia suala hili.

Mhe. Spika:

(v) Kamati imegundua ukiukwaji wa taratibu za kimazingira kuhusiana na ujenzi wa ‘jetty’ katika Hoteli hiyo.

Mhe. Spika:
Kutokana na hali hiyo, Kamati imependekeza masuala yafuatayo:

(i) Serikali (kupitia ZRB) ifanye ukaguzi maalum wa kupata taarifa sahihi za wageni wanaoingia kwenye kisiwa hicho na ni kiasi gani cha mapato huwa kinakusanywa kutokana na biashara yote inayofanyika bila ya kusahau mapato yanayotokana na makobe. Na ripoti ya tarifa hizi ziwasilishwe katika Baraza la Wawakilishi si zaidi ya miezi 3 kuanzia tarehe ya kuwasilishwa kwa ripoti hii.

(ii) Serikali ihakikishe kuwa inafanya tathmini ya ardhi inayotaka kukodishwa kabla haijakodishwa ili iweze kupatikana tathmini halisi ya kodi inayostahiki kulipwa kwa thamani ya ardhí hiyo. Aidha, Tathmini ya ardhi pia ifanywe wakati wa kufanya mapitio ya kodi kwa ajili ya kujua uongezo sahihi la thamani ya ardhi hiyo na kuweza kutoa picha halisi juu ya ongezeko la kodi kutokana na mapitio ya kodi yanayofanyika.

(iii) Kuna haja ya kufanya marekebisho ya ongezeko la kodi kwamba lisiishie 10% ya kodi ya awali kama ilivyo kwenye mikataba yote ya ukodishwaji ardhi ya Serikali hivi sasa. Na kwa hivyo basi, kifungu 46(6) cha Sheria ya Ardhi (No. 12) ya 1992 inafaa kiangaliwe upya ili kitoe nafasi ya ongezeko la kodi la zaidi ya 10% ya kodi ya awali endapo kutakuwa na ongezeko kubwa la thamani ya ardhi iliyokodishwa, pamoja na kiasi kikubwa cha mapato kinachokusanywa na Mwekezaji kwenye ardhi husika.

(iv) Serikali ichukuwe hatua za makusudi za kulinda usalama kwenye maeneo ya visiwa kama Changuu; na Serikali inapaswa kulitafakari suala hili kwa kuzingatia namna ya kuzitumia Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya.

(v) Serikali ihakikishe inamsimamia ipasavyo Mwekezaji huyu ili azifuate kwa ukamilifu sheria zinazohusiana na uwekezaji na hatua hii pia ifanywe kwa wawekezaji wote nchini.

(vi) Idara ya Mazingira na Taasisi nyengine zinazohusika, ifanye utafiti wa tathmni ya mazingira kuhusiana na ujenzi wa ‘jetty’ iliyojengwa kisiwani humo na ikiridhika kuna uaharibifu mkubwa wa mazingira, Kamati inapendekeza hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya Mmiliki wa Hoteli hiyo.

Mhe. Spika:
Hadidu yetu ya Mwisho, yaani ya Tisa ilihusika na:

“Kuchunguza hatma ya majenereta yaliyoletwa Zanzibar kusaidia shughuli za Usambazaji wa maji wakati Zanzibar ilipokosa umeme kwa miezi mitatu.

Mhe. Spika:
Katika kuichunguza hadidu hii rejea, mambo yafuatayo yamejitokeza:

(i) Mamlaka ya Maji (ZAWA) imeshindwa kuzitambua mali zake (Majenereta hayo 12) hali inayoonesha toka mwanzo kwamba hawakuwa na uchungu na kuharibika kwake.
Mhe. Spika:
Vile vile tumegundua kuwa:
(ii) Kitendo cha ya ZAWA kuwatumia watu ili kufanyakazi bila ya kuwalipa wala kuwaajiri kinakiuka haki za binaadamu na wala hakivumiliki na Kamati imegundua kuwa ni miongoni mwa sababu zinazopelekea watu hawa kutokuwa na uchungu wa mali za ZAWA (ikiwa ni pamoja na majenereta) na matokeo yake uharibifu unapotokezea, hakuna wa kuchukua hatua.

Mhe. Spika:
(iii) Kamati imegundua kuwa majenereta yote 11 iliyoyaona hayafanyi kazi na hii imesababishwa na uzembe wa ZAWA kutopeleka mafuta ili majenereta hayo yakaweza kutumika.
Mhe. Spika:
Kamati pia imegundua kuwa:
(iv) Lengo la kutolewa majenereta hayo halikufikiwa ipasavyo kwa sababu hayajakusudiwa yatumike kwa muda mdogo na kuharibika mapema kama hali ya majenereta hayo ilivyo hivi sasa.
Mhe. Spika:
Kutokana na uchunguzi huo tuliounesha kapo juu, Kamati inapendekeza hatua zifuatazo zichukuliwe:

(i) Mamlaka ya Maji (ZAWA) ilitafute jenereta ambalo Kamati imeshindwa kulitambua ndani ya miezi mitatu tokea tarehe ya kuwasilishwa kwa ripoti hii na ikishindwa, Mkurugenzi Mkuu wa ZAWA anawajibika kulilipa kupitia mshahara wake.

(ii) Majenereta yote 11 yaliyotambuliwa na Kamati yafanyiwe matengenezo ya haraka ndani ya mwezi na yapatiwe mafuta ili yaweze kutumika kama ilivyokusudiwa.

(iii) Watu wanaotoa huduma vituoni(kwenye visima vya maji) watafutiwe utaratibu wa kuajiriwa na katika kipindi chote hiki cha kusubiri ajira zao, ZAWA iwalipe posho za kufanya kazi hiyo na suala hili litekelezwe mara moja.

Mhe. Spika:
Kwa ujumla wake, Kamati inashukuru kumaliza kazi hii nzito, kwas alama na kwamba Serikali na kila aliehusika, atapata fursa ya kufahamu na hatimae kufanya marekebisho makubwa na ya kimsingi katika utendaji. Kamati inaamini kwamba, ripoti hii itaisaidia sana Serikali katika utekelezaji bora wa majukumu yake, huku ikiheshimu haki na wajibu wa Baraza la Wawakilishi katika kuisimamia, kwa maana ile ile ya kuishauri, kuielekeza na hata kuikosoa kila penye haja ya kufanya hivyo, jambo la msingi zaidi ni kuipongeza kila inapotokezea haja ya kufanya hivyo.

Mhe. Spika:
Ripoti hii ni elimu tosha na ufahamu uliofikia kilele cha mafanikio kwa wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla na wasomaji wote wanaoutumia muda wao vizuri kwa kujisomea taarifa mbali mbali ili kupata elimu na ufahamu wa kuwaongezea maarifa. Kwa kupitia ripoti hii, mambo mbali mbali ambayo kwa muda mrefu ilikuwa ni kilio kwa wananchi kwa kukosa ufasaha wake au wamekuwa wakiyalalamikia kwa kuyajua kwa kiasi, basi watapata upeo wa ufahamu na uelewa mzuri kwa kuisoma ripoti hii.

Mhe. Spika:
Kubwa zaidi, baada ya maelezo yote hayo ni kwamba, Kamati imetoa mapendekezo kadhaa kwa kila hadidu rejea. Tumefanya hivyo kwa lengo la kurahisisha ufahamu na ufasaha, lakini kwa kuweka wepesi wa kutekelezwa kwake kama inavyostahiki kufanywa hivyo. Pamoja na kwamba tayari tumeshaeleza maoni na mapendekezo yetu katika kila mwisho wa hadidu rejea husika, kwa kuwa tunatakiwa kwa maelekezo ya kanuni ya 119(5) ya Kanuni za Baraza la Wawakilishi Toleo la 2011, kutoa ripoti yetu na sehemu ya tatu ya hitimisho, tutoe maoni na mapendekezo kwa Baraza hili.

Mhe. Spika:
Dhamira kuu ya Baraza kuunda Kamati Teule ni kwa nia ya kupata ukweli juu ya hoja zinazotokana na wananchi kupitia kwa Wawakilishi wao. Ukweli utakapopatikana kupita dhamira hii, utapelekea kurejesha imani na heshima kwa chombo hichi kwa wananchi, ili kila mmoja wetu aweze kufaidi MATUNDA YA MAPINDUZI yatokanayo na azma ya Mapinduzi na malengo ya Afro-Shirazi Party, chini ya Uongozi thabit wa Muasisi wa Sheikh Abeid Aman Karume.

Mhe. Spika:
Baraza hili kama ngome ya wananchi, hatuna budi tuziendeleze kwa vitendo, dhamira ya Mapinduzi kwa kutoa haki na fursa sawa kwa wote!.

Mhe. Spika:
Kamati inazidi kuitaka Serikali kuyachukulia hatua mambo yote yaliyojitokeza katika ripoti hii na ambayo yalifanywa na awamu zilizotangulia, kwani Serikali iliyopo madarakani, ndiyo inayowajibika kwa yale yaliyotangulia kabla.

Mhe. Spika:
Naomba uniruhusu nimnukuu aliyekuwa Waziri Mkuu wa Australia Bw. Kevin Rudd alivyoomba radhi wananchi kupitia Bunge kwa kosa lililotokea 1870 kama ifuatavyo:
“The time has now come for the nation to turn a new page in Australia’s history by righting the wrongs of the past and so moving forwards with comfidence to the furture”
We apologise for the hurt, the pain and suffering”

Mhe. Spika:
Nakiri kama wajumbe wote wa Kamati hii kwamba, Kamati yetu imetekeleza majukumu yake katika mazingira mazito na magumu kwani baadhi ya walioguswa ni wenzetu wa karibu na vipenzi vyetu, lakini Kamati haikuwa na budi kulitekeleza jukumu hili la wananchi.

Mhe. Spika:
Katika hili, nakumbuka aliyekuwa Rais wa Marekani, Bw. Richard Ivikson katika sakata maarufu la ‘water gate’ , wakati akihutubia Taifa lake alisema:
“ I was determined that, we should get to the bottom of the matter, and that the truth should be fully brought out- no matter who was involved”

Mh. Spika:
Naomba nimalizie kwa kuwashukuru sana viongozi wakiwemo Waheshimiwa Mawaziri, watendaji wa Serikali wakiwemo Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wakurugenzi, Wafanyakazi na wale wote ambao walikubali kuitikia wito wa kuja kuisaidia Kamati. Wote waliofanya hivyo, walifanya kwa nia ya kutoa mchango wao katika maendeleo ya Taifa letu. Kamati inawashukuru sana, kwani bila ya kukubali kwenu, kuitikia wito wa Kamati, kungelipelekea kazi hii kutotimia kwa ujumla wenu wote, tunawashukuru sana!.

Mhe. Spika:
Kamati inatumia nafasi hii kutoa shukurani za dhati kwa Sekretarieti ya Makatibu wa Kamati, inayoongozwa na Ndg. Yahya Khamis Hamad na Ndg. Othman Ali Haji, ambao katika mazingira magumu sana, wameweza kuisaidia Kamati hadi leo ikaweza kuwasilisha ripoti hii. Mhe. Spika; naomba nitumie fursa hii, kuwapongeza na kuwashukuru wafanyakazi wote wa Afisi ya Baraza la Wawakilishi huku msisitizo tukiuweka kwa Kitengo cha Hansard, kwa juhudi zao kubwa za kuimalizia ripoti yetu kuwa katika vitabu mbali mbali, kazi ambayo ni kubwa na ilihitaji uangalizi maalum.

Mhe. Spika:
Ni imani kwamba, Waheshimiwa Wajumbe, baada ya kusikiliza Muhtasari huu, mtapata fursa ya kupitia kwa umakini ripoti husika na kufanya rejea katika vielelezo mbali mbali vya ripoti hii na kama inahitajika Mjumbe ana fursa ya kupata maelezo ya mahojiano kati ya Kamati na Mhusika, kupitia mitambo yaliyo katika mfumo wa Hansard.

Mhe. Spika:
Mfumo huu wa kidemokrasia na Utawala Bora, ni mfumo sahihi na hatuna budi kuuendeleza kwa faida na maslahi ya Taifa letu na vizazi vijavyo. Mwenendo huu utatufikisha mbali katika maendeleo ya Taifa letu iwapo Baraza la Wawakilishi na Serikali, tutaendeleza na kuyafanyia kazi yatokanayo na matokeo ya kazi kama hii ya Kamati.

Mhe. Spika:
Nakumbuka wanadamu wenzetu, yaani jamii ya Mabudha katika imani yao wana usemi maarufu usemao:
“If you find the right way, all we have to do is to keep on walking”

Mhe. Spika:
Naomba nimalizie kwa kukushukuru tena, Mhe. Spika kwa kunipa fursa hii pamoja na kuwashukuru sana Wajumbe wenzangu wote kwa kunisikiliza kwa utulivu na Umakini wa hali ya juu kabisa. Najua kuwa, utulivu na umakini wenu unatokana na hamu ya kutaka kufahamu na kuichangia ripoti hii ya Kamati Teule.

Mhe. Spika:
Namalizia muhtasari huu kwa kuwaomba Waheshimiwa Wajumbe wenzangu tujikumbushe neno moja lililomo kwenye kiapo cha wana CCM kisemacho cheo ni dhamana nasitokitumia cheo changu kwa maslahi yangu ”.

Mhe. Spika:
Naomba kutoa hoja.

Omar Ali Shehe,
Mwenyekiti,
Kamati Teule,
Baraza la Wawakilishi,
Zanzibar.

Advertisements

25 responses to “Serikali yavuliwa nguo

 1. acheni tu watu waibe si ndio mnavyotaka hivyo. Au mnataka kumuonea Mansuri kwa sababu amesema wazi anataka serikali 3. Wangapi wanaiba kuliko yeye. Nendeni ZSTC mkaone watu wanavyojijengea empires. bandari na kwengineko. Muacheni mtoto wawatu apumue.

  • wacha upenzi wewe! taarifa hii imekuja kufuatilia agiza la baraza na walifafanua sehemu ambazo nilitakiwa kuchunguzwa. Pengine ni kweli sehemu ka ZSTC ninanuka bali hazikuhusika katika report hii.
   Nadhani tuipongeze serikali kwa hatua nzuri kama hii ya kufichua machafu. Hii itapelekea walioko madaraka sasa hivi kua makina na wanachokifanya.

   Hongera kamati, Hongera GNU – kwa ushujaa wenu

  • Hapana sikubaliani na wewe hata kidogo. Waachiwe waibe? hapana. Kwanza hakuna uhusiano wa mojakwamoja ya kwamba Mansuri anataka serekali 3 na wizi uliofanyika. Bila shaka hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi yake na kama kumeonekana kosa basi ashtakiwe na hukumu ichukuwe mkondo wake. Swala la serikali tatu hata mimi naliwafiki ili zanzibar ipate kutoa maamuzi yake wenyewe.

 2. Mimi nadhani uchunguzi huu ulikua uanzie mbali kuna watu wamejimilikisha mashamba ya serikali hawaonekani, waliojiuzia magari ya serikali hawaonekani anaonekana Mansuri tu kwa kua anaunga mkono serikali 3? Miaka yote hatukuwahi kusikia ZSTC imeingiza kiasi gani katika pato la nchi, wala bandari mbona hazijachuchunguzwa?

  • Ndugu Said, please hebu usichanganye madawa. Swala la serikali tatu sisi wazanzibari walio wengi tunalitaka, lakini kwakuwa Mansuri kataka serikali tatu ndo afanye atakavyo? si halali hata kidogo, mimi sikubaliani na wazo lako. Na swala la ZSTC kweli kumetokea ubadhirifu mkubwa, sasa huwezi kusema mbona skandal la ZSTC halikufuatiliwa? Mambo hayaendi hivyo kwamba scandal zote zilizofanywa katika kisiwa hichi zichunguzwe siku moja. Haiwezekani hata kidogo, lakini huanza moja then hufuatiwa na lengine. Basi na mimi naweza kusema hivi: “MBONA UN NA HUMAN RIGHT WATCH HAWAJAWASHTAKI WAASISI WA MAPINDUZI YA ZANZIBAR?” Haliyakuwa mauaji makubwa yalitokea dhidi ya wananchi wa kawaida wasio na hatia yoyote. Ndio pale tunaposema kwamba events and time.

   Wasiwasi wangu tu upo hapa: Ivi kweli Mheshimiwa Shein ataweza kuwachukulia hatua wabadhirifu hawa? maana kashfa kama hizi zishawahi kujitokeza waziwazi na hakuna hatua yoyote iliochukuliwa dhidi yao. Na ukiangalia kauli za Mhe. Raisi huupuzwa na viongozi watendaji kama lilivopuuzwa agizo lake la wanyama wasiingie maeneo ya mji.

   Naamini umenielewa.
   HUNGERA GNU.

 3. Hivi jengo la mambo msiige linachunguzwa kitu gani wakati mkuu w nchi ambae ndie bosi wenu ameshatoa kauli mbele ya dunia nzima kua ” Jengo lile ni letu na tutafanya tunavyotaka” au mmesahau? Kama hapo kuna wa kuchukuliwa hatua basi na yeye aingizwe kwani alichangia kuidhinisha uovu na ubadhirifu wa mali za serikali.

 4. Pingback: Serikali yavuliwa nguo·

 5. huo ni mtego wa panya wataingia waliowemo na wasiokuwemo. sasa ikiwa serikali ndio imefunga mkataba m bovu kama huo.ma idear just to brush a side that things be fowards because sio huo tu ukichekecha utaiona mingi tu ndo hapo tutapotiana vidole vya macho…..ila big up kwa sana baraza letu jipya tukufu WE CAN

 6. kunya anye kuku tu akinya bata je uoze mtupu hii ni kansa hasa na dawa ya kansa ni kufa moja kwa moja au kukata sehemu husika ,dhulma tupu imetanda weziiiiiiiiiiiiiiiiiii watupu tena wotee dawa yao hawa tupate serikali ya uamsho tu basi ichukue nchi tupate zanzibar yetu huru viongozi wote wezi wote wallah inasikitisha sanaaa yani.

  • WAZANZIBARI WOTE MNATAKIWA KUFIKA BARAZA LA WAWAKILISHI CHUKWANI IJUMAA 20/4/2012 KESHO ASUBUHI

   Mzanzibari juwa kuwa siku na saa ya ukombozi imefika kwa misingi na utaratibu wa kisheria. kwa hiyo bai siku ya Ijumaasaa moja na nusu 1:30 asubuhi tunaarifiwa Wazanzibari sote wa unguja na pemba tufike katika viwanja vya BARAZA LA WAWAKILISHI Chukwani ‘Unguja’ kwa lengo la kudai haki yetu ya kikatiba juu ya kuwepo KURA YA MAONIDHIDI YA MUUNGANO kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar . Elewa kupigania haki ya nchi ni jihad. tafadhali ukipata ujumbe huu mtumie na mwengine.

 7. Hiki sasa ni kichekesho maana kwa watu ambao wanatajwa na ripoti hii naona kua ni ” the untouchables” na sizadhanii kama Baraza lina ubavu wa kuwagusa ila nasubiri nione mambo mwaka huu. Haya mambo yote yamo takriban kwenye taasisi zote za Serikali kila mtu anajua wizi tu na kujilimbikizia mali. Kama hii kamati itaendelea na kazi hii ni watu wachache sana wataobakia na kwa uono wangu naona ni Dr Shein, Maalim Seif na Balozi tu. Suala langu ni jee kama hawakulipa hizi hasra zote nini kitafuata? Na kabla ya yote Dr Shein aanze kuwachukulia hatua wote waliotajwa kwani wameitia nchi hasara kubwa. Hivi hii GSO kwani kazi yake kubwa si kuwatambua watu ambao ni wanachama wa CUF wanaotaka ajira serikalini wasipewe tu au ina kazi nyengine?

 8. WAZANZIBARI WOTE MNATAKIWA KUFIKA BARAZA LA WAWAKILISHI CHUKWANI IJUMAA 20/4/2012 KESHO ASUBUHI

  Mzanzibari juwa kuwa siku na saa ya ukombozi imefika kwa misingi na utaratibu wa kisheria. kwa hiyo bai siku ya Ijumaasaa moja na nusu 1:30 asubuhi tunaarifiwa Wazanzibari sote wa unguja na pemba tufike katika viwanja vya BARAZA LA WAWAKILISHI Chukwani ‘Unguja’ kwa lengo la kudai haki yetu ya kikatiba juu ya kuwepo KURA YA MAONIDHIDI YA MUUNGANO kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar . Elewa kupigania haki ya nchi ni jihad. tafadhali ukipata ujumbe huu mtumie na mwengine.

  • Kudai “Kura ya maoni” ni miongoni mwa aina za khatuwa za kuwania nchi yetu, lakini muhimu tuhakikishe kwamba ataepiga kura ya maoni ni Mzanzibari wa tangu kabla ya huu muungano, si Mzanzibari wa leo au Mzanzibara. Kwahivyobasi, muhimu vipatikana vitambulisho vya Mzanzibari aliekuwa ni Mzanzibari kabla ya huu muungano. Hao ndio Wazanzibari wakuulizwa kama wanautaka muungano au hawautaki. Kwa sababu suala hili halikufanywa wakatia Wazanzibari walipotiwa kwenye huu muungano. Busara zaidi ni kurejea Dola ya Zanzibar baada ya hapo ndio kupangwa kufanywa kura ya maoni kama Wazanzibari wanautaka ushirikiano, ushirikiano wa namna gani.

 9. Ripoti ya Mheshmiwa Omar Ali Shehe imenishtua ingawa si sana. Marx alinena kuwa ” It is not the consciousness of men that determines their being, but, on the contrary, their social being that determines their consciuosness.” Na Mtume SAW alisema ” Kila kinachozaliwa ni kitakatifu, lakini wazazi wake ndio hufanya awe mwema au majusi.” Ndio mana haikunishangza sana mambo haya kufanywa na baadhi ya watu wenye PhD. Unatarajia nini kwenye jamii ambayo ukifanya kosa hiwajibishwi. Watu ni kutumia vibaya madaraka! Kufuja taasisi na mali za Umma na mengine mingi. Serikali yote imeoza, Taasisi zote zimeoza, Shirika la Umeme kuna msichana aliyemaliza Form II kwa shida amelipiwa masomo Uingereza na sasa eti ana Degree. Huyu ni mwanamke wa bosi na hana akosacho. Wakati Shirika linashindwa kuagiza mita yeye alipata pesa za kusoma Unigereza hali hana hata sifa za kujiunga Chuo Cha SMZ cha Forodhani. Wizara ya Fedha tunaona Watumishi wake wanamiliki Maskuli ambayo SMZ haimudu kuyajenga, SUZA nako mambo si mazuri Watu hupewa Tender huku taratibu za Tender zikivunjwa. Kila taasisi ya Serikali ina matatizo! Kamma kuna Wakati wa kudai mambo mengi basi ni huu. Kudai Muungano tuu uvunjike haitoshi! Ningekuwa mimi ni Rais ningefumba macho nikaivunja Serikali kisha nikaiunda upya! Na safari hii kwa kuwataka watu waombe kazi katika nafasi za Kiutendaji na kila muombaji aeleze atafanya nini kuondosha uozo na kurejesha heshima ya Serikali kwenye macho ya watu. Ninge mimi ni Rais ningesahau Chama nikaheshimu “Weber’s Administrative Principles” na Wizara ya Ajira ingeongoza na mtu aliye na ABC ya nadharia za Weber na si asiyejua makulima wala mavuvi. Ningekuwa mimi ningeunda Serikali ndogo lakni yenye ufanisi. Watu ambao wametajwa katika tuhuma ningewavua uaziri. Serikali ya sasa kubwa ndio inaleta matatizo kuiyendesha. Ningekua mimi ni Rais ningeukodisha Uwanja wa Ndege, Bandari kwa watu walio seriuos si Boers au wale kutoka Venice. Ningefanya mambo mengine lakni kuivunja Serikali ingekuwa Priority !

  • Tunakumbuka wakati wa uchunguzi wa “wafanyakzi hewa” kwenye Wizara ya Afya, Waziri Kiongozi, Mhishimiwa Nahodha hakuona aibu wa nje ya uongozi pale aliposema, “mtu haibi kwao, huchukuwa”. Hapana ajabu kwa qauli kama ile.

   • Tumepinduwa na tunatanuwa kwa viskudo. Wakati wa mkoloni akiendesha mwaraabu tu. Ukiuliza hizo gari zilikuwepo ngapi kabla ya 1964? Sijuwi kama hamsini zinafika…

 10. kisiwa cha chumbe ni mali ya amani abedi karume sijuwi kwanini hawa wanafik wameshindwa kumtaja kama muhusika wa hotel hiyo jee wacheni unafik hapo hakuna kitu ni kupotezeana muda iko siku mtajuwa ukweli kwani dhulma haidumu

 11. Hongera Kamati kwa kazi Nzuri sana sasa tunaanza kuona uadilifu ukitendeka,yate haya ni kwa ajili ya GNU venginevyo misimamo ya kichama ingalichukuwa nafasi yake kama ilivyokuwa huko nyuma. Sasa kazi ni kwa Rais wa Nchi kuchukuwa maamuzi ya kiutawala kwa haraka venginenevyo Serikali itakuwa katika hali mbaya katika uso wa kijamii, ushauri wa wazim kwa Rais Shein kwanza ni kuvunja Seikali yake yote Baada ya Kikao hiki cha Baraza Kumalizika baada ya Kuivunja Basi wizara zote azigawe sawa kwa sawa kati yake na Makamo wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Wazisimamie kwa Muda usizidi Mwezi Mmmoja ili waweze sasa kupanga upya Mawaziri, manaibu mawaziri, Makatibu wakuu, manaibu , wakurugenzi, mameneja, nk, ikisha Rais aangalie uteuzi wake mpya wa Makamo wa pili wa Rais kwa kina kama katiba inavyomtaka, pia ukubwa wa Seikali aupe mtazamo upya kwa kuzingatia maoni ya umma, na hapo watutangazie serikali mpya itakayochukuwa nafasi ya hii iliopo sasa ambayo tayari kwa kiasi kikubwa imeshayumba.

 12. sasa wakati umefika ukweli mengi tumevumilia wananchi wa zanzibar sasa tutajivunia kupata viongozi kama nyinyi muioteuiwa kwenye kamati hii. kwakwei hamkuonesha kujai mtu wala wadhifa wake katika utendaji wenu na kuonesha kuwa muko tayari kwa kuwatendea kazi wanachi wenu natoa wito wa wananchi wote huu ndio mfano wa viongozi tunaowataka ikitokezea kiongozi yuo kwaajili ya masahi yake binafsi basi tusimpe kura zetu wakati wa mabadiloko na maendele sasa umefika. waheshimiwa musichoke hongereni sana kwakazi hakikisheni taarifa yenu inafanyiwa kazi ili ionekane kuwa imefanyiwa kazi basi ni lazima kila alieshiriki awajibishwe hata akiwa nani vywenginevyo itakuwa mumetumuka bure tu musikubali kupoteza wakani weni na nguvu zenu bure na sisi wananchi tuko pamja na nyie kwa lolote lile mpaka tujue haki imeatikana.
  napia nachukua nafasi hii kuliomba bareza lenu tukufu kuwa imara na makini zaidi ya hao kwani yao mengi sana hususan katika mambo ya viwaja na maeneo ya wazi se6rekali ilooita kwakweli haikutendea haki kwa baadhi ya wananchi wa zanzibar.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s