Zama mpya, fikra kongwe tutafika?

 

Na Juma Mohammed, Zanzibar

Mataifa mengi hivi sasa yapo katika harakati kubwa kugeuza mambo kutoka zama za teknolojia duni kwenda kwenye teknolojia zilizo bora na kisasa. Wavumbuzi wanaendelea na kazi ya kufikiria wanaweza kuvumbua jambo gani lenye maslahi na binadamu. Dunia ya leo sio ya mtu kulala usingizi, ni ya kufanya kazi kwa bidii, kuibua mawazo mapya,kujituma zaidi na kubwa kutanguliza uzalendo na upendo kwa raia wenzako.

Wakati wana sanyansi na vijana wakitafakari hali hiyo, mambo kwa mizimu,waganga wa jadi, wapiga ramli, nao wanatafakari namna gani wanaweza kuboresha huduma zao kwa wateja wao,lakini baadhi yetu hapa Zanzibar tukiwa katika usingizi mzito fofofo!

Usingizi wetu tunaweza kuamshwa kwa kumwagiwa maji baridi,lakini si kwa kuliondoa godoro au mkeka kwenye kitanda cha kamba. Kasi ya uwajibikaji kwa watendakazi wa umma hairidhishi,setka binafsi angalau kidogo,lakini bado tuna masafa marefu kufika safari ya maendeleo endelevu.

Kila uchao kwenye luninga, Radio, mitandao ya kijamii, tunapewa taarifa za Mataifa mengine kuendelea kiuchumi, kiviwanda, kiteknolojia huku tukishuhudia ubunifu na uvumbuzi wa wasomi na watafiti vijana katika taaluma mbali mbali za sayansi za jamii, sayansi asilia na umbile, sayansi tumizi, bioteknolojia na nyanja nyinginezo za sayansi na utafiti.

Zanzibar wazee ndio kwanza wanaendelea kung’ang’ania katika nafasi ambazo wangeshika vijana wao ili wao kubaki kama washauri, Maofisini nako utaratibu ni ule ule, utakuta barua kwenda ofisi fulani inachukua pengine hata siku kumi haijafika ilipokusudiwa!

Nchi nyingi hasa zile zilizoendelea na hata hizi zetu za Dunia ya tatu zimekuwa zikitenga fedha maalum kwa ajili ya utafiti wa mambo mbalinmbali,Sina hakika Serikali imetenga kiasi gani katika utafiti,lakini ni jambo linalohitaji kupewa kipaumbele kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Ulimwengu wa leo uko katika zama za uvumbuzi, fikra mpya sio kongwe ingawa wapo wanaosema isiyo kongwe haivushi,lakini msemo huo unaonekana kuishiwa nguvu katika dhana ya “New Ideas, new thinking” tumeshuhudia nguvu ya vijana ikileta mabadiliko katika Makampuni mengi binafsi ambayo sitaweza kuyataja kwa leo.

Hatuwapingi wazee kuwamo katika kazi,lakini tunawakumbusha kujiandaa na maisha ya kustaafu huku wakiwatayarisha vijana kuchukua nafasi zao sio kuendelea kuwa ving’ang’anizi katika nafasi za utendaji huku baadhi yao wakiwafisidi vijana kwa kutokuwapa nafasi kuonesha vipawa vyao.

Katika kufikia malengo ya ustawi siku za usoni hatuwezi kutegemea tu mafanikio ya zamani ili kuweza kustawi katika nyanja tofauti. Hii leo jamii nyingi duniani zimeathiriwa kwa kiwango kikubwa na ustawi wa kasi wa sayansi na teknolojia pamoja na matukio ya kiuchumu, kijamii na kiutamaduni.

Kwa hivyo nchi zote zinalazimika kuandaa mipango yao ya siku za usoni kwa kuzingatia matukio na mahitaji ya hivi sasa kwani Zanzibar ya leo sio ya jana wala juzi ni mpya, mahitaji mapya fikra mpya kwani idadi kubwa ya watu wake sasa ni vijana.

Mbinu na mpango mkakati uwe wa siasa,uchumi,utafiti na aina ya jambo lolote zimebadilika na hata aina ya watu wamebadilika ingawa kwenye macho ya wazee wanawaona ni wale wale,lakini hichi ni kizazi kipya kilichozaliwa mwishoni mwa karne ya ishirini na mwanzoni mwa karne ya ishirini na moja ya sayansi na teknolojia.

Katika ulimwengu wa kisasa, uendelevu, uhai na ustawi wa nchi unategemea vijana ambao wanaweza kufanya kazi kwa haraka zaidi na kutumia weledi wao katika kuongeza kasi ya maendeleo katika nyanja zote.

Rais wa Kwanza wa Zanzibar ,marehemu Mzee Abeid Amani Karume aliamini, iwapo Nchi hii haitakuwa na uhuru wa kifikra, haiwezi kupata uhuru katika sekta nyinginezo. Aliwapeleka vijana wengi masomoni akiamini kuwa watakaporejea wataweza kuwa chachu ya maendeleo na kweli tuliona kazi yao.

Nami leo naungana na fikra za wanasiasa wawili vijana, Januari Yussuf Makamba na Kabwe Zubeir Zitto kuhusu kuangalia haja ya mtu kuweza kugombea Urais sio lazima atimize miaka 40 kama ilivyo sasa kwenye matakwa ya Katiba.

Wakizungumza kwenye Kongamano la Katiba na Vijana lililoandaliwa na Taasisi ya Femina HIP, Dar es Salaam, Zitto na Makamba pia walitaka umri wa kupiga kura uanzie miaka 16 badala ya 18.

“Hatutakuwa tumeanza sisi kwa sababu nchi nyingi duniani nafasi ya urais inagombewa kuanzia miaka 35, kwa hiyo vijana tuangalie suala hilo katika mchakato wa Katiba Mpya inayokuja,” alisema Januari Makamba.

Hoja hiyo iliungwa mkono na na Zitto ambaye alizitaja nchi za Kenya, Uganda na Burundi kuwa urais unagombewa kuanzia miaka 35. Kwa hakika wanasiasa hawa vijana wamesema jambo lenya maana ambalo kwa mtazamo

Ni wakati muafaka kuelekea kuandikwa kwa katiba mpya pia kuwepo na ukomo wa umri wa mtu kuweza kugombea Urais mwisho uwe miaka 60 zaidi ya hapo apuumzike kwani umri wa kustaafu kazi Tanzania si zaidi ya miaka 60 kwa hivyo hakutakuwa na ubaya kwa nafasi ya Urais ikiwekewa ukomo wa umri.

Baada ya kifra hiyo, wanasiasa wazee, wenye umri wa kati na watetezi wa vikongwe walianza mashambulizi kama vile sasa ndio mawazo hayo yamekubalika na yamefanywa kuwa sheria!

Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kushikilia mitazamo na mapokeo ya umri mkubwa ndio usahihi wa kuongoza jambo tunaweza kuchelewa sana katika zama mpya na kifra mpya, hivi nani anadhani kuwa umri mkubwa ndio uwezo wa kuongoza vyema?

Mbona ipo mifano ya vijana walipewa madaraka wakiwa vijana na wamefanya vizuri? Hoja ya kupungunguza umri kutoka miaka 40 kwa nafasi ya Urais inapata nguvu hasa ikitiliwa maanani utafiti wa kisayansi uliobainisha muda wa kuishi katika Dunia ya tatu kuwa sio mrefu,ingawa hilo lipo katika Mamlaka ya Mwenyezi Mungu,lakini tunaona hali halisi.

Viongozi wazee tunao wengi katika nchi zinazoendelea kuanzia sina sababu ya kuwataja watu wazima hawa maana mila na silka za Afrika zinazuia kuwasema wazee hadharani,lakini bila shaka wale wanaofuatilia siasa wanaweza kuwatambua viongozi hao.

Tawala zao zinalalamikiwa na raia wao kwa kushindwa ama kutimiza malengo ya kisiasa,kiuchumi na kijamii,lakini pia kushindwa kuzifikisha nchi wanaozoziongoza katika kilele cha demokrasia ya kweli.

Watetezi wa uzee wanajenga hoja kwamba umri wa miaka 35 haufai kumfanya kijana kuweza kuongoza Dola maana mawazo na matendo yake bado ni ya utoto, yawezekana ikawa sahihi na inawezekana pia sio sahihi. Rais wa DRC,Meja Jenerali,Joseph Kabila alishika madaraka ya Urais akiwa na umri wa miaka 30 baada ya kuuwawa kwa Baba yake mwaka 2001.

Msituhukumu vijana kwa haiba ya ujana wetu, mnapaswa kuhukumu matendo ya kijana husika maana uongozi na kiongozi ni vitu tofauti na hususan kazi ya Urais maana Urais si mtu ni Taasisi.

Katika taasisi ya Urais hawi Rais peke yake, kuna wasaidizi mbalimbali wanaomsaidia Rais katika utendaji wake wa kila siku hivyo kudai kwamba Rais kijana mwenye umri wa miaka 35 atakuwa ‘hajatulia’ ni hoja dhaifu katika muktadha wa zama mpya, fikra mpya.

Falsafa ya Ujana inakwenda mbali zaidi na wanazuoni wengi wanauchukulia ujana kuwa sio suala la umri peke yake bali ni pamoja na ufahamu wa jambo wenye kuambatana na fikra sahihi na pevu.

Kupata fikra mpya katika zama mpya kunahitajika mabadiliko ya mfumo katika Mataifa yetu, ni jambo la wazi kabisa nguvu kazi ya vijana haijatumika sawa sawa, miaka takriban hamsini wimbo ni ule ule vijana Taifa la kesho badala ya Taifa la leo.

Hivi vijana wakishakuwa Taifa la kesho watoto nao watakuwa Taifa la lini? Wenye umri wa kati wanawekwa kundi lipi? Pengine upeo wa fikra pevu ndio unaotofautisha maendeleo katika Mataifa yanayoendelea na yaliyoendelea

Fikra mpya za vijana zinaweza kuwa ndio sababu na msukumo wa mabadiliko ya kiuchumi,kijamii na kisiasa Zanzibar. Hivi unatarajia fikra mpya gani kutoka kwa Wazee ambao zama zao zimeshapita?

Fikra zao za sasa zilikuwa zina tija na zenye mvuto katika enzi za ‘analogia’ hizi zama za ‘ digitali’ za G3 zimewaacha mbali mno, mwendokasi huu hawauwezi lazima watalalamika kuwa mwendo ni mkali,lakini hatuwezi tena kwenda mwendo wa kinyonga au wa kobe.

Ujana unasaidia kuharakisha mambo na hasa ikiwa kijana mwenyewe ni mwenye uelewa na mjuzi kitaaluma, mwenye ari ya kufunzwa,kujifunza,msikivu mwenye kujituma kwenye kazi au jambo lolote ambayo kwake yeye ni tunu na hazina kubwa katika nchi.

Leo sio lazima kufanyakazi ukiwa Ofisini, unaweza kuendelea na shughuli za Kiofisi ukiwa ndani ya gari, melikebu, garimoshi, ndege ilimradi popote ulipo ni Ofisi maana vijana wengi wanatumia mitandao ya kijamii,facebook, msn, twitter,skypper huku simu za kiganjani za Black Berry, Iphone 4 Nokia na nyenginezo zikiwa hewani.

Rais kijana wa Marekani, Barack Obama anatumia Black Berry sina hakika kwa Marais wazee akina Robert Mugabe wa Zimbabwe, Rais wa zamani wa Senegal, Abdoulaye Wade, Mwai Kibaki wa Kenya na wengineo kama wapo kwenye mitandao ya kijamii.

Ni hoja isiyobishaniwa kuwa nguvu ya mabadiliko katika Taifa lolote inategemea vijana , akili za Ujana tofauti na akili za Uzee na ndio maana tunashawishika kusema kuwa vijana ndio chachu ya mabadiliko, na ndio chemchem ya fikra mpya na mbadala zinazotegemewa kuondoka katika kikwazo cha kuwa nchi ya dunia ya tatu.

Advertisements

4 responses to “Zama mpya, fikra kongwe tutafika?

  1. “Nami leo naungana na fikra za wanasiasa wawili vijana, Januari Yussuf Makamba na Kabwe Zubeir Zitto kuhusu kuangalia haja ya mtu kuweza kugombea Urais sio lazima atimize miaka 40 kama ilivyo sasa kwenye matakwa ya Katiba”

    Juma leo umezungumza kweli. Hukutaka kutuvisha kilemba cha ukoka! Shida yangu mimi si Urais kama akina Zitto na January wanavyo azimia mimi nawaomba hawa “Waminkimaupaku” watuachie sisi tuendeshe nchi katika ngazi zote. Ukiacha Wateule wa Rais waliochoka ambao wanamshauri au ni vyenyeviti wa bodi za Mashirika wamo pia waku wa Wilaya ambao ukifanya nao miadi ukienda hawaja amka au ukiwakuta saa mbili asubuhi wanasinzia kama vile usiku kutwa walisali sala ya tahajudi. Hawa ngekuwa bora kama ni lazima wawepo kwa kuwa ni Quraish nafasi zao zishikwe na watoto wao. Pengine watoto wao kwa kuwa ni kizazi cha mfumo wa leo wangesaidia. Kuna Wilaya moja ambayo wakazi wake wanaamini kuwa ” Mungu aliwaumbia shida iwe nguo yao na furaha iwe mkwe wao. Hawa ambao hukiri kuwa “toka asubuhi kwao ni shida na mtu hahitaji tochi kuliona hilo.” Watu hawa hawahitaji mtu wa kuwasimulia yaliyopita wanahitaji kuambia wafanye nini wajibadilishie maisha yao ili yawe bora na hili halifanyi mtu aliyechoka kwa lahitaji nguvu na ustahamilivu ambao ukichoka hunao huu. Kwasababu ya Juma anaoita zama mpya watu wakongwe jamaa hawa wao maisha wanaishi kama ndege huamka mashariki na kutafuta riziki magharibi kisha wakala mashariki. Wakati ni huu ili Zanzibar ibadilike kipindi kijacho ni lazima tuwetayari kupokezana.

  2. mapinduziii daima kaeni na baraza lenu la mapinduzi na baraza la wawakilishi MUCHEZE SUMSUMIA kuuliza wananchi wanautaka au hawautaki muungano ngumu basi chezeni sumsumia pigeni makofi mapinduzi daima zanzibar pata poteaaa

  3. UHURU UHURU UHURU. Ewe mzanzibar shiriki katika harakati za kudai UHURU WA ZANZIBAR -2012. USIDANGANYWE NA WANASIASA ZANZIBAR BILA YA KUPATA UHURU KUTOKA MIKONONI MWA MAKAFIRI WA TANGANYIKA BASI ZANZIBAR HAITOENDELEA MILELE.

  4. MZANZIBAR ELEWA TAMBUA ZINGATIA NA FIKIRIA KUWA ZANZIBAR NI KOLONI LA TANGANYIKA. Kwa hivyo, wazanzibar tuache kuchati katika mitandao kama vile facebook twitter na marafiki mambo ya mapenzi tu bali tutumie vyombo vya habari kuhubiri na kusambaza ujumbe wa HARAKATI ZA KUDAI UHURU WA ZANZIBAR. Hakuna furaha zanzibar mpaka tupate UHURU.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s