Serikali yakiri upendeleo katika ajira

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Othman Masoud Othman

SERIKALI ya Zanzibar imekiri kufanyika kwa ajira upendeleo na kujuana katika wizara mbali mbali za serikali jambo ambalo limelazimisha kufanyia marekebisho katika sheria zake za utumishi. Hayo yameelezwa na Mwanasheria Mkuu wa serikali, Othman Masoud Othman alipokuwa akifanya majumuisho na kujibu masuala mbali mbali katika mswada wa sheria mbali mbali na mambo yanayohusiana na hayo katika kikao cha baraza la wawakilishi jana.

“Hoja ya uajiri ni kweli hilo hatuwezi kukataa kwa kweli mfumo wa utumishi ni mfumo ambao tumetoka nao huko nyuma wapo wanaobadilisha vyeti ikiwa umri wao umepita, wapo wanaoajiriwa kwa urafiki na ukaribu hilo hatuwezi kulikataa yalikuwepo huko nyuma kabla ya sheria hii lakini ndio tunasema hivi sasa tunajipanga katika hilo kuondosha malalamiko hayo” alisema Mwanasheria Mkuu.
Kauli hiyo ya serikali imekuja kufuatia baadhi ya wajumbe hao kulalamikia mfumo uliopo ambapo walisema wapo baadhi ya wafanyakazi wamekuwa wakipata ajira kutokana na kujuana huku watendaji wenye kufanya hivyo katika chombo cha utumishi ambacho kinachotegemewa na wananchi kutoa ajira kikiwa kinakiuka misingi ya haki na uadilifu.

Mwakilishi wa Jimbo la Wete (CUF) Asaa Othman Hamad alisema katika mawizara kumekuwepo na mkanyagano mkubwa ambao mara nyingi wanaofanya hivyo ni wale wafanyakazi wasio na ufanisi wa kazi lakini pia ajira zimekuwa zikitolewa kwa ubinafsi bila ya kuzingatia sifa zinzostahiki.

“Tunachukua watumishi wa umma na kuwapa mikataba ya kazi ya muda tu, serikali inawafundisha vijana na kuwasomesha lakini wanashindwa kufanya kazi hapa kutokana na sheria za utumishi zilivyo” alisema.

Alisema ipo haja ya kufanywa tathmini ya kila mwaka kwani watendaji na wafanyakazi wamekuwa wakitekeleza majukumu yao isivyo sahihi ambapo wapo walioajiriwa bila ya sifa na kutaja vitendo vya ubadhirifu wa fedha za umma ukifanyika chini ya kivuli cha wafanyakazi hewa.

“Kuna matatizo katika sekta hii ya utumishi wa umma, wapo watu wanataka kuajiriwa wenye sifa lakini badala yake wanachukuliwa wengine na kuachwa wenye sifa. Mheshimiwa Spika Wafanyakazi hewa wapo kila siku lakini wanaonekana upande mmoja tu, Pemba ndio inayoonekana kuwa kuna wafanyakazi hewa lakini hapa Unguja wapo lakini hilo halifanyiwi uchunguzi” alisema Asaa.

Naye Mwakilishi wa Ziwani (CUF) Rashid Seif Suleiman kwa mujibu wa katiba kamisheni ya utumishi ndio chombo kikuu lakini inaonesha kwamba serikali inarudi tena katika utawala wa mu binafasi na mwengine ambao mamlaka anapewa katibu mkuu kiongozi hivyo alishauri maamuzi yatokane na chombo kuliko maamuzi kutokana na mtu mmoja.

“Wizara ya utumishi na utawala bora atafanya kazi gani ikiwa maamuzi kama hayo anapewa katibu mkuu kiongozi, kwa kuwa yeye ni kiongozi basi ni bora akaendelea kuwa kiongozi wa wizara zote lakini kumuweka katika wizara moja tu ni kumuongezea msongamano” alisema mwakilishi huyo.

“Nashauri utafiti mkubwa ufanyike kuhusiana na utumishi wa umma kwani ubinafsi umetawala, umimi unatawala na ni bora kufanya uchunguzi mapema kuliko kusikia kuna ajira zimetolewa, tunataka maeendeleo lakini bado tunaendelea kutoa ajira kwa upendeleo tu utasikia anatakiwa mtu mwenye digree lakini wanachukuliwa mtu mwenye diploma wakati wenye degree wapo mitaani” alisistiza.

Aidha alisema kuna haja ya kutathimiwa kwa wafanyakazi kila mwaka, pamoja na wakurugenzi, makatibu wakuu na hata mawaziri wanaoteuliwa watizamwe kutokana na viwango vyao vinavyokubalika.

“Rais anatizama kusini sijachukua anateuliwa mmoja kaskazini sijateuwa anachukua mmoja na hachagui kwa kiwango na vigezo mpaka lini tutatumia utaratibu huo bila ya kuzingatia utumishi wa umma” alihoji mwakilishi huyo.

Naye Mwakilishi wa Jimbo la Micheweni (CUF) Subeit Khamis Faki alisema mikataba ya muda inayotolewa na serikali ni vyema ikawa inazingatia vigezo na kada maalumu na watu maalumu na sio kuacha kuwachukua vijana ambao wamesoma na hawana kazi za kufanya na kuwapa wastaafu mikataba jambo amablo linawakosesha vijana fursa za ajira.

Serikali iwaache wastaafu na iwape fursa vijana maana kuwarudisha wastaafu ni kuwanyima fursa vijana kufanya kazi hasa kwa kuzingatia serikali inao vijana wengi wenye elimu na waliosoma katika fani mbali mbali.

“Kwa nini kila siku serikali inawachuklua wastaafu na kuwapa nafasi serikali wakati kuna vijana tele ambao wana elimu ya kutosha na wanaweza kufanya kazi” alisema Subeit.

Aidha Mwakilishi huyo ameitaka serikali kuwa makini katika suala zima la kutoa uajiri wa mikataba kutokana na kufanya hivyo kuwakosesha vijana wenye uwezo wa kupata ajira.

Alisema wapo baadhi ya wastaafu ambao wanapewa mikataba ya kazi wakati utendaji wao hauna rekodi nzuri huko nyuma lakini pia kufanya hivyo ni kuwakosesha vijana kupata ajira serikalini na kuzalisha wafanyakazi wavuvi.
Alisema sheria nyingi zinatunga lakini haziwasaidii waajiri na kumekuwa na ujanja wa wamiliki wa mahoteli wanawafukuza wafanyakazi bila ya sababu za msingi kutokana na marekebisho ya sheria ile ya mishahara kwa wafanyakazi.

Kwa hivyo ipo haja kwa serikali kurekebisha sheria zetu ili ziwabane wale wote ambao watafanya vitendo kama hivi vya kuwadhulumu wafanyakazi wao na kuwanyima haki zao.

Aliomba Serikali kuchukua hatua za kisheria kama zinavyozitungwa barazani hasa kwa hao wamiliki wa mahoteli ambao wanaofanya vitendo hivyo, sheria zifanye kazi na zisimamiwe kikamilifu kama zinavyotungwa maana kutungwa kwa sheria na kusifanyiwe kazi kwa ukamilifu.

“Sheria zetu ni nzuri lakini mara nyingi tunashindwa kuzisimamia na kuzitekeleza na ingekuwa tunasimamia vyema sheria zetu basi isingekuwa mara kwa mara tunazipitia na kuzifanyia marekebisho hapa” alisema Mwakilishi huyo.

Akizungumzia suala la mishahara alisema licha ya marekebisho hayo ya mishahara imepitiwa lakini bado mishahara midogo vijana wanapomaliza kidatu cha sita na akichukua diploma, utumishi unachelewa kumfanyiwa marekebisho zaidi ya mwaka na hayo ndio mambo ambayo huwavunja moyo zaidi na kukimbia nchini na kukimbilia sehemu nyengine kufuata maslahi zaidi.

Mwanasheria Mkuu alisema alisema kuna haja ya kuiangalia katiba ya hapa nchini ingawa kuiangalia katiba na utekelezaji wake ni mambo tofauti kwani tabia zilizojengeka ni kuona kwamba wingi wa ukursa ndio muhimu.

“Katiba ya Marekani ina page 30 tu lakini sisi page 35 lakini tuna matatizo kwa hivyo ni kujitathimini sisi wenyewe tunavyoendesha mambo yetu. Tusubiri hili kubwa la kurekebisha katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania halafu mambo mengine tatakaa sawa lakini tukitizama katiba yetu sasa haitakuwa mwafaka kwa sasa lakini sote tuanze kutizama hiyo katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwanza” alisisitiza Mwanasheria Mkuu.

Akijibu hoja ya majukumu ya kamisheni, Mwanasheria Mkuu alisema mukumu ya kamisheni kwanza ni kumshauri waziri na waziri mwenyewe anatakiwa kama kujibu hoja au kusawazisha basi ajisawazishe kwani ni nzuri kumuwezesha waziri ili aweze kusawazisha kabla ya kufika kwa rais na ndio maana sheria iweke bayana hilo.

Akijibu mamlaka ya katibu mkuu kiongozi ambapo wajumbe wengi walisema majukumu hayo yanaingiliana na tume ya utumishi, alisema tume ya utumishi kila mmoja anafanya kazi yake na mamlaka aliyopewa.

Vijana wa Zanzibar kusomeshwa

JUHUDI za Makusudi zimeanza kuchukuliwa kwa vijana wa Zanzibar kusomeshwa masuala ya diplomasia ili kuweza kuchukua nafasi ya kibalozi zinazotokea nchini.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Afisii ya Makamo wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed alipokuwa akijibu suali la Mwakilishi wa Jimbo la Kojani (CUF) Hassan Haamd Omar aliyetaka kujua idadi ya wazanzibari waliopo katika ofisi za kibalozi na uwiano ukoje kati ya pande mbili hizo.

Waziri huyo alijibu kwamba jumla ya mabalozi waliopo ni 32 kati yao mabalozi wanne wanatoka Zanzibar na kuna maafisa wa mambo ya nje 35 kwneye balozi za nje ya nchi ambapo kati ya hao 10 ni wazanzibari.

“Utaratibu huu utasaidia kupunguza pengo liliopo na kuleta uwiano unaotarajiwa. Lakini jambo la msingi ni kuwaandaa vijana wetu pamoja na kufanya bidii katika masomo yao ili kukidhi vigezo na sifa katika soko la ajira” alisema Aboud.

Awali Mwakilishi huyo alisema baada ya malalamiko mengi kutoka kwa wajumbe wa baraza la wawakilishi na wananchi kuhusu kutokuwepo kwa uwiano katika kushika nafasi za ubalozi baina ya Zanzibar na Tanzania Bara, kulikuwa na matarajio katika teuzi mpya za mabalozi kungekuwa na wazanzibari wengi zaidi ili kupunguza tatizo hilo ambapo pia alitaka kujua kama suala hilo limepokewa vipi na viongozi wa Tanzania Bara.

Akijibu suala hilo Waziri Aboud, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye mwenye mamlaka ya kikatiba kufanya uteuzi wa mabalozi wa Tanzania, na uteuzi uliofanywa ni sehemu tu ya kujaza nafasi zilizowazi za mabalozi.

Alisema hakuna jitihada zilizochukuliwa kwani bado kuna nafasi takriban 14 zinazotarajiwa kuwa wazi kutokana na mabalozi hao kutarajiwa kustaafu wakati wowote kuanzia sasa ambapo ni vyema wazanzibari wakavuta subira ili kuangalia busara za rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumzia suala la kupuuzwa katika suala hilo Aboud alisema serikali zote mbili zimekuwa zikifanya kazi kutatua changamoto hizo katika kuongeza wigo wa watumishi wa Zanzibar kufanya kazi katika taasisi za Muungano ikiwemo wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa ambapo tayari imeshachukua hatua mbali mbali.

Akizitaja hatua hizo ni pamoja na usajili wa maafisa wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa uliofanyika hapa Zanzibar unaohusiana na wazanzibari peke yao ambapo hatua hiyo ni hutoa fursa zaidi kwa wazanzibari kujiunga na utumishi wa mambo ya nje.

Jembo jengine alilolitaja mbele ya wajumbe wa baraza hilo ni wazanzibari 10 wenye shahada ya kwanza waliopelekwa Chuo Cha Diplomasia (CFR) kwa ajili ya kuandaliwa na kuajiriwa na wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa mara watakapomaliza masomo yao.

Uteuzi wa Ramadhan Muombwa ambaye ni mzanzibari kuwa balozi na naibu mwakilishi wa Tanzania katika umoja wa mataifa ni miongoni mwa kilio cha mda mrefu cha Zanzibar uwakilishi wa Tanzania katika umoja wa mataifa pia ni faraja.

Wanaume waogopa kupima kongosho

 

WAZIRI wa Afya Zanzibar, Juma Duni Haji amesema wanaume wengi wamekuwa na khofu ya kwenda kufanya vipimo vya afya zao hasa katika kupima kongosho dume (cancer ya kibofu cha mkojo) kutokana na kuogopa.

“Ni kweli kila mwanamme mwenye umri unaofikia miaka 40 na kuendelea anatakiwa afanye uchunguzi wa kongosho dume  angalau mara moja kwa mwaka” alisema Duni.

Waziri Duni alikuwa akijibu suali la Mwakilishi wa Jimbo la Mpendae (CCM) Mohammed Said Mohammed aliyetaka kujua serikali inawafanya utaratibu gani kuwafanyia uchunguzi wanaume wenye umri mkubwa ili kubaini kama wamepata saratani ya kongosho dume na kupatiwa matibabu.

Amesema wanaume wengi hivi sasa wamepata matatizo ya saratani ya vipofu vya mkojo lakini pia hakuna utaratibu wa wa kuwapima kwa hiyari hadi hapo wanapokwenda katika vipimo vyengine.

“Kwa hapa Zanzibar hatuna utaratibu maalumu maalumu wa kuwachunguza waume kwa khiyari yao, isipokuwa wale wanaokuja hospitali kwa matatizo ya kuziba njia ya mkojo ndio wanaopimwa kongosho dume na kwa sababu tu ni moja ya maradhi yanayofanya wanaume wengi washindwe kupata haja ndogo” alisema Duni.

Aidha alisema sio kawaida wanaume kukubali kupimwa kongosho kabla ya tatizo la kuziba mkono halijatokeaza na iwapo ikijitokeza anapima kwa tahadhari kubwa na ni kwa sababu tu hana jinsi ya kufanya zaidi ya hilo.

Akitaja sababu ya wanaume wengi kutopenda kupima kama hawaumwi ni aina ya kipimo chenyewe kinavyofanyika ambapo vipimo vyovyote vya kidaktari lazima vianzie na mkono “Ili upate uhakika wa jambo ni lazima vianzie na mikono kwa kugusa sehemu husika” alisema Duni.

Alisema baada ya kutoka hapo ndipo hupelekwa katika maabara mbali mbali na kufuatiwa na vipimo vyengine vya kutumia vyombo vya aina ya x ray, kipimo cha kongosho kinahitaji kupitia kwenye njia ya haja kubwa.

“Wanaume wengi wakiambiwa hukimbia na kurudi kwa daktari pale tu hali inapokuwa mbaya. Pindipo mwanamme akikubali kupimwa mapema au kuchunguzwa kila mwaka anaweza kugunduliwa tatizo mapema, kutibiwa na hatimae akapona kabisa na pindipo akikataa tatizo hukuwa na mara nyingi huishia saratani ya kongosho kwa sabbau ya mabadiliko yanayotokea ndani yake” alisema Waziri huyo.

Awali Mwakilishi huyo wa Mpendae alisema Serikali ya Tanzania kupitia wizara ya afya na jumuiya ya madaktari wanawake (MEWATA) imefanya kazi kubwa ya kuwachunguza akina mama wenye matatizo ya matiti ili kubaini dalili za ugonjwa wa saratani na alitaka kujua iwapo madaktari hao wamefika Zanzibar na kufnaya uchunguzi kama huo.

Akijibu suali hilo Waziri Duni alisema Madaktari wa Mewata hawajawahi kutembelea kuja kwa madhumuni ya kuchunguza saratani ya matiti hapa Zanzibar lakini uchunguzi wa saratani ya matiti ulifanyika mara moja kwa ushirikiano wa hospitali ya Mnazi Mmoja na hospitali ya Agakhan ambapo wanawake walijitokeza kupima afya zao.

Waziri huyo akiwataja watu waliopatikana na dalili za kensa alisema kati ya hao wane walikuwa na dalili hiyo wakafanyiwa vipimo na upasuaji na wanane walikuwa na kensa iliyokuwa imefikia hatua kubwa na baadae wote walipewa rufaa na kupelekwa hospitali ya Ocean Road.

ZANZIBAR NI MDAU KATIKA BOT

 

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema Serikali ya Zanzibar ni mbia katika uanziswaji wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na ndio maana ikawa inapewa gawio lake katika benki hiyo.

Kauli imetolewa na Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Fedha, Uchumi, Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee alipokuwa akijibu suali la ngongeza lililoulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF) Ismail Jussa Ladhu ambaye alisema kwa mujibu wa sheria ya BoT, Zanzibar haitambuliwi kama ni mbia.

Mzee alisema Zanzibar inatambuliwa kama ni mbia na ndio maana ikawa inatengewa gawio lake la asilimia 4.5 katika benki hiyo kwani huwezi kupewa gawio kama sio mdau katika benki hiyo.

Akijibu suali la msingi la Mwakilishi wa Jimbo la Ziwani (CUF) Rashid Seif Suleiman aliyetaka kujua msimamo wa serikali kuhusu atahari ya kuporomoka kwa shilingi ya Tanzania.

Akijibu suali hilo Mzee alisema sababu za kuporomoka kwa thamani ya shilingi ni uzalishaji mdogo wa ndani ambao hauendani na mahitaji, hivyo kusababisha uagizaji kutoka nje na hasa wa vyakula muhimu kuwa mkubwa na kupelekea mahitaji ya fedha za kigeni kuwa makubwa.

Akitaja mambo mengine Mzee alisema kupandamara kwa mara kwa bei ya mafuta duniani, kuchafuta kwa masoko ya fedha duniani kunakosababishwa hasa na matatizo ya kifedha yanayoendelea ndani ya bara la Ulaya, kunakopelekea thamani ya dola kuimarika dhidi ya sarafu nyengine duniani ikiwa ni pamoja na shilingi ya Tanzania.

Sababu nyengine imetajwa ni utegemezi mkubwa wa fedha zilizotoka kwa wafadhili hasa zile zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya kitaifa, zinapochelewa kunfanya mahitaji ya fedha za kigeni na hasa dola kuwa makubwa na hivyo kupelekea kushuka kwa thamani ya shilingi.

Akijibu suali la kitu kinahcochangia kushuka kwa thamani ya shilingi Wziri MZee alisema kushuka kw ashilingi ya Tanzania kunamuathiri sana mwananchi wa kawaida hasa kwa kutilia mkazo kuwa bei za bidhaa mbali mbali na hasa vyakula pamoja na usafiri hupanda bila ya kujali vipato vya wananchi.

Akijibu suali la msimamo wa serikali waziri huyo alisema Zanzibar kuendelea kuwa nchi ya amani na utulivu, kuendelea kuwa na sera nzuri za kuitangaza Zanzibar zitakazovutia watalii zaidi na kuipatia fedha nyingi za kigeni.

Aidha kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza katika uvuvi wa bahari kuu pamoja na wananchi kuanzisha mashamba ya samaki na majongoo ya baharini pamoja na kuzalisha zaidi mazao ya vyakula nay ale ya bishara kama karafuu, hiliki, pilipili na viungo vyengine vinavyopatikana hapa nchini.

Alisema kuhakikisha vyakula vinavyozalishwa ndani haviuzwi nje ya nchi hadi pale litakapopatikana soko la ndani na kupunguza kwa viwango vya kodi kwa baadhi ya bidhaa muhimu hasa za vyakula na kupunguza manunuzi ya lazima kwa bidhaa zinazotoka nje.

Advertisements

One response to “Serikali yakiri upendeleo katika ajira

  1. Serikali kushindwa kuendeleza tabia ya kua mwajiri mkuu ndio chanzo cha matatizo. Zanzibar inahitaji kubadilika na kuelekea ajira nje ya Serikali ambako manunguniko ya upendeleo hakuna kwa kuwa mwenye sifa ndie anaechaguliwa. Tabia hii ya Serikali kuajiri ina changia kupunguza kiwango cha elimu kwa kuwa mtu moja moja hafanyi juhudi ya kupata zaidi ya kinachihitajika. Kwa kuwa Serikali inajali unamjua nani si unajua nini watu wanatumia nyuso za baba zao, asili zao na sehemu wanazotoka kupata ajira. Hii inawafanya hawa kusoma kiasi kidogo tu kwa kuwa inatosha kuingia serikalini kumega sehemu ya cake ya taifa. Wakati fulani nikiwa Serikalini Mhasibu Mkuu wa Wizara alikuwa na elimu ndogo na alipokea mshahara mdogo kuliko wangu. Mtu huyu hatahivyo alikuwa na mimali ya kupita kiasi. Nilikuwa najiuliza mshahara wake wa mbuzi unamtosha apate mali zote zile! Rafiki zangu walinambia nisiende mbali kwa kuwa huyu ama alikuwa Ibni Kniana au Khuzaima na haya ni makabila Ashraf! Miongoni mwa Makureish wa Unguja. Ina sikitisha pia Jamaa zangu wawakilishi kutoka Pemba ambao wanataka vijana wapate ajira Serikalini na hawafikiriii kuunganisha nguvu zao na kuanzisha mfuko wa kuendeleza ajira kule Pemba. Wao kazi wengi ni kufungua viduka vya kuuza vibakuli na vyetezo hapa Unguja. Ivo hawaoni kuwa Pemba in mito mingi ya bahari ambayo wakiunganisha nguvu waweza kuanzisha ufugaji wa samaki na mazao mengine ya bahari. Kwa wakati huu kufikiria kupitisha Sheria ya kuratibu ajira Serikalini ni kupoteza wakati kwa kuwa hili litatokea na hakuna kitachobadilika. Serikali hajiajiri jamaa zangu! Serikali inaweka mazingira mazuri ya ajira kutokea. Ajira hazitatokea kama hakutakuwa na watu jasiri wa kuanza kisha Serikali kwa kuona haya akjitune kuelekea huko mazingiira yanakotaka! Ivo sisi tunaingalia dunia kwa perspective ipi? ya kidunia au ya Kipopeni ambako kila kitu kitakuja automatically! Ukweli unatufundisha kuwa ” humam society has always been in motion.” Tutumie maelekezi kama haya kuelekea kwengine si kuangalia kisichoweza kututalia shida zetu. Serikali haiwezi kabisa – ivo hatuoni kuwa kila mtu akiingia Serikalini apate mshahara mwisho wa mwezi kunapunguza uwezo wake wa kulipia ” development project” na ndio maana unaenda taasisi za Serikali kupeleka msaada wanakudai hata pesa za kupiga rangi darasa. Ivo kuna kzai gani serikalini za kuwa Makatibu wakuu wana Masekerati wawili wawili na hivo kwa Wakurugenzi na hadi wengine unaowajua! Watu hawa waili ukienda hawajui hata kupokea mgeni au kuweka miadi ya bosi wao. Na siku bosi hayupo wote huondoka! Ivo kuna mahitaji gani kwa mahali ambapo kuna RCs na DCs kuongezwa nafasi ya Mshauri ! Katika hali ya kawaida moja wa Mawaziri asie Wizara maalumu kutoka sehemu hii angekuwa Mshauri kama RCs na DCs hawatoshi ! Mtindo huu wa kuifanya Serikali shamba la bibi au dala dala iwe pand shuka hatusaidii. Tubadilike watoto wetu wanahita utuuuzima wao uwe bora kuliko wetu na hili halitawezekana kwa kutumia budget kulipana mishahara tu !.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s