Mawaziri wa Serikali ya Zanzibar na sababu ya ubunifu

Maelekezo ya kiongozi wa nchi ni muhimu sana. Na mara nyingi kiongozi mwenye busara hutoa maelekezo na kutaraji wafuasi wake au walio chini yake watekeleze maagizio hayo bila visingizio vyovyote vile. Kiongozi wa nchi hutoa maelekezo hayo pia akiruhusu ubunifu na hata utekelezaji kwa mujibu wa hali ilivyo na sio kutekeleza maagizo kwa njia ya kulazimisha kwa kuwa tu ni kutekeleza maagizo.

Maana mwisho wa siku, kama msemo ulivyo ni kuwa mtekelezaji atapimwa kutekeleza maagizo sio kwa kuwa tu ametekeleza lakini kwa namna gari, kwa athari gani na hasa kwa kuwafika upana gani wa taifa.

Maelezo yangu hayo ya utangulizi yanahusiana na maagizo ya Rais wa Zanzibar Dk. Ali Muhammed Shein ambae mwezi Novemba mwaka jana alitoa maelekezo kuwa wasaidizi wake wafanya utaratibu wa kukutana na waandishi wa habari ili watoe taarifa juu ya utendaji wa wizara wanazozisimamia.

Niliandika wakati huo wa mwezi wa Novemba kuwa hata mwenye Rais hakuwa mfano mzuri kwa sababu ilimchukua mwaka mmoja mzima kukutana na waandishi wa habari wakati akisherehekea mwaka mmoja wa uongozi wake.

Lakini kuchelewa kwake huko tukaweza kukusamehe kwa sababu pengine wazo la kukutana na waandishi kila miezi mitatu halikuwa limekuja akilini mwake kabla, bali pia kama alivyosema Mwenyekiti Mao Dze Dung kuwa unapoamka ndio asubuhi yako, na kwa hivyo alipoanza ndipo hapo pa kuanzia.

Tulitaraji Rais Shein ataendeleza moto huo ambao alichelewa kuuanza wa kukutana na waandishi, lakini labda kwa kutingwa na kazi ahadi yake ya kukutana na waandishi haikugota katika kitambo cha miezi mitatu maana ndio muda huo sasa unayoyoma.

Wakati akizungumza na waandishi mwaka jana, Rais Shein alitoa maagizo, kama nilivyotangulia kusema ya Mawaziri kila mmoja kwa Wizara yake nao pia kuanzisha utamaduni wa kukutana na waandishi wa habari katika kuhimiza dhana ya uwazi wa Serikali.

Lakini pia iwe ni katika dhana ya kuwajuvya wananchi kinachoendelea katika utendaji wa Wizara hizo ambazo ndizo nguzo ya kila siku ya Serikali na ndio pahala ambapo wananchi wanaweza kupafika ikilinganishwa na Serikali Kuu.

Ukapita muda kidogo tu na Wizara zikaanza kutekeleza maagizo ya Rais, na utekelezaji huo ndio leo utakuwa ndio hoja yangu katika makala hii kwa nia ya kujaribu kuonyesha kasoro zaidi ili kufanya marekebisho kwa ajili ya siku za baadae.

Kwa fikra zangu, ambazo mara nyingi huonekana ni kinyume cha mambo, ni kuwa utaratibu huo naamini haukuenda kwa mujibu wa matakwa ya Rais Shein ambaye hakusema asilan kuwa ufanywe kwa kuwa umefanywa tu, ila naamini alikusudia ufanywe ili uwe na faida.

Nafasi ya Rais kukutana na waandishi wa habari haiwezi kuwa kubwa na ya mara kwa mara kama ambayo nafasi ambayo anaweza kuwa nayo Waziri mmoja mmoja na kwa hivyo kwa fikra zangu haikuwa lazima kwa kila Waziri kuitisha mkutano na waandishi wa habari kwa staili ile ile ya Rais na kukaa nao na kuwatolea taarifa kwa njia ya kusoma.

Mawaziri wangepaswa kufikiri kama kila Waziri atakuwa anasoma taarifa yake jee mwandishi wa habari ataekwenda mikutano ya Mawaziri sita tu hali yake itakuwa vipi kiakili lakini pia kimwili. Lakini pia mwandishi huyo atakuwa kweli tayari kwenda kumsikiliza Waziri mwengine wa 7 akitoa “hotuba” nyengine?

Mambo mengi ambayo Mawaziri walikuwa wakiyasema katika kipindi hicho yalikuwa tayari yameshasemwa na Rais Shein katika hotuba yake ndefu kule Ikulu, na kwa hivyo kurudiwa tena na Mawaziri hao karibu sawa na alivyosema Dr Shein hakukuwa na faida yoyote ile.

Hapa ningetaka kusema mambo mawili, kabla sijasonga mbele. Kwanza ni kwamba kile kitendo cha kila Wizara kutoa taarifa na taarifa hizo zikiambatana, pengine Wizara mbili kwa siku au moja leo na moja kesho kilikuwa kinachosha na halikuwa ni jambo la lazima.

Kungekuwa na aina fulani ya ubunifu na uratibu ambao Wizara zisingegongana lakini pia Wizara zisingekuwa zikitoa taarifa kwa njia ya “mchosho” kwa waandishi wa habari. Rais hakumaanisha katika maagizo yake kuwa kila miezi mitatu imaanishe Wizara zote zifanane, ila ubunifu ungeweza na unaweza kuruhusiwa.

Lakini mikutano ile ya Mawaziri ilikuwa kama ratiba ya Maulid ya Mfungo Sita, leo Kwahani, kesho Malindi, keshokutwa Tumbatu mradi kila mtu anafukuzia asome Maulid yake ndani ya baraka ya Mfungo Sita.

Pili, kwa fikra zangu Wizara zingekuwa bunifu kwa kupunguza “hotuba” na kwa kutoa maelezo yake kwa mifumo ya kisasa kama “power point” na kutoa taarifa kwa waandishi kwa njia ya dondoo na takwimu muhimu badala ya hotuba za kurasa 15 au 20.

Kama nilivyosema ni kwamba nyingi ya taarifa hizo za Ki-Wizara zilikwisha tolewa na Rais na kwa hivyo fikra zangu ni kuwa kama pangekuwa na ubunifu basi Wizara zisingewaita waandishi na kuwaweka kitako kwa saa kadhaa na huku wakirudia takriban yale yale.

Kwa hivyo ningekuwa mimi ningechagua maeneo machache ambayo ningeyakazia katika maelezo na kutoa taarifa za uyakinifu mambo yamefikiaje tokea kipindi ambacho Rais alizungumza ili kuonyesha kuwa Wizara inafanya kazi na mwananchi aridhike kujua hivyo. Kurudia kila kitu ni kuwatesa waandishi.

Pia kama ningeruhusiwa kufanya ubunifu basi ningechagua mfumo mwengine wa kutoa taarifa kwa waandishi badala ya ule ya kuwaita katika mkutano na waandishi wa habari. Nao ni ule wa kuwachukua katika maeneo “site visit” mbili au tatu na huku kuzungumza nao.

Rais Shein kwa mfano alisema Serikali yake imejenga skuli nyingi za mradi wa miaka mitatu kwa kipindi cha mwaka mmoja, naamini ingependeza sana waandishi wa habari wakaaenda huko na kuona kilichofanywa au Wizara ya Mawasiliano ingezungumza na waandishi wakiwa katika eneo linalojengwa sehemu ya kukaa abiria huko Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Karume, naamini mambo yangenoga.

Ubunifu pia ungeweza kuwaongoza Mawaziri kujenga ukuruba na Wahariri wa vyombo vya habari au waandishi wazoefu kwa kukutana nao kwa kikombe cha chai au kahawa na kubadilishana mawazo na kwa njia hiyo fikra nyingi mpya za miradi, mikakati kuweza kuzijua na kuzijengea hoja.

Kubwa zaidi ningefurahi iwapo angetokea Waziri akatoa taarifa moja kwa moja kwa wananchi na badala ya kuulizwa masuala na waandishi wa habari basi iwe ni fursa ya wananchi kumuuliza, maana wao ndio anaewatumikia.

Hoja ya kukutana na waandishi wa habari haiishii kila miezi mitatu, lakini kila inapopatikana nafasi, lakini taarifa ya miezi mitatu basi iwe tofauti na taarifa za kila siku, au isheheni taarifa mpya na sio kuwa marudio.

Nionavyo mimi uwazi aliokusudia Dk. Shein si lazima uwe kama ambavyo umefanywa na mawaziri wake. Kweli wote wametoa taarifa lakini zimetolewaje na vyombo vya habari, jee zimefikaje kwa wananchi, kuna mrejesho wowote kutoka kwa wananchi na muhimu kabisa zimechorwa taswira ya Wizara na Serikali kwa jumla?

Kutaka kuwa wazi ni kitu kimoja lakini kuwa wazi na umma ukajua kuwa Serikali iko wazi ni kitu chengine kabisa. Ndio maana somo la utawala bora na uwazi wa Serikali ndio kwanza bado halijasomeshwa hapa Zanzibar na wakati ndio huu.

Advertisements

3 responses to “Mawaziri wa Serikali ya Zanzibar na sababu ya ubunifu

  1. Hili ni muafaka kabisaa lakini nadhani angeanza Waziri Shamhuna akatueleza alipofikia katika kuuza rasilmali za Zanzibar. Jee ameshamaliza kazi? Na ameahidiwa kiasi gani kama comission yake? Jee kazi hii anaifanya yeye pekee au anao wenzake wanaomsapoti wamejificha nyuma ya pazia?

  2. Hii nisahihi kabisa kukumbushana sitaki kusema kwamba baadhi ya viongozi hutoa ahadi ambazo hawawzi kuzisimamia kikamilifu lakini waswhili husema ada ya mja hunena muungwana ni vitendo.Ni imani yangu baada ya utafakari ahadi yake aliyoitoa masikioni mwa wazanzibari ataitekeleza.
    Tunaweza kusema kwamba pengine anamwtingwa na mjukumu ambayo yanamaslahi zaidi kwa wazanzibari kuliko kutoa angalau saa moja kuwapa muelekeo wa uekelezaji wa ahadi zilizotolewa na tumefikia wapi,naamini kimya kikubwa kina shindo mnene

  3. Nakubaliana na wewe Ali mia kwa mia lakini vile vile nina wasi wasi na hawa watendaji wakuu katika mawizara yetu ambao ni washauri wakuu wa mawaziri wetu nao ni makatibu wakuu na wakurugenzi.Kwasababu hawa ndiyo washauri wakuu wa Mawaziri ambao wengi ni wanasiasa kuliko nikitumia neno la kiingereza technorats.Jee uwezo wao katika suala la ubunifu ni wa kiasi gani,au elimu zao walizonazo ni za darasani tu?Kwani unaweza kuwa na Phd/Master kwa kusoma darasani lakini ukija katika suala zima la kubuni mipango ni zero.Utakapokwenda po pote duniani kwa nchi zinazoendelea na zilizo endelea mabadiliko yanaletwa na technorats viongozi wao wanachotoa ni mwongozo tu wa wapi tunataka tufike.Njia ya kutumia kufikia huko ni ya wataalamu na hao hao wataalamu nao ndiyo wanaishauri serikali wapi pakwenda ili tupige hatua.Kinachoshangaza na kusikitisha kuwa juu ya ukweli kwamba M.Mungu ameturahisishia mambo katika ulimwengu wa leo ambao kamjaalia mwanadamu akili ya ubunifu kiasi kwamba kila unachotaka kimo kwenye mtandao lakini bado tuko nyuma katika mambo mengi tu.Kuna mambo hayataki hata usafiri kwenda Ulaya au Far East kuyapata ni akili yako kuitumia kwa njia ya mtandao lakini bado hao tulowapa madaraka wanatenda kana kwamba tuko 1950s.Kwa kweli Ali inasikitisha lakini sishangai kwa kuwa asilimia 70 ya watendaji wetu serikalini hawana utaalamu wa kile wanachokifanya na wengine wamepata kazi kwa kutumia vyeti vya kughushi au majina ya watu wengine.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s