Hutuba ya wiki ya maji duniani

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la MapinduziDk. Ali Mohamed Shein,(katikati) akipata maelezo kutoka kwa Mkugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji (ZAWA) Dk Mustafa ALi Garu,alipokuwa akitembelea maonesho ya siku ya maji katika Matangi ya Maji Saateni

Licha ya jitihada tunazozichukuwa katika suala hili, nafahamu kuwa tumekabiliwa na changamoto nyingi katika sekta ya maji hapa Zanzibar. Ili kuishinda changamoto zilizotukabili katika sekta ya hii ni muhimu kuiamini na kuitekeleza ipasavyo ile rai ya kuwajibika kwa pamoja “Collective responsibility”. Nachukuwa nafasi hii kuwataka wananchi kuiendeleza vizuri rai hii, kila mmoja wetu aamini kwa dhati kuwa anawajibu wa kuchangia ipasavyo kwa kila kitu muhimu kinachohusu maendeleo yake binafsi, maendeleo ya jamii iliyomzunguka pamoja na maendeleo ya nchi yetu kwa jumla.

HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA
BARAZA LA MAPINDUZI, DK. ALI MOHAMED SHEIN,
KATIKA UZINDUZI WA WIKI YA MAJI DUNIANI
SAATENI – ALHAMISI, TAREHE 22 MACHI, 2012

Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais,
Waheshimiwa Mawaziri,
Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati,
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi,
Waheshimiwa Viongozi mbali mbali wa Chama na Serikali,
Ndugu Wananchi,

Assalam Aleykum,
Awali ya yote, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyeumba uhai kutokana na maji kwa kuturuzuku uzima na busara tukaweza kukusanyika hapa katika hafla hii adhimu ya kilele cha maadhimisho ya wiki ya maji Tanzania sambamba na shamra shamra za siku ya maji duniani.

Pili, natoa shukurani zangu za dhati kwa uongozi wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kwa uamuzi wenu wa kunialika kuwa mgeni rasmi katika hafla hii muhimu katika maisha ya kila mmoja wetu.

Ndugu Wananchi,
Katika kitu kimoja ambacho dini na sayansi hazipingani basi ni ile nadharia ya kuwa “Maji ndio chanzo kikuu cha uhai wetu na viumbe vyote tunavyoviona ikiwemo mimea”. Ni dhahiri kuwa wiki ya maji duniani ni wiki moja muhimu sana kwani inatupa nafasi ya kukaa, kupanga na kujadili juu ya kitu cha lazima kwa viumbe wote. Napenda kueleza furaha yangu kuona kuwa Serikali yetu imeipa wiki hii umuhimu unaostahili. Ahsanteni sana kwa kunialika kuwa mgeni rasmi na kwa harakati mbali mbali mlizoandaa za kuadhimisha wiki hii hapa nchini petu.

Nimearifiwa kuwa sherehe kama hizi zinafanyika katika Mkoa wa Iringa kwa upande wa Tanzania Bara. Kauli mbiu ya maadhimisho haya iliyotolewa na UNESCO ni Maji na Usalama wa Chakula (Water and Food Security). Kauli mbiu hii imekuja katika wakati muafaka ambapo Serikali yetu inaendeleza juhudi za kuimarisha huduma ya maji safi na salama kwa ajili ya kunywa pamoja na kutilia mkazo kilimo cha umwagiliaji maji. Kilimo cha aina hiyo ndicho kitakachotuwezesha kufikia malengo yetu ya Mapinduzi ya Kilimo. Kwa hivyo, sote hatuna budi kuiunga mkono kauli mbiu hiyo.

Ndugu Wananchi,
Sote tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuturuzuku hidaya hii ya maji hapa nchini kwetu. Tumejaaliwa kuishi kwenye visiwa vizuri vilivyozungukwa na maji na vilivyobarikiwa mimea mingi na miongo iliyopangika vizuri. Si rahisi kukaa kutwa moja bila ya kuona maji au kupita miezi bila ya kunyesha mvua. Kwa namna hii, ni rahisi kwa baadhi yetu, kuyachukulia maji kuwa ni kitu cha kawaida. Thamani ya maji hujulikana zaidi pale yanapokuwa ni taabu kuyapata. Nachukua nafasi hii kuwataka wananchi wautumie muda huu na siku ya Maji Duniani kutafakari hali halisi ya maji nchini kwetu na ulimwengu mzima na umuhimu wake kwa maisha yetu. Kila mmoja awe tayari kuchangia katika juhudi za kuyalinda, kuyasambaza na kuyafanya maji kuwa ni hidaya endelevu. Wanasayansi wanasema Maji ndiyo yanayoendesha kila kitu (Water is the driving force of all nature).

Ndugu Wananchi,
Kutokana na mabadiliko ya hali ya tabianchi na harakati za maisha ya binaadamu, hivi sasa upatikanaji wa maji katika vianzio vya maji asilia umeshaanza kuleta taharuki kwa maendeleo ya jamii mbali mbali duniani. Maji kutoka katika maziwa na mito mikubwa yanatumika kwa kilimo na uzalishaji wa nishati. Janga la ukame limekuwa likizikumba sehemu mbali mbali za dunia; vianzio vya maji kama vile chemu chemu vimekuwa vikitoa maji kwa uhaba zaidi na tafiti mbali mbali zimethibitisha kupungua kwa maji toka kwenye vianzio vyake chini ya ardhi.

Ndugu Wananchi,
Hayo ni miongoni mwa mambo muhimu ya kuyatafakari na kuyapatia ufumbuzi. Ni dhahiri, tukiyawachia tutakuwa hatuvitendei haki vizazi vyetu vijavyo. Matatizo haya, yanaikabili dunia nzima, tofauti ni kuzidiana kwa viwango vya athari.

Kwa upande wetu, nasi tumeshaanza kubaini kuwa tatizo kama hilo limeshaanza kujitokeza lakini habari nzuri ni kuwa hatujafikia kiwango cha kutisha kama baadhi ya wenzetu hivi sasa. Hata hivyo, muhimu kuzingatia hekima ya wazee wetu isemayo: “Tahadhar- Kabla L-athar”

Ndugu Wananchi,
Licha ya kuwa dunia yetu imekabiliwa na tatizo la upungufu wa maji, ninafuraha kuona Serikali zote duniani na mashirika ya kimataifa na jumuiya nyengine mbali mbali za maendeleo zimeongeza juhudi zinazohakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa watu wote duniani. Na bila shaka mkusanyiko huu wa leo wenye lengo la kusherehekea siku ya Maji Duniani ni miongoni mwa juhudi zinazochukuliwa na Serikali yetu, kuwazindua wananchi juu ya umuhimu wa maji na kuhamasisha kuyatumia kwa uangalifu.

Siku ya tarehe 6 mwezi huu wa Machi, nilifurahi sana kusoma taarifa kutoka Umoja wa Mataifa inayothibitisha kuwa moja kati ya Malengo Makuu ya Milenia lile la kusambaza maji safi na salama kwa jamii mbali mbali kwa asilimia 88 ifikapo mwaka 2025, limefikiwa miaka mitano kabla mwaka huo uliopangwa.

Taarifa hii inatupa faraja kubwa sote kwa kujuwa kwamba baina ya mwaka 1990 na 2010 zaidi ya watu bilioni mbili ulimwenguni wameweza kupatiwa huduma za maji safi. Taarifa ilibainisha kuwa hadi mwisho wa mwaka 2010 zaidi ya asilimia 89 – (ambayo ni sawa na watu bilioni 6.1) ya wakaazi wote duniani tayari inafaidika na huduma za maji safi. Wakati huo huo lengo lilikwishafikiwa na kupindukia kwa asilimia moja zaidi. Na bila shaka hadi leo wakati tunaadhimisha wiki hii ya Maji Duniani zaidi ya mwaka mmoja toka zilipokusanywa takwimu hizo, idadi hiyo itakuwa imeshaongezeka.

Nachukuwa nafasi hii kutoa wito kwa jumuiya na washirika mbali mbali waliofanikisha jitihada hizi kuongeza juhudi ili kuwanufaisha wale waliobakia, kwani hadi sasa taarifa hiyo hiyo imethibitisha kwamba wako wakaazi zaidi ya milioni 800 ulimwenguni ambao bado hawajafaidika na huduma za maji safi na salama. Inasikitisha zaidi kuona kuwa asilimia 40 ya wakaazi hao waliobaki wanaishi katika nchi zilizo Kusini mwa Sahara.

Ndugu Wananchi,
Wakati tunaadhimisha Wiki ya Maji Duniani, ningependa kugusia baadhi ya juhudi tunazuchukua katika kuwafikishia wananchi maji safi na salama na jinsi Serikali inavyojitahidi katika kuhakikisha inafikia yale malengo muhimu yanayowekwa na Jumuiya za Kimatafa juu ya huduma za usambazaji maji na hatua za kuyafanya maji yetu kuwa endelevu.

Napenda kuwajuilisha wananchi kuwa jana tulizindua mradi mkubwa wa kusambaza maji safi na salama utakaowanufaisha zaidi ya wakaazi 46,000 wa majimbo ya Mfenesini, Bumbwini, Kitope na Maeneo ya Jirani. Kwa mara nyengine tena nawashukuru wahusika wote walioshiriki na kujitolea kwa hali na mali katika kufanikisha dhamira yetu. Pia, nawashukuru sana wananchi ambao walionesha ari kubwa ya kujitolea kupitia kamati zao za maendeleo. Na matumaini yangu kuwa wananchi wa majimbo mengine watafuata mfano huu mzuri waliouonesha wananchi wa majimbo haya toka mwanzo hadi kufikia uzinduzi wa mradi huu. Ni dhahiri kuwa mradi huu ni miongoni mwa vielelezo halisi vya jitihada za Serikali yetu.

Ndugu Wananchi,
Natumai mtakumbuka kwamba katika hotuba yangu ya Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 48 ya Mapinduzi niliyoitoa mwezi wa Januari, nilibainisha miradi mbali mbali na juhudi zilizochukuliwa na zinazochukuliwa na Serikali katika uenezaji na uimarishaji wa huduma za maji safi na salama kwa wananchi. Miongoni mwa mambo niliyobainisha ni kuwa Serikali imechukua mkopo mkubwa wenye thamani ya T. Shs. 33 bilioni kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa lengo la kugharamia upatikanaji wa maji safi. Fedha hizi zitatumika kwenye mradi wa uimarishaji wa miundombinu ya maji, ujenzi wa visima na kuijengea uwezo zaidi Mamlaka yetu ya Maji ya Zanzibar (ZAWA).

Katika siku hii ya Maji duniani, napenda kuchukua nafasi hii kutoa shukurani maalumu kwa Serikali ya Japani, Shirika la JICA, Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, Jumuiya ya Nchi za Ulaya ( EU), Benki ya Maendeleo ya Afrika na washirika wetu wote wa maendeleo katika sekta hii kwa jitihada na michango yao katika kusambaza na kuimarisha huduma za maji nchini petu.

Ndugu Wananchi,
Napenda kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitosita kuimarisha utoaji wa huduma za maji hadi itakapohakikisha kuwa lengo la kusambaza maji kwa wananchi wote wa Zanzibar linatekelezwa kama vile lilivyodhamiriwa na waasisi wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 na pale tunapofikia malengo yanayowekwa na Jumuiya za Kimataifa katika kukidhi mahitaji ya maji kwa wananchi wetu. Serikali inatambua upatikanaji wa maji safi ni chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Miongoni mwa faida kubwa zinazopatikana ni kuwapa nafasi zaidi watoto wetu hasa wale wa vijijini ya kujishughulisha na masomo yao, kuimarisha huduma za kilimo na kuiwezesha jamii yetu kujenga afya bora.

Ndugu Wananchi,
Licha ya jitihada tunazozichukuwa katika suala hili, nafahamu kuwa tumekabiliwa na changamoto nyingi katika sekta ya maji hapa Zanzibar. Ili kuishinda changamoto zilizotukabili katika sekta ya hii ni muhimu kuiamini na kuitekeleza ipasavyo ile rai ya kuwajibika kwa pamoja “Collective responsibility”. Nachukuwa nafasi hii kuwataka wananchi kuiendeleza vizuri rai hii, kila mmoja wetu aamini kwa dhati kuwa anawajibu wa kuchangia ipasavyo kwa kila kitu muhimu kinachohusu maendeleo yake binafsi, maendeleo ya jamii iliyomzunguka pamoja na maendeleo ya nchi yetu kwa jumla.

Aidha, tuache ile tabia ya kuilaumu serikali kwa kila kasoro inayojitokeza kwenye jamii yetu. Napenda kuwahimiza wananchi waendeleze tabia ya kuchukua jitihada zao binafsi kwanza, pindi wakibaini maji kwenye mifereji yanamwagika katika maeneo wanayoishi, ikishindikana au ikibainika kuwa tatizo ni kubwa au ipo hatari ya kiufundi inayotishia usalama basi watoe taarifa kwa taasisi husika. Pia, nawasihi wananchi kuweka maslahi ya wengi mbele kwa kuepuka kujenga kwenye vianzio vya maji. Vile vile, tujenge uzalendo wa kulipia michango midogo ya kifedha tunayotozwa yenye lengo la kuendeleza na kuimarisha huduma za maji. Kadhalika, tuwe wakali na wenye busara pindi tukiona ubadhirifu na israfu inafanyika kwenye maji au miundo mbinu ya maji. Kwa pamoja, ni imani yangu tutafikia malengo tuliyojiwekea na tutashinda.

Ndugu Wananchi,
Kwa kumalizia, natoa shukurani zangu kwa mara nyingine kwa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati na wote walioshiriki katika kuandaa hafla hii muhimu ya Wiki ya Maji Tanzania na Siku ya Maji Duniani kwa maadalizi mazuri na kazi kubwa waliyoifanya. Natoa shukurani maalum kwa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kwa juhudi zao za kila siku za kuwapatia maji safi na salama wananchi wote wa Zanzibar. Pia, shukurani za pekee ziende kwa wananchi kwa michango na ushirikiano wao wa karibu na Mamlaka yetu ya Maji na nawataka watekeleze kwa vitendo yale yote waliyoelimishwa na kuelekezwa kuhusu maji kwa jumla kupitia Redio na Televisheni. Aidha, maonesho haya tunayoyazindua leo yatadumu kwa muda wa siku tatu ili kutoa fursa zaidi kwa wananchi kuona mambo mbali mbali yanahusu historia ya huduma ya maji hapa Zanzibar, upatikanaji wa maji safi na salama, changamoto zinazoikabili sekta ya maji na mipango ya kukabiliana na changamoto hizo kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji mzuri na endelevu wa huduma ya maji hapa nchini.

Natoa wito kwa wananchi wote kuhudhuria maonesho haya ambayo yameandaliwa maalum kwa ajili yenu.

Baada ya kusema hayo, pamoja na kukata utepe sasa natamka kwamba maonesho ya siku ya maji duniani yamefunguliwa rasmi.

Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.

Advertisements

One response to “Hutuba ya wiki ya maji duniani

  1. Hi there, just became aware of your blog through Google, and found that it’s truly informative. I am gonna watch out for brussels. I will appreciate if you continue this in future. Lots of people will be benefited from your writing. Cheers!

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s