Wajumbe waikataa ripoti ya serikali

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Dk Mwinyihaji Makame Mwadini

BAADHI ya Wajumbe wa baraza la wawakilishi jana wameikataa ripoti ya serikali kuhusu baraza la Manispaa ya Mji wa Zanzibar kutokana na ripoti kushindwa kukidhi haja na makudio ya uchunguzi. Wajumbe hao wamesema sababu kubwa ya kuikataa ripoti hiyo ni kutokana na kushindwa kutoa maelezo yanayojitosheleza kwa wajumbe wa baraza hilo jamboa mbalo awali wajumbe hao waliomba kamati teule ya baraza la wawakilishi inudwe ili kuchunguza ubadhirifu uliofanyika katika baraza la manispaa.

Wakichangia katika kikao cha baraza la wawakilishi wajumbe hao walisema ripoti iliyowasilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Mwinyihaji Makame Mwadini imeshindwa kutoa maelezo ya kutosha juu ya ubadhirifu mkubwa uliofanyika katika baraza hilo. Walisema ripoti iliyowasilishwa imeleelea mambo mengine na haijagusia suala la ubadhirifu na upotevu wa fedha uliofanyika wakati wajumbe walikuwa na hamu ya kutaka kujua fedha za serikali zinavyotumiwa vibaya na kutaka kuwajua wahusika wa upotevu huo.
Omar Ali Shehe Mwakilishi wa Jimbo la Chake Chake (CUF) alisema Serikali imewatupotezea muda wajumbe wakisubiri ripoti hiyo lakini kilicholetwa mbele ya wajumbe hao hakiendani kabisa kilichokuwa kikitakiwa na baraza hilo.
“Mheshimiwa Spika serikali imetupotezea muda bure …na ripoti hii tunaikataa na hivi ndio serikali inavyoshindwa kufanya kazi na hili tulisema mapema kwamba haiwezekani serikali ifanye manyago halafu ijichunguze wenyewe na tukaomba kamati teule iundwe ili kuchunguza haya lakini leo tunaletewa urojo” alisema Mwakilishi huyo.
Akichangia ripoti hiyo Mwakilishi wa Jimbo la Kitope (CCM) Makame Mshimba Mbarouk aliwaomba wajumbe wenzake kutoipokea ripoti hiyo kutokana na kuwa serikali imefanya mchezo na sio kuchunguza suala zima la ubadhifiru wa fedha.
“ Rais leo ndio atajua kuwa hana watendaji kutokana na ripoti hii, Mheshimiwa suala hili hatukubali hata siku moja ripoti haina kichwa wala miguu tunasema ripoti hii hatuitaki ifanywe tena uchunguzi” alisema Mshimba kwa hisia kali.
Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani (CUF) Hija Hassan Hija alisikitiswa na serikali ilivyopoteza muda wa wajumbe hao na baadae kuwasilishia ripoti ambayo haina maana kwa taifa.
“Serikali tuliituma itufanyie utafiti na ichunguze upotevu wa fedha za umma leo tunaletwa hadithi badala ya ripoti kamili ya ubadhirifu .. hivi aliagizwa atuletee upotevu wa fedha au aliagizwa ametuletea masuala ya karo, serikali za mitaa na mambo mengine, Mheshimiwa Spika kweli tupo serious sisi” alihoji Hija.
Aidha Mwakilishi huyo alisema ni jambo la kusikitisha kuona mpaka leo serikali ya aamu ya saba bado inaendeleza mchezo na watendaji badala ya kuchukuliwa hatua waliovunja sheria bado wanapewa muda wa kujirekebisha wakati sheria inasema anayevunja sheria achukuliwe hatua za kisheria.
“Naomba wachunguzwe katika hili iundwe kamati teule uchunguze maana tumeshaona haiwezekani watu tumewaamini tuliowapa madaraka halafu wanatuletea mchezo, kumbe muda wote ule Mheshimiwa Waziri aliochelewa kutuletea ripoti kumbe alikuwa akichakachua na wala asidhani kuwa wawakilshi ni wapumbavu kiasi kicho kweli hatukusoma lakini tumejifunza” alisema kwa hasira Mwakilishi huyo.
Mwakilishi huyo wa Kiwani aliongeza kusema kwamba “Leo mwakilishi akatoke hapa awapelekee wananchi wake ni aibu mheshimiwa Spika, sheria inavunjwa halafu tunaambiwa kwamba kuanzia sasa usifanye tena kosa wakati sheria zimetajwa katika sheria kwamba unayevunja sheria uchukuliwe hatua kisheria lakini leo, Waziri anatuletea hapa hadithi za kuwasamehe” alisema Mwakilishi huyo.
Naye Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF) Ismail Jussa Ladhu alianza kuikataa ripoti hiyo kabla ya kuichangia kama walivyofanya wajumbe wenzake wlaiomtangulia.
“Awali ya yote kwanza naikataa ripoti hii kama walivyoeleza wajumbe waliotangulia, Mheshimiwa msingi wa ripoti hii ni wajumbe kutoridhishwa na utendaji kazi wa Baraza la Manispaa na jinsi upotevu wa fedha, ukiukwaji wa sheria na uovu lakini badala ya kuletewa ripoti tunaletewa mambo ya serikali za mitaa heee” alisema Jussa na kuonesha kushangazwa na ripoti hiyo.
Jussa alisema waqjumbe wa baraza hilo hawajakataa kutaka serikali za mitaa lakini walichotaka kichunguzwe na wakaomba baraza la wawakilishi liunde kamati teule ili kuchunguza mambo na vitendo viilivyofanyika katika baraza hilo la manispaa lakini serikali ilikubali kubeba dhima ya kuunda tume lakini matokeo yake badala ya kuwasilishwa ripoti waziri amekuja na mashairi.
“Sisi tulitaka ripoti lakini sijui niite jina gani sina jina la kuiita Mheshimiwa Spika maana inasikitisha…..ahhhhh” alisema akionesha huzuni.
Alisema Juni 2011 wakati wa michango yote ya wajumbe wa baraza la wawakilishi waliligusa baraza la manispaa na walitaka hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika waliendesha vitendo vya ubadhirifu wa fedha lakini matokeo yake serikali ilikuja na lugha nzuri ya kuwaomba wajumbe wakubali kuundwa tume ya serikali.
“Baada ya serikali kutuomba tuwaachie wafanya wao uchunguzi, Mheshimiwa Spika tuliiamini serikali ikaunda tume lakini badala yake imetuleta habari za mageuzi wa serikali za mitaa, haya hayakhusu hapa ingawa tunayataka lakini tulikuwa tunataka utaratibu wa upotevu wa fedha na waliohusika” alisema Jussa.

MWISHO

MAHABURI KUPEWA MILO MITATU KWA SIKU

SERIKALI imesema imeanzisha utaratibu wa kuwalisha wanafunzi wa vyuo vya mafunzo (mahabusu) milo mitatu kwa siku baada ya kuongezewa bajeti ya serikali katika vyuo hivyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Mwinyihaji Makame Mwadini aliwaambiwa wajumbe wa baraza la wawakilishi alipokuwa akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni (CCM) Jaku Hashim Ayoub aliyetaka kujua ni sababu gani zinazopelekea wanafunzi hao kulishwa mlo mmoja kwa siku.
Alisema katika mwaka wa fedha wa 2012/2013 serikali imeamua kuwapatia chakula mara tatu kwa siku baada ya kuongezewa bajeti hiyo kwa vyuo hivyo.
Waziri huyo alisema serikali kupitia vyuo vya mafunzo inahitaji kuhakikisha kwamba wanafunzi waliomo ndani ya vyuo hivyo wanapata chakula kilicho bora.
Alisema katika baadhi ya siku wanafunzi hao hupewa nyama na samaki hususan katika siku za sikukuu mbali mbali zinazosherehekewa hapa nchini.
Akijibu suali lililoulizwa kuwa ni kiasi gani katika bajeti kilichotengwa kwa ajili ya wafungwa hao, Waziri alisema kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012, serikali imepanga kutumia jumla ya shilingi 400, 480,000 kwa bajeti ya chakula kwa wanafunzi wa vyuo vya mafunzo.
Alisema Serikali imekamilisha ujenzi wa vyoo vya kutumia sink katika vyuo vya mafunzo vya Kangagani na Tungamaa kwa upande wa Pemba.
Akitaja kwa upande wa Unguja, Waziri alisema Langoni na Kinumoshi na sehemu ya wanawake katika chuo cha mafunzo cha Kiinua Miguu nayo pia vimejengwa vyoo vya aina hiyo ambapo kazi ya kuendeleza ujenzi wa vyoo katika vyuo vilivyobaki inaendelea.
Awali Mwakilishi huyo aliwakumbusha wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba ripoti za haki za binaadamu na utawala bora ya mwaka 2007/2008 hapa Zanzibar imebainisha kuwa wafungwa wamekuwa wakipewa mlo mmoja badala ya kupewa milo mitatu kwa siku.

MWISHO
MAPAMBANO YA MALARIA

WIZARA ya Afya Zanzibar imesema imekuwa ikitumia dawa mchanganyiko za Artesunate na Amodiqune kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa malaria nchini ambapo kwa kiasi kikubwa imesaidia kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo.

Waziri wa Afya, Juma Duni Haji aliwaambia wajumbe w abaraza la wawakilishi jana alipokuwa akijibu suali la Mwakilishi wa Jimbo la Ziwani (CUF) Rashid Seif Suleiman aliyataka kujua dawa gani zinazotumika kutibu malaria kwa uhakika katika maeneo ya Zanzibar.

Akijibu kiwango gani cha imechangia kuwepo kwa malaria, Waziri Duni alisema kiwango cha ongezeko la ugonjwa wa malaria iliripotiwa katika wiki ya 47 ya mwaka 2011.
Alisema wastani wa wagonjwa wane waliriputiwa wiki ya 46 mwaka 2011 wastani wa wagonjwa 17 hadi 63 waliripotiwa kwa wiki ya 47 ya mwaka 2011 ambapo wiki ya tano ya mwezi wa febuari mwaka 2012.

Awali Mwakilishi huyo alisema pamoja na mafanikio ya jitihada za kupambana na malaria inaonekana bado kuna dalili za kuibuka kwa kasi kwa malaria katika baadhi ya maeneo na kutaka kujua ni maeneo gani ambayo yamegundulika kuwa na idadi kubwa ya malaria.

Akijibu suali hilo Waziri Duni alisema maeneo ambayo yaligundulika kuwa na ongezeko la wagonjwa wa malaria ni pamoja na Micheweni katika kijiji cha Tumbe, Msuka Makangale, Konde, Kinyasini, Sumba viamboni na Kiuyu.

Maeneo mengine ambayo Waziri huyo ameyataja ni Kipangani, Mkia wa Ngombe, na katika wilaya ya chake chake ni katika vijiji vya Ziwani, Mkoani na Wambaa.
Sehemu nyengine ambayo imegundulika kuwa na wagonjwa wa malaria ni katika wilaya ya Wete katika vijiji vya Junguni, Ukinjwi, na wilaya ya Kaskazini B Unguja ni Donge Mchangani, Donge Vijibweni, Bumwini na Zingwezingwe.

Katika wilaya ya kati Waziri huyo alizitaja sehemu zenye wagonjwa waliogundulika na malaria ni pamoja na vijiji vya Jendele, Uzini na Mchangani.
Dini aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba serikali imefanya juhudi kubwa kutokomeza malaria Zanzibar na sasa imepungua chini ya silimia moja ambapo bado juhudi zaidi zinahitajika katika kutokomeza ugonjwa huo.

Aliwaomba wajumbe wa baraza hilo kuisaidia serikali katika juhudi zake za kupiga vita ugonjwa huo kwani ni ugonjwa hatari ambao unahitaji kutokomezwa kabisa nchini ili usirejee tena.  Wakati huo huo Waziri Duni alisema alisema ujenzi wa Chake Chake

katika wodi ya kuzalia ilijumuisha wodi mbili, moja kabla nay a baada ya pili baada ya kujifungua.
Alisema kuna chumba cha kuzalia ambacho kimetengwa kidogo na wodi nyengine kwa madhumuni ya kuwapatia utulivu akina mama ili waweze kupima maendeleo ya uchungu na hatimae kujifungua.

Alisema hospitali ya Chake Chake iko katika mipango ya kuifanyia marekebisho na wizara baada ya kuliona hilo na serikali itahakikisha kuifanyia marekebisho sehemu hiyo ili baadae kupatikana faragha na stara ya akina mama wanaojifungua.

Mwakilishi wa Nafasi za Wanawake (CCM) Panya Ali Aballah alisema hospitali ya Chake Chake katika eneo la kujifungulia hakuna stara na hata asiyehusika anaweza kupita na akaona shughuli zote za uzalishaji zinavyokwenda ambapo alitaka kujua serikali ina mpango gani katika hilo.

MWISHO
Hali ya kiwanja cha ndege

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema wataalamu kutoka Afika Kusini wameshafanya utafiti wa uwekaji wa taa za njia ya kutulia katika kiwanja cha Kisiwani Pemba.
Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Issa Haji Gavu wakati akijibu swali la msingi la Mwakilishi wa Jimbo la Ziwani (CUF) Rashid Seif Suleiman aliyetaka kujua serikali imefikia wapi katika suala la utengenezaji wa kiwanja cha ndege ya Pemba.

Alisema tayari wataalamu hao wameshafanya utafuti juu ya uwekaji wa taa za njia za kutulia ndege na kurukia (runway) na serikali hivi asa inasubiri taarifa yao ili iweze kuendelea na hatua ya utekelezaji.

“Hatua hii itakifanya kiwanja chetu cha Pemba kutua na kurukia ndege wakati wowote usiku na mchana” alisema Naibu huyo. Alisema hatua ya kutafuta jenerata la dharura (standby generator) ya uwezo wa KVA nazo zimeanza.

Akijibu suali la Mwakilishi huyo aliyataka kujua makisio ya ukarabati Gavu alisema majengo hivi sasa ambayo yatagharimu kiasi cha shilingi 2.75 millioni ambayo yameshafanywa na serikali inasubiri upatikanaji wa fedha ili kazi hiyo iweze kuanza.

Alisema trekta la kukatia majani kiwanjani hapo ambalo kwa muda mrefu lilishindwa kufanya kazi kutokana na ubovu wake lakini sasa limeshafanyiwa matengenezo na litaanza shughuli za ukataji wa majani wakati wowote kuanzia sasa baada ya matengenezo hayo.

Awali Mwakilishi huyo alisema kiwanja cha ndege Pemba kinasikitisha kutokana na hali yake ilivyo, Naibu Waziri alisema katika juhudi za kukifanya kiwanja hicho kuwa ni cha kisasa serikali kwa ujumla kupitia wizara yake ya miundo mbinu na mawasiliano na mamlaka ya viwanja vya ndege ina juhudi maalumu za kuhakikisha inakitengeneza kiwanja hicho.

Akitaja juhudi hizo ni kuweka mfumo kamili wa umeme (generator) utakaotumika endapo umeme wa line kubwa utakatika na kujenga jingo jipya la abiria la kisasa (new passenger terminal) kukidhi matumaini makubwa ya kiwanja hicho.

Juhudi nyengine ni kuongeza urefu wa njia ya kurukia (runway) kutoka mita 1550 hadi mita 1850 ambapo ndege kubwa zaidi zitaweza kutua na kuruka ambapo hatua nyengine alizitaja ni kupata wafadhili ama kwa mkopo nafuu au njia nyengine muafaka ili serikali iweze kutekeleza mradi huo muhimu wa maendeleo ya wananchi.

 

Advertisements

2 responses to “Wajumbe waikataa ripoti ya serikali

  1. Jamani eheee! Mengine nkinehe! Nani asiyejua kuwa manispaa kumeoza Dr mwinyi haji taire! Huwezi kinga maji kwa kutumia pakacha! Ukweli ni Nuru hukuonesha njia! . Mr Duni hongera malaria yapo! Huo ndio ukweli ! Yataendelea kuwapo mazingira bado ni machafu! Gavu hongera pemba nayo ni sehemu yenye binaadam , kunahitajika huduma bora ili kutononesha uchumi wa watu wake! Wazanzibar tunahitaji mabadiliko yatotupatia uhuru wa kweli ! Zanzibar kwanza ! Vyama baadae!

  2. Jibu la Manispaa ni Serikali kukubali kurejesha mfumo wa Utawala ma Majimbo. Haiwezekani kabisa kwa Mambo ya Manispaa yaamuliwe Wizarani. Jamani tuwe wakweli. Mambo haya ya Waminki- mau Pau hayafai tena!

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s