Watoto wa Kizanzibari muhimu walindwe

Baadhi ya wanafunzi wa skuli za Zanzibar wakiwa nje ya skuli yao wakifanya masomo ya vitendo

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar inayoendeshwa kwa mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) imepiga hatua katika kukomesha ufisadi na kulinda na kumhifadhi mtoto. Kwa mara kwanza katika miaka 20 hivi, SUK imefanikiwa kutunga sheria ya kupambana na ufisadi, au rushwa; iliyokuwa imekwama kwa sababu watawala hawakujiamini kuipitisha. Nitaijadili sheria hii wakati muafaka, baada ya kwanza kujadili tatizo linalokua la kudhalilisha na kunyanyasa watoto.

Rais Dk. Ali Mohamed Shein amesaini Sheria Na. 6 ya mwaka 2011 baada ya kupitishwa na Baraza la Wawakilishi katikati ya mwaka uliopita.

Kujua ukubwa wa tatizo la unyanyasaji watoto, fuata mtiririko huu: Katika kitongoji cha Kwarara, jimbo la Fuoni, Wilaya ya Magharibi, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, kuna mtu anajivuna kwa kuharibu watoto.

Mara mbili amebainika. Katika tukio la pili, alipelekwa mahakamani baada ya wasimamizi wa Masjid Taalim, Kwarara kulivalia njuga tukio hilo .

Hata hivyo, mahakama ya wilaya ya Mwera iliitupa kesi na kumwachia mtuhumiwa kwa kukosekana ushahidi. Silaumu hilo maana mahakama humshika mtuhumiwa penye ushahidi makini kwani ni chombo kinachosimamia utoaji wa haki.

Ushahidi wa shitaka lolote liliopo mbele ya mahakama, lazima utolewe kisheria na ni pale tu utakapoiridhisha mahakama pasina chembe ya shaka, ndipo mtuhumiwa hutiwa hatiani.

Huo ndio mtizamo wa kisheria. Ushahidi dhaifu hauwezi kuzingatiwa na hakimu yeyote mwenye maadili; na hivyo mtuhumiwa ataachiwa.

Mtuhumiwa huachiwa huru na mahakama kwa kuwa hakubanwa vilivyo na ushahidi uliowasilishwa wakati wa kesi kusikilizwa, lakini haina maana kuwa hakutenda alichotuhumiwa.

Mfano wa ukweli huu, ni huyu muovu wa Fuoni. Ni mwanamume maarufu kwa kuhujumu watoto wa kike, lakini hajapata kutiwa hatiani. Ni ushahidi tu wa kisheria unakosekana. Hili ni jambo la kiufundi.

Moja ya udhaifu ni kuupoteza ushahidi mara tu tukio ovu linapotendeka. Unapoosha mbegu za uzazi zilizokutwa kwa mtoto, unapoteza ushahidi.

Ameshaharibu watoto wengi, inavyosemwa. Anatumia usomi wake wa ilmu ya dini na fedha kulaghai familia za watoto anaowaharibu. Anatumia nguvu hizo hata kwa mamlaka ili kukwepa mkono wa sheria.

Wakati wanaharakati wa Masjid Taalim walipoamua kufuatilia mpaka mwisho tukio la pili, kama jitihada zao za kukomesha unyanyasaji, kitangi huyo alikuwa anatamba hakuna mtu atakayemtia jela.

“Mimi ninafahamika… mpaka hao wakubwa wenu wananijua. Nina pesa na pesa ndio zinawatia kiwewe viongozi wa serikali yenu. Hawathubutu ng’o kunifunga,” akitamba.

Vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti matukio mengi ya uharibifu wa watoto visiwani Zanzibar yakihusisha watu wa umri wa zaidi ya miaka 30 kuendelea wakiwemo walimu wa madrasa.

Walimu wa madrasa wanaaminiwa sana katika jamii ya Kiislamu kama wanavyoaminiwa wenzao wanaofundisha watoto wa Kikristo. Wanaheshimiwa hasa.

Utamaduni huo unawalemaza wale wachache wanaoamua kuiga hulka za kinyama. Wanajenga kiburi na kujifanya hamnazo. Wanakula matunda wasiyoruhusiwa yakiwemo waliyokabidhiwa na wazazi kuyajenga kiimani.

Inapotokea wamekula matunda kinguvu, baadhi ya wazazi huwa wazito kuachia mkono wa sheria ufanye kazi ili kuwadhibiti waovu hawa. Uzoefu unaonesha huthubutu hata kupokea fedha kuzima kesi.

Vitangi walikuwepo Zanzibar miaka ya 1980 mpaka 1990. Hawakukoma. Inawezekana wamekuwa wakiendelea na hujuma hii kwa siri kubwa. Watoto wangapi wameathirika.

Serikali imeamua kukazia sheria ya kumlinda mtoto. Sheria Na. 6 ya mwaka 2011 ilisainiwa na Rais Dk. Ali Mohamed Shein katikati ya mwaka uliopita.

Ni sheria iliyokuja baada ya huzuni, vilio na malalamiko mengi ya umma. Matukio mengi yametokea na kuthibitisha kiwango cha ukatili wa binadamu dhidi ya watoto kilivyoongezeka.

Kwa hapa, serikali inastahiki heshima. Imesikiliza vilio. Imeona ukubwa wa tatizo ikaleta sheria ya kulinda mtoto wa Kizanzibari dhidi ya ukatili.

Isitoshe, imeanzisha kituo ndani ya Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, mjini Zanzibar, cha kushughulikia kwa haraka kesi zinazoripotiwa kabla ya kufikishwa mahakamani.
Kituo hicho kiitwacho Mkono kwa Mkono, kinajumuisha maofisa wa idara muhimu kama vile Polisi, wanasheria na madaktari. Hata polisi kwenyewe, sasa kuna dawati maalum kuhusu kesi hizi.
Ni hatua inayolenga kudhibiti ushahidi uliojijenga pale tukio lilipotendwa dhidi ya mtoto. Itaharakisha uchunguzi na upelekaji mashitaka mahakamani ili kudhibiti waovu.
Sheria inamlinda mtoto wa chini ya miaka 18 dhidi ya kufanyishwa kazi za kumvunja nguvu, kuonyeshwa picha za kumkuza mapema na kumkinga na kutumiwa kibiashara kufanywa mtumwa kikazi, kingono na kutolewa viungo vyake.
Vipengele vinataka mtoto asilazimishwe kupimwa ukimwi, lakini kinachotia moyo zaidi ni kuanzishwa kwa Mahakama ya Watoto itakayowezesha kesi za watoto kusikilizwa katika mazingira mahsusi badala ya hadharani kama ilivyokuwa.
Mahakama maalum itawezesha kesi hizi kusikilizwa haraka na zikamalizika.
Sheria inaainisha haki mbalimbali za mtoto akiwa ulezini, iwe kwa wazazi wake au walezi. Haki hizi, ukiacha zile za msingi kama kuishi, kula na kupata elimu, ni pamoja na kupewa jina (zuri), kuwa na uraia, kutobaguliwa.
Nyingine ni kushiriki katika harakati za makuzi yake kwa mujibu wa umri na watu wa rika lake, kusikilizwa maoni yake, kuujua utamaduni wake na kushiriki kuuenzi, kushiriki michezo.
Kipo kifungu kinachomlinda mtoto anayeishi na ulemavu. Kinazuia mtu yeyote kumdharau au kumnyanyasa mtoto huyu mlemavu wa chochote kati ya viungo, akili, ngozi. Hali yake hiyo haitamzuia kupata elimu.
Kifungu kingine kinataka mtu au ofisa anayeshughulikia ustawi wa watoto, kama vile mwalimu, daktari, mwanasheria, kuripoti haraka anapokutana na kesi yoyote ya unyanyasaji mtoto husika. Ina maana asipotoa taarifa, aweza kuwa mkosa.
Taarifa itatolewa kwa mkurugenzi wa ustawi wa jamii au maafisa walio chini yake, polisi, au Sheha ambao mmoja wapo, ataanza kuchukua hatua za kukabiliana na tatizo linaloripotiwa.
Sheria inazuia uchapishaji au utangazaji wa tukio hilo, bila ya amri ya mahakama. Zipo adhabu za mkosaji.
Katika hali kama hii, sasa haitaeleweka kukuta kesi za unyanyasaji watoto zinamalizwa kwenye vituo vya polisi au kwa maelewano katika familia.
Kila mtu atambue kuwa wakati familia zinatafuta maelewano nje ya mkondo wa sheria, machungu yanabaki kwa mtoto aliyedhulumiwa. Wataalamu wa saikolojia wanasema huchukua mpaka miaka 15 kabla ya machungu haya kukoma.
Bado suala zima la kulinda watoto linahitaji elimu kwa umma. Ni wajibu wa vyombo vya habari kutoa mchango huu. Lakini taasisi husika za serikali na za kiraia, zapaswa kuwa mbele katika kufanikisha elimu kwa umma.

Advertisements

3 responses to “Watoto wa Kizanzibari muhimu walindwe

  • ASALAM ALAYKUM!

   Kweli GNU inastahiki kupongezwa.

   Huyu jama wa Kwarara siamini hayo anayoyafanya na siamini hao wanaomshatki kuwafanyia kiburi. Ikiwa Msikiti una waumini 100 ingebidi badaa ya sala ya aubuhi kumwndea kwake na kumuamsha na kumtandika kwa mikwaju sawasa kisha wakawa tayari lolote lile litalotokea kukabiliana nalo, tukaona nani wakuwekwa nadani?

   Jamaa huko bara alikwenda kwenye gazeti la Annur kutaka msada kua Quraan inadhalilishwa huko kwa na wakiristo kafika hapo kwa kutaka msada mmoja alimjibu uletwe mkwaju atandikwe kwanza, kwani wao huko wamefanya nini? Uislamu kwani upo DaresSalaam tu? Waumini wa Masjid Taalim bado hawajakua na mkakati, huyu jmaa atawataabisha sana, lazima afanyiwe Uhhuni kama anavyowafanyia wakaazi wa Kwarara, ataendelea na atendelea ikiwa unatafutwa Ushahidi. Suala lake likaekewa Shura ya Ma-Imam ikatafutwa Fatwa atafahamu kua watu wameamua.

   Ben Rijal

 1. Hili suala ni la kweli
  Huyu jamaa ilikuwa wakutane vijana barabara na wazee wa hapo wamwendeee wamtandike bakora hadharani , then na nyumba yake waichome moto wahakikishe anahama hapo mtaani
  Kesi baadae

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s