Imani ya wazanzibari kwa serikali yao imeingia dosari

Mwakilishi wa Mji Mkongwe (CUF) Ismail Jussa Ladhu

Na Ally Saleh

Wiki iliyopita faida ya teknolojia ilionekana wazi wazi kwa Wazanzibari na ile dhana ya uwazi ikawa ina maana halisi kwao, maana kwa kweli kila kitu kilikuwa wazi kwao. Safi kabisa bila mizengwe. Kilichokuwa safi bila mizengwe ni mjadala juu ya mabadiliko ya Sheria ya Utalii ambayo yalikuwa yamefikishwa Baraza la Wawakilishi  katika kuiimarisha sekta hiyo  kisheria kwa vile kwa sasa sekta hiyo inaitwa Sekta Kiongozi na kiongozi kwa ajira na mapato.

 

Na hivi karibuni pia Sekta ya Utalii imepewa bango jipya ambapo ingawa bado halijaenea lakini angalau katika rubaa za juu limeanza kutumiwa nalo ni lile la Utalii kwa Wote ambapo mabadiliko hayo pia yalilenga hilo.

Utalii ni sekta ambayo ilianza kuchapuka katika mwaka 1986 pale Serikali ya Zanzibar ilipopitishwa Sheria ya Uwekezaji Vitega Uchumi na eneo hilo likadakwa haraka haraka na wawekezaji hasa kutoka nje na hasa kutoka Italia ambako Serikali ya Zanzibar ilikwenda kufanya mipango maalum kuwashawishi.

Mongo mitatu baadae sekta hiyo inashindana na Serikali katika ajira, zikiwa ni ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja na inachangia karibu asilimia 80 ya mapato ya Serikali hivi sasa.

Sekta za ujenzi, usafiri wa baharini na nchi kavu, barabara na simu  zote zimeimarika kwa sababu ya kukidhi mahitaji ya utalii. Kutoka hoteli mbili au tatu zilizokuwepo mwaka 1986 sasa Zanzibar inajivunia zaidi ya 100 za kiwango cha nyota tatu, nne hadi tano.

Kutoka wakati ambapo wageni wote walikuwa wakifikia Dar es salaam au Nairobi sasa ndege kadhaa kubwa zinakuja moja kwa moja hadi Zanzibar na upanuzi wa uwanja wa ndege umekuwa kipaumbele kikubwa kwa Serikali kukidhi haja ya watalii zaidi.

Inakisiwa kuwa sasa watalii karibu 180,000 wanaingia hapa Zanzibar kwa mwaka na karibu thuluthi mbili lazima wapiti Mji Mkongwe na huku pia mbinu  zikifanywa kuvumbua vyanzo vipya vya vivutio ili kuleta watalii zaidi ingawa pia kuna hoja ni kiasi gani cha watalii kinatosha kwa Zanzibar bila ya kushindana na rasilmali.

Pia kuna mjadala mkubwa unaoendelea miongoni mwetu Wazanzibari juu ya nafasi yetu katika sekta hiyo ambayo kwa hakika haionekana na haina athari yoyote ile na hiyo ni tokea sababu za kisera, za kifedha na pia zile za kisheria.

Sheria na sera zetu hazimlindi mwenye nchi Mzanzibari ambaye anatambuliwa kuwepo kikatiba kabisa ndani ya nchi yake na ni yeye mwenye kutakiwa kumiliki uchumi wa nchi yake kwa njia zozote zile.

Ikifika wakati uchumi wa nchi unamilikiwa na wageni, basi sio tu nchi inakuwa rehani kwa uhuru  wake bali pia wananchi wake wanakuwa watumwa kwa wageni na nchi inakuwa ikiendeshwa na nguvu za makampuni ya kimataifa. Na taifa hilo linakuwa limeoza.

Kilio ambacho kiko wazi na wakati wote ni kile cha ajira. Ajira imekuwa ngumu kwa Wazanzibar na ilhali kila uchao ndivyo inavyozidi kuwa ngumu kwa mambo ambayo yana ukweli na mengine hayana ukweli hata kidogo.

Yasio na ukweli ni yale ya kusema kuwa Wazanzibari wavivu au Wazanzibari hawaishi dharura yaani maziko na harusi. Hili limetumiwa dhidi yetu na kwa kuwa tumelikubali basi limeganda hata katika akili zetu na matokeo yake ni kwamba kijana wa Kizanzibari anakosa mtetezi katika ajira ndani ya nchi yake mwenyewe.

Pili, ni kusema kuwa Wazanzibari hawana elimu. Hili liko namna mbili. Lipo lile la kwamba vijana wetu wanaosoma katika Chuo cha Utalii hawapati elimu ya kutosha ya ushindani na wenzao kutoka vyuo vya Kenya na Tanzania Bara lakini pili elimu yetu ya shule za kawaida haitoi vijana wanaoweza kusomesheka au kufanya kazi za kitalii.

Mimi nimekuwa mpinzani wa dhana zote mbili. Siamini kuwa sisi ni wavivu na kama dhana ni hiyo basi ni rahisi kutengeneza progamu ya kubadilisha mawazo hayo. Siamini kuwa Chuo cha Maruhubi kinatoa pumba isioajirika na kama hivyo ni rahisi kufanya mabadiliko kwa sababu sekta hii inachangia chuo na ni wadau. Na wala siamini kuwa wanafunzi wetu ni dhaifu kuwa hawawezi kusomesheka kinachoweza kufanywa ni kuwasomesha kwa mwelekeo wa sekta ndani ya kazi.

Mfano wa kusomesha ndani ya kazi nimeuona hivi karibuni katika Hoteli ya Residency ambako wamefungua academia inaotoa mafunzo kwa wafanyakazi wakiwa ndani ya kazi ili wafikie katika kiwango cha kuhudumia wageni wao. Hii inapaswa kuigwa na kutiwa moyo na Serikali.

Lakini hali ikiwa hivyo wiki iliyopita na kuonekana moja kwa moja na wananchi pale Baraza la Wawakilishi lilipokuwa likijadili Sheria ya Utalii kuonekana kushindwa kulinda maslahi ya ajira kwa Wazanzibari, ambapo Sera ya CCM inayoendesha nchi inasema kuwa itaongeza ajira kwa vijana.

Ila katika hilo ikatisha umma kwa kuwa pia Wawakilishi wa CUF nao pia walishiriki kupiga kura kumlinda Mzanzibari katika ajira kwenye nchi yake ilhali pia Sera ya CUF ingawa haina nafasi Serikalini lakini pia inasema kuwa ajira kwa vijana ni jambo la msingi kwao.

Kwani ilikuwaje? Kifungu kimoja katika Sheria ya Utalii iliokuwa Barazani kilikuwa kikitoa sharti kuwa mtu yoyote au kampuni ambayo imo kwenye sekta ya utalii itapaswa kumpa umuhimu  wa kwanza Mtanzania katika utoaji wa ajira. Mwakilishi wa Mji Mkongwe Ismail Jussa akatoa hoja kuwa neno Mtanzania lifutwe na badala yake liandikwe Mzanzibari ili kuhakikisha Mzanzibari ndie anaefaidika kwanza kwenye ajira isipokuwa mtu mwenye sifa inayotakiwa iwe hakupatikana.

Ukazuka mjadala mkubwa na huku upande wa Serikali ukijaribu kutetea Muswada wake na mwisho ikalazimika kupiga kura ambapo mara ya kwanza wengi  walitaka kifungu  hicho kiseme kinamlinda Mzanzibari lakini kwa kuwa palikuwa na utata kura ikarudiwa na matakwa ya Serikali yakabakia kwa kifungu kusema ajira ilindwe kwa Mtanzania.

Hili kwa hakika limedhaisha umma. Umma hauamini kuwa Baraza la Wawakilishi limejificha kwenye visingizio kadhaa na Serikali kujikita kulinda Muswada wake na hivyo kusahau kuwa umma ndio uliopiga kura kwa matumaini kuwa utapata matunda kikamilifu kutoka Serikali yao.

Toka hapo Serikali haijatimiza ahadi yake ya kutengeza ajira, bali pia inazipeperusha chache ambazo zinaweza kuwafikia Wazanzibari. Kwa hakika sijafikiria vipi niishauri Serikali katika hili ila ninachoweza kusema imewakosea sana Wazanzibari na imani yao imeingia dosari.

Hatua za haraka zichukuliwe kurudisha imani hiyo. Serikali ya Kitaifa ilitarajiwa iwe ni nguzo ya kutetea haki za Wazanzibari ambapo si kosa wala si ubaguzi  kumuweka mbele Mzanzibari, maana ndio mkaazi mkuu wa Zanzibar na yeye ndi afaidike kwanza si tu kwa rasilmali lakini pia kwa ajira.

Mitaani suali ni jee, kama hili Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeweza kwenda na Muswada kama huu Barazani, jee makubwa zaidi itaweza kusimama upande wa wananchi? Waswahili walisema kuambizana kuko kusikilizana ni hiari.

Napenda kuwaarifu wasomaji wa safu hii ya Hoja kutoka Zanzibar, kwamba hii yaweza kuwa makala yangu ya mwisho kwa vile natarajia kula kiapo Ijumaa hii kuwa Kamishna katika Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba kazi ambayo nitakuwa ndani humo kwa miezi18.

Nawashukuru kwa kuwa nami muda wa zaidi ya miaka mitano.


Advertisements

12 responses to “Imani ya wazanzibari kwa serikali yao imeingia dosari

 1. Assalam alikum!
  Kwanza shukran ndugu Ally Saleh, na haya ni nyongeza tu ya hayo ulioyaweka wazi hapa.
  Wazanzibar wote! Napenda kutoa ushauri kidogo katika suala hili la KATIBA ambalo limetuelekea, kwani hili nathubutu ni letu sisi Wazanzibar kuliko hata Watanganyika maana wao sasa wanataka tu nyongeza ya faida katika hili la katiba.
  Nawatabahisheni Wazalendo wa Jamhuri tukufu ya Zanzibar kuwa mchakato huu wa katika unaokusudiwa na Watanganyika tayari umashatutia sisi Wazanzibar kaitka mtego waliokusudia, na yote hii imetokana na UBUBU wa Wawakilishi wetu wote BLW na BUNGE kushindwa kuitetea Zanzibar kisheria na hoja wakiongozwa na Serikali hii ya Umoja wa kitaifa nayo kueka chonjo majukumu yake.
  Hapa nataka niweke wazi pamoja na juhudi za wazi za makundi mbalimbali yanatoa elimu ya mchakato wa katiba lakini yajuwe kuwa uhalali wa kisheria ya mabadiliko ya katiba hakuna kuuajdili muungano kwa nia ya kuuvunja au kuubadilisha muundo wake ila ni kuuimarisha zaid ikiwa na maana ya kuuendeleza kwa serikali 2 au 1 kuongeza mali za Zanzibar ndani ya muungano na si vyenginevyo kwa hiyo lililo baki ili kujitoa kwenye mtego huu nni kwa Wanzibar kuomba KURA YA MAONI hivi sasa ili kutoa fursa ya fursa kwa Wazanzibar kuujadili Muungano na namna ya Muundo wautakao kama watuhitaji kuendelea, na kazi hii ni lazima ifanywe na wanachi wote wa Zanzibar kwa kushinikiza Serikali iitishe kura ya maoni. Tume ya kukusanya maoni ilioteuliwa na kikwete haina mamlaka kisheria kusikiliza maoni ya Muungano ila jukumu lao ni kusikiliza maoni kuhusu katika mpya Jamhuri ya Muungano.
  KAZI KWETU WAZANZIBAR KUSIMAMA IMARA KUJINASUA NA HILI JOKA LIITWALO MUUNGANO AU KUBWETEKA NA KUENDELEA KULALAMIKA NA TABU ZA MUUNGANO KILA SIKU.
  Assalaam alaikum!

 2. Nakutakia kazi njema katika tume ya katiba naomba na huko ussisahau wajibu wako wa kuwatetea na kuwaamsha wazanziabri

 3. MZANZIBAR KWA KUTUMIA NJIA MBALI MBALI ZA VYOMBO VYA MAWASILIANO KAMA VILE FACEBOOK, BADOO, MARAFIKI, TWITTER NKHAMASISHA WAZANZIBAR WOTE KUSHIRIKI KATIKA HARAKATI ZA KUDAI UHURU WA ZANZIBAR KUTOKA MIKONONI MWA MAKAFIRI WEUSI WA TANGANYIKA- 2012 ILI ULIMWENGU UELEWE KUWA TANGANYIKA INAITAWALA ZNZ KAMA KOLONI LAKE.

 4. suala la baadhi ya wazazi kuwazuia watoto wao na baadhi ya watu pia kukataa kazi hii unaichukuliaje je hilo si tatizo la wazanzibari linalosababisha hizo nafasi za ajira zimilikiwe na wageni? tunapiga kelele nafasi zinachukuliwa na watu kutoka nje ya zanzibar jee sisi tumezichangamkia ipasavyo? Pia naunga mkono hoja ya kuacha kumilikisha sekta za kiuchumi kwa wageni hii nchi ni yetu sio ya wazungu au wageni wasio watanzania. wazawa ndio wawe na control ya uchumi wao

 5. Tunakushukuru kwa makala zako ambazo zimekuwa ni mwanga kwa wazanzibari niliposoma kitabu cha” Kivuli Kinaishi” cha Saidi Mohamedi kuna hadithi ya mtolewa na bikirembwe .Bikirembwe alikuwa akiwapa raia wake unga wa ndere na Mtolewa alikuwa akiwapa raia uanga warutba. Baada ya kuwapa watu unga warutba umebahatika kuingia ndani ya giningi .Tunatarajia utasimamia vema matkwa ya wae waioshiba unga w rutba.Binafsi nakutakia kazi njema na uwe na afya njema.allah awatangulie kwa kila mnatalolifanya kw maslahi ya wazanzibari.kila a kheri

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s