Viongozi wa wizara ya habari ni hamnazo

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar akifuatilia kwa umakini malalamiko ya wafanyakazi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo katika kikao alichokiitisha hoteli ya Bwawani kwa ajili ya kusikiliza maoni yao. Kulia ni Waziri wa Wizara hiyo, Abdillahi Jihad Hassan

Na Salim Said Salim
Yapo mambo katika maisha ambayo  mtu hawezi kutoa au kupokea nusu. Ni lazima mtu aamue kutoa au kupokea chote kiliopo mbele yake na sio nusu nusu. Miongoni mwao ni mapenzi, ya aina moja au nyengine. Hivyo hivyo ni kwa suala la chuki na uhasama.
Hapa nataka kutoa mfano wa mafunzo ya kihistoria yaliyopatikana wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia (1938-45)  wa mtihani uliomkuta dada mmoja wa Poland, Sophie Zawistowka.  Dada huyu alikuwa na asili ya Kiyahudi (angalia filamu ya sinema iliopata tunzo mwaka 1982 iitwayo “Sophie’s Choice”, yaani Chaguo la Sophie).
Dada Sophie alikamatwa Austria na wanajeshi wa Kinazi wa Ujerumani na kupelekwa katika kambi. Siku moja alitakiwa aamue mtoto wake yupi kati ya wawili aliokuwa nao atiwe kwenye tanuri la gesi na kuangamizwa na yupi abakishiwe. “Unanitaka nichaguwe?”, Sophie alimuuliza daktari wa kijeshi huku machozi yakimtoka na kutoamini aliyokuwa akiambiwa.
Daktari alimjibu :” Tumekuonea huruma. Wengine wanapoteza maisha ya watoto wao wote na baadaye wenyewe”.
Huku akilia na kusema “ Siwezi…siwezi” mwanajeshi mmoja alimchukuwa mtoto aliyekuwa mdogo kati ya wale waili na kumpeleka kuangamizwa na gesi.
Hali hii ukiitafakari utaona jinsi chuki zinavyomfanya mtu awe jahili na jinsi mzazi anaposhindwa kuchagua mtoto wake yupi auawe na yupi abakie naye. Ninapoangalia namna Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar inavyofanya kazi ninaona  yaliomkuta Sophie ndio waliyonayo baadhi ya viongozi wa ngazi za katikati, hasa katika Wizara ya Habari.
Watu hawa bado hawawezi kuchagua. Ni watu hawa, kwa kauli na vitendo vyao vya dhahiri na vya chini ya mvungu, wanajidai kuikubali SUK nusu na wanaikataa nusu.Sikushangaa niliposikia wanapewa jina la kisebusebu. Watu hawa wamekuwa wakibuni mambo na kutaka uzushi wao ukubaliwe na uaminike na jamii. Masikini watu hawa, wanasahau kuwa vitendo vyao vya siku za nyuma vimewajengea umaarufu wa kutokuwa wakweli na kwa hivyo kila wasemalo au watendalo huchambuliwa na jamii, wakiwemo waandishi wa habari, kwa uangalifu mkubwa.
Vipindi vyao vya siku za nyuma katika Televisheni ya Zanzibar ni ushahidi tosha wa namna ambavyo walivyojitwisha mzigo wa kugonganisha na kugawa watu. Miongoni mwa eneo linaloangaliwa kupita nia yao kwa Zanzibar ni namna walivyokuwa wakati wa kampeni ya kura ya maoni na wakati wa kutafuta mgombea wa CCM katika uchaguzi wa Rais wa Zanzibar mwaka 2010. Masikini roho zao, wanafikiri watu waamesahau nyendo zao wakati ule.
Siku hizi baadhi ya watu hawa wamejikita kuandika makala zinazochochea chuki na uhasama kwa kutumia majina bandia. Wanafanya hivyo kwa kuwa hawana ujabari wa kutumia majina yao halisi, lakini matumizi yao ya maneno yanawaumbua na watu kujuwa kila makala ya uchochezi wanayoaandika.
Katika taaluma ya habari watu wa aina hii wnaaotumia majina bandia huonekana zaidi kuwa ni wanafiki na sio wakweli na wengine ambao niliwafunza taaluma hii niliwataka watmie majina yao halisi ili watu wawaamini na waelewe wanayemjibu kwa heshima na adabu.
Lakini wanaficha majina yao kwa sababu makala zao ni za uchochezi na hawataki wajuline. Eneo ambalo hivi sasa linaonekana kuandamwa sana na watu hawa wanaopendelea kuona kuna mvutano na migongano ya kisiasa Zanzibar ni sekta ya habari.

Nilishangazwa mwezi uliopitakuona wanamdanganya waziri wa habari na kueleza  ndani ya Baraza la Wawaklishi kuwa rasimu ya muswaada wa sheria ya uhuru wa habari uliopelekwa Baraza la Wawakilishi haukushirikisha wadau wote, wakati karibu wasaidizi wote wa wazi walishiriki kikamilifu na kuchangia. Kilichoelezwa na wizara ni uwongo, unafiki na uzandiki.

Hapa ninaona unataka kuanzishwa mradi wa kula fedha, kama inavyofanyika kwa taasisi ziliopo chini ya wizara (kimojawapo ni chuo cha habari ambacho mimi ni mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi)  na kukandamiza uhuru wa habari Visiwani.
Masikini roho za watu hawa. Inaonekana bado hawakubali kuwa huwezi kuzuwia maji kujaa na kukupwa. Hivyo hivyo, huwezi kuzuwia mageuzi, unachoweza kufanikiwa kufanya ni kukawikilisha mageuzi kupatikana, lakini yatakuja tu. Nataka kueleza wazi kuwa  tayari wakati wowote ule kuwa na mjadala wa wazi na maofisa waandamizi wa wizara ya habari kuonyesha kwamba wameudanganya umma. Kama kweli wanao uhakika na waliyoyafanya na tuwe na mjadala huo na umma utaamua nani ni mkweli.
Baada ya hapo wamebuni unafiki wa kueleza kwamba vijana wawili waliokuwa wanafanya kazi Television Zanzibar (TVZ) walikuwa wanawachonganisha Rais Ai Mohamed Shein na Makamo wake wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad.

Hata wenyewe wahusika walijikanganya. Mmoja anasema ni uhamishio w akawaida na mwengine anazungumzia uchinganishi.kati yao nani alikuwa aneleza kweli? Huu nao ni uwongo na ubunifu  mwengine ambao ninaanza kuamini kuwa huenda ukawa na ajenda ya siri. Lakini wahusika, wanapswa kujuwa kuwa uwongo, hata uukiwa umepambwa vipi, huwa na mwisho wake na Wazanzibari (Unguja na Pemba)  hawapo tayari kugongeshwa vichwa na kuanza kutukanana, kupigana na hata kuuwana.
Watu hawa wanapaswa kuelewa kuwa hapo baadaye watakuja kujijutia kwa wanayoyafanya hivi sasa  na kama hawajajifunza kwa maovu waliyoyatenda siku za nyuma watajifunza kwa maovu yao ya sasa siku za mbele. Ipo siku, ni vizuri wakajifunza haraka na kujirekebisha.
Hapana uchonganifu wowote uliofanywa na wale waandishi wawili. Habari inayolalamikiwa na watu hawa ya Dk. Shein kupewa muda mdogo kuliko Maalim Seif ni usanifu ambao haukuifanywa kisayansi. Kwa kweli habari ilitoka Ikulu na kutolewa kama ilivyopelekwa TVZ na muda wake ulikuwa mkubwa kuliko ule wa habari ya Maalim Seif.
Kama kwatu hawa walikuwa wanataka kutenda haki wale vijana wawili wangepewa nafasi ya kujieleza na sio kusukumiwa shutuma nzito za ubunifu. Kutowapa nafasi kwa sauti zao kusikika ni dhulma. Jamani tukumbuke kuwa vyeo tulivyonavyo ni dhamana na katika kutekeleza dhamana hizi tusiwaonee wadogo zetu.
Ni vizuri watu hawa wakaamua wanaiunga mono SUK au wajitokeze wazi kuwa wahafidhina wasiotaka Zanzibar kuwa na amani na utulivu. Tabia ya kisebusebu haiwasaidii na Wazanzibari hawatawafumbia macho na kuziba masikio.
Wazanzibari wamechoshwa na uchonganishi na wamejifunza gharama zake. Huu ambao watu hawa wanaoubuni  hivi sasa na kujifanya wazalendo na kumbe ni wasalito hauwezi kukubaliwa na umma.
Ni vizuri wakajirekebisha haraka. Historia haitawavumiulia na maovu yao yatapokuja kuanikwa wasije kusema wanaonewa. Mtu huvuna anachokipanda na wao watavuna kwa wanayoyapanda hivi sasa.
Kwa muda mrefu tokea ulipokuja mfumo wa vyama vingi vya siasa watu wa Zanzibar wameteseka vya kutosha. Tuwaache wapumue na kuangalia hatima ya maelewano yaliokuwepo na tuache kuwachonganisha viongozi. Nawaomba wale ambao inaonekana hawaitakii mema Zanzibar basi angalau wasiitafutie balaa. Yatosha..yatosha…tuliyoyaona.

Advertisements

2 responses to “Viongozi wa wizara ya habari ni hamnazo

  1. “Watu hawa” ni watu gani ni bora kuanika majina yao hadharani ili tupate kuwajua maadui wa Zanzibar yetu.

  2. Ni kweli sasa wakati umefika kwa watu kama hawa kutoonewa haya Hata kama ni nani aanikwe tu. Hawa hawafai kwenye jamii ya Wazanzibari. Hivi kwa nini bado Serikali inawakumbatia tu mpaka leo? Au inakubaliana na mambo wanayoyafanya? Honger sana muandishi kwa kua jasiri kufichua maovu yanayofanyika. Hivi ndivyo tunavyotaka mambo yende. Utaratibu wa viongozi kupitia mawizara na kuongea na wafanyakazi wa chini uwe ni wa kudumu. Kuna mengi sana huko maofisini ambayo watumishi wanataka wayaseme.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s