Maalim Seif atoa somo la Muungano wa Mkataba

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad akihutubia mkutano wa hadhara huko Wambaa, kusini Pemba jana ambapo mamia ya wananchi walihudhuria na kumsikiliza

KATIKA kuondosha manunguniko juu ya Muungano wa serikali mbili ya Tanzania na Zanzibar, njia pekee ya kuondosha hilo ni kujitokeza kwa wingi katika kutoa maoni wakati wa mchakato wa uundwaji wa katiba mpya. Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad jana alipokuwa akihutubia kwenye mikutano ya hadhara ya Chama cha Wananchi CUF huko Kisiwa Panza na Wambaa, Mkoa wa Kusini Pemba ambapo pamoja na mambo mengine aliwataka wazanzibari bila ya woga kutoa maoni yao ili kupata Muungano usiokuwa na manung’uniko na wenye kujali maslahi ya pande zote.

Maalim Seif alisema baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, wa Tanzania Dk. Jakaya Kikwete kuunda Tume ya kuratibu maoni ya wananchi, ambayo ina uwakilishi sawa wa wajumbe kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, sasa ni wakati wa Wazanzibari kujiweka tayari kusema aina ya Muungano wanaoutaka utakaokidhi matakwa yao kwa mujibu wa wakati uliopo.
Alisema wananchi wenyewe ndio wenye maamuzi juu ya aina ipi ya Muungano wanaoutaka, iwe wa serikali mbili, tatu, moja au aina nyenginezo, ikiwemo Muungano wa Mkataba.  Akifafanua aina hiyo ya Muungano wa mkataba kwa wanachama, wafuasi CUF na wananchi waliohudhuria kwa wingi katika mikutano hiyo, alisema mnaweza kuwa na serikali mbili ambazo kila moja inakuwa na mamlaka kamili, na baadaye kuwe na mkataba kati yao hizo, juu ya baadhi ya mambo wanayokubaliana yawe ya pamoja.
Alifahamisha chini ya utaratibu kama huo, kila serikali inakuwa na mamlaka kamili, ikiwemo kiti katika Umoja wa Mataifa, lakini katika baadhi ya mambo wanayokubaliana yawe ya pamoja wanawekeana mikataba ya kuyaendesha na kuyasimamia.
Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF, alisema Muungano wa aina hiyo hivi sasa umekuwa maarufu na hata nchi 27 zinazounda Umoja wa Ulaya (EU) zimeamua kuwa na utaratibu huo, na zinaenda vizuri bila ya matatizo.  Alitoa mfano, licha ya kuwa na Muungano huo, nchi hizo wanachama bado huwa na uhuru na maamuzi yao kamili na kwa mfano EU zimekubaliana baadhi ya mambo, kama vile kuwa na sarafu ya pamoja, lakini hata hilo, Uingereza ambayo ni mwanachama haijaingia kwenye sarafu hiyo.
“Hatafungwa mtu wala kunyanyaswa kwa kutoa maoni ya Muungano anaotaka, hatuhitaji kuwa na Muungano wa karatasi ambao haumo katika mioyo ya watu lakini tunataka kila mmoja atoe maoni yake huru kabisa”, alisisitiza Maalim Seif.
Maalim Seif alisema kwa Wazanzibari ambao tayari wana katiba yao, suala la Muungano ndilo jambo muhimu na linalowagusa zaidi katika kuandika katiba mpya, hivyo ni jukumu lao wajiandae vizuri juu ya hilo. Aidha aliwahimiza wananchi kuitumia fursa hiyo kikamilifu kumaliza kilio chao cha muda mrefu ndani ya Muungano. Na kusema Wazanzibari wakiwa na sauti moja katika kumaliza malalamiko yao ndani ya Muungano, itakuwa jambo zuri zaidi.
Makamu wa Kwanza wa Rais alisema baada ya hatua ya wiki iliyopita kwa Rais Kikwete kuitangaza Tume hiyo, karibuni inatarajiwa itaanza kupita mitaani kuchukua maoni ya wananchi.
Alieleza kuwa huo utakuwa wakati wa Wazanzibari kujitokeza kikamilifu na waitikie wito aliokwisha utoa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein alipowataka wananchi wajitokeze kutoa maoni bila ya woga.

Maalim Seif alisema baadaye katika hatua za kupata katiba mpya wananchi wa pande mbili yaani Tanzania Bara na upande wa Zanzibar watalazimika kupiga kura ya maoni, ili kusema iwapo wanakubalina na katiba hiyo au hapana.
Alieleza kuwa, ili Wazanzibari waweze kushiriki kikamilifu katika kupiga kura ya maoni, kila mmoja anapaswa kuwa na kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi na kuwataka wale amabo wahajenda kuchukua vitambulisho vyao wafanya hivyo haraka.
Kutokana na hali hiyo, Makamu wa Kwanza wa Rais aliwahimiza wananchi ambao hawana vitambulisho hivyo, wale ambao hawajaenda kuvichukuwa au hawajavipata kutokana na sababu nyengine wahakikishe wanavipata ili kuweza kuvitumia wakati wa mchakato huo utakapofika.
“Kuna watu wengi vitambulisho vyao vimeshakuwa tayari kwa muda mrefu, lakini kutokana na ajizi zao, hawajaenda kuvichukua, nawasihi wakavichukue vitambulisho vyao ili isje ikawa ni kikwazo wakati ukifika”, alisema Makamu wa Kwanza.
Hata hivyo, alisema pamoja na ajizi hiyo ya baadhi ya watu, ni ukweli kuwa wapo baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa (Masheha) wanashindwa kuwapa vitambulisho wananchi wenye sifa za kupewa, bila ya sababu za msingi.
Aidha, aliwasihi Masheha hao kuacha tabia hiyo na kujali zaidi maslahi ya nchi kuliko ya vyama, kwa sababu vitambulisho hivyo havitumiki katika kupigia kura peke yake, bali vinatumika katika shughuli zote za kimaisha kwa Mzanzibari.  Akizungumzia uhai wa chama cha CUF, Katibu Mkuu huyo alisema katika ziara yake amebaini matawi mengi wanachama wako hai, isipokuwa machache ambayo wanachama wake wanasinzia na kuwataka viongozi wa Matawi, Majimbo na Wilaya kuwazindua.
Alisema wanachama walio hai hukipa nguvu kubwa chama na kuweze kufikia malengo yake, ambapo kwa upande wa chama cha CUF malengo yake ni kushika dola katika uchaguzi mkuu wa 2015.  Aliwatahadharisha wanachama wa CUF kuwa chama si viongozi, bali ni wanachama, hivyo wahakikishe wanashiriki vikao kwa mujibu wa katiba na kulipa ada wanazostahili kulipa.

Advertisements

21 responses to “Maalim Seif atoa somo la Muungano wa Mkataba

 1. A’alaykum ni kweli muungano hatuutaki hata kuusikia lakini jamani nawaombeni someni maneno ya baloz seif apo juu mutajua nani wa kushambuliwa?

 2. Balozi seif Iddi na Seif Sharif wote tumbo moja. Hawana mapenzi na Wazanzibari. wanamapenzi ya maslahi yao na kujipendekeza kwa bwana zetu wa Tanganyika

 3. Mimi Upande wangu sifurahii muungano tuliokuwa nao sasa, ni wa kihuni wala hauna maslahi kwetu, ila kwa upande moja muungano kwetu ni muhimu ila sio huu tulio nao sasa. Visiwa vyetu vidogo na tupo wengi leo tukisema muungano umevunjika kwa upande moja bila ya wengi kujua si upande wa bara wala zanzibar, sisi wazanzibari tumeumia. Wafanya biashara wote wakubwa bara ni wazanzibari. Tumetawanyika kila mikoa, wazanzibari wengi wanafanya kazi bara tushakuwa wasomi wengi na sehemu za kufanya kazi zanzibar ni kidogo. tuseme ukweli.
  Zanzibar Bishara haina mzunguko mkubwa kwa sababu population ni ndogo tofauti na bara, zanzibar mishahara midogo haikidhi maisha.
  Hapa ni kuwa na Muungano wa mkataba ila ikiwa wao hawako radhi si tatizo tutavunja Na Allah Ndie Anae jua zaidi

  • Salem usiwe na mawazo finyu kuwa zanzibar ni ndogo na tutakosa kazi endapo muungano utakatika, biashara inaruhusika ulimwengu mzima bila ya muungano,wazanzibari wako dunia nzima hata katika nchi tusizoungana, binaadamu ni huru muhimu kukaa katika nchi nyengine bila ya kuvunja sheria, ebu niambie wapi utaenda leo usimkute mzanzibari anaishi na anafanya biashara na anamiliki raslmali kubwa tu…kuvunjika muungano hakuna maaana kuwa wazanzibari wahame bara au watanganyika wahame zanzibarila ni kupata heshima ya nchi kama nchi…..

 4. Maalim kutotolewa vitambulisho kwa wanaostahiki si matatizo ya masheha. Watu kutoka bara wanapata vitambulisho kupwesa nikukawia lakini wazaliwa ambao ndio wenyewe hawapewi. Sababu za kutopewa zinajuilikana. Kuwalaumu masheha ni kuwaonea bure. Masheha wanapokea amri kwa wakubwa zao. Hebu wafanye kama kujaribu wakuu wa wilaya wawaambie masheha kila anaestahiki apewe tuone hawatapewa? Sio ahatubie mkutano wa hadhara mkuu wa wilaqya kisha aseme “masheha wapeni vitambulisho” baadae kwenye viakao vyao huambiwa msimamo ni ule ule.

 5. Mimi nadhani hawa masheha wamewekwa kuwa vikwazo ktk vitu mbali mbali na sio tu vitambulisho hata barua za passport na vinginevyo,waulize kutaka pesa na kula jasho la wananchi tu!.

 6. Pingback: Maalim Seif atoa somo la Muungano wa Mkataba·

 7. jamani msiwe wakali Mkumbuke kwamba Maalim ni kiongozi katika serikali, hivyo kama yeye kutamka neno kama hilo inazingatiwa ni jinai kubwa, hivyo anajaribu kulipiga vita kwa kutumia njia za kidiplomassia tusiwe wakali nakuombeni ishaallah mungu yu pamoja nasi
  unaweza pia kupata habari za zanzibar yetu na dunia kwa ujumla kupitia http:zenjibarza.wordpress.com

 8. TUMESHAELEWA NANI NI WABAYA/ WACHAWI KWA ZANZIBAR. KAZI ILYOBAKIA NI MOJA TU KUIUNGA MKONO UAMSHO NA KUHAKIKISHA KUA MAAMUZI YA WAZANZIBARI YANAKUBALIKA. TUKIAMUA KUACHA VYAMA TUNAWEZA. TUPIMENI HOTUBA ZA VIONGOZI HAWA WAWILI NA TUTAJUA NANI ANAJALI MASLAHI YA TANGANYIKA NA NANI ANAJALI MASLAHI YA WAZANZIBARI. BAADAE TUFANYE MAAMUZI. MUUNGANO KWISHAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAA .

 9. hee mbona wazenji hatuna umoja? baadhi wanahimiza serikali mbili, wengine moja, mara tatu, kesho mkataba,wengine usiwepo kabisa! lakini si mtego huu ili ajenda ya siri ipite?

 10. assallaaaamu aleikum: mimi nipo na Maalim Seif. Hajasema kosa kabisa. Tukumbuke Maalim ni makamo wa kwanza. Kwa hivo anajukumu, mbali na chama cha CUF, wananchi kwa jumla. Muungano tujaua wazi umekwisha. hilo halina mjadala. Hakuna anaetaka liishie kwake. Mh. Kikwete anajua kuwa wazanzibari hawataki tena muungano lakini kuna process ya kufuata kuuvunja huo muungano. Tusitarajie kuamka asubuhi na kuona muungano umevunjika. Hebu angalieni walioteuliwa kwenye wakusanyaji maoni ya wananchi. Angalieni picha vizuri kisha mujijibu wenyewe. Basi katika mchakato musiwe na pupa. Tumieni vichwa vyenu musikurupuke tu.

 11. Ni vizur mtu kupigania alitakalo lkn lililo bora zaid ni kusoma alama za nyakat na kufuata hatua stahili.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s