Ripoti ya uchunguzi, chanzo cha udanganyifu wa mitihani

Mwanasheria wa Kamati ya Wazazi ya kushughulikia matokeo ya kidatu cha nne na Mkurugenzi Mtendaji (DCPM) Najma Murtaza Giga akitoa hutuba katika kongamano la leo lililofanyika Aecrotanal Mjini Zanzibar kushoto ni Mjumbe wa kamati hiyo Abdulkadir Mohammed Aboud

Wakati NECTA imetoa ushahidi, kwa kutumia barua za walimu wachache sana, wanaosemekana kuiandikia barua NECTA kwamba wamekubali kuwa udanganyifu umefanyika na wanafunzi, na kwamba wanaomba wasamehewe, sisi katika uchunguzi wetu tumegundua kuwa, baadhi ya waalimu, waliiandikia NECTA barua ya kutoridhika na maamuzi yake, kwa kutowashirikisha wakuu hao, lakini hawakupata jibu lolote, pamoja na kuwa madai yao mengi yalikuwa na msingi. Kwa upande mwingine, tumegundua kuwa baadhi ya waalimu, waliandika ripoti ya yale yaliyotokea wakati wa mitihani, mara tu baada ya mitihani kumalizika, na kupeleka wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali hapa Zanzibar. Jambo la kushangaza ni kwamba, barua na ripoti kama hizi NECTA hatujasikia kuzitaja. Hivyo kutokana na hali kama hii, bado tunapata mashaka makubwa na utendaji huu wa taasisi hii na wizara kwa ujumla.

JUMUIYA YA KUZUIA, KUKINGA NA KUONDOSHA MAAFA NA MAJANGA ZANZIBAR (ZANZIBAR DISASTER CONTROL PROTECTION AND MANAGEMENT ORGANIZATION) DCPM

21/03/2012

RIPOTI YA UCHUNGUZI KUHUSU CHANZO CHA UDANGANYIFU ULIOFANYWA NA WANAFUNZI KATIKA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE MWAKA 2011 ZANZIBAR

UTANGULIZI
Ni muda wa mwezi mmoja hivi sasa, tokea tutoe ripoti yetu ya tathmini, ya matokeo ya mtihani wa kidato cha nne, uliofanywa mwaka 2011, na athari zake kwa mustakabali wa elimu ya sekondari hapa Zanzibar.

Ripoti hiyo ya awali, ambayo ilibeba zaidi hoja za kisheria na ushahidi wa kimazingira, tuliwasilisha kwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Ndugu Joyce Ndalichako, kupitia kwa mwakilishi wa NECTA hapa Zanzibar, Maalim Kasim, wiki tatu zilizopita, kwa lengo la kupata ushirikiano wa taasisi hii husika ya serikali, katika kukabiliana na janga hili la kielimu hapa Zanzibar. Hali kadhalika ripoti hiyo tuliipeleka sehemu mbalimbali za wakuu wa serikali hapa Zanzibar, pamoja na spika wa Baraza la Wawakilishi, kama taarifa, kwa vile tuliona ni muhimu na wao, kuwa na taarifa ya jambo hili zito, linaloikabili jamii yetu na taifa kwa ujumla. Mpaka muda huu hatujapokea jibu lolote kutoka NECTA.

Jumuiya ya DCPM na kamati ya wazazi, imesikitishwa sana na ukimya huu wa Baraza la mitihani na wizara zetu za elimu, jambo ambalo limepelekea tuamini kuwa maamuzi ya NECTA yaliyotokana na ushahidi wa kimazingira, wenye mshiko wa hoja zilizojaa shaka umesababisha kuipotosha serikali na hata baadhi ya wajumbe wa Baraza letu la Wawakilishi hapa Zanzibar, kiasi cha kuamini kwamba NECTA iko sahihi. Pamoja na vilio vya jamii kuzidi, na wazazi wengine kupeleka malalamiko yao moja kwa moja, kwa Katibu Mtendaji wa baraza kwa njia ya barua, bado taasisi hii husika ya serikali, haijawa tayari kubadilisha msimamo wake na kusikiliza kilio hiki cha jamii, chenye haki ya msingi za kisheria na kikatiba, huku muda unazidi kupita, na wanafunzi wa kidato cha tano wanaendelea na masomo.

Wakati vilio vya jamii vinaendelea, Jumuiya na Kamati, bado tunaendelea kuipa muda NECTA ili waweze kutafakari zaidi juu ya suala hili, huku tukiwa tunaendelea kuisaidia serikali, katika kufanya utafiti zaidi, kwa vile tunaamini kuwa serikali peke yake, kutokana na majukumu iliyo nayo, inaweza kuchukua muda mrefu zaidi, hadi kugundua chanzo cha tatizo hili, ambalo linaweza kuleta mgogoro wa kisiasa na kidini ndani ya jamii.

Jumuiya pamoja na kamati kwa kiasi kikubwa, zimeweza kubaini, yale yaliwayopelekea wanafunzi, kufanya udanganyifu katika mitihani yao, hali kadhalika makosa yaliyofanyika kabla, na wakati wa kufanya mitihani, pamoja na uzembe uliotokea, hadi kusababisha jambo hili, kukosa uhalali unaostahiki katika kutoa maamuzi.

MATOKEO YA UCHUNGUZI

Chanzo cha wanafunzi kubainika kuwa wadanganyifu katika mitihani.
Baada ya kuzitembelea shule kadhaa, zilizoathirika zaidi na janga hili la kielimu hapa Zanzibar, Jumuiya na kamati imejiridhisha kwa kiasi cha kutosha, kwa vile tayari tuna ushahidi mkubwa, kwamba mitihani ilipatikana mapema sana, kabla ya kufika wakati wake, (“kuvuja kwa mitihani”) na katika uchunguzi wetu tumebaini kwamba, baadhi ya Maofisa wa NECTA waligundua hali hii mapema, wakati mitihani inafanyika, na hivyo ilikuwa ni wajibu wao, kutoa ripoti hiyo kwa Mkuu wao, lakini cha kushangaza, Katibu Mtendaji alisema, hakupokea taarifa yoyote ya kuvuja kwa mitihani.

Miongoni mwa shule tulizotembelea ni: – Hamamni, Jang’ombe, Mikunguni, Chuo cha kiislam, Bilal Islamic Seminary, na Mwanakwerekwe c. Wakati tunaendelea na uchunguzi wetu katika shule nyinginezo, tayari tumeshapata ushahidi wa kutosha kuwa, karatasi za kujibia mitihani, (booklets) ambazo tumegundua kuwa hazina nambari maalum, (yaani “serial number”) zilipatikana mapema. Hii ni kwa mujibu maelezo ya wanafunzi, waliokamatwa na karatasi hizo kabla, na wakati wa kufanya mitihani, na kwa maelezo yaliyotolewa na wanafunzi hao, ni kwamba walinunua booklets hizo kwa bei ya shilingi 5000/= kila moja, kutoka kwa mwanafunzi mwenzao, mtahiniwa wa kujitegemea (Private candidate) wa Kiboje, na kwamba maswali ya mtihani, walitumiwa kwa njia ya ujumbe, kwenye simu na huyo huyo aliyewauzia booklet hizo.

Wakati huo huo mwanafunzi mmoja mtahiniwa wa kujitegemea, (private candidate) alikamatwa na booklets nne tofauti za kujibia maswali, alipokuwa anatoka chooni, booklets ambazo zilikuwa zimeshajibiwa mtihani mzima, ambao ulikuwa unafanyika kwa wakati ule, na kila booklet ilikuwa na nambari tofauti za watahiniwa. Baada ya kubanwa, kijana huyu alisema kwamba, alipata mtihani na booklets hizo kutoka kwa tajiri yake ambaye yuko Mwanza, Tanzania Bara. Kijana huyu alitaja jina la tajiri yake na kutoa nambari ya simu ya tajiri huyo. (Majina tunayahifadhi). Jambo la kushangaza ni kwamba kijana huyu ambaye alikamatwa na karatasi za majibu na ripoti ya udanganyifu wake kupelekwa NECTA, majibu yake ya mitihani yalitolewa, lakini baada ya walimu kuuliza kulikoni, matokeo hayo yakafutwa.

Hata hivyo, ofisa mmoja wa NECTA (jina tunalihifadhi) alikuja katika shule mojawapo, miongoni mwa shule tulizopitia kufanya uchunguzi, na kwamba, kabla ya wanafunzi kuingia katika ukumbi wa mitihani, ofisa huyo aliwakagua, na kuzichukua simu zote alizowakuta nazo wanafunzi hao, pamoja na karatasi walizokuwa wakizisoma, kabla ya kuingia kwenye mtihani. Kwa mujibu wa mashuhuda wawili waliokuwapo na ofisa huyo, walieleza kuwa, ofisa huyo aliwaambia waziwazi kwamba “mtihani umevuja”, kwani yale yaliyomo kwenye karatasi zile, alizozichukua kutoka kwa wanafunzi, na ujumbe uliopo kwenye simu za wanafunzi hao, ndio hasa mtihani uliokuwa unafanywa kwa wakati ule. Pamoja na kuwepo kwa ripoti kama hizi, ambazo tayari tumezipatia ushahidi wa baadhi ya vielelezo, na mashuhuda wenyewe, jumuiya na kamati inazidi kushangazwa kwanini taarifa hizi hazikufika kwa mhusika mkuu.

Pamoja na hayo, jumuiya na kamati zimesikitishwa pia, kuona kwamba siyo siyo ofisa mmoja tu aliyepata ripoti hii, bali kuna baadhi ya maofisa wengine, nao pia walipokea ripoti hii mapema, wakati mitihani inaendelea kufanyika. Jumuiya mpaka hivi sasa haioni sababu iliyowapelekea maofisa hawa kutowasilisha ripoti hizi kule kulikohusika. (Ushahidi wa hayo tunauhifadhi, hadi utakapohitajika).

Ni jambo la kusikitisha kuona kwamba, NECTA imewaandikia barua wakuu wa shule, na kuwaeleza kuwa, wanafunzi wao wengine wamefutiwa matokeo kwa vile skiripti zao za kujibia maswali, zina miandiko ya watu tofauti, na kwamba wataalam wa miandiko wamethibitisha hayo, kwa vile walimu hao na wasimamizi hawakuwa makini, kwa maana ya kwamba, wanafunzi hao inawezekana wameandikiwa, wakiwa kwenye chumba cha mtihani.

Katika uchunguzi wetu tumegundua kuwa, wakaguzi wa NECTA walishabaini kwamba wanafunzi waliandika skiripti hizo nje ya chumba cha mtihani, kwa vile walipokamatwa nazo, zote zilikuwa zimejazwa na huku mtihani ndio kwanza unafanywa, na kwamba mwanafunzi mmoja alikutikana na skiripti zaidi ya moja, ambazo hakuzipata humo kwenye chumba cha mtihani, bali alitoka nazo nje, kabla ya kuanza mtihani. Hivyo, ikiwa NECTA inasema wasimamizi hawakuwa makini, je maofisa wao wa NECTA waliokuja kukagua na wakagundua hali hii mapema, na wakashindwa kutoa ripoti kwa mkuu wao aliyewatuma, Je hawa wana umakini katika kazi yao?

Wakati NECTA imetoa ushahidi, kwa kutumia barua za walimu wachache sana, wanaosemekana kuiandikia barua NECTA kwamba wamekubali kuwa udanganyifu umefanyika na wanafunzi, na kwamba wanaomba wasamehewe, sisi katika uchunguzi wetu tumegundua kuwa, baadhi ya waalimu, waliiandikia NECTA barua ya kutoridhika na maamuzi yake, kwa kutowashirikisha wakuu hao, lakini hawakupata jibu lolote, pamoja na kuwa madai yao mengi yalikuwa na msingi. Kwa upande mwingine, tumegundua kuwa baadhi ya waalimu, waliandika ripoti ya yale yaliyotokea wakati wa mitihani, mara tu baada ya mitihani kumalizika, na kupeleka wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali hapa Zanzibar. Jambo la kushangaza ni kwamba, barua na ripoti kama hizi NECTA hatujasikia kuzitaja. Hivyo kutokana na hali kama hii, bado tunapata mashaka makubwa na utendaji huu wa taasisi hii na wizara kwa ujumla.

Katika hali kama hii NECTA pia imewatwika lawama, baadhi ya wakuu wa shule/vituo, kwa kuwaandikia barua ya kwamba, hawakuwajibika vema katika kuhakikisha kuwa, vituo vyao vina mazingira tulivu na mitihani inafanyika kwa kufuata utaratibu, na hivyo kuwataka watoe maelezo, ni kwanini Baraza la Mitihani Tanzania, lisifute usajili wa vituo hivyo.

Kutokana na uchunguzi tulioufanya, tumebaini kwamba, hakuna kituo kilichoripotiwa kuwa na mazingira yasiyo na utulivu, miongoni mwa vituo vilivyotakiwa kujieleza, na hakuna ripoti iliyokwenda NECTA ya kushindikiza kwamba kuna vituo vilikosa utaratibu, isipokuwa ripoti ya wale wanafunzi wachache sana, waliokamatwa wakati wa mitihani.

Hivyo jumuiya na kamati imeona kuwa, maamuzi haya ya kuwataka wakuu hawa wajieleze siyo sahihi, na kwamba Baraza linakwepa jukumu hili ambalo linawahusu wao zaidi, kwani suala la ukaguzi wa mazingira ya mitihani, ni jukumu la wakaguzi wao, kuliko hao wakuu wa shule/vituo, kwani vituo hivyo ni shule kamili zenye mazingira yanayokubalika, na zipo kwa miaka mingi, na wakati wote majengo hayo yanatumika vyema, katika kuhifadhi zana mbali mbali, na pia ni sehemu tulivu za kufundishia wanafunzi, hali kadhalika wakaguzi wao walikagua majengo hayo ipasavyo, na wanafunzi pia walikaguliwa, na ulinzi ulikuwa wa hali ya juu. Hivyo jambo hili kama halifanyiwa uchunguzi wa kina na kuzingatiwa vema, litaleta athari ya kupunguzwa kwa vituo vya kufanyia mitihani bila sababu za msingi.

Wakati huo huo, uchunguzi wetu umethibitisha kauli ya kuwa, baadhi ya wanafunzi waliofutiwa matokeo, na kupewa adhabu ya kutofanya mitihani kwa kipindi cha miaka mitatu, wengine matokeo yao wamerejeshewa. Mara tu baada ya kuhakikisha ukweli wa kauli hii, na kwa vile tumeshapata ushahidi, jumuiya na kamati tunaomba kuiuliza NECTA, ni utaratibu gani uliotumika kuwasamehe baadhi ya wanafunzi, miongoni mwa waliofutiwa matokeo, ambapo hapo mwanzo wote walihukumiwa pamoja?

Kwa vile Jumuiya na kamati imeona kuwa huu siyo utaratibu, kisheria wala kinidhamu, hivyo tunaiomba NECTA itupe ufafanuzi wa kubadilika huku kwa maamuzi yake, bila taarifa maalum. Kwa vile hakuna asiyejua kwamba, hukumu ikishapita, hakuna tena kusamehewa wala kujitetea, isipokuwa mpaka yule aliyehukumiwa akate rufaa, na rufaa yake ikubaliwe na kusikilizwa, hivyo kuwarejeshea matokeo, baadhi ya wanafunzi ambao walifutiwa matokeo hayo, ni kutowatendea haki wale ambao matokeo yao bado yamefutwa na adhabu yao inaendelea.

Kama ingekuwa NECTA haina uhakika, kabla ya kutoa adhabu ya jumla kwa wanafunzi hao, ni bora wangesema kwamba baadhi ya matokeo ya wanafunzi, yamesitishwa kutolewa, mpaka ufanywe uchunguzi, kwa vile kumebainika mashaka kwenye matokeo hayo. Katika hali kama hii ya utata, tunaiomba NECTA ifute adhabu ya wanafunzi wote 3303 wa Tanzania nzima, na kuwapa matokeo yao, kwani kutofanya hivyo ni kutowatendea haki wale wanaoendelea na adhabu.

Kwa upande mwingine, tumegundua udhaifu uliojitokeza katika kuwabaini wanafunzi wenye mfanano usio wa kawaida, katika majibu ya kuchagua, (multiple choice and matching items).

Katika shule nyingi tulizokwenda kufanya uchunguzi, wanafunzi wengi wamefutiwa matokeo kwa kuoneakana kuwa wamekopiana, kwa vile wameonekana kuwa na mfanano usio wa kawaida, lakini cha kushangaza ni kwamba, somo moja tu la kiingereza ndilo wanafunzi wengi katika darasa wamegundulika na mfanano huo, lakini kwa masomo mengine mengi ni wanafunzi wachache tu miongoni mwa darasa lenye wanafunzi wapatao ishirini ndio wameonekana na mfanano huo.

Wakati huo huo, bado tuna mashaka na ushahidi uliotolewa na baraza kwamba, wanafunzi wengi miongoni mwa waliobainika, ni katika makosa tu, hatukupewa mfano au ushahidi, wa wale walio na mfanano usio wa kawaida, ambao wamejibu kwa usahihi. Jumuiya na kamati zimeona wazi kuwa ushahidi uliotolewa, ni wa shule chache zenye kuwa na matatizo ya aina walizotaja, na pia ni madarasa machache sana yenye hali hiyo, lakini baraza limejumuisha ushahidi huo kwa shule zote 58 za hapa Zanzibar.

Jambo hili linatia shaka katika ushahidi huo wa kimazingira, na kwa utaratibu wa kisheria, ushahidi hautakiwi uwe na hata chembe au aina yoyote ya shaka.

Kwa mfano masomo kama vile chemisty, book keeping, geography, physics, biology n.k, utakuta darasa zima la wanafunzi ishirini ni wanafunzi wanne, watano, hadi kumi, waliofanana majibu, tena kwa baadhi ya maswali au vipengee tu, na wengine wako masafa marefu baina yao, jambo ambalo linawezekana kabisa kwa maswali ya kuchagua. Na kwa baadhi ya wanafunzi tuliowahoji, walisema kwamba, baada ya kupata baadhi ya maswali ya mtihani, walikaa pamoja na kufundishana wenyewe kwa wenyewe, na wengine kutafuta mtu wa kuwasaidia, hivyo kutokana na wote kufundishwa na mtu mmoja, wote wakaandika sawa wakati wa mtihani, hivyo pamoja na kuwa wengine walikuwa vyumba tofauti, na wengine masafa marefu katika chumba cha mitihani, wote wakaonekana na mfanano wa majibu.

Hata hivyo, baadhi ya wanafunzi walipinga kabisa kuwa wao hawakupata mtihani, wala baadhi ya maswali, na kwamba walijitahidi katika kujiandaa, na kwamba walikuwa na matumaini mazuri kuwa wangefaulu. Hivyo maamuzi ya NECTA bila kuwa na ushahidi madhubuti, kutoka kwa wahusika, ambao kwa mazingira ya kesi hii, ilikuwa watiwe hatiani kwanza, ili ushahidi wa uhakika upatikane, na wanafunzi wanaostahiki kuadhibiwa, ndio wapewe adhabu, kama kanuni ya baraza kifungu cha 6 (2) (c) inavyosema.

Hali kadhalika, kumetokea mapungufu ya kiutendaji kwa upande wa Baraza la Mitihani, kwa kutokuwa makini katika kutoa matokeo ya wanafunzi, tumegundua kuwa kuna wanafunzi waliofanya masomo ya sayansi wameletewa majibu ya arts, au mwanafunzi hakufanya somo fulani,
lakini katika matokeo, ameletewa majibu kuwa amefanya somo hilo. Kesi hii aliwahi kuambiwa Katibu Mtendaji wa Baraza alipokuja hapa Zanzibar, lakini alieleza kuwa hilo ni kosa la kibinaadamu, wakati matukio kama haya yapo, na siyo moja tu.

Na pia, katika shule moja, darasa nzima limefanya mtihani wa fine arts, lakini wote hawakuletewa matokeo ya somo hilo, na walipohoji waliambiwa mtihani wao haukufika katika baraza la mitihani, na haijulikani umetoweka kwa mazingira yepi, na kwamba hivi sasa, wanafunzi hawa wamepewa taarifa ya kuwa, huenda wakafanya tena mtihani huo. Kwa mapungufu kama haya, jumuiya na kamati ya wazazi zinaendelea na mchakato wa kukusanya ushahidi kuhusiana na kuwepo kwa mapungufu kama haya.

Kwa ripoti hii fupi ya uchunguzi wa Jumuiya ya Kuzuia, Kukinga na Kuondosha Maafa na Majanga Zanzibar, na Kamati ya Wazazi wa wanafunzi, tunaliomba baraza kwa mara nyingine tena, lizingatie vema na kutafakari zaidi, kabla janga hili la kielimu halijazidi kuleta athari katika taifa letu.

Jumuiya ya DCPM na kamati ya Wazazi zipo tayari kukutana na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania, endapo ataona kuna ulazima wa kufanya hivyo, ili tuweze kulijadili suala hili na hatimaye kufikia maamuzi ya busara.

Hata hivyo Jumuiya na kamati, bado zina matumaini makubwa kwamba, serikali kupitia taasisi zake, pamoja na kuwa na majukumu mengi, watakaa na kutafakari, na hatimaye kushirikiana nasi katika harakati, za kulitafutia ufumbuzi muafaka suala hili. Na kwa upande wa Baraza letu la Wawakilishi hapa Zanzibar, ambalo hapo mwanzo walipotoshwa kisheria kwa ushahidi wa upande mmoja wa baraza la mitihani, mpaka ikabidi waamini.

Ni wazi kuwa, mara tu wajumbe wetu hawa wa Baraza la Wawakilishi, pindipo wakizipata ripoti hizi, ni hakika watakuwa makini na kuzingatia vyema ushahidi wa pande zote mbili, na hatimaye kuweza kutafuta ufumbuzi wa kina, katika kulitatua janga hili la kielimu hapa Zanzibar, bila jumuiya na kamati kulazimika kuendelea na taratibu zaidi za kisheria, katika Mahakama.

Naomba kuwasilisha
Najma Murtaza Giga
Mwanasheria wa Kamati ya Wazazi/
Mkurugenzi Mtendaji, DCPM

Advertisements

4 responses to “Ripoti ya uchunguzi, chanzo cha udanganyifu wa mitihani

  1. Ripoti ya uchunguzi wa kina, nimeipenda na Inshaallah Mungu awape subra na busara ili kuweza kulitatuta hili suala. NECTA wameonyesha wazi kuwa maofisa wazembe wasiojuwa kufanya kazi zao kwa ufanisi.

  2. Mimi naona tungekuwa wakweli n tukubali kuwa kizazi chetu kina matatizo. Mtu akubalie kuiba hata kama anachoiba kime lala nje bado ni mwizi na hana tofauti na aliyeiba kwa kuvunja nyumba. Wawili hawa wanaweza kutofautiana kwa misiamiati. Ivi kweli watoto wasingekuwa corrupt yangetokea haya. Ivi huyu wa kiboje aliyeuza booklet za kujibia mitihani angemuuzia nani angekosa wateja. Mimi hili la booklet naona tusilitumie kwa kuwa leo watu wanaweza kutengenea chochote.

  3. Ni wazi kuwa, mara tu wajumbe wetu hawa wa Baraza la Wawakilishi, pindipo wakizipata ripoti hizi, ni hakika watakuwa makini na kuzingatia vyema ushahidi wa pande zote mbili, na hatimaye kuweza kutafuta ufumbuzi wa kina, katika kulitatua janga hili la kielimu hapa Zanzibar, bila jumuiya na kamati kulazimika kuendelea na taratibu zaidi za kisheria, katika Mahakama

    Mimi naona waheshimiwa hawa tusiwape jukumu la kufatilia. Wao wanatengeneza moja ya mihimili mitatu ya Dola. Kazi hii ni ya kufanywa na taasisi za kiraia wakishirikiana na polisi ili chanzo cha tatizo kieleweka. Kuwakabidhi Wawakilishi hili ni kutumia gear ya mwisho na wakishindwa itakuwa imeshindwa nchi na hakutakuwa na sehemu ya kukata rufaa. Wale wanaoendelea sasa waendelee na wakiridhika kuwa NECTA ina kesi ya kujibu waipeleke Mahkamani. Mimi na wasi wasi kwa watoto hawa tulionao ambao kutwa ni simu kama matajiri wa masoko ya hisa tunaweza kupoteza kaa na gando – tahadhari yahitajika – tusife kama nguruwe aliyezeeka

  4. Kutokana na ripoti hii nimelazimika kukubali kuwa kweli watoto (wazee/walimu) wameshiriki kufanya udanganyifu. Nawapongeza walimu waliopeleka barua NECTA kuomba radhi.

    Hapa hakuna cha kutetea, ni kucheza na lugha tu. UAMIZI WA NECTA NI HALALI
    Awali kabla ya kusomaripoti hii nilikuwa nikiaminikuwa Watanganyika wanatuonea, lakini sasa Mh……………

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s