Viongozi Zanzibar wacheni ubaguzi

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Dk Mwinyihaji Makame Mwadini akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za wizara ya Fedha na Uchumi ambapo alionesha ubaguzi wa waziwazi kwa waandishi wa habari wa BBC, Ally Saleh na Salma Said wa DW waliokaa viti vya mbele wakati akijibu masuala ya waandishi hao aliyoulizwa katika mkutano huo,

Leo nataka nizungumzie kuhusu suala la ubaguzi ambalo limekuwa tatizo sugu
hapa Zanzibar na zaidi ubaguzi huo ni ule wa kumtizama mtu kwa dhana za
kisiasa, jambo ambalo linaviza maendeleo ya visiwa hivi.

Tokea mabadiliko makubwa ya kisiasa ya 1964 kufuatia Mapinduzi nimekuwa
nikisema mara nyingi Zanzibar kama nchi ilishindwa kuandaa mikakaati ambayo
ingesaidia kuondosha tatizo la chuki za kisiasa zilizojengeka kabla ya
Mapinduzi hayo.

Chuki za Zanzibar Nationalist Party ZNP, Zanzibar and Pemba Peoples Party
ZPPP kwa upande mmoja na upande mwengine ikiwa ni chama cha ASP, nja ambazo
zilifikia kilele pale vyama hivyo vilipouungana na kuchanganya kura zao na
kwa hivyo kuchukua Serikali ya kwanza ya Uhuru hapo 1963.

Ubaya ni kuwa chuki hizo zimeachwa zikuwe na zimee, pengine wengine
wamekuwa wakifaidika nazo na ndipo pia zikajitokeza wakati siasa za vyama
vingi 1992 ziliporudi na kuzagaa kwa hatari sana hata katika kizazi kipya
ambacho hakikuwa kikijua ZNP, ZPPP wala Afro Shirazi zaidi ya ngano
walizokuwa wakisikia.

Chuki hizo zilipelekea maovu mengi kutokea katika jamii na familia
kutengana. Mizizi yake iliingia katika uendeshaji wa Serikali ambapo mtu
yoyote ambaye angedhaniwa asie wa chama kilicho madaraka imemuia vigumu
kupata ajira au kupata cheo.

Baada ya muda mrefu na jamii na nchi kutanabahi kuwa tumekuwa tukienda
kusiko na hilo si jambo la tija kwetu, viongozi wawili wakuu wa vyama
kinzani, Dk Amani Karume na Maalim Seif Shariff ambavyo kwa sababu zisizo
za msingi vilikuwa vikiendelea kuhusisha na siasa za kabla Mapinduzi
vilipoamua kuwa imechosha na imetosha.

Wakasema chuki na ubaguzi iwe basi. Wakasema ni hatari kwa maslahi na
mustakbali wa nchi ambapo athari yake ilionekana pia katika kila msimu wa
uchaguzi kwa kukosekana mshindi aliyepata imani ya nchi na kwa hivyo kuwa
vigumu kushika hatamu za uongozi.

Wakachoka kuonekana kila siku kuna magomvi katika nchi na kuona nchi
inaendelea kugawika nusu kwa nusu na kuwa wanaofaidi fursa za nchi ni
upande mmoja tu wa siasa na mwengine ukiula huu, chembilecho msemo maarufu
wa Mombasa hapo zamani.

Lakini wiki tatu nyuma nilibahatika kuwasilisha makala katika semina ya
REDET ambapo nilitakiwa nitizame suala la ushirikishi tokea kuundwa kwa
Serikaliya Umoja wa Kitaifa (SUK) , ambayo moja ya jukumu lake lilikuwa au
lingekuwa kujaribu kumaliza suala la ubaguzi ndani ya jamii kutokana na
siasa.

Ilikuwa ni fikra yangu kuwa hapana juhudi maalum iliyochokuliwa kuhakikisha
chuki kama hizo zinazikwa na ndio maana hakuna kikubwa kilichobadilika kwa
sababu ushiriki wa kujenga nchi bado una masharti na unalalia upande mmoja
na hilo linaiweka SUK njia panda.

Katika mkutano huo ilitokana kauli ambayo mpaka leo inanitetemesha pale
nilipotoa hoja ya kukata mizizi ya ubaguzi kwa kuondosha kipingamizi cha
Wazanzibari wasio na asili ya Kiafrika kuweza kujiunga na vikosi vya ulinzi
kama watapenda, lakini kauliya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Mustafa Muhammd
kusema, “ Haiwezekani kwa bunduki na risasi kupewa kwa mpinzani.”

Ilibidi nifungue darasa kuelezea tofauti ya mpinzani na raia. Kwamba raia
wote katika nchi wanatakiwa wawe na haki sawa bila ya kujali asili zao, na
nikatoa mfano wa Marekani ambapo hata raia wenye asili Iran wana haki
kamili ya kuingia jeshini.

Kumbe kauli ya kiongozi huyo bado inaashiria kuwa hali haijabadilika ndani
ya jamii na kuwa bado chuki za kisiasa zipo na mara hii zikijitokeza
kupitia kiongozi ambaye ni Waziri tena katika Ofisi ya Rais, Dk. Mwinyihaji
Makame.

Katika sehemu kubwa mno ya maisha yangu nimekuwa nikibaguliwa hapa
Zanzibar. Nimefukuzwa kazi, nimezuiliwa kuingia sehemu kadhaa, nimetishiwa
maisha hadharani hata mbele ya Rais Mkapa, nimebandikwa majina mengi,
lakini hili alilonifanyia Waziri Dk Mwinyihaji nimeshindwa kulistahamilia
kwa sababu nilikuwa najaribu kujenga imani kwamba ubaguzi unaondoka, ingawa
najua bado upo.

Nilisikitishwa kauli ya ubaguzi kutoka kwa Waziri ambaye ni msaidizi muhimu
wa Rais na bila kisisi, aibu wala majuto yoyote akatoa kauli kama jambo la
kawaida tu, kitendo ambacho kimedhihirisha labda pengine yeye si muumini
mzuri wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo msingi wake mmoja ni kuondosha
ubaguzi wa kisiasa.

Tulikuwa katika mkutano wa waandishi wa habari ambapo Dk. Mwinyihaji
alikuwa akikaimu nafasi ya Waziri wa Fedha na kuitishwa kueleza hali ya
nishati ndani ya nchi ambapo kulikuwa na uhaba mkubwa wa petroli.

Nilimbana Waziri katika hoja mbili. Kwanza kitendo cha Serikali kukaa wiki
mbili bila taarifa ya si uhaba bali ukosefu wa nishati hiyo na nikasema
hilo haliwezi kukubalika. Pili nilijaribu kujenga hoja kuwa uchumi wa nchi
ulisimama nikimtaka Waziri atoe takwimu Serikali imekosa mapato kiasi gani
na uchumi umeathirika kiasi gani nikitaka takwimu.

Kwa kiasi kikubwa mkutano huo ulikuwa mkali na mimi na mwandishi Salma Said
tukawa hatumpi Waziri nafasi ya kuvuta pumzi, na kwa kiasi aliona huo ni
utovu wa nidhamu kwa kuwa pengine amezoea mikutano ya waandishi wa habari
ambapo anasema mpaka anakwisha bila ya kukatishwa au kutupiwa suala la
kumkinza. Katika hili nafikiri anapaswa kupata mafunzo upya.

Basi Waziri hakuweza kuchukua na usthamilivu ukamshinda na hapo akajivua
gamba na kujionyesha rangi zake halisi, Ah…utanambia nini bwana…nyie
kama baba mmoja mama mmoja mna yenu mengine twambieni….sio haya bwana. Sote
Wazanzibari bwana msitudanganye bwana…Wewe Buto (albarto yaani ally
saleh) nakufahamu toka uko wapi mpaka leo…na huyu (mwandishi salma said)
nakufahamu toka zamani mpaka leo”Sote Wazanzibari bwana msitudanganye. Wewe
Albarto nakufahamu toka uko wapi huko mpaka leo…na wewe Salma nakujua
uzuri…”

Kwa hakika nilimuonea huruma sana Waziri Dk. Mwinyihaji kwa kuwa mpaka leo
ana fikra kuwatizama watu kwa kuamini anawatia kwenye dema la kisiasa. Kwa
wageni wa siasa za Zanzibar alichokusudia kusema Dk Mwinyihaji kuwa anatua
kwamba mimi na mwenzangu anatuhusisha na chama cha CUF na kwa hivyo ni
wapinzani hata sasa ambapo CUF imo ndani ya Serikali.

Upande mwengine niliumia kuona kuwa bado kunaweza kuwa na mawazo kama hayo
miongoni mwa watu ambao Dk. Ali Muhammed Shein amewapa vyeo vya uwaziri na
unajiuliza kwa mtizamo huu nchi inakwenda wapi na kweli ubaguzi nchi hii
utaondoka?

Wiki chache nyuma niliandika makala katika safu hii ya kuwataka Watanzania
waache kulalamika na wachukue hatua kadri watavyoweza na mimi nikafanya
hivyo kwa kuamini kiasi changu kilitosha lakini muhimu zaidi ni kufikisha
ujumbe.

Nilitangaza kususia shughuli za Serikali ya Zanzibar kwa wiki moja na mgomo
wangu unaisha leo nikiamini roho yangu imekuwa safi ijapo mgomo wangu
haukuitikisa Serikali lakini angalau na mimi nimesimama kupinga ubaguzi
ambao nimefanyiwa sana lakini sitokubali kuustahamilia tena.

Ningependa pia kutoa wito kwa Wazanzibari wenzangu kukataa kubaguliwa na
kuwapinga akina Dk Mwinyihaji wengine iwe ni mawaziri, watendaji au hata
Wazanzibari wenzao wa kawaida. Kwamba ubaguzi hauna nafasi tena na kuwa
Zanzibar bila ya ubaguzi inawezekana, uwe ndio wito wetu kwa kila ngazi.

Advertisements

16 responses to “Viongozi Zanzibar wacheni ubaguzi

 1. mm nilishangaa baada ya ccm moja alipo niambia RAISI HATOKI PEMBA HASA IKIWA NI CCM yaani nilimshangaa na nikahisi hata chama chao hawakiamini maana sababu aliyo itowa anasema mpemba akiwa raisi hasa wa ccm huwa tamaa sana na atauza nchi kirahisi MM NILIMUULIZA KWANI NCHI HII TANGU MAPINDUZI KUNA MPEMBA ALIE ONGOZA AKAJIBU HAKUNA NIKAMUULIZA KWA NINI NCHI IKAFIKA HAPA NDANI YA MUUNGANO AKAKOSA JIBU MM NIKAMUAMBIA KAMA KUIZAMISHA NA KUIJINI NCHI BASI NI WAZANZIBAR WOTE MHUHINDI MUARABU MSHIRAZI MUAFRIKA SABABU WATU WAKE MASLAHI MBELE UBAGUZI
  KUHUSU HUYU WAZIRI HAJIJUWI HAJITAMBUWI YAANI ZANZIBAR LAZIMA IWEKE MAWAZIRI WALAU WENYE DIGREE NA WAWAKILISHI WALAU WENYE DEGREE MAANA MTU INAFANYIKA MIUJIZA MPAKA ANAKUWA WAZIRII SASA IMEFIKA WAKATI TUBADILIKE KUHUSU WATU WENYE ASILI YA KIARABU BASI HAPATI JESHI AU POLISI BASI AKIPATA UJUWE MWANA MAPINDUZI KAMSAIDIA SANA HUU NI UBAGUZI WA WAZI NA UNAPANDIKIZWA NA WATANGANYIKA NA UKABEBWA NA WAZANZIBAR WACHACHEEE

 2. “Ali Saleh na Salma Said tunakujueni tokea zamani” Hivi haya matamshi ni ya kibaguzi? Nadhani maneno haya yanahitaji mbaguzi ili ayaite ni ya kibaguzi.
  Tatizo waandishi walikosa subira, ueledi, dharau na heshima wakayapa kipa umbele hisia zao za kisiasa mbele.
  Tunawajua akina Aly Saleh na wenzake wanavyocheza na ajenda yao ya siri kutaka kufifirisha ukweli wakitumia mwanya wa SUK.

  Nd. yangu Aly Saleh, yametokea mambo mazito sana Zanzibar kama kuzama kwa meli, kukataza kuagiza bidhaa za eleetroniks na magari yaliotumika, je wewe ulipata kwenda kuwahoji wahusika wakuu kuhusu kadhia hizo? Si kwa sababu Mawaziri waliohusika ni kutoka chama cha CUF? TUNAKUJUENI VIZURI na hatutachoka kukwambieni mpaka pale mtakachoacha ubaguzi wenu.

 3. Kwa Taarifa yako. Dr. Mwinyi Makame ni msomi wa hali ya juu. Ana degree ya falsafa kwenye fani ya Kilimo na naamini zaidi yako.

  Usiandike kitu usiokijua. Rais Jumbe alikuwa tayari kutaka kututoa kwenye makucha ya kutawaliwa na Tanganyika, lakini ni MPemba Maalim Seif alierubuniwa na kupenda ulwa akamuangamiza Jumbe. Tunajua na hatujasahau, Mwanasheria Mkuu aliemungoza Jumbe akatimuliwa kazi na akina Seif Sharif. Dourado aliwekwa ndani kwa siku mia bila kushtakiwa. Maalim Sief akamwita Dourado haini kwa vile alitaka kuvunja muungano. Maalim Seif huyohuyo akasimama kidete kuunganisha usalama wa taifa kuwa wa muungano.
  Tumenyamaza lakini hatujasahau

 4. Aslam aleikum,
  Unajua kunawatu nao wanataku kujulikana kama wapo yale maneno ya Dr, Mwinyi ni yakibaguzi waziwazi kama wewe hujui kiswahili sema ufundishwe. Wewe Ally Saleh na Salama Said nawajua tangu zamani nini? ni nini maana yake? au yeye kakasirika kwa kubanwa na maswali.
  Hiyo ndiyo kazi ya waandishi wa habari wao ndio wanau fikisha ujumbe wetu kwa wakubwa mimi siwazi nikamuliza Dr, Mwinyi lakini muandishi huwa rahisi kumuliza na kila mtu anasikia au kashindwa kujibu utumbo wake anao ufanya. Ni lazima wa banwe nchi wanaipeleka sipo kama nyinyi mutakasirika kazi kwenu.

  Ni digree gani alinyo nayo au kilamtu dio prof ? hata halikuniki anaitwea prof je ana digree gani? wacheni kuwatetea wauza nchi tusha choka nao.

 5. Huo ubaguzi watu wengi hufikiri ni kwa mtu mweusi kwa mweupe lakini kwa kweli ubaguzi kwetu ni mkubwa mno hata kuliko Ulaya.Kuna ushahidi wa kutosha wa Waziri ndani ya SUK aliefika kutamka kuwa nafasi za masomo mambo ya mafuta hawatopewa wapemba na watu wa rangi.Jee na hou tuuite nini kama si ubaguzi wa wazi???

 6. Huyo ali saleh ameona hilo tu? amesahau jinsi gani wasiowaislamu wanavyobaguliwa waziwazi na kuitwa makafiri hata kama ni mzaliwa wa zanzibar? au yeye ameona ubaguzi ni kwenye ukafu na sisiemu tu. As long wazanzibari bado wanayo damu hiyo ya kibaguzi hawatakaa salama asilan mpaka siku ya kiama.

 7. oya uyo fala anaemtetea kiongozi mbaguzi na yeye ni mbaguzi..kwanza ungeimaliza hiyo comment halafu ndo ukaichanganua Ah…utanambia nini bwana…nyie
  kama baba mmoja mama mmoja mna yenu mengine twambieni….sio haya bwana. Sote
  Wazanzibari bwana msitudanganye bwana…Wewe Buto (albarto yaani ally
  saleh) nakufahamu toka uko wapi mpaka leo…na huyu (mwandishi salma said)
  nakufahamu toka zamani mpaka leo”Sote Wazanzibari bwana msitudanganye. Wewe
  Albarto nakufahamu toka uko wapi huko mpaka leo…na wewe Salma nakujua
  uzuri…”umesoma iyo part aliposema “nyie kama baba mmoja mama mmoja mna yenu twambieni” sasa wana yao vipi ebu tufahamishe kabla hujamtetea babako ..tatizo jamaa hawezi kazi ni mzembe amezoea zanzibar ya kizamani kwamba viongozi hawawajibiki na hakuna wa kuwauliza maswali kuhusiana na wajibu wao ..alishindwa kujibu suala akatumia ujanja wa kumuattack mwandishi wa habari kubabaisha mada husika.

 8. Ahsanteni kw amaoni yenu nyote lakini jambo la msingi na la kusisitiza tukatae ubaguzi kwa hali yeyote ile maana mtu asitete leo kwa sababu yupo madarakani au aliyefanya kitendo hicho ni bosi wake au ni jamaa yake ajue kwamba uongozi ni wajibu kwa jamii na ni wajibu kwa Mwenyeenzi Mungu leo unaweza kuwa kiongozi na kesho ukaondoshwa katika uongozi lakini jengine leo unaunga mkono aliyefanya ubaguzi unasahau kwamba leo amefanyiwa Salma Said na Ally Saleh lakini kesho atafanyiwa ubaguzi mwanao au ndugu yako jee utafurahia hilo? kwa hivyo lazima tuwe makini katika kukataa ubaguzi na kuiweka jamii yetu iwe yenye kuheshimu haki za binaadamu na kuacha ubaguzi, Ndugu Mkombe kama sio ubaguzi ni nini huo? Ndugu A.O Said ni kweli ubaguzi upo mpaka leo lakini ndio kazi tunayoifanya kuondosha huo ubaguzi, Ahsante Chris kwa ufafanuzi wako nakushukuru sana, Ndugu Kim usidhani mwandishi anakuwa anajua kila kitu ufahamu na yeye ni binaadamu ikiwa hajapata ushahidi hawezi kuandika chochote lakini pale mtu anapokuw ana taarifa kamili na ushahidi anaweza kuandika lakini sio kama unavyofikiria tu na kulaumu tu, mbona watu wameshaandika sana habari kama hizo lakini kwa jamii yetu hatuwezi kusema waislamu wanabaguliwa tunasema watu wanabaguliwa maana tunajijua hapa zanzibar asilimia kubwa ni waislamu na wanaobaguana ni hao hao waislamu wenyewe kwa wenyewe kwa hivyo kinachotakiwa kuondoshwa na ubaguzi wa hali zote, Ndugu Ali Majid ahsante kwa maoni yako na wengine nyote ahsanteni, Ndugu Wail jibu ni nadhani utalipata kwa uliyemuuliza suali

 9. Ndugu Ali Saleh mada yako ni nzuri sana, na mimi ninakuelewa wewe vizuri sana lakini ilikuwa siamini kwamba huelewi kama nchi hii ni ya kibaguzi mpaka mpaka leo ndio umeelewa
  Tena kwa taarifa yako si rahisi kuendelea kwa sababu ubaguzi na ubinafsi umewajaa hasa viongozi wa nchi hii
  Katika nchi hii ukiwa Mzanzibari utabaguliwa kuna Wazanzibara , ukiwa mpemba utabaguliwa kuna Waunguja , ukiwa Cuf utabaguliwa kuna Ccm , hapo ukiwa una kirangirangi ndio hufai katika nchi hii si kwenu hapa , kwenu arabuni wakati hata babu yako huko arabuni hakujuwi
  Hiyo ndiyo hali halisi, lakini kwa kweli Mzanzibari halisi tena awe mwislamu hambaguwi mwananchi mwenzake hata kama ana asili ya bara au ni muasia
  Yeyote tena narejea yeyote yule ukimuona ubaguzi kauweka mbele basi ana walakin
  Itakuwa ana uwalakin labda anafoss kuwa ni mzanzibari, au elimu aliyonayo ni ndogo ukilinganisha na cheo alichonacho serikalini, au ana nafasi ya wizi hapo alipo , au pengine ni mwanamme mushkel
  Lakini muungwana hasa aliyetimia hawezi akambagua mwenzake
  Wazanzibari sote hapa ni kwetu, mbora wetu ni yule nchi inayomuuma zaidi kuliko mwengine

 10. assalam alaykum
  Mimi nina wasia mmoja muhimu kwa dada yangu Salma. Muandishi siku zote hatakiwi kuonyesha hisia zake za kisiasa hadharani au kuonyesha kutoa favour kwa upande mmoja katika pande mbili zinazoshutumiana. Hiyo humshushia hadhi na kumjengea chuki kwa upande wenye upinzani na mitazamo yake. Kwa kweli mtu yeyote anayemjua Salma Said hawezi kukosa kujua msimamo wake wa kisiasa. Nimejaribu kufatilia nyenendo za mwandishi Salma Said nikagundua ana udhaifu mkubwa katika suala Zima la kubalance habari.

  Kwa mfano kulipotokea kesi ya mgogoro wa Hamad Rashid kama ungekuwa unasoma habari zake ni kwamba alikuwa anamuelezea Hamad Rashid sawa sawa na jinsi upande wa wenye mgogoro na Hamad Rashid unamueleza. Msaliti, ana ajenda ya siri, kanunuliwa nk. Mwenendo huu sio mwenendo wa mwanahabari. Mtoa habari hatakiwi kubase upande mmoja katika suala la mgogoro

  Pia nimechunguza na nikaona kuna kiongozi Fulani anapenda kumsifu na kila habari inayohusu kiongozi huyo basi huipamba na haijawahi kutokea siku ikaelezwa katika mtazamo negative kwa kiongozi huyo

  Kwa mujibu wa habari zake anazozitoa Facebook Salma Said ana kawaida ya kutoa comment juu ya habari aliyoiweka na kuonesha msimamo na hata kuanza kuwapinga baadhi ya watoa comment au kuwasupport wengine. Tabia hiyo inaweka wazi misimamo na mitazamo ya Mwandishi huyu jambo ambalo hatakiwi kufanya

  Namshauri kama anata kuwa professional na aheshimike kama muandishi na sio mpiga debe wa mtu, kundi, au mitazamo Fulani basi ajaribu kuchunga suala Zima la kubase upande Fulani unaohusu habari yake.

 11. A.alekum nyote nimekueleweni maneno yenu ila maskini asilaumiwe salma wala ali saleh kwani ni waandishi wazuri tu sana na nyie ambao mliokuwa si waandishi jamani hajui ya ndani na hasa muandishi akiwa wa serikalini huwa hana sauti kabisa japokuwa hili ni la ubaya sasa wao kina salma wana free line to tolk kabisa ila sio wao wa serikalini.
  mie nilikueko kwenye kikao hicho kusema la ukweli kweli Waziri maneno hayo kasema na kwlei yana ubagusi kabisa wallahi unajuwa hii serikali ya kimataifa ila haina mpangi wowote mana hadi leo maendeleo hatuyaoni kubwa wameongeza mshahara ila mshara wameongeza na maisha piaya yameongezeka juu zaid halafu inachoumiza zaidi ni kuwa wakubwa hawa huwa wanakula wao tu. Mfano Wizara ya fedha kuna uchafu zaid pale mana kuna jengo lile la pemba hadi leo pesa zake shungunzima zimepoteya na tunamjuwa hasa alokula pesa zile ni Mkuregenzi Senga yaani huu jamaa hai hasa tena hapo Katibu wake anamteteya sana Watu kama hawa lazima wachukuliwe hatuwa haiwezekani pesa za serikali kama milioni mia 3 watu wale tu bure na itakuwa Katibu wake Khamiss mussa na yeye kala au wana siri za ajenda hawa watu 2 mana ofisi nzima hawamtaki bado tu kaekwa mana utashangaa ana uroho wa madaraka na ana roho mbaya sana jamani serikali ndo iko pale watu kma wale wakiweka hawafai anakula yeye tu na sio yeye wapo watu tele serikalini wahafai bado Rais kawaweka naona mie bora Rais angaliye Serikali yake mana bila ya hivyo hao watendaji wake watamuangusha kama kina Mwinyi haji na Wakurugenzi kama Senga

 12. QADHIA YA UBAGUZI NA CHANZO CHAKE

  Qadhia ya Waziri wa Nchi Ofsi ya Raisi Dr. Mwinyihaji Makame kudhihirisha matamshi ya kibaguzi waziwazi hadharani kwa waandishi Ali Saleh (BBC) na Bi Salma Said (DW) ni lenye kumsikitisha na kumhuzunisha kila mwenye tembe ya ubinaadamu. Kwa kuwa ubaguzi haukubaliki kwa hoja za kiakili wala za kidini. Uchafu huu umekuwa ukiikabili Zanzibar kwa muda mrefu, umezua mabalaa mengi yasiokuwa ya lazima na kuisambaratisha jamii vipande vipande. Na kutolewa matamshi kama haya kutoka katika kinywa cha mtu wa daraja ya uwaziri, ni dhihirisho kuwa saratani ya ubaguzi bado imekita na kumakinika licha ya kuundwa ‘serikali ya umoja wa kitaifa’. Halkadhalika, uovu huu umekita na kuota mizizi katika nchi nyengine mbali mbali ukiwemo kwa bahati mbaya ulimwengu wote wa kiislamu. Jambo hili ni kwa sababu biladi zetu za kiislamu zimeacha misingi yake ya asili ya kiislamu na kufakamia mfumo wa kibepari/kidemokrasia wa kimagharibi kwa shinikizo la madola makubwa. Mfumo ambao kimaumbile umejaa ubaguzi ndani ya moyo wake.
  Kwanza, mfumo wa kibepari/kidemokrasia unashikilia fikra chafu na za hatari za Machieveli katika mambo yake hususan katika siasa. Fikra zinazobainisha wazi kwamba, njia yoyote itakayokufikisha katika lengo lako la kisiasa ni njia halali. Kanuni hii hukusudiwa: ‘lengo huhalalisha njia na njia huhalalisha lengo’ (‘ends justify means and ‘means justify ends’) Kwa hivyo, imekuwa ni ada maarufu katika nidhamu ya kidemokrasia/kibepari kutumia njia yoyote hata ya ubaguzi, uwe wa rangi, kabila, mahala ulipotoka na dini ikiwa kufanya hivyo kutamfikisha mwanasiasa katika malengo anayokusudia kisiasa. Kama tunavyoona leo wanasiasa hususan ndani ya nchi za magharibi, kwao ubaguzi dhidi ya Waislamu ni turufu ya hali ya juu ya kujinyakulia kura za wananchi wao katika chaguzi zao. Aidha, wakati mwengine wanasiasa katika mfumo huu huutumia ubaguzi kama chaka la kujifichia badala ya kukabili matatizo msingi, au ubaguzi hutumika kama mbinu ya kujihami na kukimbia hoja msingi katika kukabili masuala msingi mbele ya mwanasiasa kama ilivyodhihiri katika qadhia hii.
  Pili, udhaifu mwengine wa mfumo wa kibepari/kidemokrasia kamwe haukujifunga na dini, na kamwe haufungamanishi mambo yake na Mola Mumba. Kwa sababu, kimsingi suala la mtu kazaliwa na nani, kabila gani, koo gani au kizazi cha nani, mambo haya ni yenye uhusiano moja kwa moja na suala la Uumbaji, mbalo ni suala la kidini na si vyenginevyo. Kwa bahati mbaya, mfumo huu dini umeipa daraja duni kwanza kwa kukifanya kitu cha khiyari kwa anetaka kuamini kuwepo kwake. Pili kwa kuifungia katika pembe nne za majumba ya ibada pekee. Na tatu kwa kuitenga mbali kabisa na mambo ya utawala.
  Uislamu unaikataa moja kwa moja nadharia potofu ya Machiveli ya kutumia njia yoyote kufikia lengo lako, bali umeweka msingi wa ‘halali’ na ‘haramu’ pekee. Na kamwe hairuhusiwi kutoa kisingizio cha kudai una lengo halali kwa kupitia njia haramu. Na ukatowa ufafanuzi wa kila lengo na njia ya kulifikia. Aidha, ukatamka wazi kwamba ni haramu kumbagua mtu mwengine. Uwe ubaguzi wa kikabila, kimaeneo, kinchi, taifa, rangi na mwengineo, na huu wote katika Uislamu huitwa ‘assabia’.
  Mtume SAAW anasema:
  ‘Si katika sisi anayelingania katika assabia ,au naepigana kwa lengo la uassabia au anayekufa kwa ajili ya uassabia. (Abu Daud)

  Pia akasema tena SAAW:
  “Kwa hakika watu wote tangu zama za Adam mpaka zama zetu hizi ni kama meno ya kitana, hakuna ubora kwa muarabu kwa asiyekuwa muarabu wala ubora wa mwekundu kwa mweusi, ila kwa uchaji Mungu”
  (Mustadraku-u lWasail)

  Aidha, katika msingi wa imani ya Kiislamu (aqeeda) unalihusisha suala la mtu kuzaliwa katika koo fulani, kabila fulani, au rangi fulani si matakwa katika matakwa ya mwanadamu. Bali mambo haya kapangiwa na Mola Muumba. Na haya huingia katika mambo yanayoitwa ya Al-Qadhaa” ambayo yako nje ya mamlaka ya mwanaadamu, wala mwanaadamu hahojiwi kwa mambo haya.

  وَرَبُّكَ يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ وَيَخْتَارُ مَا كَانَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ سُبْحَانَ اللَّهِ وَتَعَالَى عَمَّا يُشْرِكُونَ (القصص:
  ‘Na Mola wako huumba na huteuwa atakavyo. Viumbe hawana khiyari. Mwenyezi Mungu ametukuka na ametakasika na hao wanaowashirikisha naye.’ (TMQ 28:68)
  Amma, ubaguzi kwa misingi ya kivyama ulioitafuna Zanzibar kihistoria, baada ya kurejeshwa tena vyama vingi na unaoendelea hadi leo. Kiislamu, jambo hili huzingatiwa katika hali mbili: Kwaza, hawakupaswa kamwe Waislamu kuunga mkono vyama vya kidemokrasia kwa kuwa vimesimama juu ya msingi wa kikafiri wa kutenganisha dini na maisha (secularism), na kuviunga mkono vyama hivyo ni dhambi isiyo na shaka. Pili, baada ya kushikamana na vyama hivyo, na mmoja akambagua mwengine kwa msingi wa vyama hivyo, hapo huongezeka dhambi ziada kwa kitendo hicho cha ubaguzi. Lakini kwa upana wake ubaguzi huu nao si zaidi ya mbinu ile ile ya kimachieveli kwa lengo linalosukumwa na uroho wa madaraka wa chama cha pili. Ilhali kimsingi vyama vyote vya kidemokrasia vinashikilia misingi sawa, na hutofautiana tu katika masuala ya kimatawi. Kwa hivyo, iweje mfuasi wa chama kimoja kumbagua mfuasi wa chama chengine chenye misingi na usajili sawa kama chama chako, kama hiyo si mbinu chafu na dhihirisho la uroho wa madaraka?

  Zaidi ya yote Uislamu chini ya kivuli cha dola yake ya kiislamu ya Khilafah Rashidah huwatumikia raia wote kiudalifu na kuwaangalia kwa jicho moja tu, jicho la uraia bila ya kuzingatia dini, kabila, rangi wala eneo analotoka. Ndio maana Mtume SAAW akawahi kutamka wazi kwamba yoyote atakaemdhulumu dhimmiy (kafiri, raia ndani ya dola ya kiislamu ), yeye Mtume SAAW atasimama kuwa wakili wa kafiri huyo siku ya Qiyama.

  MASOUD MSELLEM MASOUD
  NAIBU MWAKILISHI KWA VYOMBO VYA HABARI – HIZB UT-TAHRIR AFRIKA MASHARIKI. jukwalakhilafah@gmail.com

 13. Poleni albarto na anti salma hamupaswi kuvunjika moya ongezini bidii katika kutafuta habari bila ya kupata mitihani hamuwezi kusonga mbele allah atakusaidieni

 14. br & sister
  Nilichokibaini mimi katika kauli ya MW/HAJI NI HASIRA TU NA WALA SI UBAGUZI.
  ila suala la ubaguzi hapa kwetu lipo.ila katika mazingira ya mada hii ubaguzi haukuwepo.
  kanda niliisikiliza vizuri na nikasikia “kasiriko tu “na hilo ndio lilikuwa kosa la MW/haji

 15. Jamani nakuusieni, kila mkiendelea kuzoza na ndio TANGANYIKA wanajipanga na kupata mwanya Zaidi wa Kuichukuwa nchi, nyote mliochangia mada hii kuanzia mwanzishaji mada… nakuombeni acheni kulumbana, kina CCM na CUF hivi sasa nyote ni wamoja, tumieni nguvu zenu kuitetea ZANZIBAR na sio kugombana nyinyi kwa nyinyi…

  MOH’D J. ABDALLA
  From ITB Berlin, Germany

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s