Adhabu ya miaka mitatu ni kubwa -Maalim Seif

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akimkabidhi cheti maalum mjumbe wa bodi ya Skuli ya Sunni Madressa aliyemaliza muda wake Mhe. Haroun Ali Suleiman katika mahafali ya kidato cha nne na sita ya skuli hiyo

Kwa kweli suala hili limewafadhaisha sana wanafunzi hao waliofanya mtihani wa kidato cha nne, walimu na wazazi, lakini pia serikali. Pamoja na uongozi wa Baraza la Mitihani Taifa kujaribu kutoa maelezo na ufafanuzi wa kilichotokea hadi wanafunzi hao kufutiwa matokeo kwa wingi, bado inaonekana sehemu kubwa ya jamii ya Wazanzibari haijaridhika na maelezo hayo.Nashawishika kusema hivyo, kwa sababu mara kwa mara tumekuwa tukiona makongamano na mikutano mingi ya wazazi, wanafunzi na wadau wengine kujadili suala hilo, na baadhi ya wakati washiriki, huwa wakali juu ya jambo hilo. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatambua kuwepo kwa hali hiyo na kwa kweli kuna haja pande zote zijiridhishe na hali iliyotokea hadi kuzua mtafaruki huo, ili isitokee tena. Hivyo basi imebidi Wizara zetu mbili za elimu ya hapa Zanzibar na Tanzania Bara kukubaliana kufanya uchunguzi wa kina kwa minajili ya kuchimbua sababu halisi za hali hiyo kutambua udhaifu uliopo katika skuli na hata katika Baraza la Mitihani lenyewe. Moja ambalo ni dhahiri ni kuwa adhabu ya kuwafungia wanafunzi waliohusika miaka mitatu bila ya kufanya tena mitihani ni kubwa mno na hivyo Baraza la Mitihani linapaswa kuiangalia tena adhabu hiyo.
HOTUBA YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR MHE. MAALIM SEIF SHARIF HAMAD KATIKA SHEREHE ZA MAHAFALI YA 11 YA KIDATO CHA NNE NA MAHAFALI YA TISA KIDATO CHA SITA SKULI YA SUNNI MADRESSA TAREHE 10 MACHI, 2012
Mheshimiwa Kaimu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali,
Mheshimiwa Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika,
Mheshimiwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali,
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi,
Mheshimiwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali,
Waheshimiwa viongozi, walimu na wanafunzi wa skuli ya Sunni Madressa,
Waheshimiwa waalikwa nyote, Mabibi na Mabwana,

Assalm Alaykum
Kwanza kabisa sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha sisi sote kuwepo hapa leo katika kusherehekea kuhitimu masomo vijana wetu wa kidato cha nne na kidato cha sita ambao wamemaliza skuli hivi karibuni.

Vile vile natoa shukurani zangu za dhati kwenu nyinyi viongozi wa skuli hii ya Sunni Madressa kwa kuamua kunialika nije kujumuika nanyi katika hafla hii muhimu. Kwangu mimi binafsi naona hii ni heshima kubwa, kwa sababu najua wapo watu wengi ambao wangeweza kuwa wageni rasmi, lakini mukaamua kunialika mimi, nasema ahsanetni sana na ninathamini sana heshima mliyonipa.

Lakini pia nachukua fursa hii kuwapongeza sana vijana wetu mliomaliza kidato cha nne na kidato cha sita, kutokana na uvumilivu wenu mkubwa na kuacha mambo mengine mkajishughulisha zaidi na masomo hadi hii leo mnahitimu. Wapo wengi ambao huishia njiani na kushindwa kuhitimu, hivyo mnastahili pongezi.

Waheshimiwa Viongozi, Walimu wenzangu na Wanafunzi
Skuli hii ya Sunni Madressa ina historia kubwa katika nchi yetu, na imekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu tokea wakati wa ukoloni hadi hivi sasa. Kama ambavyo baadhi yetu tunaelewa wakati wa ukoloni elimu katika skuli za Zanzibar ilikuwa ya namna mbili. Ya kwanza ni ile iliyokuwa ikitolewa na serikali katika skuli zake na ya pili ni ile iliyokuwa ikisomeshwa katika skuli za binafsi, ambazo nyingi kati yake kwa wakati huo zilikuwa na mwelekeo wa kikabila zaidi.

Baada ya Mapinduzi ya Januari 1964, Serikali ilizifunga skuli zote za binafsi na kuzifanya zote kuwa skuli za serikali. Sabubu mbili kubwa ndizo zilizopelekea uamuzi huo ambazo ni;
1. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilitangaza elimu yote katika visiwa vyetu itakuwa bila ya malipo.
2. Elimu hasa katika skuli za binafsi ilikuwa ikitolewa katika misingi ya ubaguzi, ambapo watu wenye vipato vya chini ambao ndio waliokuwa wengi, walishindwa kumudu elimu hiyo, jambo ambalo lilikuwa kinyume na misingi ya serikali hiyo, msingi ambayo ililenga kufuta ubaguzi katika upatikanaji wa huduma zote muhimu, ikiwemo elimu.
Hata hivyo, kwa kuwa mambo hubadilika, baadaye serikali iliamua kurejesha tena skuli binafsi. Hali hiyo ilitokana na mabadiliko makubwa ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na hata kifikra, lakini pia hali ya ongezeko kubwa la idadi ya watu ilichangia kuangaliwa upya utaratibu wa utoaji elimu. Skuli ya Sunni Madressa ilikuwa katika skuli za kwanza kuitumia fursa hiyo hapa Zanzibar mara baada ya utaratibu wa skuli binafsi kurejeshwa tena.

Tangu wakati huo mwaka 1994, skuli nyingi za binafsi zimeanzishwa, kuanzia ngazi ya maandalizi hadi sekondari kwa lengo la kuisaidia serikali kupunguza uzito wa mzigo wa wanafunzi, lakini pia kupanua fursa za ajira kwa wananchi wake.

Naweza kusema lengo hilo kwa kiasi kikubwa limeweza kufikiwa kwa sababu hivi sasa, skuli hizo zina maelefu ya wanafunzi ambao wanapata elimu na baadaye kujiunga na vyuo vikuu tafauti nchini na nje ya nchi. Bila ya skuli kama hizi ingekuwa vigumu skuli za serikali kumudu ongezeko la wanafunzi. Tunaelezwa kwamba katika elimu ya msingi wanafunzi wameongezeka kutoka 214,096 mwaka 2007, hadi 237,690 kufikia mwaka jana, hilo ni ongezeko kubwa.

Aidha, kupitia skuli hizi za watu binafsi wananchi wengi wameweza kupata ajira, kuanzia za ualimu, utawala na nyenginezo, ambazo zinawasaidia kuinua vipato vyao na familia zao. Mafanikio haya katika skuli binafsi bila shaka yanatokana na nia na dhamira ya kweli ya serikali yetu kuziendeleza kwa kuzipa msukumo mkubwa, kwa vile inatambua mchango wake mkubwa katika kukuza elimu nchini mwetu.

Serikali itaendelea na azma hiyo, na kama ambavyo alisisitiza Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein juzi, wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Elimu ya Lazima wa Karne ya 21, pale skuli ya Mwanakwerekwe C, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali itaendelea kuwa karibu zaidi na skuli hizi za watu binafsi na wawekezaji.

Aidha, natoa pongezi zangu za dhati kwa uongozi mzima wa skuli ya Sunni kwa kufanya kazi zenu kwa ufanisi wa hali ya juu. Ushahidi wa hayo ni kwamba mmeweza kupasisha wanafunzi wote wa kidato cha nne kwa miaka 11 mfululizo katika mitihani ya Taifa, ambapo pia matokeo ya kidato cha sita nayo yanaridhisha.

Lakini pia nakupeni pongezi za dhati kabisa kwa kuwa skuli hii ya Sunni Madresaa ni miongoni mwa zile skuli zilizo tufuta machozi mwaka huu, na kutuosha uso katika sakata la matokeo ya mitihani ya kidato cha nne, ambapo skuli nyingi, zikiwemo za Zanzibar zimekumbwa na balaa la wanafunzi kufutiwa matokeo kwa kile kinachoelezwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) kujitokeza vitendo vya udanganyifu.

Kwa kweli suala hili limewafadhaisha sana wanafunzi hao waliofanya mtihani wa kidato cha nne, walimu na wazazi, lakini pia serikali. Pamoja na uongozi wa Baraza la Mitihani Taifa kujaribu kutoa maelezo na ufafanuzi wa kilichotokea hadi wanafunzi hao kufutiwa matokeo kwa wingi, bado inaonekana sehemu kubwa ya jamii ya Wazanzibari haijaridhika na maelezo hayo.
Nashawishika kusema hivyo, kwa sababu mara kwa mara tumekuwa tukiona makongamano na mikutano mingi ya wazazi, wanafunzi na wadau wengine kujadili suala hilo, na baadhi ya wakati washiriki, huwa wakali juu ya jambo hilo. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatambua kuwepo kwa hali hiyo na kwa kweli kuna haja pande zote zijiridhishe na hali iliyotokea hadi kuzua mtafaruki huo, ili isitokee tena.

Hivyo basi imebidi Wizara zetu mbili za elimu ya hapa Zanzibar na Tanzania Bara kukubaliana kufanya uchunguzi wa kina kwa minajili ya kuchimbua sababu halisi za hali hiyo kutambua udhaifu uliopo katika skuli na hata katika Baraza la Mitihani lenyewe. Moja ambalo ni dhahiri ni kuwa adhabu ya kuwafungia wanafunzi waliohusika miaka mitatu bila ya kufanya tena mitihani ni kubwa mno na hivyo Baraza la Mitihani linapaswa kuiangalia tena adhabu hiyo.

Papo hapo nichukue nafasi hii kuwaasa wanafunzi, walimu na wazee kote nchini wajiepushe na tabia ya kutaka kuonesha wanafunzi wao wanapasi kwa njia yoyote ile, iwe halali au haramu. Tunataka vijana wetu wakifaulu wawe wamefaulu kikweli kweli kutokana na uelewa wao, juhudi zao na kwa bidii zao.

Tukiruhusu mtindo wa kutafuta ufaulu kwa njia za mkato basi tutambue athari zake zitakuwa kubwa sana kwa vijana wenyewe na nchi yetu. Tutakuwa hatuna wataalam walioendeleza vipaji vyao na badala yake tutakuwa na wataalamu feki.

Skuli hii ya Sunni Madressa ni mfano wa kuigwa kwani mafanikio yake ni endelevu. Skuli nyengine ziwe za serikali au za binafsi hazina budi kujiuliza kwa nini skuli hii ipate mafanikio. Je wana miujiza?

Kwa maoni yangu skuli hii haina miujiza, isipokuwa kuna mambo ambayo yanaifanya ijichomoze kuwa miongoni mwa skuli bora.
Miongoni mwa mambo hayo ni:-
1. Uongozi bora wa skuli, uongozi uliojiwekea malengo yake wazi, kupanga mikakati ya kuyafikia na kuitekeleza ipasavyo mikakati hiyo.
2. Juhudi na moyo wa kujitolea wa walimu na wafanyakazi wengine wote kwa kuamini kuwa ualimu ni kazi ya wito na hivyo kuitekeleza dhana hiyo.
3. Mashirikiano baina ya uongozi, walimu, wanafunzi na wazee. Mashirikiano huzaa mashauriano na kuondoa misuguano isiyokuwa na sababu.
4. Nidhamu ya uongozi, walimu na wanafunzi wenyewe.
Tukumbuke kuwa, bila ya nidhamu hapana maendeleo wala ufanisi.
5. Kuwepo walimu wenye sifa zinazotakiwa na walimu wenyewe kuwa tayari kujituma.
6. Kuwepo kwa vifaa na vitendea kazi vinavyomuwezesha mwanafunzi, sio tu kupata elimu ya nadharia, bali pia elimu ya vitendo.
7. Uongozi kuwajali walimu, wafanyakazi wengine, wanafunzi na wazazi.
8. Kuweka maslahi ya wanafunzi na wananchi mbele, badala ya kuifanya skuli hii kuwa taasisi ya kitegauchumi.
9.
Hivyo, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali inahitaji kufanya uchambuzi wa kina wa mafanikio ya skuli hii, na kisha kuona vipi mafanikio haya yataweza kumwagikia katika skuli nyengine.

Sasa basi nichukue muda mfupi kuzungumza na wanafunzi. Kwa wanafunzi waliohitimu nawapongeza sana. Mmemenyeka kwa miaka mingi, mkachimba na kuchimbua mkapalilia, kutoa magugu na wakati wa kuvuna mmeona matokeo ya jasho lenu.

Mmekubali kuwa kazi ya mwanafunzi ni kusoma na kujielimisha. Wengi wenu hamkupoteza muda wenu kwa kazi za anasa na starehe. Wakati wa anasa kwenu haujafika. Sasa mmehitimu vizuri, lakini bado hamjafikia mwisho. Kila mmoja anawajibika kujiwekea malengo. Uwe na “ambition”: kuwa Daktari, kuwa Muhandisi, kuwa Rubani kuwa mtaalamu wa “Geology”, kuwa Mwana Diplomaisia wa Kimataifa, na hata kuwa Rais au Makamu wa Rais. Ukishajiwekea shabaha ujipinde kwa mintaaraf ya kufikia shabaha hiyo. Kwa hivyo bado hamjamaliza kazi. Bado mna kibarua kipevu mbele yenu.

Jambo zuri siku hizi kuna mtandao wa Internet, kwa kweli umerahisisha kwa kiasi kikubwa shughuli za kimasomo. Nawaombeni mzidishe juhudi, ili mfikie malengo yenu. Taifa linahitaji wataalamu wa kila fani na baadhi ya wataalamu hao watatoka miongoni mwenu.
Kwa wale wanafunzi mnaondelea na masomo yenu niwaombe mfuate nyayo za wenzenu waliohitimu. Mnajukumu la kusoma kwa juhudi, ili kulinda heshima ya kaka na dada zenu walio watangulia.

Baada ya kusema hayo, sasa nachukua fura hii kutoa nasaha kwa vijana wetu wote wa Zanzibar. Katika risala yenu mmegusia masuala ambayo ni tatizo kubwa katika nchi yetu, hasa kwa vile yanagusa moja kwa moja rika yenu vijana. Matatizo hayo ni utumiaji wa madawa ya kulevya, pamoja na ugonjwa wa ukimwi.

Tukianzia na madawa ya kulevya, vijana lazima mjue kuna vijana wenzenu wengi hivi sasa wamepoteza mwelekeo kwa sababu ya kujiingiza katika matumizi ya madawa ya kulevya. Vijana hao na familia zao wamekata tamaa, kwa sababu watumiaji wa madawa hayo hupoteza nguvu, heshima na uwezo wa kufanya kazi.

Mara nyingi vijana mnaingia katika mtego huu wa matumizi ya madawa hayo kutokana na vishawishi kutoka kwa mrafiki wasio kuwa wema.

Hivyo basi, vijana lazima mujitafutie marafiki wazuri na msiache kupeana nasaha, hasa pale mnapowaona vijana wenzenu wanapotea kwa kujiingiza katika vikundi viovu, vinavyo jihusisha na matumizi ya madawa hayo.

Halikadhilika, hivi sasa dunia yetu imekumbwa na maradhi ya ukimwi, maradhi haya hadi sasa hayana dawa, njia pekee ni kujikinga usiambukizwe virusi vya ukimwi. Na ili umudu kujikinga huna budi kujiepusha na mambo ya kufanya mahusiano ya kimapenzi kabla ya kuoa au kuolewa.

Vijana nyinyi ndio mnaotegemewa na jamii, mnachopaswa kufanya ni kuongeza mkazo katika kusoma, kwani kiwango mlichokwishafikia cha kidato cha nne au sita, na hata wale waliomaliza vyuo vikuu, bado msiridhike na viwango hivyo, hasa kwa kuzingatia kuwa elimu haina mwisho.

Maadili yetu Wazanzibari yanatukataza kujihusisha na vitendo viovu vinavyosababisha kuambukizwa ukimwi, ambapo pia wale wanaotumia madawa ya kulevya ni miongoni mwa watu waliopo katika hatari kubwa ya kuweza kuambukizwa ukimwi.

Aidha, ni jukumu lenu walimu, wazazi na jamii nzima kuendelea kuwanasihi vijana wetu juu ya mambo haya kila mara. Lakini vile vile msiache kuhimiza elimu ya kuhifadhi mazingira, ili kuinusuru nchi yetu na madhara ya uchafuzi na uharibifu wa mazingira.

Napenda kuwashukuru tena walimu, wazazi na wanafunzi kwa juhudi zenu za kuiendeleza skuli hii, hadi kuweza kupata mafanikio haya makubwa, nakuombeni mafanikio haya muyaendeleze, ili skuli hii iwe bora zaidi.

Na mwisho kabisa nakushukuruni nyote mliohudhuria hapa kwa kunisikiliza kwa makini na kuwa watulivu wakati wote nilipokuwa nikizungumza nanyi.
Ahsanteni.

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s