Tumejitayarisha kwa mvua za masika

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiangalia uchafuzi wa mazingira nje ya uzio wa uwanja wa Amaan wakati alipofanya ziara ya kutembelea maeneo yaliyovamiwa. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na MBM Dr. Mwinyihaji Makame, na katikati (mwenye suti) ni Waziri wa Maji, Makaazi, Maji na Nishati Mhe. Ali Juma Shamhuna

Na Ally Saleh

Leo ni March 28 na kwa mujibu wa kalenda ya misimu tumo ndani ya wiki moja tokea kuanza kwa msimu wa mvua wa Masika kama ilivyo ada ya kila mwaka. Hizi ni tarehe ambazo mwananchi wa kawaida kama ilivyo kwa Serikali, anatakiwa azijue kwa sababu ni tarehe ambazo zina athari katika maisha yetu ya kila siku kwa sababu misimu ni jambo la lazima kwetu. Msimu wa Masika unakuja kuanzia Machi 21 hadi Mei 21 na ndio msimu mkubwa wa mvua katika eneo letu na ndio mvua zinazotegemewa kwa aina nyingi ya kilimo na mazao.

Ni hizi mvua za masika ndizo ambazo huchangia kiasi kikubwa cha upatikanaji wa maji katika nchi zetu, maana mvua hizi ndizo ambazo zinaleta ujazo mkubwa zaidi katika vyanzo vya maji na kwa hivyo pia ni mchango mkubwa katika eneo la umeme.

Hoja yangu mara hii ni kutizama ujio wa mvua hizo za Masika ambazo sasa sio zimepiga hodi, lakini kwa kweli hasa ziko ndani na kwa kweli hasa ni kutizama ni jinsi gani tumejitayarisha kumpokea mgeni wetu huyu ambaye kwa njia zote ni mgeni mwenyeji.

Lakini mgeni mwenyeji huyo mbali ya kutuletea neema ambazo nimezitaja hapo juu, kwa bahati pia mara kadhaa hutuletea ziada ya kheri hizo mpaka zikatuchukiza kwetu hasa iwapo hatujajitayarisha kwa hayo.

Na kwa kweli mara nyingi tunajisahau. Msimu wa mvua ni wa kila mwaka na kila mwaka, au tuseme takriban kila mwaka tunakutwa hatuko tayari kupokea mvua kubwa ambazo msimu wa Masika ndio sifa yake.

Mamlaka ya Hali ya Hewa kila mwaka hutoa taarifa za awali juu ya ujio wa mvua hizo za Masika na mara nyingi hutoa makisio ya kiwango cha mvua kitakacho kuja ingawa kila mtu anajua kuwa mvua za Masika zinakuwa kubwa.

Lakini pengine kutokana na kutoboka kwa tabaka la Ozone na mabadiliko ya tabia nchi, ujio wa mvua inawezekana umeathirika kwa njia moja au nyengine lakini bado hakuondoi ukweli kuwa Masika ndio mvua kubwa kwetu na huja na hizo neema na hizo ziada za neema nilizozisema.

Mvua inahitajika lakini ikiwa nyingi, kwa kukosa matumizi ya neno bora, inakuwa ni kero na kero hiyo mara nyengine hupelekea kuzuka kwa majanga kama vile ya mafuriko, miripuko ya maradhi na hata madhara mengine mengi ambayo ni hatarishi kwa binaadamu.

Tuanze kwenye mafuriko. Tuna ushahidi wa kutosha wa matukio ya mvua kusababisha mafuriko kwenye makaazi na kuziharibu nyumba za wakaazi na kupelekea watu kukosa makaazi.

Mara nyingi mafuriko hutokea kwa sababu ya kukosa kujitayarisha na sio tu milimita nyingi za maji kumiminika kwa muda mdogo au kuendelea kumiminika kwa muda mrefu. Kwa maana nyingi mvua nyingi hazileti hasara kama kuna matayarisho.

Matayarisho yepi? Moja wapo ni elimu kwa raia na hasa kuwakumbusha kuwa mvua kubwa zinakuja na kila mmoja kwa nafasi yake atizame ni kitu gani anaweza kufanya ili kujilinda na kuwalinda wengine.

Pili ni kwa Serikali kuhakikisha kuwa kama kuna mitaro au mifereji yoyote katika maeneo yetu imezibuliwa au imefunguliwa ili maji yapite katika mikondo yake na yasituwame au kwenda katika njia yasikopangiwa na hivyo kuleta hiyo hasara tunayosema ambayo hatimae huwa mzigo kwa Serikali.

Ni wakati sasa, kama kwa kweli haikuwa jana na juzi, kwa Serikali kufanya ukaguzi katika maeneo mbali mbali, hasa yale ambayo mafuriko hutokea mara kwa mara, ili kuhakikisha usalama wa maeneo hayo kabla ya mvua za Masika kuchanganya.

Lakini badala ya mitaro na misingi kuzibwa, sehemu kadhaa za Wilaya ya Mjini utaona ndio kwanza mitaro imechimbwa na imewachwa wazi. Mtu unafika kujiuliza huyu ni mkandarasi wa aina gani anaechimba mitaro wakati wa mvua za Masika.

Moja ya mtaro huo uko Jan’gombe ambako mwaka jana tu mtoto mmoja alifariki kwa kuingia katika mtaro huo lakini pia ni wazi mtaro kama huo utakuwa ni chanzo cha maji kukusanyika na kuingia mitaani na kuweza kusababisha madhara.

Mbali ya suala la mitaro, lakini jengine ni lile la uchafu na taka ambazo Manispaa haiwezi kukusanya sehemu kubwa ya taka zinazozalishwa kila siku hapa Zanzibar ambazo kwa takwimu zangu za mwisho nilizokuwa nazo ni kuwa huzalishwa tani 250 kwa siku.

Hivi sasa kwa uwezo huo mdogo wa Manispaa kuna sehemu kadhaa ambazo taka zimerundikana na kushindwa kukusanywa kwa siku kadhaa na huku tukijua mvua huambatana na miripuko ya maradhi kama cholera au mengine ya matumbo.

Hatujakuwa kabisa na uwezo wa kujilinda na maradhi ya miripuko na huwa ni utata zaidi iwapo maradhi hayo yakishakutokea. Tunajijua jinsi tunatapatapa maradhi hayo yakitokezea kwa kuhangaika kwa madawa, vifaa na hata maeneo ya kuwatibia wagonjwa tukijua kuwa hata hospitali zetu huwa hazitoshi.

Na si sisi Waswahili ndio ambao tunasema kinga ni bora kuliko tiba? Kwa nini Serikali isitumie muda huu kwa kuongeza fedha na vifaa kwa Manispaa na kuimarisha ushiriki wa umma katika kuhakikisha usafi zaidi katika maeneo yetu kujiepusha na uwezekano wa miripuko hiyo ya maradhi?

Lakini pia huu ndio wakati wa Kamati ya Majanga kujitayarisha kwa umakini zaidi kwa vifaa vyote na dawa ili likitokea la kutokea basi tuwepo pazuri zaidi kufanya kazi kwa kasi kunusuru maisha ya watu wetu.

Upande mwengine ambao unahitaji ufanyiwe kazi ni ule wa kilimo. Kilimo chetu ni cha kumwagilia maji lakini tunashindwa kuyatumia vyema maji ya neema yanayokuja kila msimu wa Masika zaidi ya ule muda wa Masika yenyewe. Tumeshindwa kabisa kujikusuru kuyatunza na kuyakusanya maji yatufae nje ya kipindi cha Masika.

Hali kadhalika tumejipweteka sana katika suala la kuyalinda maji vyema ili yaingie katika mfumo wetu wa maji ambayo tunayatumia kwa matumizi yetu mbali mbali na ya kila siku. Maji mengi ya mvua hayaingia katika mfumo wa vyanzo vyetu na hupotea na kwenda arijojo mara baada ya neema ya kushuka kutoka mawinguni.

Kwa hivyo napenda kutoa wito kwa Serikali kuu nayo itoe wito kwa Serikali zake za Wilaya na Mikoa na taasisi nyengine nyingi zinazohusika na kilimo, afya, maji, mazingira, mawasiliano ili nazo kila moja ichukue wajibu wake katika kujitayarisha kwa mvua hizo za Masika.

Isiwe kila siku tunakamatwa suruali kiunoni tukiadhirika kama tusiokuwa na mipango wakati tuna uwezo wa mipango na kila aina ya matayarisho maana sisi ni nchi na nchi ambayo sio tu ina ustaarabu wa karne nyingi lakini pia ni nchi ambayo ina uzoefu wa kila aina na uzoefu huo ndio ambao unapaswa kutuzindua juu ya matendo yetu ambayo lazima siku zote yalenge kwenye maslahi mema ya wananchi wetu.

Advertisements

2 responses to “Tumejitayarisha kwa mvua za masika

  1. Big up. Hii ni story nzuri tu. Another side of the coin (Ally Saleh). Take this to the stream media.

  2. ZANZIBAR BILA ZA KUPATA UHURU KUTOKA MIKONONI MWA MAKAFIRI WA TANGANYIKA BASI ZNZ HAITAENDELEA MILELE. Ewe mzanzibar usimpigie kura kiongozi yoyote asiyeshiriki katika harakati za kudai UHURU WA ZANZIBAR-2012 Kutoka mikononi mwa MBWA WEUSI WA TANGANYIKA.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s