Nyakati za Wahafidhina Zanzibar

Aliyekuwa Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume,akisalimiana na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamadi,Ikulu Mjini Zanzibar Novemba 5, 2009 baada ya kukutana kwa mara ya kwanza kuacha tofauti zao za kisiasa, kuameheana na kuijenga Zanzibar mpya

Na Juma Mohammed, Zanzibar

Ujio wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na mageuzi ya hali ya siasa ni moja kati ya mambo ambayo leo yameifanya Zanzibar na watu wake kuwepo katika ramani ya mwelekeo wa kilele cha demokrasia sio tu Afrika,bali kuzishinda hata nchi za Ulaya ambazo baadhi yake demekrasia inasuasua. Ingawa haikuwa jambo jepesi kubadili mambo yaliyokuwa yamezoeleka kwa miaka mingi,lakini hatimaye viongozi waliweka kando utashi binafsi na kutanguliza maslahi ya wengi katika ujenzi wa jamii mpya Zanzibar.

Tatizo kubwa ambalo linazikabili nchi nyingi hususan zile zinazoendelea na zaidi Mataifa ya Afrika ni uwajibikaji mbovu kuanzia kwa watumishi wa umma,viongozi na hata jamii yenyewe kukosa vipaumbele katika mambo yao.

Zanzibar ya leo imetulia, ni shwari kabisa hakuna upepo mbaya unaovuma,maji yametulia baharini. Ni mwaka wa pili unaingia tangu kufanyika kwa kura ya maoni iliyoamua kuzika ‘maiti’ kisasi na chuki zitokanazo na tofauti ya itikadi ya siasa na ushabiki wa vyama vya siasa miongoni wa wananchi.

Wahafidhina walipaza sauti kupinga maridhiano,kupinga muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na yote yenye mwelekeo huo, kupinga kwao ni sawa na kisa cha kutaka kumpiga mawe mchunga kondoo ili kondoo wa kundi lake(umma) watawanyike,lakini hali haikuwa hivyo.

Maisha ya wakati ule yalikuwa ni ya ovyo, watu waliwakataa wachumba wao kwa chuki iliyopandikizwa ya tofauti ya itikadi ya kisiasa huku wengine wakitengena na familia zao kwa dhambi ile ile ni jambo la kusikitisha.

Shafi Adam Shafi ameeleza katika kitabu chake cha vuta nikuvute vitendo vya ubaguzi na athari zake katika jamii, “akapeleka posa kwa Gulam. Gulam alipojidai kumtilia nakshi Kermali akibwata na kufoka kuikataa posa ya golo,Kermali akamwambia “ho! Mbona wewe unaye golo umemficha Vikokotoni”

Wahafidhina walikuwa wakiwaeleza vijana kuacha kuchumbia katika nyumba fulani kwa sababu wazee wa binti au kijana wa kiume ni wenye asili ya Hizbu(Zanzibar Nationalist Party) huku kwa upande wa upinzani kwa maana ya CUF nako kulikuwapo wahafidhina wakiwaeleza vijana wao matamshi yanayofanana na hayo ya upande wa wenzao wa Chama tawala.

Kwenye sehemu za kazi ikiwa hupendezi kidogo, Wahafidhina wanakusukia zengwe unaambiwa mtoto wa nyoka huyo(mtoto wa Hizbu),huyo ni CUF, mwarabu, basi hali ilikuwa hivyo wengine ikiwaumiza,lakini wahafidhina ikiwaneemesha!

Wahafidhina hawakupenda kuona ushirikiano wowote na vyama vya upinzani,kiongozi mmoja mmoja, kila siku walihubiri siasa za chuki na baadhi ya wakati kuvuka hata mipaka.

Hali hiyo imeiumiza Zanzibar na watu wake, hakuna hatua ya maana iliyokuwa ikifikiwa katika suala la maendeleo, wataalam wakiacha kazi kwa hofu, utengano uliota mizizi, Serikali ililazimika kutumia nguvu kubwa kuzima vuguvugu la demokrasia,uchumi uliyumba na washirika wa maendeleo wakaipa kisogo Zanzibar.

Tunahitaji kumpongeza Dk.Amani Abeid Karume,Rais wa awamu ya sita Zanzibar aliyeamua kwa dhamira ya dhati kumkaribisha Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi(CUF),Maalim Seif Shariff Hamad Ikulu kuzungumzia mustakabali wa wakati ule na wa baadaye Zanzibar.

Hatimaye mazungumzo hayo yalizaa maridhiano ambayo nayo yakazaa mtoto anayeitwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na leo hali ya siasa imetulia mambo shwari.

Karume ameweza kucheza karata yake vyema baada ya kuiacha Zanzibar ikiwa katika hali ya amani,utulivu na mshikamano wa wananchi ambao wamesahau zile siasa za mti kwa macho ambazo watu walifikia hata kususia maziko,kuchagua misikiti kwa misingi ya itikadi za kisiasa na wengine hata kuacha wake au kudai talaka kwa waume zao kwa sababu za tofauti ya vyama vya siasa.

Hivi leo baada ya ujio wa SUK ni Wahafidhina wale wale waliopinga na kuapa kila aina ya viapo ndio waliokumbukwa kwa vyeo wamesahau kadhia yao,lakini ndio hulka ya mla kunde, sisi wengine hatushangai sana na yanayotokea leo katika siasa hizi na zile.

Kama walivyoshindwa wapinga maridhiano ndivyo alivyoshindwa kuhimili vishindo vya upendo na umoja Gulam aliyepinga binti yake kuolewa katika kitabu cha Vuta ni kuvute ukurasa wa 275, Shafi Adam Shafi ameeleza kwa kina suala hilo akihusisha ndoa ya Bukheti Madoriani na Yasmin.

“Na siku ya saba,Yasmin akatolewa ukumbini. Cheusi dawa wakamwagika uwanjani,uwanja wa jumba la Karagosi ukajaa tele.Bwana Bashir na mama Somoye walicheza na kutimka kila walipoitwa. “Yuwapi? Aje hapa tuhangaike naye” Bwana Bashir babaye arusi,mama Somoye mamaye arusi.Gulam naye alisahau Uhindi wake naye pia akatoka uwanjani alipoitwa “babaye arusi” upande wa Bi arusi.Kermali na Kulsum walikuwemo kwenye shangwe na hoihoi tokea mwanzo mpaka mwisho.Ugolo na uponjoro ukaisha.

Kama ulivyozikwa uponjoro na ugolo,siasa za mti kwa macho nazo zimezikwa kwani ndani ya CCM na CUF hivi sasa wapo watoto, wajukuu na vitukuu vya waasisi wa ASP,ZNP,Umma Party ,hoja ya kupinga SUK inapata nguvu wapi ikiwa Gulam na Kermali walizika tofauti zao na kushirikiana katika shughuli ya arusi?

Wamarekani nao walikuwa na ubaguzi wa rangi, walibaguana sana,lakini mwishowe wakaamua kuachana tabia mbaya na kuona kwamba kila mtu ana haki katika Marekani, nitawakumbusha kicha kimoja kilichomtokea Mchungaji Leo Sullivan,Mmarekani mweusi na mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu.

Mchungaji Sullivan siku moja alienda kunywa soda kwenye hoteli moja kule Marekani, alipoingia akanyimwa kiti kwa vile yeye alikuwa mtu Mweusi. Kitendo hicho kilimfanya kuuchukia ubaguzi wa rangi na ubaguzi wa aina yoyote.

Tuliko toka hatuwezi kurejea tena kwa namna yoyote ile, dunia ya leo sio ile ya kibaguzi,udikteta,ubabe. Ulimwengu huu ni ule wa mashauriano na maridhiano, wanasiasa awaliotupa mgongo suala hilo yamewakuta kwa kuondolewa na nguvu ya umma.

Kwa sasa dhiki ya kisiasa imewashukia wahafidhina maana sisasa za Uliberali zimeshika kasi huku ujamaaa ukiwa ICU maana watetezi wa mfumo huo wamekata tamaa maana kila uchao mambo ya utandawazi yanazidi kuongezeka na kuimarika zaidi.

Je baada ya SUK na ujio wa teknolojia mpya ya mawasiliano kama ipad 4, iphone s,marck book pro,black berry porsche, ambazo ukiwa nazo muda wote unakuwa kwenye ulimwengu wa facebook,twitter,skyper,youtube.

Ni jambo lisilobishaniwa kuwa katika hali ya siasa za majitaka zilizosheheni Tanzania huwezi kumpata mwanasiasa mjamaa ikiwa mtu atajifanya mjamaa basi kaa ukijuwa anacheza kibepari kuimba kwake ndio kijamaa!

Miaka 48 ya Mapinduzi Zanzibar na miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika bado adui mkubwa wa nchi hizi ni ujinga, umaskini,maradhi na naongeza la kwangu rushwa.

Mzigo wa mambo hayo ni mkubwa huku juhudi ikionekana isiyoleta manufaa hali za wananchi ni zile zile kipato chini ya Dola moja ya Marekani nazikumbuka ile misemo ya kale mdharau mwiba mguu uota tende, usipoziba ufa,utajenga ukuta, leo miguu yetu mizito haiwezi kwenda mbio ni kama vile imefungwa kidhibiti mwendo ndio kasi ya ukuaji wa uchumi wetu.

Wakati tukiwa katika hali hii, wale wasioitakia mema SUK wanaanza kuchelekea wakisema kiko wapi si tulisema,sawa mlisema,lakini kisemo chenu ndio mauti yetu mlisema kwa faida zenu binafsi sio za wengi.

Ni muhimu katika hali hii, Viongozi wa SUK kujidhatiti kutokubali kuyumbishwa na ‘Wahafidhina’ kwani mnapoyumba nyinyi viongozi sisi wananchi hatujui la kufanya na mkumbuke pia wale ving’ang’anizi wa sera na imani za Kihafidhina watakuwa wanachekea chooni tena kwao wao ni kama ule msemo wa kuvuja kwa pakacha nafuu kwa mchukuzi.

Jukumu kubwa lililopo ni namna gani SUK inavyoweza kutafsiri sera na mikakati mbalimbali katika kukuza uchumi na zaidi kusimamia kilimo maana viwanda ni msamiati mgumu,huwezi kuendelea kutegemea sekta moja tu ya kilimo kuwa uti wa mgongo wa uchumi wako,mataifa yaliyoendelea yamegemea viwanda zaidi,lakini wache tujikita hapo kwanza.

Yale matamko ya siasa ni kilimo, kilimo cha kisasa twendeni vijijini tukalime hayasaidii kitu ikiwa hakuna dhamira ya kweli kuinua sekta hiyo kwa vitendo kwani wahenga walisema upendo huanzia nyumbani, hivi mpaka lini Zanzibar itaselelea kuelezea matukio ya kihistoria kuhusu kilimo?

Kwamba Kizimbani kilikuwa kituo bora cha utafiti wa kilimo,kwamba tulikuwa na shamba la Makurunge kule Bagamoyo Mkoa wa Pwani tena utawasikia baadhi ya Wawakilishi wakiulizia hatimiliki mbona hamuulizi mali zilizokuwa kwenye shamba hilo zimeishia wapi?

Wanasiasa kwa misamiati na maneno mapya ndio wenyewe, wakiwa kwenye majukwa utasikia wakisema kuwa kuna mkakati mkubwa na madhubuti unakuja kuhusu kuendeleza kilimo, mapinduzi ya kijani, kilimo kwanza, maofisa ugani wanarudi hadi vijijini,ukiuliza utekelezaji wake hupati jawabu yenye kukuridhisha.

Wataalam wetu katika sekta ya kilimo nao wanakimbilia kwenye siasa,wanautaka Ubunge na Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi maana huko ndiko kwenye kipochi kinene, U-bwana na Ubibi-shamba hauna tija kwao na hawa ni miongoni mwa watu waliopata ujuzi katika tasnia yao.

Lakini wengine wanakimbilia sekta nyengine wanazoziona zina tija kwao na hasa kukimbilia kuongeza shahada za Uzamili na Uzamivu na kubobea kwenye sekta nyingine, wakikiacha kilimo na ufugaji kuwa kama yatima.

Hakuhitajiki mshauri mwelekezi au mtafiti kubaini chanzo cha mdororo wa kilimo , mambo yote yapo hadharani hakuna kichocheo cha wao kuwa huko kwenye kilimo na ufugaji, hakuna motisha,mazingira mabovu ya kazi, upungufu wa vitendea kazi, hawawezi kwenda kuishi Kibonde mzungu, Bumbwisudi, Cheju, na kwengineko kwa vijisenti au posho ya mkia mbuzi wakati wanaopiga siasa wanapata mamilioni ya shilingi.

Nchi za eneo la Pembe ya Afrika zikiwemo Djibouti, Ethiopia, Eritrea, Kenya, Somalia, Sudan na Uganda zinakumbwa na tatizo la ukosefu wa chakula. Wiki iliyopita Shirika moja la Kimataifa la lilionya tishio la njaa sehemu ya Afrika Magharibi na Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Ikumbukwe kuwa tangu mwaka jana, ukame mkali ambao haujawahi kutokea katika miaka 60 iliyopita umekuwa ukilisumbua eneo hilo. Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa linakadiria watu zaidi ya milioni 10 wanakabiliwa na tishio la njaa katika nchi za Kenya, Ethiopia na Somalia.

Jumuiya ya kimataifa inajitahidi kuwasaidia watu hao, lakini mgogoro wa kibinadamu hauwezi kuepukika. Ni ukweli usiopingika kwamba Dadaab, ambayo ni moja ya kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani iliyopo kaskazini mashariki mwa Kenya yenye eneo la kilomita 50 za mraba inazidiwa na kasi ya ongezeko la wakimbizi.

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa linakisia kiasi cha wakimbizi 1,300 kutoka Somalia Taifa lisilokuwa na Serikali madhubuti kutokana na kukosekana kwa utulivu wa kisiasa unaosababishwa na uroho wa madaraka wamekuwa wakiingia Daadab kuomba hifadhi ili kupata vyakula, maji na dawa.

Ni jukumu la viongozi na wananchi Zanzibar kujipanga katika kukabili hali hiyo isiweze kutokea, Mwenyezi Mungu aivushe salama katika janga hilo. Lakini wakati tukimuomba Mwenyezi Mungu atuepushe na njaa, ni wajibu wetu wananchi kufanya kazi kwa bidii, kuzalisha sana na kutanguliza uzalendo mbele.

Wale waliopewa dhamana wawajibike ipasavyo, wawatendee raia wenziwao haki bila kuonea,chuki wala kulipiza kisasi kwa jambo fulani,lakini watendakazi nao kwa nafasi zao kuwajibika kwa mujibu wa majukumu yao,kufika kazini kwa wakati na umma pia kuthamini mchango wao.

Advertisements

One response to “Nyakati za Wahafidhina Zanzibar

  1. YAANI TUNASHKURU MUNGU SI HABA TULIPO FIKA NA NDIO MAANA NASEMA KUTOKANA NA MFUMO WA SIASA NA UPEPO WAKE SAIVI UNAVOKWENDA INATULAZIMU HUU MUUNGANO UVUNJIKE MAANA BARA BADO SIASA ZILIZO TAWALA NI SIASA ZA CHUKI NA NDIO MAANA HATA INADIRIKI CHAMA CHA CUF KINAITWA CCM B KUTOKANA KUWA NIAJABU KUONA AFRICA WAPINZANI WANASHIRIKIANA NA CHAMA CHA TAWALA KUJENGA NCHI HIVO BASI UNAFIKA KUONA KUNA BAADHI YA WANANCHI HUKO ZANZIBAR WANAAMINI HIVO NA UKIANGALIYA UTAONA HATA MAMBO YA HAMAD RASHID YALIPAMBA MOTO KUTOKANA NA CHUKI ZILIZO PANDIKIZWA NA HAMADI RASHIDI MWENYEWE , AMA MM KWA UPANDE WANGU NA CHUKIA SANA SIASA ZA CHUKI NA MATUSI NA WALLAH NDIO MAANA UKAONA UKITAJA HABARI ZA MTU HAMADI RASHID HATA KAMA NIWANYUMBANI PAMOJA BASI HUKARIBIA KUSEMA LAANATULLAH KWAKUWA UKIONA HATA WAPAMBE WAKE NI WATU WA JAZBA TU NA WAKIINGIA SEHEMU HUSABABISHA FUJO NA VITA HAYA SIO TENAA HAYASHA ISHA MDA WAKEEE!
    NAOMBA NISIWE JAMBAZI WASHUKURANI NI WASIFU RAISI KIKWETE NA COMMISSIONER WAKE AMBAYE KWETU ZANZIBAR HUMWITA RAIS WA ZANZIBAR HAWA WATU WAMEJITAHIDI KUFIKIA HAPA NA MUNGU AWASAIDIE WAWEZE KUSIKILIZA KILIO CHA WANANCHI KWAKWELI SISI WAISLAM HUSEMA MTU AKIWA MUISLAM HATA KAMA NIMCHENZI ILA JAPO KIDOGO HOFU HUMUINGIA YAANI NIKIKUMBUKA UTAWALA WA MKAPA MUNGU AMLANI TOKA HAPA HAPA DUNIANI JINSI ULIVOKUWA WACHUKI NA WATU KUULIWA YAANI SIAMINI HADI SASA KAMA WAZANZIBAR NA WATANGANYIKA TUMEFIKA HAPA.
    MUNGU ISAIDIYE ZANZIBAR NA WAZAZIBARI WOTE.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s