Spika akerwa na uzembe barazani

Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho akitoa taarifa kwa wajumbe ambapo amekerwa na wajumbe wanaofanya uzembe katika baraza hilo

SPIKA wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho jana aliwakemea viongozi wanaokosekana barazani bila ya kutoa sababu maalumu na kusema tabia hiyo ni utovu wa nidhamu ambayo huharibu shughuli za ratiba za shughuli za baraza hilo. Akizungumza baada ya kipindi cha masuali na majibu katika kikao kinachoendelea huko Chukwani, Mjini Zanzibar, Kificho alionekana kukasirishwa na kitendo hicho huku akisisitiza nidhamu kuwekwa katika kipindi chote cha shughuli za baraza hilo.

Kukasirishwa na Spika kumefuatiwa na tukio la wiki iliyomalizika ambapo Mwenyekeiti wa kamati ya Mawasiliano na Ujenzi, Makame Mshimba Mbarouk kutoa ripoti ya Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi iliyopangwa kutolewa Ijumaa iliyopita, lakini hakufanya hivyo kwa sababu hakuwepo barazani.

Alisema kukosekana kwa viongozi wakati shughuli za kikao zinaendelea kunakwamisha baraza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na katika muda uliopangwa na hivyo kuharibu utaratibu mzima uliopangwa.

“Waheshimiwa wajumbe Ijumaa shughuli za kamati ya mawasiliano na ujenzi, zilikwama kwa sababu mwenyekiti hakuwepo barazani, bila taarifa, huu ni utaratibu mbaya na ni nidhamu mbovu utaratibu huu unatuvurugia shughuli zetu, tunataka viongozi serious,… baraza linatumia fedha za serikali,” alisema Spika Kificho akiwa amekunja uso.

Spika Kificho alisema amelazimika kukemea jambo hilo ili viongozi wote wakiwemo mawaziri waweze kufanyakazi za baraza kwa nidhamu na kuona umuhimu wa chombo hicho kwa maendeleo ya wananchi huku wakizingatia wananchi wamekuwa wakifuatilia chombo hicho muhimu kupitia vyombo vya habari.

“Tunawaambia mawaziri wawepo na kama hawapo tunawaambia wajieleze mimi kama Spika hili silikubali lazima tuwe serious lazima tuwe committed na haiwezekani hili kulisamehe” alisema Spika huyo.

“Wananchi wanatutizama na kufutilia shughuli zetu tunazozifanya lakini ikiwa mheshimiwa anaitwa halafu taarifa zinasema hatupo hilo ni jambo baya na wananchi watahoji fedha za serikali zinavyotumika vibaya bila ya maelezo ya kina” alisema Kificho.

Kificho alitoa karipio hilo kabla ya kumruhusu Mwenyekiti huyo kuja mbele kusoma ripoti yake ambapo alisema baada ya kuripoti taarifa yake lazima andike barua ya kujieleza na aliombe radhi baraza hilo ili kuonesha umakini wa chombo hicho muhimu.

Lakini wakati Mbarouk anajiandaa kwenda kwenye kipaza sauti baada ya kuruhusiwa na Katibu wa Baraza hilo, Kificho alinyanyuka haraka na kusema: “Sijakuita kaa kwanza.” Na Mwenyekiti huyo kulazimika kukaa chini huku wajumbe wengine wote wakiwa kimya katika viti vyao.

Sio mara nyingi kwa Spika Kificho kuwa mkali kiasi kama alichoonesha na mara nyingi huwa anaenesha vikao akiwa anatumia sana maneno ya busara na kuwalainisha wajumbe amabo wamekuwa na maneno makali akiwataka wawe wanaongea kwa utulivu bila ya jabza lakini jana hali ilibadilika na kuonekana amewiva kutokana na kitendo hicho.

Muda mfupi baada ya Mwenyekiti huyo kukaa kwenye kiti chake, Spika Kificho alimwamuru Mwenyekiti anayehusika na  kamati hiyo kuomba radhi kwa kukosekana kikaoni bila taarifa kabla ya kumruhusu kuanza kutoa ripoti hiyo na kumwambia afuate utaratibu wa kuomba radhi.

Baada ya kupewa taarifa hiyo, Mbarouk alianza kusimama na kujitambulisha kuwa yeye ndio mwenyekiti kwa kuwa wakati Spika akizungumza yote alikuwa akitaja Mwenyekiti bila ya kutaja jina lake.

Ijumaa iliyopita Mwenyekiti huyo ambaye ni Mwakilishi wa Jimbo la Kitope (CCM) alitakiwa kuwasilisha repoti yake hiyo laini alikosekana barazani hapo bila ya sababu zilizotolewa na kusababisha baraza la wawakilishi kuakhirishwa kabla ya wakati wake.

“Mheshimiwa Spika, sisi ni binadamu, kuna mambo tunafanya kwa sababu zisizozuilika,” alisema Mbarouk na kusababisha Kificho kuzidi kuja juu akimwambia: “Umeambiwa uombe radhi, kuna barua utaipata uijibu kwanza utoe maelezo kwa maandishi, utaratibu wa kuijibu barua itafuata baadae soma ripoti yake” alisema Spika huku akionesha kuwa makini sana.

Kificho alionya kuwa kukopsekana kwa viongozi, barazani wakiwemo mawaziri kunasababisha baraza kuongeza muda wa shughuli hizo na kusababisha kutumika kwa fedha nyingi za serikali pasipo lazima jambo ambalo sio busara kuitia hasara serikali.

Z’bar inaongoza Tanzania watoto kula sukari nyingi

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar jana imesema watoto wa Visiwa wa vya Unguja na Pemba wako hatarini kupata magonjwa ya sukari kutokana na kukithiri kwa ulaji wa sukari utafiti umeeeleza.

Kwa mujibu wa utafiti unaonesha watoto wa Zanzibar wanaongoza kula vitu vya sukari ikilinganishwa na watoto wa Tanzania Bara jambo ambalo huhatarisha afya zao.

Waziri wa Afya, Juma Duni Haji alisema katika kikao kinachoendelea cha baraza hilo kwamba utafiti umegundua ulaji sukari kwa wingi unachangia watoto kupata maradhi ya moyo visiwani hapa.

“Kuna utafiti umefanya umegundua ulaji mkubwa wa suakari kwa watoto na umeonesha ukilinganisha na Dar es Salaam, watoto Zanzibar wanakula sukari nyingi, uzito ni tatizo kwa maradhi ya moyo,” alisema Waziri huyo.

Waziri huyo amesema hayo kufuatia suali la Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini (CCM) Ali Abdalla Ali, aliyetaka kujua ni vyakula gani ni hatari kwa wagonjwa wa sukari na shinikizo la damu.

Akijibu suala hilo, Waziri Duni, alisema vyakula vyenye viashiria vya ugonjwa huo vipo vingi kutokana na baadhi ya watu kuamua kula vyakula bila ya kufanya mazoezi.

Alisema hali hiyo inaonekana kuwa mbaya zaidi kwa watoto kutokana na utafiti uliofanywa kati ya watoto wa Zanzibar na Tanzaania bara, ambapo watoto wa Zanzibar wamebainika wamekuwa wanakula kiasi kikubwa cha sukari katika vyakula wanavyotumia katika milo yao.

Duni alisema hali hiyo inaonesha kuwapo viashiria vinavyochangia kuongezeka kwa wagonjwa wa sukari katika makundi ya watoto mbali mbali kutokana na kukithiri kula vyakula hivyo.

Waziri Duni alisema tabia na matumizi ya vitu hatarishi vinavyosababisha maradhi hayo ni pamoja na matumizi ya sukari nyingi na ukosefu wa mazoezi.

Pia utumiaji sukari kwa kiwango kikubwa na kutokufanya mazoezi ni miongoni mwa sababu zinazosababisha mwili kupokea kwa urahisi maradhi hayo kwa mujibu wa wataalamu  wa afya.

Akizungumzia ugonjwa wa moyo alisema unawakumba watu wa makundi yote katika jamii, wakiwemo matajiri na wale wanaoishi kwa wasiwasi kutokana na umasikini.

“Mimi nimesema huko nyuma na leo narejea tena kusema sio mtaalamu wa afya lakini maisha magumu yamo katika kundi la vitu hatarishi vinavyochangia watu kupata maradhi ya moyo, sawa na watu matajiri, ndio wataalamu wanavyotwambia” alisema Duni.

Awali akijibu suala la msingi la Mwakilishi wa Kojani (CUF), Hassan Hamad Omar, alietaka kujua kama serikali imewahi kufanya utafiti kufahamu chanzo cha kuongezeka kwa maradhi ya moyo, kisukari na shinikizo la damu.

Waziri Duni akijibu suali hilo alisema tayari serikali imeshafanya utafiti juu ya ugonjwa huo kwa kushirikiana na wafadhili kutoka DANIDA Copenhagen na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Alisema baada ya utafiti huo kazi kubwa ambayo serikali inaendelea kuifanya ni juu kurejesha matokeo hayo kwa kuanzisha uchunguzi wa afya kwa Masheha wa Unguja na Pemba ambapo tayari zoezi hilo limeanza kufanyika kisiwani Pemba.

Waziri huyo alisema masheha hao watapewa elimu ya kuisaidia jamii katika maeneo yao hatua ambayo itaenda sambamba na kufanyiwa vipimo vya maradhi hayo pamoja na kuvitumia vyombo vya habari kutoa elimu zaidi kwa wananchi.

Alisema hivi sasa katika kupambana na tatizo hilo Wizara hiyo imeshawapeleka watoto 62 kwenda kutibiwa ugonjwa wa moyo nchini India kwa msaada wa serikali ya Oman.

Alisema katika matibabu hayo serikali imeshatumia milioni 600 na fedha kwa kipindi cha mwaka mmoja na kwa ajili ya kupeleka wagonjwa nje zimefikia shilingi bilioni moja.

Alisema hali hiyo inatokana na wengi wa wagonjwa waliojitokeza kuhitaji matibabu hayo ni walio katika hali duni kiasi ambacho serikali inalazimika kugharamia matibabu yao kwa asilimia 100.

Alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilitumia  shilingi bilioni moja kupeleka watoto nchini India kwa matibabu ya ugonjwa wa moyo mwaka jana na shilingi nyingine milioni 600 kwa matibabu ya aina hiyo mwaka huu ambapo Waziri huyo alisema serikali inalazimika kugharamia wagonjwa hao wasio na uwezo kwa asilimia mia moja.

Wajumbe wa baraza hilo walishauri serikali kuzingatia suala la wataalamu kuwepo nchini na kutoa huduma hiyo badala ya kutumia mabillioni ya shilingi ya kusafirisha wagonjwa.

Viongozi wa majimbo washirikiane na wizara

WIZARA ya Mawasiliano na Miundombinu, imewataka Viongozi wa Majimbo kushirikiana na Wizara hiyo kuweza kutatua matatizo ya njia ziliomo katika majimbo wanayoyaongoza.

Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na Miundombinu, Issa Haji Gavu, aliyasema hayo jana wakati akijibu suala la Mwakilishi wa Mkwajuni (CCM) Mbarouk Wadi Mussa Mtando, aliyetaka kujua ni lini Wizara hiyo italipatia ufumbuzi tatizo la barabara za ndani katika Jimbo la Mkwajuni.

Akijibu suala hilo Naibu Waziri huyo, alisema tatizo liliopo hivi sasa ni kuwapo kwa uwezo mdogo wa Halmashauri ambazo ndizo zinazotakiwa kufanya ujenzi huo na ni vyema viongozi wa majimbo wakashirikiana na Wizara hiyo kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.

Alisema hivi sasa nyingi ya njia za ndani ni mbovu lakini Wizara hiyo imekuwa ikishirikiana na uongozi wa Halmashauri kuzipatia ufumbuzi.

Alisema katika kukabiliana na hali hiyo Wizara hiyo imeweza kuzifanyia matengenezo baadhi ya bara bara za ndani za Wilaya ya Kaskazini ‘A’ katika shehia ya pita na zako yenye urefu wa kilomita 1.5.

Bara bara nyengine ambazo Naibu huyo alizitaja ni pamoja nay a Chaani Mtakuja yenye urefu wa kilomita 1.2, bara bara ya Chaani yenye urefu wa kilomita 500, barabara ya Kinyasini Ziwani  kilomita 800 na barabara ya Nungwi yenye urefu wa kilomita 1.2.

Naibu huyo alisema katika Jimbo la Koani, barabara ambazo zimejengwa ni pamoja na ya Kidimni hadi Ubago na Koani Kibonde maji na barabara ya Kinuni kwa Wilaya ya Magharibi.

Alisema katika muendelezo wa ujenzi wa barabara hizo, hivi sasa wanatarajia kujenga barabara ya Mkunazini ambapo ujenzi wake utafanyika kwa kushirikiana na viongozi wa Jimbo hilo .

Alisema mpango huo pia unatarajiwa kufanyika katika Jimbo la Uzini kwa kuzitengeneza njia za ndani kwa kushirikana na  viongozi wa jimbo hilo .

Katika kikao hcho Mwakilishi wa Jimbo la Kitope (CCM) Makame Mshimba Mbarouk  alimuomba Naibu Waziri huyo kumpa ufafanuzi wa neno ushirikiano akisema halifahamu.

Akijibu neon hilo, Naibu Waziri huyo,  Issa Haji Ussi  alisema ni kutoa ushauri kwa viongozi wa majimbo kuipa wizara yake ushirikiano inapotekeleza miradi ya maendeleo, kama ya ujenzi wa madaraja na  barabara za ndani, yaani feeder roads katika maeneo yao.

Mapema Waziri Ussi akijibu swali la awali la nyongeza la Mwakilishi wa (CCM) Mussa Ali Hassan juu ya kuchelewa kukamilika kwa kazi ya ujenzi wa madaraja Mkokotoni na  Mtoni Pwani alisema madaraja hayo ambayo kwa ujumla ni manne yamekamilika na kwamba yote yameanza kutumika.

Ussi alisema  kwa upande wa daraja la Tingatinga utekelezaji  unaoendelea ni ukamilishaji wa hatua ndogo ndogo za ujenzi.

Alisema kuchelewa kwa ujenzi wa madaraja hayo kumetokana na sababu mbali mbali, ikiwemo ukosefu wa mafuta kwa ajili ya magari ya kusoma kifusi na kushauri viongozi wa majimbo kutoa ushirikiano kama vile kutoa fedha za kusaidia kuimarisha miradi ya madaraja na barabara.

Hata hivyo, katika swali lake pia la nyongeza lilioambatana na ombi la kuomba ufafanuzi wa neno ushirikiano, Mbarouk alitaka kujua juu ya ushirikiano anaotaka Naibu Waziri huyo kutoka kwa viongozi majimbo.

“Ni ushirikiano gani unaotaka kutoka kwa viongozi majimboni? aliuliza Mbarouk.”

Mbali na kuuliza swali hilo, Mbarouk pia alisema hakubaliani na maelezo kwamba madaraja hayo yote yamekamilika kwa sababu Tingatinga Tingatinga mpaka sasa wananchi bado hawajaanza kulitumia.

Swali la Mwakilishi wa Jimbo la Koani (CCM) Mussa Ali Hassan aliyetaka kujua iwapo serikali imechukua hatua za kuwatoza faini wajenzi wa mradi huo, Ussi alisema kuchukua hatua hiyo kungekwamisha utekelezaji wa mradi wakati kesi inaendelea.

Kuchelewa kukamilika kwa ujenzi wa madaraja katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, Serikali imesema tatizo hilo limechangiwa na mfadhili wa mradi huo kushindwa kumlipa Mkandarasi wa ujenzi huo.

Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na Miundombinu, Issa Hasji Gavu, aliyasema hayo jana wakati akijibu suala la Mwakilishi wa Mkwajuni Mbarouk Wadi Mussa Mtando, aliyetaka kujua sababu za kuchelewa kwa ujenzi wa madaraja hayo.

Akijibu suala hilo alisema ujenzi wa madaraja hayo yanajengwa na benki ya Maendeleo ya Afrika ADB, ndio ambao wamechelewesha kufanyika kwa ujenzi huo.

Alisema hivi sasa ujenzi wa madaraja hao tayari yamekamilika lakini kumesalia kufanyika kazi ndogo ndogo ambapo mfadhili wa mradi huo bado hajawapatia wajenzi malipo yao .

Alisema sababu nyengine ni pamoja na hali ya hewa baada ya kujitokeza kwa mvua nyingi ambazo zilisababisha ujenzi huo kusita.

Alisema ujenzi huo unaambatana na ujengwaji wa barabara ya Amani Dunga na mfenesini hadi Bumbwini ambazo tayari zimshakamika.

SERIKALI INAJIANDAA NA ICU PEMBA

 

 SERIKALI ya Zanzibar inajiandaa kujenga Chumba cha Wagonjwa mahatuti katika kisiwa cha Pemba ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa hospitali mpya ya Mkoani.

Waziri wa Afya Zanzibar, Juma Duni Haji, aliyasema hayo jana wakati akijibu suala la Mwakilishi wa Ziwani Rashid Hemed Suleiman, aliyetaka kujua ni kwa nini serikali haioni haja kujenga chumba cha wagonjwa mahatuti kisiwani Pemba .

Akijibu suala hilo Waziri Duni, alisema Wizara yake ina nia ya kujenga jengo hilo baada ya kuona umuhimu mkubwa wa kufanya hivyo kutokana na wagonjwa wengi kupata usumbufu pale inapotakiwa kusafirishwa kuja Unguja.

Alisema utaratibu wa sasa Wizara hiyo haikubaliani nao kutokana na wagonjwa wamekuwa wakilalamikia jambo ambalo serikali imeona umuhimu wa kujenga jengo hilo kisiwani Pemba .

Alisema mradi wa ujenzi huo utafanyika baada ya serikali ya China kukubali kujenga hospitali mpya kisiwani Pemba ambayo  itajengwa katika eneo la Mkoani.

Akijibu suala la msingi la Mwakilishi wa Kojani Hassan Hamad Omar, aliyetaka kujua serikali imejiandaa vipi kuwa na vifaa vya uchunguzi katika Hospitali Chake Chake,

Akijibu suala hilo Waziri huyo alisema vifaa vya uchunguzi kwa ajili ya hospitali za Pemba hivi sasa zipo kwa kulingana na daraja za mashine hizo.

Akifafanua kauli hiyo alisema mashine aina ya X-ray,  na Utra Sound  ndizo ambazo hutakiwa kuwapo katika hosptali hizo kwa daraja lake na mashine ya CT- Scan hutakiwa kuwepo katika hospitali ya Rufaa. Kutokana na hali hiyo waziri huyo, alisema hivi sasa vifaa hivyo vipo katika hospitali hizo kulingana na daraja zinazotakiwa kimatibabu.

Wajumbe waikataa ripoti ya serikali

BAADHI ya Wajumbe wa baraza la wawakilishi jana wameikataa ripoti ya serikali kuhusu baraza la Manispaa ya Mji wa Zanzibar kutokana na ripoti kushindwa kukidhi haja na makudio ya uchunguzi.

Wajumbe hao wamesema sababu kubwa ya kuikataa ripoti hiyo ni kutokana na kushindwa kutoa maelezo yanayojitosheleza kwa wajumbe wa baraza hilo jamboa mbalo awali wajumbe hao waliomba kamati teule ya baraza la wawakilishi inudwe ili kuchunguza ubadhirifu uliofanyika katika baraza la manispaa.

Wakichangia katika kikao cha baraza la wawakilishi wajumbe hao walisema ripoti iliyowasilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Mwinyihaji Makame Mwadini imeshindwa kutoa maelezo ya kutosha juu ya ubadhirifu mkubwa uliofanyika katika baraza hilo.

Walisema ripoti iliyowasilishwa imeleelea mambo mengine na haijagusia suala la ubadhirifu na upotevu wa fedha uliofanyika wakati wajumbe walikuwa na hamu ya kutaka kujua fedha za serikali zinavyotumiwa vibaya na kutaka kuwajua wahusika wa upotevu huo.

Omar Ali Shehe Mwakilishi wa Jimbo la Chake Chake (CUF) alisema Serikali imewatupotezea muda wajumbe wakisubiri ripoti hiyo lakini kilicholetwa mbele ya wajumbe hao hakiendani kabisa kilichokuwa kikitakiwa na baraza hilo.

“Mheshimiwa Spika serikali imetupotezea muda bure …na ripoti hii tunaikataa na hivi ndio serikali inavyoshindwa kufanya kazi na hili tulisema mapema kwamba haiwezekani serikali ifanye manyago halafu ijichunguze wenyewe na tukaomba kamati teule iundwe ili kuchunguza haya lakini leo tunaletewa urojo” alisema Mwakilishi huyo.

Akichangia ripoti hiyo Mwakilishi wa Jimbo la Kitope (CCM) Makame Mshimba Mbarouk aliwaomba wajumbe wenzake kutoipokea ripoti hiyo kutokana na kuwa serikali imefanya mchezo na sio kuchunguza suala zima la ubadhifiru wa fedha.

“ Rais leo ndio atajua kuwa hana watendaji kutokana na ripoti hii,  Mheshimiwa suala hili hatukubali hata siku moja ripoti haina kichwa wala miguu tunasema ripoti hii hatuitaki ifanywe tena uchunguzi” alisema Mshimba kwa hisia kali.

Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani (CUF) Hija Hassan Hija alisikitiswa na serikali ilivyopoteza muda wa wajumbe hao na baadae kuwasilishia ripoti ambayo haina maana kwa taifa.

“Serikali tuliituma itufanyie utafiti na ichunguze upotevu wa fedha za umma leo tunaletwa hadithi badala ya ripoti kamili ya ubadhirifu .. hivi aliagizwa atuletee upotevu wa fedha au aliagizwa ametuletea masuala ya karo,  serikali za mitaa na mambo mengine, Mheshimiwa Spika kweli tupo serious sisi” alihoji Hija.

Aidha Mwakilishi huyo alisema ni jambo la kusikitisha kuona mpaka leo serikali ya aamu ya saba bado inaendeleza mchezo na watendaji badala ya kuchukuliwa hatua waliovunja sheria bado wanapewa muda wa kujirekebisha wakati sheria inasema anayevunja sheria achukuliwe hatua za kisheria.

“Naomba wachunguzwe katika hili iundwe kamati teule uchunguze maana tumeshaona haiwezekani watu tumewaamini tuliowapa madaraka halafu wanatuletea mchezo, kumbe muda wote ule Mheshimiwa Waziri aliochelewa kutuletea ripoti kumbe alikuwa akichakachua na wala asidhani kuwa wawakilshi ni wapumbavu kiasi kicho kweli hatukusoma lakini tumejifunza” alisema kwa hasira Mwakilishi huyo.

Mwakilishi huyo wa Kiwani aliongeza kusema kwamba “Leo mwakilishi akatoke hapa awapelekee wananchi wake ni aibu mheshimiwa Spika, sheria inavunjwa halafu tunaambiwa kwamba kuanzia sasa usifanye tena kosa wakati sheria zimetajwa katika sheria kwamba unayevunja sheria uchukuliwe hatua kisheria lakini leo, Waziri anatuletea hapa hadithi za kuwasamehe” alisema Mwakilishi huyo.

Naye Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF) Ismail Jussa Ladhu alianza kuikataa ripoti hiyo kabla ya kuichangia kama walivyofanya wajumbe wenzake wlaiomtangulia.

“Awali ya yote kwanza naikataa ripoti hii kama walivyoeleza wajumbe waliotangulia, Mheshimiwa msingi wa ripoti hii ni wajumbe kutoridhishwa na utendaji kazi wa Baraza la Manispaa na jinsi upotevu wa fedha, ukiukwaji wa sheria na uovu lakini badala ya kuletewa ripoti tunaletewa mambo ya serikali za mitaa heee” alisema Jussa na kuonesha kushangazwa na ripoti hiyo.

Jussa alisema waqjumbe wa baraza hilo hawajakataa kutaka serikali za mitaa lakini walichotaka kichunguzwe na wakaomba baraza la wawakilishi liunde kamati teule ili kuchunguza mambo na vitendo viilivyofanyika katika baraza hilo la manispaa lakini serikali ilikubali kubeba dhima ya kuunda tume lakini matokeo yake badala ya kuwasilishwa ripoti waziri amekuja na mashairi.

“Sisi tulitaka ripoti lakini sijui niite jina gani sina jina la kuiita Mheshimiwa Spika maana inasikitisha…..ahhhhh” alisema akionesha huzuni.

Alisema Juni 2011 wakati wa michango yote ya wajumbe wa baraza la wawakilishi waliligusa baraza la manispaa na walitaka hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika waliendesha vitendo vya ubadhirifu wa fedha lakini matokeo yake serikali ilikuja na lugha nzuri ya kuwaomba wajumbe wakubali kuundwa tume ya serikali.

“Baada ya serikali kutuomba tuwaachie wafanya wao uchunguzi, Mheshimiwa Spika tuliiamini serikali ikaunda tume lakini badala yake imetuleta habari za mageuzi wa serikali za mitaa, haya hayakhusu hapa ingawa tunayataka lakini tulikuwa tunataka utaratibu wa upotevu wa fedha na waliohusika” alisema Jussa.

Wafungwa kupewa mlo mara tatu

SERIKALI imesema imeanzisha utaratibu wa kuwalisha wanafunzi wa vyuo vya mafunzo (mahabusu) milo mitatu kwa siku baada ya kuongezewa bajeti ya serikali  katika vyuo hivyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Mwinyihaji Makame Mwadini aliwaambiwa wajumbe wa baraza la wawakilishi alipokuwa akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni (CCM) Jaku Hashim Ayoub aliyetaka kujua ni sababu gani zinazopelekea wanafunzi hao kulishwa mlo mmoja kwa siku.

Alisema katika mwaka wa fedha wa 2012/2013 serikali imeamua kuwapatia chakula mara tatu kwa siku baada ya kuongezewa bajeti hiyo kwa vyuo hivyo.

Waziri huyo alisema serikali kupitia vyuo vya mafunzo inahitaji kuhakikisha kwamba wanafunzi waliomo ndani ya vyuo hivyo wanapata chakula kilicho bora.

Alisema katika baadhi ya siku wanafunzi hao hupewa nyama na samaki hususan katika siku za sikukuu mbali mbali zinazosherehekewa hapa nchini.

Akijibu suali lililoulizwa kuwa ni kiasi gani katika bajeti kilichotengwa kwa ajili ya wafungwa hao, Waziri alisema kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012, serikali imepanga kutumia jumla ya shilingi 400, 480,000 kwa bajeti ya chakula kwa wanafunzi wa vyuo vya mafunzo.

Alisema Serikali imekamilisha ujenzi wa vyoo vya kutumia sink katika vyuo vya mafunzo vya Kangagani na Tungamaa kwa upande wa Pemba.

Akitaja kwa upande wa Unguja, Waziri alisema Langoni na Kinumoshi na sehemu ya wanawake katika chuo cha mafunzo cha Kiinua Miguu nayo pia vimejengwa vyoo vya aina hiyo ambapo kazi ya kuendeleza ujenzi wa vyoo katika vyuo vilivyobaki inaendelea.

Awali Mwakilishi huyo aliwakumbusha wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba ripoti za haki za binaadamu na utawala bora ya mwaka 2007/2008 hapa Zanzibar imebainisha kuwa wafungwa wamekuwa wakipewa mlo mmoja badala ya kupewa milo mitatu kwa siku.

Mapambano ya Malaria

WIZARA ya Afya Zanzibar imesema imekuwa ikitumia dawa mchanganyiko za Artesunate na Amodiqune kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa malaria nchini ambapo kwa kiasi kikubwa imesaidia kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo.

Waziri wa Afya, Juma Duni Haji aliwaambia wajumbe w abaraza la wawakilishi jana alipokuwa akijibu suali la Mwakilishi wa Jimbo la Ziwani (CUF) Rashid Seif Suleiman aliyataka kujua dawa gani zinazotumika kutibu malaria kwa uhakika katika maeneo ya Zanzibar.

Akijibu kiwango gani cha imechangia kuwepo kwa malaria, Waziri Duni alisema kiwango cha ongezeko la ugonjwa wa malaria iliripotiwa katika wiki ya 47 ya mwaka 2011.

Alisema wastani wa wagonjwa wane waliriputiwa wiki ya 46 mwaka 2011 wastani wa wagonjwa 17 hadi 63 waliripotiwa kwa wiki ya 47 ya mwaka 2011 ambapo wiki ya tano ya mwezi wa febuari mwaka 2012.

Awali Mwakilishi huyo alisema pamoja na mafanikio ya jitihada za kupambana na malaria inaonekana bado kuna dalili za kuibuka kwa kasi kwa malaria katika baadhi ya maeneo na kutaka kujua ni maeneo gani ambayo yamegundulika kuwa na idadi kubwa ya malaria.

Akijibu suali hilo Waziri Duni alisema maeneo ambayo yaligundulika kuwa na ongezeko la wagonjwa wa malaria ni pamoja na Micheweni katika kijiji cha Tumbe, Msuka Makangale, Konde, Kinyasini, Sumba viamboni na Kiuyu.

Maeneo mengine ambayo Waziri huyo ameyataja ni Kipangani, Mkia wa Ngombe, na katika wilaya ya chake chake ni katika vijiji vya Ziwani, Mkoani na Wambaa.

Sehemu nyengine ambayo imegundulika kuwa na wagonjwa wa malaria ni katika wilaya ya Wete katika vijiji vya Junguni, Ukinjwi, na wilaya ya Kaskazini B Unguja ni Donge Mchangani, Donge Vijibweni, Bumwini na Zingwezingwe.

Katika wilaya ya kati Waziri huyo alizitaja sehemu zenye wagonjwa waliogundulika na malaria ni pamoja na vijiji vya Jendele, Uzini na Mchangani.

Dini aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba serikali imefanya juhudi kubwa kutokomeza malaria Zanzibar na sasa imepungua chini ya silimia moja ambapo bado juhudi zaidi zinahitajika katika kutokomeza ugonjwa huo.

Aliwaomba wajumbe wa baraza hilo kuisaidia serikali katika juhudi zake za kupiga vita ugonjwa huo kwani ni ugonjwa hatari ambao unahitaji kutokomezwa kabisa nchini ili usirejee tena.

Wakati huo huo Waziri Duni alisema alisema ujenzi wa Chake Chake katika wodi ya kuzalia ilijumuisha wodi mbili, moja kabla nay a baada ya pili baada ya kujifungua.

Alisema kuna chumba cha kuzalia ambacho kimetengwa kidogo na wodi nyengine kwa madhumuni ya kuwapatia utulivu akina mama ili waweze kupima maendeleo ya uchungu na hatimae kujifungua.

Alisema hospitali ya Chake Chake iko katika mipango ya kuifanyia marekebisho na wizara baada ya kuliona hilo na serikali itahakikisha kuifanyia marekebisho sehemu hiyo ili baadae kupatikana faragha na stara ya akina mama wanaojifungua.

Mwakilishi wa Nafasi za Wanawake (CCM) Panya Ali Aballah alisema hospitali ya Chake Chake katika eneo la kujifungulia hakuna stara na hata asiyehusika anaweza kupita na akaona shughuli zote za uzalishaji zinavyokwenda ambapo alitaka kujua serikali ina mpango gani katika hilo.

Hali ya kiwanja cha ndege

 

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema wataalamu kutoka Afika Kusini wameshafanya utafiti wa uwekaji wa taa za njia ya kutulia katika kiwanja cha Kisiwani Pemba.

Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Issa Haji Gavu wakati akijibu swali la msingi la Mwakilishi wa Jimbo la Ziwani (CUF) Rashid Seif Suleiman aliyetaka kujua serikali imefikia wapi katika suala la utengenezaji wa kiwanja cha ndege ya Pemba.

Alisema tayari wataalamu hao wameshafanya utafuti juu ya uwekaji wa taa za njia za kutulia ndege na kurukia (runway) na serikali hivi asa inasubiri taarifa yao ili iweze kuendelea na hatua ya utekelezaji.

“Hatua hii itakifanya kiwanja chetu cha Pemba kutua na kurukia ndege wakati wowote usiku na mchana” alisema Naibu huyo.

Alisema hatua ya kutafuta jenerata la dharura (standby generator) ya uwezo wa KVA nazo zimeanza.

Akijibu suali la Mwakilishi huyo aliyataka kujua  makisio ya ukarabati Gavu alisema majengo hivi sasa ambayo yatagharimu kiasi cha shilingi  2.75 millioni ambayo yameshafanywa na serikali inasubiri upatikanaji wa fedha ili kazi hiyo iweze kuanza.

Alisema trekta la kukatia majani kiwanjani hapo ambalo kwa muda mrefu lilishindwa kufanya kazi kutokana na ubovu wake lakini sasa limeshafanyiwa matengenezo na litaanza shughuli za ukataji wa majani wakati wowote kuanzia sasa baada ya matengenezo hayo.

Awali Mwakilishi huyo alisema kiwanja cha ndege Pemba kinasikitisha kutokana na hali yake ilivyo, Naibu Waziri alisema katika juhudi za kukifanya kiwanja hicho kuwa ni cha kisasa serikali kwa ujumla kupitia wizara yake ya miundo mbinu na mawasiliano na mamlaka ya viwanja vya ndege ina juhudi maalumu za kuhakikisha inakitengeneza kiwanja hicho.

Akitaja juhudi hizo ni kuweka mfumo kamili wa umeme (generator) utakaotumika endapo umeme wa line kubwa utakatika na kujenga jingo jipya la abiria la kisasa (new passenger terminal) kukidhi matumaini makubwa ya kiwanja hicho.

Juhudi nyengine ni kuongeza urefu wa njia ya kurukia (runway) kutoka mita 1550 hadi mita 1850 ambapo ndege kubwa zaidi zitaweza kutua na kuruka ambapo hatua nyengine alizitaja ni kupata wafadhili ama kwa mkopo nafuu au njia nyengine muafaka ili serikali iweze kutekeleza mradi huo muhimu wa maendeleo ya wananchi.

 

 

Advertisements

3 responses to “Spika akerwa na uzembe barazani

  1. Nimefurahi kuona Falsafa ya kujivua Gamba inanyemelea kuingia Barazani. Speaker Kificho kuwa mkali sasa ni vizuri lakni amechelewa mno. Ukiritimba katika Baraza ndio unaochangia hili. Wawakilishi lazima waendelee kufanya hivyo kwa kuwa wapiga kura wao wako busy wakiuliza habari za kifo cha Kanumba kana kwamba huyu Kanumba ni wa Mwanzo kuonja mauti. Katika hali hii ya kuwa na Wapiga kura ambao hawakuelimika au wamelimika kidogo wanasisa lazima wafanye watakavyo. Watachelewa ripoti na watafanya makubwa zaidi madamu tu ni watawala na hakuna wa kuuliza. Tokea Baraza hili lianze tunaona tuu watu wakizungumza kwa jazba lakini mwisho huwa kama povu la soda!. Kulikuwa na habari ya Bahari na Tibaijuka, Ripoti ya Manispaa na njyenginezo kisha kimyaa! Mheshimiwa Speaker asijali watu wanaoangalia Baraza hawashi wala hawazimi! Wengi wao husubiri mtu fulani atajwe wagune au wapige makofi. Chuki na na ubinafsi ndio imani zao, ibada zao na Muungu wao, ingawa misikitini wanaabudia Mungu moja na kumtaka awaonyooshe njia iliyonyooka njia ya wale ambao hawakughabikiwa wala kupotea! Watu wanawwangalia ni akina wanaoamini Faslafa ya Kanisa Kkabla kuja Galileleo na nadharia iliyozua kizaa zaa Ulaya katika karne hizo za kiza. Kiasi akina Wenyeviti wa Kamati wa wafanye watakavyo kwa kuwa hata vyama vyao havina nguvu za kuwawajibisha na vikijaribu Mahkama huingilia kati ikahalalisha batili kama ilivyo genesis yake. Hakuna wa kuhoji hili. Tulifikiri katiba mpya ya Jamhuri itatoa fursa ya kutokea mabiliko lakini wapi – Terms of Reference are in place to guide the commission. How can a person set guidelines kwa namna watu watakavyosema vipi mahusiano ya watawala na watawaliwa yawe. Kama majibu ya Mchakato wa Katiba yapo ni Kwani Rais aunde Tume kukusanya maoni ! ivi twaelekea wapi !

  2. HIYO TUME YA KIWETE HAINA MAANA YOYOTE NA KATIBA ITAKAYOTOKA HAPO SIO YA WANANCHI BALI NI YA KIWETE. INAKUAJE ANAANZA KUIEKEA MIPAKA LIPI LIJADILIWE NA LIPI LISIJADILIWE. KWA MAONI YANGU NAHISI KUA MCHAKATO MZIMA UNALAZIMISHWA UFUATE MKONDO WA MATAKWA YA CCM YA KUBAKIA NA MUUNGANO HUU MBOVU AMBAO WAZANZIBARI KWA NAMNA ZOTE WAMEONYESHA KUA HAWAUTAKI. HATA RAISI KIWETE UKILAZIMISHA HIYO KATIBA YAKO UNAYOITAKA ITADUMU KWA MUDA MFUPI NA TATIZO LITARUDI PALEPALE. HAKUKUA NA HAJA YA KUPOTEZA MAMILIONI YA FEDHA ZA WATANZANIA KWA JAMBO AMBALO HALINA MASLAHI NA NCHI. WAACHWE WANANCHI WAZUNGUMZE CHOCHOTE KILE AMBACHO WAO WANAHISI HAKIKO SAWA BILA YA VIKWAZO TOKA KWA RAIS AU CCM NA HAPO NDIO KATIBA ITAKUA IMETOKANA NA WANANCHI VYENGINEVYO ITAKUA NI YA KIWETE NA CCM.

  3. HAWANA LOLOTE WOTE NI KIKUNDI CHA WALAJI WA HAKI ZA WATU TU. TUMEWAPA DHAMANA YA NCHI WANAIUZA REJAREJA HALAFU UTASIKIA WANAJIDAI KUPIGISHANA MAKELELE BARAZANI NA MWISHO WA SIKU NCHI INAUZWA REJAREJA. MFANO MZURI NI SAKATA LA SHAMHUNA NA BAHARI. TULITEGEMEA KUA WANGESIMAMA KIDETE LAKINI WAPI MILIONI 4 KWA MWEZI SIO MCHEZO.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s