Polisi Jamii Zanzibar ni Janjaweed

Salim Said Salim

Vikosi vya ulinzi na usalama vya serikali Zanzibar vilivyokuwa ikiitwa 'Janjaweed' kutokana na kuwapiga na kuwaadhibu wafuasi wa CUF wakati wa chaguzi mbali mbali zilizowahi kufanyika hapa nchini, wananchi wengi walikuwa hawana imani na vikosi hivi lakini sasa Alhamdulillah wamebadilika

TANZANIA ni nchi yenye misimu sio ya hali ya hewa tu na baadhi ya mazao kuonekana kwa muda maalum katika mwaka, bali pia wa matukio mbali mbali. Hata baadhi ya maneno yanayotumika katika maisha ya kila siku huwa ya msimu. Maneno haya yanapoingia mitaani utaona watu wengi hutafuta kisingizio, hata kikiwa hakina mshiko, cha kutumia neno hilo ili naye aonekane anakwenda na wakati na hajaachwa nyuma.

Katika miaka ya mwisho ya 1980 kila pembe ya nchi zilisikika sauti za watu wakizungumzia “woo…woo…woo”, yaani kina dada wanene; baadaye tukasikia “Da Mwati” (hawa ni watu waliovaa nguo ya rangi ya njano). Hii ilipelekea soko la nguo na vitambaa vya rangi ya njano nchini kuporomoka kwa vile walichelea kuchekwa wakionekana wamevaa “Da Mwati”.

Hivi karibuni watu ambao mambo hayakuwaendea vizuri wakaelezwa kama “wamefulia”. Hapo tena kila mtu akaonekana kuhangaika kupata sababu ya kumueleza mwenzake kuwa kafulia. Haukupita muda ukazuka utapeli wa kuchanganya mafuta na kupewa jina la “kuchakachuwa”.

Hii ndio Tanzania yetu, bara na visiwani. Kila kinachoingia mjini au kijijini utaona kinapokewa kwa shangwe na kila mtu hutaka naye awe nacho na kama ni msemo basi aonekane anajua kuutumia.

Siku hizi imekuwa kawaida akitokea mtu kuanzisha katika eneo moja aina ya biashara basi kila mfanyabiashara naye atafanya biashara hiyo; na kama mtu kafungua kijiduka mtaani cha kuuza pilipili na ndimu wengine nao watafanya hivyo.

Kilichoingia nchini kwetu sasa ni hicho kinachoitwa “Polisi Jamii” au polisi shirikishi. Siku hizi katika kila pembe kunaanzishwa vikundi hivi vya ulinzi, bila ya maandalizi mazuri.

Sababu kubwa ni kwamba kama watu wa maeneo mengine wameanzisha polisi jamii kwa nini na wao wawe nyuma? Hapo tena vibaka, watumiaji gongo na dawa za kulevya na hata majambazi husonga mbele na kujiunga na polisi jamii.

Wakati hali ni nzuri katika baadhi ya sehemu, kama Mji Mkongwe na Mpendae, sura isiyofurahisha inaonekana katika sehemu nyingi za Mji wa Zanzibar na vitongoji vyake.

Hii inatokana na vibaka kupata sehemu salama ya kujificha na kuweza kufanya uhalifu wao kwa “njia halali”. Hawa wanaoitwa polisi jamii hivi sasa ni kero na wamezusha balaa kubwa Zanzibar.

Karibu katika kila sehemu watu wanalalamika kupigwa, kuibiwa, kuteswa na kudhalilishwa na hawa polisi jamii. Ni balaa ya aina yake.

Nimeshuhudia mara mbili mnamo kama saa 3 usiku katika maeneo ya Kianga, nje ya Mji wa Zanzibar, vijana hawa wanaobeba jina la polisi jamii wakiwa barabarani na kuwasimamisha wenye pikipiki na vespa na kuwatandika mijeledi.

Wapo wanaodai kuporwa fedha na simu za mkononi.

Hali haitofautiani na wakati wa utawala wa Rais wa Awamu ya Nne, Komandoo Salmin Amour Juma. Wakati ule vijana waliojulikana kama Janjaweed walipiga sana watu mitaani na majumbani na hata kuuwa watu sehemu mbalimbali za Unguja na Pemba kwa madai ya kulinda heshima ya utawala wa Komandoo.

Uhuni huu ulisitishwa baada ya kuwapiga bakora Abeid, mtoto wa Rais mstaafu Amani Karume, na aliyekuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Utawala Bora na sasa Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Makungu.

Hakuna mtu aliyewajibishwa kisheria kwa uhalifu ule na mateso haya ni miongoni mwa mambo yaliyopelekea watu kutosahau utawala wa mabavu wa Salmin.

Leo Komandoo, hata waliokuwa wakimpigia debe na Janjaweed wake, wapo mbali naye. Hili ni somo kwa kila mmoja wetu.

Hivi karibuni mzozo mkubwa ulitokea Mwanyanya, mjini Unguja, ambapo hawa askari jamii walivamia majumba na kupiga watu.

Kinachosikitisha ni maelezo waliyoyatoa watu wa eneo hilo kupitia vyombo vya habari, akiwemo Mwakilishi wao, kwamba yupo askari polisi aliyeshirikiana kikamilifu na hawa polisi jamii kufanya uhuni na uhalifu ule.

Wakati umefika wa kujuliza: polisi jamii, kwa hali ilivyo sasa Zanzibar, inasaidia kuondoa au kuongeza uhalifu visiwani.

Kwa mtazamo wangu kutokana na ninayoyaona na kuyasikia, hali ni mbaya na inawatia watu wasi wasi na kuona aina mpya ya Janjaweed imeruhusiwa na serikali iliyo madarakani hivi sasa.

Ukweli ni kwamba watu wengi hivi sasa wanaishi kwa hofu na katika maeneo mengi ya visiwani wananchi wanawaona polisi jamii kama kizazi cha Janjaweed. Huu ndio ukweli. Ni vyema kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo imetokewa kupendwa sana na watu kujenga matumaini ya kheri huko usoni ikaliangalia suala hili kwa kina na kuchukua hatua za kurudisha imani ya wananchi kwa serikali na Jeshi la Polisi.

Ni vyema kufanya uchunguzi ni nani waliojiunga na polisi jamii na kutengeneza utaratibu utakaohakikisha kwamba majambazi na vibaka hawapati mwanya wa kujiunga na polisi jamii na kuendeleza wizi na ujambazi wao.

Huu mtindo wa kupokea na kufurahia kila jambo jipya kama tulivyozoea kupokea maneno ya mtaani ya Da Mwate au kusema fulani amefulia utatuponza na gharama zake ni kubwa sana.

Tunapoamua kuwachagua vijana kujiunga na Jeshi la Polisi au kuwa polisi shirikishi basi ufanywe uchunguzi wa kutosha wa hao wanaotaka kuiunga. Tuwe macho na makini.

Matukio mbali mbali ya watu kutotendewa haki na polisi jamii yaliyolalamikiwa katika sehemu mbali mbali za Zanzibar yanapaswa kutupa mafunzo ya kujirekebisha haraka sana.

Vinginevyo, tutakuwa tunatengeneza mazingira ya kuruhusu vibaka na majambazi kufanya maovu yao kwa mapana na marefu, mchana na usiku, na hakuna anayeweza kuwasumbua.

Watu wa Zanzibar wameishi katika maisha ya hofu na mateso kwa miaka mingi, tokea zama za lile liliokuwa linaitwa Jeshi la Valantia (askari wa kujitolea) mara baada ya Mapinduzi ya 1964. Hivi sasa migongo yao imechoka kucharazwa bakora.

Wanachotaka ni kuheshimiwa kama watu na kupewa haki zao za kimaisha na kuweza kuishi na kufanya kazi bila ya hofu.

Sio busara kufumbia macho vitendo vya uonevu; kwani umma ukichoka kustahamili tunaweza kujikuta katika hali mbaya zaidi. Ni wajibu wetu kuhakikisha polisi jamii inatumikia umma na sio kutesa watu na kuwaibia mali zao.

CHANZO: TANZANIA DAIMA

Advertisements

2 responses to “Polisi Jamii Zanzibar ni Janjaweed

  1. DUH! JANJAWEED NOMA WANAKUNUTA VIBAYA SANA HAWA. HIVI NI KWELI POLISI JAMII NI JANJAWEED. HICHI KITU MIMI NA PINGA KWANI POLISI JAMII WAMETUNGUZA UHALIFU ZANZIBAR KWA 89% UKIZINGATIA JANJAWEED WALIKUWA NI WAHALIFU KWA 100%

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s