Waziri Jihad Agombezwa mbele ya wafanyakazi

Mfanyakazi wa Shirika la Utandazaji Zanzibar (ZBC) Televisheni, Nassra Nassor akitoa dukuduku lake mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad huko hoteli ya Bwawani.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,Maalim Seif Shariff Hamad ‘amemlipua’Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na  Michezo, Abdillah Jihadi Hassan  mbele ya wafanyakazi wa Wizara yake kwa kushindwa kutoa maelezo aliyotakiwa na Kiongozi huyo.

 

Akizungumza katika mkutano na wafanyakazi wa Wizara ya habari utamaduni utalii na michezo katika hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar, Makamu wa Kwanza alisema anashangazwa na kitendo cha Waziri Jihadi licha ya kumwandikia barua kumtaka maelezo ya sakata zima la kuondolewa  wahariri wawili Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) hakuna jibu alilopewa hadi ameitisha mkutano huo.

Amesema aliitisha mkutano huo makusudi kwa ajili ya kusikiliza malalamiko ya wafanyakazi, huku akiweka wazi kuwa hawezi kusikiliza maelezo ya viongozi pekee, kwa kuwa wakati mwengine hutoa maelezo ya kujilinda na kujijenga kuliko kuwasilisha mawazo ya wafanyakazi.

Maalim Seif ameitaka Wizara hiyo kuacha tabia ya kutoa majibu ya mkato kwa wafanyakazi kuwa matatizo yao “yatashughulikiwa”, bali ametaka malalamiko yaliyotolewa yawekewe utaratibu wa kuyashughulikia, na yeye apewe ripoti juu ya utekelezaji huo.

Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, pia ameonya juu ya kitendo cha kuwahamisha kazi wahariri wawili wa shirika la Utangazaji la Zanzibar upande wa Televisheni kwa visingizio visivyoeleweka.

Maalim Seif alipinga uamuzi wa kuondolewa wahariri katika nafasi zao kwa kuwa hawakutendewa haki na uonevu ndio uliotawala. “Watu wawili waliondolewa ni uonevu, mie nasema zama za uonevu zimekwisha haiwezekani kuwaonea wafanyakazi namna hii” Alisema Maalim Seif.

 

Alisema haoni mantinki kuondolewa kwa Wahariri hao na katika kulifuatilia suala hilo ndipo alipotaka kupata maelezo ya kujiridhisha kutoka kwa Waziri Jihadi amuonesha ni miongozo ipi waliyokiuka Wahariri hao hadi kufikia hatua ya kuondolewa katika nafasi zao,lakini hakuna jibu lolote kutoka kwa Waziri huyo.

 

Hivi karibuni Mhariri Mkuu wa ZBC, Juma Mohammed na Msaidizi wake Ramadhan Ali waliondolewa katika nyadhifa zao kwa madai kwamba wanawagonganisha Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein na Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Shariff Hamad kwa kumpa muda mwingi Makamu wa Kwanza kuliko Dk Shein.

 

Mmedai kwamba Wahariri hao wamekiuka miongozo, mbona Waziri umeshindwa kunijibu ni miongozo ipi waliokiuka? Alihoji Makamu wa Kwanza wa Rais katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa pia na Waziri Jihadi na Watendaji mbalimbali wa Wizara hiyo. Lakini Katibu Mkuu wa wizara hiyo Ali Saleh Mwinyikai hakuwepo katika mkutano huo uliofanyika Bwawani Hoteli.

 

Makamu wa Kwanzaa wa Rais ameahidi kulifuatilia suala la kuondolewa kwa Wahariri hao hadi mwisho kupata ukweli wa mambo ikiwemo kuoneshwa kuoneshwa miongozo ya ZBC inayodaiwa kukiukwa.

Wanavyodai viongozi wa Idara hiyo na Wizara kuwa wamekiuka muongozo, lakini nimewambia waniletee huo muongozo hawajaleta hadi sasa. Hivyo inaelekea kuwa hawa wameonewa tu na hatuwezi kukubali kwenda namna hiyo”, alionya na kuongeza;

Lazima tubadilishe utamaduni wa kuoneana katika serikali, huwezi kumuadhibu mtu kwa kuwa humpendi, mpe vitendea kazi na umuwezeshe, halafu hapo akishindwa mchukulie hatua, lakini sio kwa kuoneana kama hivi. Tena nasema hili halijaishia hapa, nitalifuatilia mpaka nilitie mwisho na nijue ukweli wake”, alifafanua Maalim Seif Seif.

Jumla ya wafanyakazi 12 kutoka Idara mbali mbali za Wizara hiyo walipata fursa ya kutoa maoni yao ambapo wengi walielezea kufarajika kwao na uamuzi wa Makamu wa Kwanza wa Rais kusikiliza maoni ya wafanyakazi.

Wengi kati ya waliopata fursa hiyo walielezea juu ya mazingira magumu ya kazi yenye upungufu wa vitendea kazi vikiwemo usafiri pamoja na ufinyu wa maeneo ya kufanyia kazi.

Sambamba na hilo, wafanyakazi hao walilalamikia maslahi duni wanayopata kutokana na kazi ngumu wanazofanya huku wakikosa malipo ya muda wa ziada pamoja na pesa za likizo.

Wafanyakazi wa Shirika la Utangazaji upande wa Televisheni wamesema wanafanya kazi hadi saa 8 usiku na wakati mwengine hushindwa kurejea majumbani kwao kutokana na tatizo la usafiri na kulazimika kulala kituoni hapo, huku wale wa upande wa Redio wakikabiliwa na tatizo hilo la usafiri na kupelekea kufunguliwa kwa matangazo ya asubuhi kwa wakati.

Katika mkutano huo wafanyakazi wa ZBC walieleza matatizo na changamoto zinazowakabili ikiwemo maslahi duni, ukosefu wa usafiri, mazingira magumu ya kazi, ukosefu wa vitendea kazi na mambo mengine mengi ambapo walimuomba Makamu wa Kwanza kulichunguza suala hilo.

 

Sehemu kubwa ya malalamiko ya wafanyakazi yameshindwa kupatiwa ufumbuzi kwa muda mrefu na uongozi wa ZBC chini ya Mkurugenzi Mkuu, Hassan Abdallah Mitawi ambapo alikuwepo katika kikao hicho.

 

Kwa kweli leo tumefarijika sana kupata fursa hii kukueleza hali zetu pale ZBC hususan TV, Mimi nimebakisha mwaka mmoja kabla ya kustaafu kazi mwakani,lakini tunakwambia Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais tunamatatizo utusaidie…mishahara duni, hakuna posho la saa za ziada, likizo, hakuna anayetujali” Alilalamika Abdulhakim Mfanyakazi wa ZBC (Televisheni).

 

Nassra Nassor wa ( ZBC TV) alisema hali ya wafanyakazi wa Shirika hilo inahuzunisha sana kwani wanafanyakazi katika mazingira magumu hakuna usafiri, hakuna motisha yoyote ni mateso kiasi wafanyakazi wanavunjika moyo, lakini hawana pa kwenda.

 

Mheshimiwa Makamu wa Kwanza TV imefikia pahala baadhi ya wafanyakazi wanalala pale pale tena wake za watu kwa ukosefu wa usafiri wa kuwarudisha majumbani wakati wa usiku…tunaambiwa hakuna usafiri ni mtihani kwa kweli matatizo haya tumeyaeleza sana kwa viongozi, lakini hakuna ufumbuzi tunakuomba utusaidie kuondokana na hali hii” Alisema Nassra.

 

Aidha, Makamu wa Kwanza katika utangulizi wake alisema yeye hakwenda katika mkutano huo kutoa hotuba wala kusikiliza maneno ya Viongozi Wakuu wa Wizara na Idara za Wizara hizo bali amekwenda hapo kuwasikiliza wafanyakazi maoni yao kwani mara nyingi Watendaji Wakuu huficha mambo kwa kueleza yale mazuri tu.

 

Pia ameagiza Uongozi wa Wizara hiyo kumplekea ripoti ya kila jambo namna ilivyotekelezwa na yaliyoshindikana kutekelezwa na maelezo yake kwanini hayakutekelezwa.

 

Alisema hatokuwa na mzaha katika kushughulikia maslahi ya Wafanyakazi na kwamba matatizo yote atayafanyia kazi yale yaliyo makubwa atayawasilisha katika ngazi za juu kuyapatia ufumbuzi na yale ambao ana uwezo nayo atayashughulikia huku akisisitiza wakati wa kuoneana umepitwa na wakati.

Maalim Seif alisema zama za kufanya kazi kwa uzalendo zimepitwa na wakati na sasa wafanyakazi wanahitaji kufanya kazi kwa kupewa motisha na kulipwa vizuri kwani viongozi wanapokwenda safari huwa wanajua pa kuzipata fedha lakini kwa kuwapa wafanyakazi ndio wanashindwa.

Aidha Maalim Seif ameuagiza uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kuyafanyia kazi malalamiko ya wafanyakazi wa sekta hiyo, ili kuwawezesha kufanya kazi kwa umakini zaidi.

Bw. Mohammed Mustafa Mohammed kutoka kamisheni ya Utalii, amesema wakati serikali inajiandaa kuingia katika mpango wa “Utalii kwa wote” ni vyema kituo kikuu cha habari kwa watalii kikafufuliwa ili kutoa taarifa sahihi kwa watalii.

Kabla ya kukutana na wafanyakazi hao Maalim Seif alifanya ziara ya kutembelea Kamisheni ya Utalii na taasisi zake na kuonesha kusikitishwa na mmomonyoko wa fukwe katika chuo cha maendeleo ya Utalii Maruhubi. Ameitaka Wizara hiyo kulishughulikia kwa haraka tatizo hilo ili kunusuru athari kubwa zinazoweza kujitokeza

Advertisements

2 responses to “Waziri Jihad Agombezwa mbele ya wafanyakazi

  1. Heko Maalim Seif kwa msimamo wako huu!! tupo nyuma yako Inshallah tutafika!! Ule wakati wa porojo na kuoneana na kutesana umepitwa na wakati !! jenga nchi Maalim,wakati ndio huu!! hakuhitaji jukwaa la siasa kuelekeza yaliosawa na ya haki !!

  2. Inashangaza kwa nini mtendaji mkuu wa wizara hii yaani katibu mkuu hakuhudhuria kwenye mkutano huu. Nafasi walioipata wafanyakazi ya kutoa malalamiko yao mbele ya makamo wa kwanza wa rais ni hatua moja ya kubwa lakini pia nafasi inaweza kutumiwa vibaya na viongozi wa wizara hiyo pindipo madai hayo yakichukuliwa kisiasa. Suala la kuwahamisha maofisa wawili wa ZBC ni nyeti. Suala hili niliwahi kumsikia mkurugenzi mkuu bwana Mwintawi akisema kuwa uhamisho wa watumishi hao ni uhamisho wa kawaida. Suali la ukiukaji wa maadili alisema bwana Mwintawi kuwa ni siri ya wizara lakini uhamisho huo hauhusiani na tatizo hilo. Kwa mawazo yangu liko jambo hapa na jambo hilo linwaeza kuzua jambo. Hayo ni mawazo yangu. Mwenyezimungu atusaidie. ..

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s