Hatutakubali amani ya Zanzibar ichezewe – Maalim

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad akiwahutubia wananchi wa Jimbo la Wete baada ya kukabidhi vifaa mbali mbali kwa jimbo hilo huko viwanja vya Jadida Wete

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad amesema serikali haitovulimia vitendo vyovyote vinavyoashiria uvunjifu wa amani vyenye lengo la kuvuruga umoja wa Zanzibar. Kauli hiyo ya Maalim Seif imekuja kufuatia kitendo cha kushushwa bendera ya Chama Cha Wananchi (CUF) huko Wawi Kisiwani Pemba kilichofanywa na kikundi cha watu fulani kwa lengo la kukidhoofisha chama hicho.

Maalim Seif alisema Zanzibar haitorudi tena nyuma, licha ya kuwepo baadhi ya watu wasiopenda maendeleo ya Zanzibar, na kwamba wanaotumiliwa kwa ajili ya kuendesha vitendo hivyo watapambana na mkono wa sheria. Alitoa onyo hilo huko Jadida kisiwani Pemba, alipokuwa akizungumza na wananchi wa jimbo la Wete, mara baada ya kukabidhi vifaa kadhaa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni ishirini na tisa (milioni .29) vilivyotolewa na mbunge na mwakilishi wa jimbo hilo.
Hali hiyo imekuja kufuatia kujitokeza viashiria vya kuwepo kundi la watu wanaotumiliwa kwa lengo la kuvuruga umoja wa Zanzibar, baada ya kundi hilo kupachua bendera ya chama kimoja cha siasa katika eneo la Wawi hivi karibuni.
“Nchi yetu imetulia na hatutovumilia vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani, tena nasema hatutorudi nyuma”, alisisitiza Maalim Seif.
Akizungumzia kuhusu vifaa vilivyotolewa vikiwemo gari moja ya jimbo hilo, pasola moja na baiskeli 23 kwa ajili ya maendeleo ya chama na printers 5 kwa ajili ya skuli, Maalim Seif amewataka wananchi kuvitunza na kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa. Pia alikabidhi vifaa mbali mbali vya michezo vikiwemo mipira 195 na jezi seti 11.
Amewapongeza  viongozi wa jimbo hilo kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi walizozitoa kwa wananchi, na kuwataka  kuongeza mashirikiano kwa wananchi, ili mafanikio zaidi yaweze kupatikana.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Dadi Faki Dadi alisema serikali bado haijapokea malalamiko hayo ya kupachuliwa bendera katika eneo la Wawi, lakini ameshtushwa kupokea taarifa hizo na kuahidi kuwa serikali italifanyia kazi na kuwachukulia hatua watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo.
Dadi alisema hivi sasa Zanzibar imetulia kufuatia kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa ambapo huko nyuma wananchi na viongozi walikuwa wakiishi kwa khofu licha ya kuwa ulinzi lakini bado viongozi walikuwa wakihofia usalama wao kutokana na hali tete ya kisiasa iliyokuwepo.
“Mimi nilikuwa nikitembea na walinzi lakini sikuwa najiona nipo salama…lakini leo hali imetulia naweza kutembea Pemba nzima bila ya mlinzi hata mmoja lakini hali hii ya usalama na amani iliyopo mnataka kuichezea na kuturejesha tulipotoka? …” alihoji Dadi.
Aidha alipongeza maamuzi hekma na ya kijasiri yaliyofanywa na Rais mstaafu Dk. Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad ya kufikia maridhiano ya kisiasa ambayo yamewawezesha wananchi wa Zanzibar kuishi kwa amani na utulivu na kurejesha mshikamano na umoja miongoni mwa wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salim Bimani alisema wapo baadhi ya watu wanatamani kukivuruga chama hicho lakini alisema wamechelewa kwani chama hicho kipo imara na hakiwezi kuvurugwa na watu wachache.
Bimani aliwataka wananchi kutulia na kutobabaishwa na watu wachache ambao hujitokeza na kutaka kuleta fujo katika nchi na badala yake alisema waimarishe chama chao kwani amani iliyopo inapaswa kulindwa na kuendelezwa zaidi ili wananchi wa zanzibar wapate kuletewa maendeleo.
“Hapa tulipofika tuseme mwisho kurudi tulipotoka tumegombana vya kutosha lakini tukasema basi sasa tunataka kujenga nchi yetu….msiwe na wasiwasi nchi hii ipo salama na viongozi hawatavumilia hata siku moja kuona watu wachache wanataka kutuvuruga na kutoondoshea matunda na amani yetu hii” alisisitiza Bimani ambaye ni Mkurugenzi wa CUF.
Mbunge wa Jimbo la Wete Mhe. Mbarouk Salum Ali na mwakilishi, Assaa Othman Hamad wameahidi kuendeleza mashirikiano ya wananchi kwa lengo la kukabiliana na kero zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo.

Advertisements

One response to “Hatutakubali amani ya Zanzibar ichezewe – Maalim

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s