Dk Shein ni Nelson Mandela wa Zanzibar

Na Juma Mohammed

Mwanasiasa na mshindi wa tunzo ya amani ya Nobel,Nelson Mandela ni miongoni mwa watu waliopata shida,misukosuko na wakati mwengine aliweza hata kuhatarisha maisha yake. Serikali ya Kibaguzi ya Makaburu ilimfunga jela alikoishi miaka 27 alianzia kizuizini gereza la Kisiwa cha Robben nje kidogo ya Jiji la Cape Town na baadaye Gereza la Pollsmoor katika madai ya kupika ya kutaka kuipindua Serikali ya Kikaburu dhidi ya Mandela katika kesi maarufu ya Rivonia iliyotolewa hukumu Juni 12,1964.

Wahenga wanasema hakuna lisilokuwa na mwisho,hatimaye mwanasiasa na kiongozi wa Serikali ya Kibaguzi ya Makaburu Afrika Kusini, Frederick De Klerk alimkarisha Mzee Naelson Mandela Ikulu kuzungumzia mustakabali wa wakati huo na baadaye wa Afrika Kusini.

Ilikuwa Februari 2, 1990, Rais de Klerk aliachana na ukale kwa kupuuza amri na misimamo ya Kihafidhina ya kupiga marufuku shughuli za ANC na vyama vingine vya kupambana na ubaguzi wa rangi, na kutangaza kuwa Mandela muda mfupi atafunguliwa kutoka gerezani.

Mandela ilitolewa kutoka gereza la Victor Verster Februari 11, 1990. Tukio hilo lilitangazwa moja kwa moja duniani kote kama ambavyo siku alipokutana Maalim Seif na Dk Karume Ikulu ingawa halikuwa tukio la kutangazwa moja kwa moja,lakini vyombo vya habari viliriripoti kwa uzito mkubwa tukio hilo.

Mandela hakufanya nongwa, alikwenda Ikulu ya Makaburu kama ambavyo Katibu Mkuu wa Chama cha CUF,Maalim Seif Shariff Hamad alivyokwenda Ikulu ya Zanzibar kwa mazungumzo na Rais mstaafu ,Dk. Amani Abeid Karume yenye lengo la kumaliza na kutandika misingi imara ya uzalendo Zanzibar.

Kufuatia kuachiliwa kwake kutoka gerezani, Mandela akarudi kwenye uongozi wa ANC na, kati ya 1990 na 1994, alikiongoza chama katika mazungumzo ya vyama vingi ambayo yalisababisha uchaguzi wa kwanza nchini humo usio wa ubaguzi wa rangi.

Mwaka 1994 uchaguzi huru na haki ulifanyika,African National Congress( ANC) Mgombea wake wa Urais alikuwa Mzee Mandela kama ilivyokuwa kwa Zanzibar uchaguzi wa mwaka 2010 unatajwa kuwa ni moja kati ya Uchaguzi uliokuwa wa mfano Afrika usiokuwa na chembe ya malalamiko kutoka kwa vyama vyote vilivyoshiriki,CCM walimsimamisha Dk. Ali Mohammed Shein kuwa mgombea wake.

Rais wa kwanza kuchaguliwa chini ya katiba mpya alikuwa Nelson Mandela, kama ilivyo kwa Zanzibar baada ya Maridhiano,Dk Ali Mohammed Shein alichaguliwa kuwa Rais chini ya Serikali yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa.

Kwa mnasaba huo nachukua maudhui ya maridhiano ya Afrika Kusini na maridhiano ya Zanzibar kwa kiasi fulani yameshabihiana kwani Mzee Mandela alimteua De Klerk kuwa Makamu wake huku Dk. Shein akimteua Maalim Seif kuwa Makamu wake wa Kwanza.

Dk Shein kama angetaka kupuuza Katiba angeweza kufanya hivyo kwani wapo viongozi wengi Afrika wanapuuza katiba,lakini yeye akiwa mzalendo na mwanasiasa aliyetukuka kisiasa ndani ya CCM na nje ya Chama chake,ametanguliza maslahi ya wengi na upendo kwa Zanzibar.

Kwa mfano,mara baada ya kumalizika kwa Uchaguzi wakati wa kuunda Serikali angeweza kuweka kando katiba iliyoelekeza Serikali ya Umoja wa Kitaifa nay eye kuunda Serikali anayoitaka ambayo taathira yake ingekuwa mbaya zaidi kwa Zanzibar.

Watu wangeandamana, Serikali ingetumia Vyombo vyake vya Dola kuzima maandamano hayo, yangetokea kama ya Januari 26 na 27 mwaka 2001, washirika wa maendeleo wangeisusia,maisha ya watu yangeendelea kuwa ya dhiki na shida,lakini Rais na Serikali yake angendelea kuwepo madarakani.

Rais Dk Shein si kiongozi wa maneno matupu au porojo, ni Rais mtendaji anayejali ubinadamu,uungwana na kubwa zaidi ni mcha mungu anayeamini ipo siku atarejea kwa Mola wake na siku ya siku atasimamishwa na kuulizwa aliyoyafanya duniani.

Ni ukweli usiokuwa na usbishi kuwa Dk Shein hakuyumba wala hakubabaika katika utekelezaji wa katiba,SUK imesimama imara na itaendelea kuwa imara kwa maslahi ya wengi Zanzibar.

Nampongeza Dk Shein katika kusimamia mustakabali mwema kwa Zanzibar kwani ilitaka moyo kweli katika mazingira ya hali ya kisiasa ya Zanzibar yalivyokuwa kabla na siku chache baada ya maridhiano kuweza kutekeleza kwa dhati na moyo mkunjufu katiba kwa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo leo imeiweka Zanzibar pahala pazuri.

Ikiwa kuna watu ambao wanastahiki kupata tunza ya nishani ya kimataifa ya Nobel ya Amani ni Dk Shein, Maalim Seif na Dk Amani Karume,hawana tofauti na hatua walizochukua Mzee Mandela na De Klerk ambao wametuzwa nishani hiyo.

Zanzibar ya kabla ya maridhiano wapo watu waliamini kwamba haiwezekani katu wapinzani wa CCM kufanya nao kazi pamoja, hawa hawana tofauti na kaburu Pieter Botha, aliamini kuwa mtu mweusi, abadan hawezi kutawala nchi.

Muhafidhina huyo Kaburu katika utetezi wa hoja yake alidai Waafrika hawana uwezo wa kuongoza nchi ikawa na maendeleo, ikawa na amani, ila kuchinjana, dhuluma inayotokana na kusheheni kwa ufisadi, pengine na ubaguzi!

Matamshi kama hayo yalitolewa na Wahafidhina wengine kama Dk. Watson aliyedai Waafrika hawawezi kujitawala na kujiletea maendeleo kwa hiyo eti Mwafrika hakustahili kuwa huru milele?

Tulisikia wakati ule haiwezekani kushirikiana na wapinzani Serikalini, utendaji utakuwaje,sera ipi itatekelezwa na mengi mengineyo yaliyokuwa na mwelekeo wa kukatisha tamaa na dhamira njema ya maridhiano na ujenzi wa umoja wa kitaifa Zanzibar.

Kwa upande wa CUF nako mambo karibu sawa na upande wa CCM kulikuwa na watu walioguna wakisema CCM hawaaminiki,hawatatekeleza katiba huku wakimshutumu Katibu Mkuu wao,Maalim Seif kwanini amekuwa mwepesi kukubali maridhiano.

Machi 13, 1995 Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,Rais wa Kwanza wa Tanzania alizungumza katika klabu ya waandishi wa habari wa Dar es Salaam na kukemea vikali sana tabia ya ubaguzi na akasema

“Makaburu wa Tanzania ni wale wanaojiita wazawa. Ni Makaburu kwa sababu ,kama una mawazo yale yale ya kaburu wa Afrika Kusini ,ila tofauti yako kwamba ni mweusi, ni kaburu tu. Wazungu wa Afrika Kusini tulikuwa hatuwapingi kwa rangi yao. Tulikuwa tunawapinga kwa ubaguzi wao.”

Wengine walitamka CUF hawatakuwa na utii katika Serikali,hawaaminiki,lakini wananchi wa Zanzibar ni mashuhuda wa namna Mawaziri kutoka vyama vyote wanavyofanyakazi kwa uzalendo,upendo na ushirikiano mkubwa huku wakiwa wasikivu kwa Rais Dk Shein.

Hivi sasa tanga la jahazi la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye mfumo wa SUK limeshiba upepo wa Kaskazi na kusi baadaye, Komamanga imelala upande mmoja inakata maji kama papa, Rais Dk Shein amesimama tezi akiangalia Kisiwa cha uhasama,chuki kilichokuwa na siasa za kushupaliana kikitoweka katika ramani ya dunia huku katika upeo wa macho yake kisiwa cha upendo na mshikamano amekikaribia ili kutia nanga.

Mzee Madiba aliamini uhuru binafsi toka gerezani haukuwa jambo la msingi kwake kuliko uhuru wa wengi katika Afrika Kusini ndio maana Dk Shein mara baada ya kushinda Uchaguzi hakutaka,hapendi na hatakuwa dikteta kwa kuwa dhamira yake,misimamo yake ni kuona Zanzibar moja, watu wake wamoja katika ujenzi wa maendeleo endelevu.

Dk Shein ameweka bayana msimamo wake kwamba hatokuwa na mchezo katika suala la umoja,mshikamano na upendo,atawachukia daima wale wanaopinga maridhiano kwa kuwa hawaitakii mema Zanzibar na watu wake.

Kwa viongozi wazalendo wa aina ya Dk Shein ni bahati kubwa kwa Zanzibar kwani tunasikia na kuona katika Mataifa mengine viongozi wasiojali wananchi wao ambao kipaumbele chao ni matumbo yao na familia zao, jamaa zao, lakini uadilifu wa Rais Shein hauwezi kubishaniwa na mtu yoyote yule,labda awe na lake jambo.

Umakini wake ndio umemsukuma katika kipindi cha mwaka mmoja Serikali anayoiongoza kupeleka mswada wa sheria Baraza la Wawakilishi kupambana na rushwa.

Mbali na Rais Dk Shein kuwa muumin wa dhati wa maridhiano,lakini jamii inapaswa kutambua na kuthamini mchango uliotolewa na Rais wa awamu ya sita, Amani Karume kufikia maridhiano kwani angeweza kumaliza muda wake wa uongozi huku akiiacha Zanzibar ikiwa yenye mgawanyiko,lakini Karume hakulitaka hilo kwa uzalendo wake.

Bila shaka Karume ni Kiongozi shupavu ambaye hakuchukua ubinafsi kama dira na mwelekeo wake katika maisha yake ya siasa. Kwa wale wataalam wa Tasnia ya uongozi wanaelewa vyema msamiati wa “The Courage of Leadership.” Ushupavu wa Uongozi.

Advertisements

9 responses to “Dk Shein ni Nelson Mandela wa Zanzibar

 1. Bado ni mapema mno kumwaga sifa nyingi namna hii. Kuna mambo bado hatujayaona hasa yale ya kuwachukulia hatua Wapinga maridhiano au Wahafidhina. Ni kweli Dr Shein ni msafi ila ndani ya Serikali yake mna watu ambao sio wasafi na hawa lazima awakunjulie makucha yake mapema kabla hawajaota mizizi na kuanza kutoa mbegu. Pia kuna kasoro kubwa ya watendaji wengi wasio na uwezo. Wamechaguliwa zaidi kwa sababu ni mtoto wa Bin nani au ni mtoto wa Mwenzetu au baba yake alifadhili ASP. Hili la RUSHWA bado Serikali inanuka rushwa sana. Unaweza kua na sheria kali ya rushwa kama ambavyo Serikali imetunga ila tatizo linakuja kwenye utekelezaji wa hio sheria. Kama nia ni kupambana na rushwa, lazima Dr Shein aache kutazama watu usoni. Waswahili wanasema, Ukitaka kumuua nyani usimuangalie usoni. Kwani wengi wa wala rushwa ni watu waliomzunguka na pia kumpigia debe wakati wa kampeni. Sheria, Sheria, Sheria chambilecho KOMANDOO DR SALMIN.

 2. bado mapema kama ni mkweli aungane na wazanzibar katika kuileta jamuhuri ya watu wa zanzibar pili atowe huyo seif aly idy na muhamed abood na wako watendaji hawana uwezoo ngowa sheni ninamnkubali ila ungana na uamsho na vijana wa kitaisa

 3. EWE MZANZIBAR USIMPIGIE KURA KIONGOZI YOYOTE ASIYESHIRIKI KATIKA HARAKATI ZA KUDAI UHURU WA ZANZIBAR -2012 KUTOKA MIKONONI MWA MAKAFIRI WA TANGANYIKA.

 4. Sifa ni nyingi kuliko alivyo. Mandela kapata tabu nje mpaka jela. Je shein kapata tabu gani baada ya kuupata urais ki ulaini? Afadhali makamo wake wa kwanza Maalim Seif shida alizopata anafanana na Mandela. Ni mapema kumpa sifa hizo wala hastahiki maana kama angekataa kupewa ushindi wa kuiba basi kweli angefanana na Mandela lakini anapewa haki isiyo ya kwake nae anaikubali je uchaMungu uko wapi hapo? Tusiandike makala kwa kutaka sifa au kuitwa Ikulu.

 5. Alieandika makala hii nna wasiwasi ni nduguyake maana anaitwa Juma Mohammed kasoro hakuweka jina la babu tu Shein kama alivyo Ali Mohammed Shein.

 6. Mimi naona bado tuna mda wa kumpima na hawezi kuwa kama Mandela kama mwandshi alivyo fananisha, tuna mengi yanayosubiri maamuzi magumu kutoka kwake:-
  i.Kuwasikiliza Waznzbari kwa hatma yao kuelekea uhuru.
  ii.Hatima ya Znzbar kama nchi huru
  iii.Kujitoa Znbar ktk muungano wa kidhalimu.

  Atakapoyakamilisha hayo ndio tunaweza kumwagia sifa kamahizo, otherwise hastahiki kupewa sifa hizo.

 7. Juma unegeandika juu ya kiti chochote lakini si kumfananisha Dr. Shein na Mandela. Mandela ni wa aina yake katika viongi wa Karne ya 20. Dr. Shein sasa ni mwaka kashindwa kuleta ” reconclliation” kama tulivyo tarajia! Masheha MDCs na RCs ambao waliktaa na wanaendelea kukataa muafaka bado wamo ndani ya Serikali! Dr. Shen kama ni kusifiwa basi ni kukaa kwake kimya watu wakaendelea kupokea na kutoa rushwa, ofisi za serikali zikabinfasishwa na vyombo vyake kutumiwa bila mpango!

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s