Viongozi wanachuma madhambi tu

Katibu Mkuu wa wizara ya Habari, Utalii, Utamdini na Michezo Ali Saleh Mwinyikai

Na Jabir Idrissa

WATENDAJI wa staili ya Ali Mwinyikai wamejaa serikalini. Hawajali kama wanakosea, asilani abadan. Hawajali kwa sababu labda wanajua, hata wakibainika kutenda sivyo, wanaachwa vivyo. Huu ni utamaduni uliozoeleka katika serikali ya Zanzibar – wakosaji kulindwa.

Hakuna wamuogopae.

Wahasibu fulani walipata kunieleza miaka miwili iliyopita, mkasa wa kuhamishwa kutoka Wizara ya Fedha kwa sababu tu hawaelewani na Mhasibu Mkuu wa Serikali.

Niliripoti mkasa huu lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa kutazama maslahi ya wahasibu hawa. Na inajulikana wazi jinsi wahasibu walivyo wachache nchini.

Jamii inayopiga hatua ya maendeleo, hata kusifiwa na jamii nyingine, huwa inaamua hasa kujali utu, muda, raslimali za nchi, haki, usawa na inaridhia haja ya kila mtu kupata fursa ya kutenda linalomsaidia kuendelea na papohapo kuendeleza nchi yake.

Watu hawajui. Penye jamii inayoishi katika kuamini mambo hayo muhimu maishani, amani husawiri. Amani husawiri pasipo chuki, fitina na hasadi. Watu ni kupendana tu.

Watu wakiwa wanaamini katika kupendana tu, hapana shaka watasaidiana, na watakuwa kwa makusudi mazima, wanaamua kuipenda nchi yao .

Watu wanaopenda nchi yao , wanakuwa tayari kuisaidia iendelee mbele – kule kwenye asali, maziwa na ma apple aliyowahi kuyaahidi Dk. Salmin Amour Juma.

Watu wa namna hiyo siku zote huwa tayari kila mmoja kwa nafasi alipo, kutoa mchango unaolenga kuiwezesha nchi kupata maendeleo na mafanikio.

Zanzibar, kwa muda mrefu, kumekosekana jamii iliyoshikamana sawasawa. Zilipokuja tena siasa za ushindani, mfumo wa vyama vingi, mwaka 1992, ilitarajiwa mambo yabadilike kuwa mazuri. Wapi!

Mambo yalizidi kwenda kombo. Ubinafsi, siasa za chuki na fitina ukaoteshwa kuanzia juu ya safu ya uongozi wan chi mpaka chini mitaani. Viongozi wa serikali waliamua kutumia siasa kuendesha udhalimu.

Hawakuchagua kamwe uongozi mwema ili kuleta neema katika nchi. Hawakuchagua uongozi mwema ambao ungeiinua nchi na kuondokana na barabara mbovu, kilimo duni, uvuvi wa kale, usafiri wa hatari wa baharini na kwa jumla uchumi dhaifu.

Walichagua siasa za chuki. Wakaziamini na kuziendekeza. Wakaachia hata wananchi kwenye mitaa waishi kwa kuchukiana na kufitiniana. Basi jamii ikazidi kugawanyika. Masikini, siasa chafu mkosi.

Siasa wenzetu wameitumia kujenga jamii zao, wamefanikiwa. Leo, tunaona baadhi ya zile nchi zilizopata uhuru nyakati zinazokaribiana nasi, na zenyewe zikiwa hohehahe wakati ule, zimepiga hatua isiyo kifani ya mafanikio, zinang’ara.

Nitaje Oman, nchi iliyokuwa haina cha maana wakati Zanzibar inapata uhuru wake tarehe 10 Desemba 1963 na baadaye serikali yake huru kupinduliwa siku 33 baadaye kwa mapinduzi.

Haikuwa na chochote ilipoachiwa na Waingereza miaka ya 1970 baada ya kuwahi kukaliwa na Wareno hadi mwaka 1650. Misuguano ya koo ilikoma mwaka 1975.

Ilikuwa jangwa tupu na shida kubwa ya maji. Leo ina kila kitu na moja ya nchi zilizofanikiwa sana kimaendeleo katika eneo la Ghuba ya Uajemi.

Nyingine ni Singapore . Nayo ilikuwa ovyo wakati inapata uhuru 9 Agosti 1965, miezi 19 baada ya mapinduzi ya Zanzibar , 12 Januari 1964.

Nchi hizo leo siyo tu zimepiga hatua, bali zinaitwa za dunia ya kwanza. Kihistoria , Oman kwa sehemu kubwa imejengwa na Wazanzibari waliokimbia hatari ya kuuawa baada ya mapinduzi.

Walifikaje walipo leo? Tuna mambo mengi ya kujifunza kwao na kuyaiga kwa manufaa ya kubadilisha hali za watu wetu. Walifanyaje?

Haya ndio masuala ya kuyatafakari. Jambo lolote la kimaendeleo lazima lianzie kwa viongozi. Wao wakishashiba elimu ya kutenda mema, wanaowaongoza huwa rahisi kufuata.

Uongozi ndio kioo cha jamii. Wanachokifanya viongozi watu hukiamini na kuamua kukiiga. Kweli, viongozi wa Zanzibar walipoamua kuongoza kikatili, na watu walichinjana, walichukiana na kufitiniana.

Basi viongozi waongoze kwa mema siyo mabaya. Kiongozi aongoze kwa kujua hasa ana jukumu kusaidia mambo kwenda mbele, siyo kuyarudisha nyuma.

Kiongozi atambue wajibu wake ni kutengeneza vitu ambavyo vikileta tija, matunda ya tija hiyo yafikie na kuenea kwa wananchi.

Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Wananchi (CUF) mwaka 2010, ilinivutia sana . Ilikuwa na jambo muhimu la kuleta uongozi mwema katika nchi kuanzia na kwenye serikali.

Hawakupata ridhaa ingawa waliitarajia na hakika walihakikishiwa kwingi walimopita kuinadi ilani yao . Hawakupata ridhaa; angalau waliyoyakusudia yangechukuliwa na kufanyiwa kazi. Hili si baya.

Nataka kuamini hasa kuwa staili ya uongozi inayoendelea kushuhudiwa ndani ya serikali, inathibitisha pasina shaka kuwa uongozi mwema ungali ndoto serikalini.

Yale niliyobainisha katika makala iliyopita, kuhusu wizara ya habari, utamaduni, utalii na michezo, ndio ushahidi. Hakuna dhamira ya uongozi mwema serikalini.

Haiwezekani katibu mkuu wa wizara anafikia kuandika barua ya “kuzuia” ajira za watumishi bila ya kuwaeleza tuhuma zao na kuwapa nafasi ya kujitetea.

Zile nchi zilizofanikiwa kimaendeleo ndani ya miaka 30, viongozi wake waliamini katika kujali raslimali, ya watu ni moja wapo. Huwezi kuendelea kwa kuwa na wafanyakazi waliojaa hofu – hawajatulia akili.

Ukishakuwa na ardhi hata ndogo, unahitaji watu kuendelea. Siasa safi na uongozi bora hufuata. Zanzibar ardhi ipo, japo haitoshi, watu Alhamdulillah, wapo, tena wasomi wa kutukuka wa fani tofauti. Nini tena?

Wazanzibari wanahitaji uongozi bora. Uongozi bora unatarajiwa kuiendesha siasa iwe nzuri, iliyonyooka; siasa inayozingatia umuhimu wa serikali kubadilisha hali za wananchi.

Siasa njema iondoe chuki, hasadi, hasama, jeuri, udhalilishaji, ukandamizaji na maonevu ya aina nyingine yanayodhoofisha umoja wa kitaifa katika jamii.

Je, Zanzibar tunaweza kujivuna kuwa viongozi waliopita na waliopo sasa wametoa mchango katika kuelekeza watu kupata neema? Nisaidieni kujibu.

Nimekuwa nikiona viongozi wananeemeka. Pengo la wananchi masikini na wale wanaoshiba na kwa wakati muafaka, linazidi. Kweli, kiongozi upo furahani huku watu wakizidi ufukara?

Hizo ni siasa muflis. Wananchi wanabaki wanyonge katika nchi wanayoipenda. Kwa hakika kabisa, kwa siasa hizo, viongozi wajue wanachuma dhambi tupu.

Nashajiisha viongozi kubadilika. Watambue wajibue wao. Watambue dhamana waliyopewa na wananchi wenyewe. Watambue kuwa kuna leo na kesho, na huko twendako waataulizwa walitumikiaje wananchi waliowaamini?

Najiuliza mpaka leo, hivi uko wapi ule mji wa kisasa uliokusudiwa kujengwa Fumba? Nani amegawa maeneo ya misitu na ardhi adhimu ya Masingini, Kizimbani, Selem, Tunguu, Micheweni, Wete, fukwe mwanana za baharini, zikiwemo zilizoko kwenye visiwa vidogo vya kitalii Unguja na Pemba ? Nani?

Ugawaji holela wa raslimali ardhi umesaidia vipi kubadilisha hali za wananchi walio karibu na maeneo haya au waliokuwa wakiyatumia kujipatia riziki?

Advertisements

5 responses to “Viongozi wanachuma madhambi tu

  1. WAPE VIDONGE VYAO sHKH JABIR MAANA HAWA NI KAMA MBUZI HATA UKIWAPIGIA GITAA HUA HAWASIKII. UROHO WA MALI NA MADARAKA UMEWAJAA. WANASAHAU KUA CHEO NI DHAMANA NA KESHO MBELE YA HAKI WATAULIZWA. WALE WALIOFURUTU ADA MWENYEZI MUNGU ATAWAONYESHA KABLA YA KUFIKA HUKO. DUNIA NJIA TUNAPITA TU. HATA UKIWA NA CHEO NA MAGARI NA MALI UTAYAACHA HAPAHAPA. KWA MUNGU KIONGOZI NA OMBAOMBA WOTE SAWA TU.

  2. Jamani huku zanzibar ni ukweli usiofichika kuwa viongozi waliowengi si waadilifu na si wawajibikaji kwa wananchi wao. MAFISADI WA ZANZIBAR HAWAVUI GAMBA WAANDISHI WA HABARI MFUATILIENI JUMBE WA FISHERIES AMEIBA COMPUTER ZA MACEMP.

  3. Jabir

    Ni sawa unayosema matarajio yetu yalikuwa makubwa kwa Serikali ya Umoja wa kItaifa lakini Wapi. Hutoba ya Waziri fulani Barazani iliwataja watu wa kundi fulani kuwa wanaongoza kwa uharibifu wa fedha ya Serikali. Because of this government to able adrees itself to inpunity this group linaendelea na Serikali iliwashutumu kwa kuiharibia fedha yake! siajabu kwa Zanzibar kuona mtu binaffsi anafanya atakavyo kwa kuwa mfumo rasmi haufanyi kazi. Ivo nina asie jua kuwa kuna mashirika ya Serikali watu wamo wao, wake zao, baba zao na hata wakwe zao. Pale ambao kanu za Webber za bureaucracy zinafatwa ” formalization” mtu na mkewe, au mwanawe au mkwewe hawawi na sifa za kupata ajira taasisi moja. Ukisikia Shirika lina wafanyakzai wengi wafagiaji kuliko mafundi hii ni ajabu kwa taasisi ya kiufundi huajiri mafundi na kazi ufagiaji zikafanya on Outsourcing basis. Nenda SUZA kwa mfano wapo wafagiaji wengi kuliko Lectureres! Nenda na pengine utaona hivyo hivyo au pengine zaidi. Hata barani vyama vimepeleka watu watu tu! eti ni wakereketwa !

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s