Maprofesa wazalendo waahidi kuisaidia Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,akizungumza na Ujumbe wa wahadhiri wa Kimataifa (wazalendo) walioshiriki katika warsha ya utayarishaji wa
Mitaala ya masomo ya Uzamili na Uzamivu katika Kiswahili,ukiongozwa na Mwenyekiti wao Prof Said Ahmed wa Ujerumani, (wa pili kulia) walipofika Ikulu Mjini Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amekutana na Wahadhiri wa Kimataifa wakiwemo wenye asili ya Zanzibar na kupongeza azma yao ya mikakati ya kutaka kuanzisha masomo ya Uzamili, Uzamivu na Uzani katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA). Dk  Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar, wakati alipokuwa na mazungumzo na Wahadhiri hao wa Kimataifa ambao walikuja hapa nchini kwa lengo la kutayarisha Mitaala ya Masomo ya juu ya Kiswahili kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha SUZA.

Miongoni mwa Wahadhiri hao ni Profesa Abdulaziz Lodhi kutoka Sweden, Profesa Said Ahmed kutoka Ujerumani, Profesa Mohamed Bakari kutoka Uturuki, Profesa Saida Yahya kutoka Chuo Kikuu cha Dar-es Salaam, Dk. Farouk Topan kutoka Uingereza na Dk. Alwiya Omar kutoka Marekani wakiwa na wenyeji wao uongozi wa chuo cha SUZA.

Katika maelezo yake Dk. Shein aliwaeleza Wahadhiri hao kuwa yeye mwenyewe binafsi amefurahishwa na hatua yao hiyo ya kuonesha uzalendo mkubwa wa kuimarisha sekta ya elimu hasa katika lugha ya Kiswahili ambayo ina chimbuko kubwa hapa Zanzibar.

Dk. Shein alitoa pongezi kwa Makamo Mkuu wa Chuo cha SUZA Profesa Idrisa Rai kwa juhudi zake za kuwatafuta wahadhiri hao na kukaa nao pamoja kwa lengo la kutayarisha Mitaala ya Masomo ya juu ya Kiswahi katika chuo kikuu hicho.

Alieleza matumaini yake makubwa kutoka na Wahadhiri hao kuwa na uzoefu mkubwa wa kusomesha katika vyuo vikuu mbali mbali duniani na kueleza kuwa uzoefu wao huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo yaliyowekwa na chuo kikuu cha SUZA.

Dk. Shein alieleza kuwa Kiswahili kinataka kuendelezwa ili kiweze kukuwa zaidi duniani na kutokana na kuwa lugha hiyo hapa Zanzibar ni kwao ipo haja kuikuza na kuiimarisha zaidi ikiwa ni pamoja na kuendelea kutunga na kuandika vitabu vyenye mnasaba na lugha hiyo sanjari na kuwasomesha vijana waliowengi lugha hiyo katika elimu yao ya juu.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa umefika wakati kwa lugha ya Kiswahili kutumika katika kusomesha masomo mbali mbali katika vyuo nchini licha ya kuwa hatua hiyo iliwahi kuanzishwa lakini ilishindikana.

Alisema kuwa viongozi waasisi wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume walifanya jambo la maana la kukitangazia Kiswahili kuwa ni lugha ya Taifa, hatua ambayo imesaidia kukiendeleza kiswahili lakini hata hivyo ipo haja ya kukiimarisha zaidi ili kitumike zaidi kutokana na kukua kwake.

“Wenzetu baadhi ya nchi lugha zao za taifa ndizo wanazozisomeshea vyuoni mwao mwote……lengo na nia yetu ni moja na katika kukiendeleza na kukiimarisha Kiswahili na ifahamike kuwa Zanzibar itajengwa na Wazanzibari wenyewe”,alisema Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa licha ya kuwepo changamoto kadhaa katika uanzishwaji wa masomo hayo lakini juhudi za makusudi zitaendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha lengo linafikiwa huko akisisitiza haja ya kuwashajiisha vijana kuanza kusoma lugha hiyo kwa kiwango cha elimu ya juu.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alisisitiza haja ya kuwa na watafiti wa Lugha ya Kiswahili wa kutosha kwani wanahitajika zaidi katika kuiimarisha lugha hiyo na kueleza kuwa hivi sasa kiswahili kina changamoto nyingi kutokana na kukua na kuanza kutumika ambapo miaka minne iliyopita kimeanza kutumika katika mikutano ya Umoja wa Nchi za Afrika.

Alieleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete aliweza kuhutubia kwa lugha ya Kiswahili katika mkutano ya Umoja huo mnamo mwaka 2006 kwa kuonesha wazi upana na ukubwa wa lugha hiyo Kimataifa hivi sasa.

Sambamba na Dk. Shein alisema kuwa kwa upande wa Umoja wa Mataifa tayari mchakato unaendelea wa kuiimarisha lugha ya Kiswahili ambapo tayari kuna baadhi ya machapisho yameanza kuchapishwa kwa lugha hiyoya Kiswahili.

Nao Wahadhiri hao walimuhakikishia Dk. Shein kuwa wataendelea kutoa mchango wao mkubwa katika kuhakikisha azma hiyo ya Chuo na Serikali ya Mapinduzi kwa ujumla inafikiwa huku wakitambua kuwa wanachokifanya kitasaidia nyumbani. Wahadhiri hao pia, waliahidi mashirikiano zaidi na kujitolea kwa moyo wao wote.

Nae Makamo Mkuu wa Chuo Hicho alitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein na kumueleza kuwa hatua hiyo ni juhudi za kutekeleza maagizo yake katika kukiimarishwa Kiswahili hapa nchini, kwa kutambua kuwa lugha ya Kiswahili ina historia kubwa hapa Zanzibar.

Aidha, alieleza kuwa Wahadhiri hao wamekubali kuutumia muda wao kwa wale watakao pata nafasi ya kuja kusomesha wakati wao wa mapumziko na baadae kuweza kuwasiliana na wanafunzi wao kwa kutumia njia mbali mbali ikiwemo njia ya Teknohama.

Advertisements

4 responses to “Maprofesa wazalendo waahidi kuisaidia Zanzibar

  1. We raelly need comitte people like these professors. Wazanzibari popote pale mlipo Maprofesa wametuonyesha njia. Tuachane na siasa za kijinga tujenge taifa letu la Zanzibar. Wa Israel popote pale walipo duniani pia ni raia wa Israel na wana haki zote. Sisi bado mpaka leo kuna Wazanzibari wa asili fulani wana haki ya mambo fulani nusu tu. Kama kiongozi wa juu wa nchi atakua mkweli na kusimama juu ya kauli yake basi tunaamini Taifa la Zanzibar litakua ni fundisho kwa majirani zetu. LONG LIVE REPUBLIC OF ZANZIBAR.

  2. thts gr8.
    I like it.
    I hop other Zanzibari professors who are in different countries may come back so as 2 rise SUZA 2 be among the best quality International Universities.

  3. laiti ningekuwa professor, nisingerudi nyuma ningeungana na maprofessor wezangu kulifanikisha hili. m/mungu awape moyo wa uzalendo waendelee kutusaidia na kukuza chuo chetu cha taifa ca SUZA.

  4. Maprofesa hawa na Madaktari waje kabisa wazalishe Wazanzibar watakao hitimu masomo ya kweli na kisha waongoze kuelekea kupata jamii ya watu walioelimika kwa kuwa hili litapunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi. Mapofesa anzeni Zanzibar inaelekea siko – ni Bora kuwa na Population kubwa iliyosoma na kuelemika hata kama itakuwa shida kuiajiri.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s