SMZ ipanie kuanzisha makumbusho ya Kiislamu

Marehemu Maalim Muhammed Idrissa

Na Ally Saleh

Katika miaka hii mitatu nimeshuhudia matukio ya vifo matatu ambayo kwangu nimeona ni makubwa na kwa kweli yalinitikisa pamoja na kujua kifo ni wajibu kwa kila binaadamu na kila moja kati yetu ataona mauti. Na sio tu yalinitikisa lakini kwa kweli yameniwachia kumbukumbu kubwa moyoni na akilini mwangu na ningependa kubaki na kumbukumbu hizo maana vifo vya watu hao ni alama kubwa ya mafanikio na uzalendo wa watu hao.

Huku nyuma nilikuwa siamini kuwa kufa kunaweza kusherehekewa baada ya kusikitika, sio badala ya kusikitika. Kwa maana kifo kitaleta huzuni na utasikitika lakini baada ya masikitiko kuna nafasi ya kusherehekea.

Lakini sio vifo vyote vinavyosherehekewa. Inategema mtu na mtu na kwa maana ya makala haya juu ya watu ambao nimewataja kuwa ni matukio yalio kwangu ni makubwa vifo vyao tumevisikitikia lakini kisha tumevisherehekea na kila mmoja bado anavisherehekea na vizazi kwa vizazi watavisherehekea.

Ila hofu yangu isie tu kuvisherehekea kwa maana ya kuvitukuza lakini ifuatiwe na kuvihifadhi na kuvijengea kumbukumbu kwa sababu kusherehekewa kwao kunatokana na kufanya mema wakati wa uhai na sio mema tu lakini kutumikia ubinadamu kadri walivyoweza.

Na hii ndio maana yangu ya kusherehekea. Wanaosherehekewa baada ya kufa ni wale watu ambao kuja kwao duniani hakukuwa kuongeza takwimu tu lakini wameacha athari ambayo inakuwa ni chachu ya elimu na mabadiliko kwa wale ambao wataendelea kuishi.

Kwa sababu kifo ni wajibu, na aliyekufa ametimiza azma zote katika maisha yake na kutoa mchango maridhawa, tena kwa nini tusifurahie kifo chake? Sio ndio mpaka leo tunasherehekea vifo vya nyota wengine kadhaa na viongozi maarufu duniani basi kwa nini tusisherehekea watu wema wanaokufa katika jamii yetu lakini maisha yao yamewacha mwanga mkubwa kwetu tuliobakia, lakini zaidi kwa vizazi na kama taifa?

Na watu kama hawa hawawi wengi katika jamii. Nani kasema vito vinakuwa vingi? Vito ni vichache tu na hivyo ndivyo ambavyo jamii ina vitizama maana hata kabla ya vifo vyao kila mtu anajua kuwa wanachokifanya ni cha faida ya umma na sio wao binafsi.

Watu walio karibu nao na hata walio mbali hawachelewi kubaini uwezo wao ambao mara zote kuwa ni kipaji wanachopewa na Muumba na hicho huwasaidia kila wakigusacho kubadilika na kuwa chanya hata kama kilikuwa ni hasi kwa kiasi gani, lakini wakiingia wao kubadilika.

Huwa na kauli thabiti, huwa watu wa ahadi lakini pia huwa watu wa watu. Kwao inakuwa rahisi kushirikiana na yoyote maana kwa maumbile huwa ni wasikivu na huwa ni waongozaji wakati wote na huwa ni rahisi kupata wafuasi lakini mara zote huwa na kundi la kubwa la watu linalowahusudu kwa mafanikio yao.

Watu kama hawa huwa ni muongozo katika jamii kwa kauli zao lakini zaidi huwacha vitendo vyao kuonekana na watu kuwaamua kwa vitendo, maana tumeambiwa kuwa Ada ya Mja Kunena Muungwana ni Vitendo na hilo kwao huwa halijifichi kabisa kwa kila jicho linalotaka kukubali ukweli.

Basi watu ambao sifa zao nimezitaja hapo juu na ambao nimesema kuwa ni mfano kwenye jamii (role model) na ambao hatunao na wametuhama duniani ni Maalim Khalfan Hemed, Professor Haroub Othman na Maalim Muhammed Idrissa ambaye yeye alifariki wiki iliyopita wakati Maalim Khalfan alifariki miaka miwili mitatu iliyopita na Professa Haroub akafuatia.

Kwa leo sina haja ya kuelezia wasifu wala sifa za Prof. Haroub au Maalim Khalfan ambao wengi wetu tunawajua, lakini natamani sana Wazanzibari na Watanzania wajue sifa za Maalim Muhammed Idrissa ambaye ni shujaa mwengine ambae tumempoteza na hatuna budi kuona kuwa anaenziwa.

Lakini kubwa ninalotaka kuandika leo kuhusu Maalim Muhammed Idrissa ni wazo au kazi ambayo alikuwa ameianza na kuifikisha sehemu nzuri kabisa kwamba isipotee wala isife na hatua zichukuliwe kuhakikisha kuwa inalindwa, inadumishwa na inatunzwa kwa vizazi vijavyo.

Maalim Muhammed Idrissa alianza kazi ambayo pengine wengi wangefikiri kwamba ilikuwa ianzwe na mtu mwengine yoyote huko nyuma, lakini hakuna alojaaliwa na kwa hivyo akawa ni yeye aloona thamani ya historia ya Kiislamu ya Zanzibar ambao inakwenda karne nyingi nyingi zilizopita.

Hakuna ubishi kuwa historia ya Zanzibar ni historia ya Kiislamu. Wahamiaji takriban wote waliofika Zanzibar walitokea katika nchi zenye Uislamu na hadi sasa asilimia kubwa ya wakaazi wa Visiwa hivi ni Waislamu lakini Serikali haikuwahi kuchukua hatua za kuulinda utamaduni, silka na thakafu za Kiislamu kama sehemu ya urithi muhimu wa nchi na vizazi vyake.

Kwa hali inavyoonekana sasa Uislamu ni kama dini tu, lakini kuwa una mizizi katika mavazi, malezi, ndoa, mazishi, mapishi, mahusiano, elimu yetu si jambo ambalo linaweza kuwa limetunzwa.

Lakini Uislamu wa Zanzibar una athari kwenye majengo, nyumba zake za ibada na kuna watu wengi ambao mchango wao ni mkubwa sio tu kwenye dini lakini kwenye kujenga maadili ya jamii kwa sababu ya usafi wao, elimu yao, uongofu wao na hao ni wengi wa mashekhe ambao walivuma nchini na nje ya nchi. Orodha yake nikiitaja siwezi kuimaliza kabisa na nikitaja mafanikio yake hayatatoshi kwa kitabu labda kwa makumbusho (museum).

Kwa hivyo kila kitu kinakwenda kama kawaida tu na kuna hatari itafika siku hatutajua utamaduni wetu ndio upi, malezi yetu ndio yepi, mavazi yetu ndio yepi na kadhalika. Tumekuwa kama taifa lilokosa uchungaji, maana ndio taifa lisiloweka kumbukumbu zake.

Maalim Muhammed Idrissa amethubutu kufanya kazi kubwa ya kihistoria kwa kujitolea kama mtu binafsi kukusanya nyaraka, picha, vifaa na mambo mengine mengi ambayo yana mnasaba wa moja kwa moja na historia ya Kiislamu ya Zanzibar ambapo vitu hivyo vilikuwa nyumbani kwake Mtaa wa Kelele Square na akivionyesha kwa wageni na wenyeji mbali mbali.

Wasi wasi wangu ni kuwa vitu vyote hivyo visipotee na kuondoka lakini pia dhana na fikra yake ya kuanzisha Makumbusho ya Kiislamu isiende arijojo ila itunzwe na kukamilishwa katika ukamilifu wake wote kwa kuwa na kitu rasmi na ambacho kiwe ni hazina ya taifa.

Naamini vitu vilivyokusanywa na Maalim Muhammed Idrissa ni kidogo tu ikilinganishwa na vile ambavyo viko mitaani kwetu na majumbani mwa watu ambapo kama Serikali itaanzisha Makumbusho rasmi inayolenga kutunza historia ya Kiislamu basi vitu hivyo vitaweza kutunzwa chini ya paa moja kwa faida kubwa zaidi ya taifa na vizazi vijavyo.

Kila siku hapa Zanzibar kuna mjadala wa kuanzisha au kuvumbua vyanzo vipya vya kuvutia watalii na miaka ya karibuni Serikali ya Zanzibar kwa ushirikiano na taasisi ya Aga Khan ilikuja na wazo la kutunza Historia ya Bahari ya Hindi ( Indian Ocean Maritime History) na jengo kwa ajili ya kazi hiyo limeshatengwa.

Wazo langu ni kuwa hatua nayo pia ichukuliwe kutafuta jengo, na kutafutiwa fedha ama za ndani au nje ili tuwe na Makumbusho ya Historia ya Kiislamu Zanzibar ( Zanzibar Islamic History Museum) ili nchi hii iweze kusimama kifua mbele kwa miaka mingi ijayo kwa kutunza utamaduni wake.

Tusichelewe zaidi, maana tokea hapo tumechelewa. Wazo la Maalim Muhammed Idrissa lifanyiwe kazi kabla ya kupiga kelele akiwa kaburini kuwa kwa kuwa amekufa basi kila kitu chake kimesambaratika…basi hata mbegu aliyoipanda tumeshindwa kuitilia maji?

Advertisements

5 responses to “SMZ ipanie kuanzisha makumbusho ya Kiislamu

  1. Assalamualaykum. Mimi naungana nawe katika jambo hili na ni jambo zuri sana kuliendeleza. Itafikia wakati wazanzibari hatutakuwa na historia hata chembe. Kuwaenzi na kutunza mashekhe na wanazuoni pamoja na majengo na makaburi ya wanazuoni hao yatosha kuwa ni historia kwa zanzibar. Suala la kujiuliza ni Jee kuna kijana wa rika kama langu atakubali kufanya kazi hiyo? na kama yupo Jee wazee waliobaki wanaowajua hao watakubali kutoa mashirikiano? Tatizo kubwa la Zanzibar ni UBINAFSI. Mara nyingi unaangaliwa usoni, ni mtoto wa nani? au baba yako alikuwa nani?

  2. INNALILAH WAINNAILAIH RAJU’UN. Ni ukweli usiofichika kuwa zanzibar haina uwezo wa kuanzisha MAKUMBUSHO YA KIISLAM kwani MAKAFIRI WA TANGANYIKA HAWATOKUBALI. Na lakuzingatia ni kuwa zanzibar ni koloni la TANGANYIKA kwahivyo, zanzibar haina mamlaka ya kuamua chochote bila ya kupangiwa na TANGANYIKA. WAZANZIBAR HATUUTAKI MUUNGANO NA MAKAFIRI WA TANGANYIKA.

  3. Kuna nyingi simulizi, ambazo zatia hamu
    Za kale na siku hizi, kuzitunza ni muhimu
    Tusiige upuuzi, ja kuabudu mizimu
    Utamaduni udumu, vizazi hadi vizazi.

  4. Kwa kweli Ally Saleh umeeleza kitu muhimu sana n a ni vyema kuungwa mkono na kila mpenda utamaduni mwema wa Kizanzibari ambao umeungana sana na utamaduni wa kiislam. Mimi nakuomba Ally Saleh hata baada ya kuyaweka haya kwenye maandishi uwe msitari wa mbele kuifuata SMZ na kuishawishi ili iianzishe Maonyesho hayo.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s