Mradi wa Wanawake wa kupinga ukatili Zanzibar wazinduliwa

Wajumbe wa mkutano wa uzinduzi wa mradi wa wanawake wakimsikiliza Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad katika uzinduzi wa mradi huo huko hoteli ya Ocean View, Kilimani

Vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia ni miongoni mwa matukio mabaya yanayoendelea kujitokeza katika jamii mbali mbali duniani na kusababisha madhara makubwa katika ustawi, maendeleo na uhai wa binaadamu. Matukio ya aina hiyo tunayashuhudia yakiongezeka pamoja na juhudi kubwa zinazochukuliwa katika ngazi za kitaifa na kimataifa kuyakomesha.
HOTUBA YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR, MHE. MAALIM SEIF SHARIF HAMAD KATIKA UZINDUZI WA MRADI WA KUPINGA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE ZANZIBAR HUKO ZANZIBAR OCEAN VIEW RESORT, TAREHE 8 MACHI, 2012
Mheshimiwa Waziri wa Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto,
Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara mbali mbali,
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi,
Mheshimiwa Filiberto Ceriani Sebregondi, Mwakilishi wa Jumuiya ya Ulaya Tanzania,
Viongozi wa Shirika la ActionAid,
Waheshimiwa waalikwa nyote Mabibi na Mabwana,
Asslam Alaykum.
Awali ya yote sina budi kuelekeza shukurani zangu kwa Mwenyezi Mungu kwa kutujaaliya uhai na uzima wa afya na kuweza kukutana hapa leo kuzungumzia mambo muhimu yanayogusa ustawi na maendeleo ya nchi yetu na watu wake.

Lakini vile vile nitowe shukurani zangu za dhati kwa Shirika la ActionAid kwa kuandaa mradi wa kupiga vita ukatili dhidi ya wanawake wa Zanzibar, Aidha niwashukuru kwa kuona haja ya kunialika mimi kuja kujumuika nanyi katika uzinduzi wa mradi huo.
Najisikia faraja sana kuona wenzangu wamenikumbuka na kuamua nije hapa siku leo kusema japo mambo mawili matatu juu ya maudhui ya shughuli yenyewe, ambayo ni kupinga matendo maovu yanayoelekezwa kwa wanawake katika jamii yetu. Nasema kwangu mimi binafsi hii naona ni heshima kubwa mliyonipa.

Waheshimiwa viongozi na waalikwa
ActionAid ni shirika la Kimataifa ambalo limekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya umasikini na kupiga vita vitendo vya uvunjifu wa sheria. Shirika hili ambalo linafanya shughuli zake katika nchi zaidi ya 40, linatoa mchango mkubwa katika kukuza maendeleo ya watu wote Tanzania, ikiwemo Zanzibar na hatua hii ya kuanzisha mradi wa kupinga ukatili dhidi ya wanawake Zanzibar itasaidia sana kulinda haki za jinsia hiyo na jamii nzima ya Wazanzibari.
Lakini vile vile hatua hii ni muhimu katika kusaidia juhudi za serikali yetu hasa katika kazi muhimu inayoendelea ya kupiga vita aina zote za ukatili na udhalilishwaji wanawake na watoto.

Waheshimiwa viongozi na waalikwa
Vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia ni miongoni mwa matukio mabaya yanayoendelea kujitokeza katika jamii mbali mbali duniani na kusababisha madhara makubwa katika ustawi, maendeleo na uhai wa binaadamu. Matukio ya aina hiyo tunayashuhudia yakiongezeka pamoja na juhudi kubwa zinazochukuliwa katika ngazi za kitaifa na kimataifa kuyakomesha.

Kimataifa takwimu zinaonesha mwanamke mmoja kati ya watatu amekumbana na vitendo vya ukatili, iwe wa aina moja au nyengine, hali ambayo inasababisha madhara makubwa, sio tu kwa wanawake waliohusika kufanyiwa vitendo hivyo, bali kwa watoto katika familia ambao hushuhudia vitendo hivyo. Miongoni mwa madhara makubwa yatokanayo na ukatili dhidi ya wanawake ni kukosekana usawa katika jamii, athari za kisaikolojia, kurejesha nyuma maendeleo pamoja na kuchangia kukosekana hali ya amani.

Ukatili wa kijinsia ukiwemo ule unaolengwa wanawake hivi sasa ni suala la haki za kibinaadamu, jumuiya ya kimataifa inalazimika kupitisha maazimio na mikakati mbali mbali kwa nia ya kutokomeza kabisa matendo hayo, miongoni mwa maazimio hayo ni lile na kupiga vita ubaguzi na ukatili dhidi ya wanawake la mwaka 1993, ambalo limeweka bayana vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa aina hiyo.
Aidha, azimio maarufu la Beijing mwaka 1995 ambalo limeweza kutoa mwamko mkubwa kwa mataifa katika vita dhidi ya ukatili kwa wanawake, pia limesaidia sana mataifa mbali mbali kuweka mikakati na malengo ya utekelezaji katika kuinua hali za wanawake, iwe katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii, na vile vile limesaidia kuibua harakati za kuelimisha jamii umuhimu wa kukomeshwa ukatili dhdi ya wanawake na kuondoa vikwazo vinavyorejesha nyuma maendeleo yao.

Tanzania inaunga mkono kwa dhati hatua za kupiga vita aina zote za ukandamizaji, ukatili na ubaguzi wa kijinsia, ikiwemo dhidi ya wanawake na watoto na imetia saini makubaliano na itifaki mbali mbali zinazohusu mambo hiyo na sasa inazitekeleza.
Waheshimiwa viongozi na waalikwa
Hata hivyo, lazima tukiri kwamba pamoja na mataifa, ikiwemo nchi yetu kuchukua hatua tafauti kukomesha ukatili dhidi ya wanawake, bado safari ndefu ipo mbele yetu kwasababau matukio hayo bado yanaendelea kujitokeza kwa wingi. Sababu zinazoelezwa kuchangia ukatili dhidi ya wanawake ni nyingi na zinatafautiana kutokana na mazingira au jamii moja hadi nyengine, miongoni mwa hizo ni mifumo kandamizi ya kimaisha ambayo imeota mizizi katika jamii zetu na kuonekana kama ndio utaratibu wa maisha.
Kutokana na hali hiyo, ili tuweze kuiong’oa mifumo ya aina hiyo na kuleta usawa miongoni mwa jamii pamoja na kukomesha kabisa ukatili dhidi ya wanawake, sote tunahitajika tushiriki katika vita hivi, kuanzia serikali, jumuiya zisizokuwa za kiserikali kama hii ActionAid na nyenginezo, lakini pia jamii nzima.

Waheshimiwa Viongozi na Waalikwa
Kwa masikito makubwa jamii ya Wazanzibari ni miongoni mwa zinazokabiliwa na aibu hii ya ukatili dhidi ya wanawake pamoja na watoto. Tafiti chache zilizofanyika katika baadhi tu ya maeneo zinadhihirisha ukubwa wa tatizo hilo, hali ambayo inatulazimisha tusimame kidete kukabilina na vitendo hivyo, ili wanawake nao waishi kwa amani bila ya bughdha kutoka kwa watu wengine na waweze kuchangia kikamilifu kukuza maisha yao na taifa lao.
Hapa Zanzibar miongoni mwa sababu zinazoelezwa kuchangia vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake ni kuwepo mitazamo potofu juu ya wanawake, ukimya miongoni mwa wanawake wenyewe na jamii inayowazunguuka, kuona aibu na muhali kwa wanawake wanaofanyiwa vitendo hivyo na hivyo kushindwa kuwafikisha wahusika mbele ya sheria.

Matokeo ya hali hiyo ni matukio mengi ya udhalilishwaji wanawake kutoonekana kuwa ni makosa ya jinai, na badala yake jamii inayaona kama ni masuala ya kifamilia na hivyo kuyamaliza nje ya taratibu za kisheria ambapo haki za waliodhulumiwa hazizingatiwi.

Kwa upande mwengine kupungua kwa imani ya wananchi kwamba wanaweza kupata haki katika mifumo rasmi, kama vile Polisi na Mahakama kutokana na hali ya ucheleweshwaji wa kesi, ada za mahakama, gharama za usafiri kufuatilia kesi, pamoja na kuwepo vitendo vya rushwa, ambapo hata wale wanaotiwa hatiani ni wachache, hakuzuwii wahalifu kushawishika kuachana na matendo kama hayo.

Tatizo la ndoa za utotoni, ambapo wazazi huweza hata kuwatoa skuli watoto wao wa kike ili wakaolowe, nalo pia linachangia sehemu kubwa ya kushamiri kwa ukatili dhidi ya wanawake. Tukio moja lililoripotiwa katika siku za hivi karibuni katika visiwa vyetu, ambapo wazazi wamemsusa mtoto wao, kumfichia sare zake za skuli, pamoja na kuyachoma moto madaftari yake kwa sababu amekataa kuolewa linadhihirisha wazi kwamba bado tuna kazi kubwa mbele yetu katika kupiga vita kadhia hii.

Matukio ya wanawake kupigwa na waume zao na mara nyengine hata kujeruhiwa, vile vile yanaripotiwa siku hadi siku ndani ya jamii yetu ya Wazanzibari. Kiasi kwamba wanaume tunaonekana tumesahau hata yale mafunzo mema ya ndoa tunayopewa na watu wazima kwamba ‘Mke hapigwi kwa fimbo wala mateke, bali hupigwa kwa mapambo’. Bila shaka tabia ya kuacha na kudharau maadili yetu mema ina sehemu katika kukithiri kwa ukatili na udhalilishaji wanawake.

Waheshimiwa Viongozi na Waalikwa
Ukatili dhidi ya wanawake wenye ulemavu ni mkubwa zaidi na unaoonesha sura mbaya zaidi ya kutojali utu na ubinaadamu katika jamii zetu. Tabia ya wanawake wenye ulemavu hasa wa akili kubebeshwa ujauzito mara kwa mara na kufanyiwa, kupigwa na kufanyishwa kazi nzito na aina mbali mbali za udhalilishaji unaonesha jinsi jamii isivyowajali wenzetu hao.

Aidha, katika siku za hivi karibuni, kumeripotiwa tukio la mwanamke mmoja ambaye wana familia yake walikuwa na tabia ya kumfunga kamba nyumbani kila anapopata ujauzito katika muda wa miezi yote wa ujauzito, huku akipata mateso makubwa. Tukio hilo linasikitisha sana na hata Waziri wetu mmoja, alipopata taarifa hizo na kufunga safari hadi eneo alipo mwanamke huyo mwenye ulemavu wa akili na kujionea mwenyewe hali halisi hakuweza kujizuia na alitokwa na machozi.

Waheshimiwa Viongozi na Waalikwa
Sasa baada ya kugusia mifano michache inayodhihirisha ukubwa wa tatizo la ukatili dhidi ya wanawakehapa nchini, napenda kulishauri shirika la Actionaid, pamoja na taasisi nyengine katika mapambano dhidi ya ukatili dhidi ya wanawake kuzingatia mambo haya mawili matatu katika utekelezaji wa majukumu yao;
Wanaume washirikishwe kikamilifu
Baadhi ya miradi na mikakati kama hii ya inayolenga kuwakomboa wanawake siku za nyuma iliwatenga wanaume, kiasi kwamba baadhi ya wanaume hao kuanza kuielewa na kuitangaza vibaya na hivyo kupata upinzani mkubwa katika utekelezaji wake.
Mkiwashirikisha wanaume kikamilifu wataona hili ni jambo lao na watahisi wanahusika moja kwa moja katika kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na hivyo watakuwa mstari wa mbele kukomesha maovu hayo.

Mkazo mkubwa uwekwe kuwasaidia waliofanyiwa ukatili
Itakuwa jambo jema iwapo mradi huu utakuwa na utaratibu wa kuwasaidia hata kwa mawazo wale walioathiwa na vitendo vya ukatili mbinu za kujikwamua kimaisha, ili waweze kukabilina na hali ngumu wanayopambana nayo. Uzoefu unaonesha pale wanawake wanapopatiwa nyenzo na kushirikishwa kikamilifu hupata mafanikio makubwa katika kujikwamua na hali ngumu za kimaisha. Mafanikio ya wanawake katika vikundi vya ushirika vinavyowezeshwa kupitia Wizara ya Uwezeshaji Wananchi pamoja na mradi wa Kuwawezesha Wanawake Zanzibar uitwao WEZA unaoendeshwa na Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA), umewasaidia wanawake katika baadhi ya mikoa Zanzibar kupiga hatua kubwa. Nimeeelezwa kuwa ActionAid linamchango wake katika miradi hiyo, nawapa hongera nyingi.

Misaada hiyo pia ilenge kuwasaidia wanawake hao kuweza kuona umuhimu wa kuzitumia taasisi za kisheria, kama vile Polisi na Mahakama, ambazo zina nafasi kubwa katika kusaidia kukomesha matendo ya ukatili na udhalilishaji.
Elimu kwa umma ipewe kipaumbele
Nimeelezwa kwamba elimu juu ya kupiga vita vitendo vya ukatili ndio kipaumbele katika mradi huu, lakini kama nilivyogusia hapo awali, baadhi ya sababu za kujitokeza kwa matukio haya ya ukatili dhidi ya wanawake zinagusa desturi zetu na zimeota mizizi katika mfumo wa maisha yetu, baadhi ya watu wanasema umetawalia na mifumo dume, ni dhahiri elimu ya kina inahitajika, ili kujua mambo gani yanafaa na yepi hayastahiki katika jamii zetu Zanzibar.

Mradi uwasaidie sana wanawake wenye ulemavu
Wanawake wenye ulemavu wanakabiliwa na matatizo makubwa zaidi, mbali na kufanyiwa ukatili tulioutaja, ni miongoni mwa wanajamii wenzetu, tatizo la umasikini uliokithiri kutokana na kukosa nyenzo na kutengwa katika mambo ya kimaendeleo pia ni tatizo jengine kwao. Wenzetu hawa lazima tuwe nao bega kwa bega katika miradi kama hii na tuwawezeshe kuondokana na kudhalilika katika jamii zetu.
Waheshimiwa viongozi na waalikwa
Kwa upande wake serikali itaendelea kuchukua hatua mbali mbali kukomesha aina zote za ukatili dhidi ya Wanawake pamoja na watoto wetu, kwa kuweka sheria mpya na kuzirekebisha zile ambazo zitaonekana hazikidhi haja kutokana na wakati uliopo, pamoja na kuwapa nguvu kubwa wanawake katika masuala ya kiuchumi na kimaendeleo, ikiwa ni pamoja na kuzipa msukumo wa kipekee jumuiya na taasisi zisizokuwa za kiserikali zinazojitokeza kukomesha matendo maovu dhidi ya wanawake na watoto na kujenga mazingira ya kukuza maendeleo yao.
Miongoni mwa hatua ambazo serikali ya Mapinduzi Zanzibar inazipa kipaumbele hivi sasa ni uanzishwaji wa Benki ya Wanawake, hatua hiyo inachukuliwa kupitia Wizara ya ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Wanawake na Watoto, ili wanawake wawe na sehemu ya kuwajengea uwezo na kuwapa nyenzo katika shughuli zao za kiuchumi na maendeleo yao kwa ujumla.
Baada ya kusema hayo niruhusuni tena nitoe shukurani zangu kwenu nyote kwa kunisikiliza na kuwa watulivu katika muda wote wa hotuba yangu. Na sasa natamka rasmi kwamba, MRADI WA KUPINGA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE ZANZIBAR, umezinduliwa rasmi.

Ahsanteni.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s