Maalim Idrissa afariki dunia

Marehemu Maalim Mohammed Idrissa wakati wa uhai wake akiwa kijana wake mpenzi Mohammed Khamis (Eddy Calipso) nje ya msikiti wa Shangani mkabala na Mambo msiige. Maalim Idrissa amefariki leo asubuhi na maziko yake yatafanyika kesho katika msikiti wa Muembe Shauri Rahaleo na kuzikwa Mwanakwerekwe saa 4 asubuhi. Inna lillahi wainna ilayhi rajiiun

Alisema anawaomba walimu wa Madrasa wabadilike baada kumaliza Jengo la chuo hicho waanze kusomesha watoto na kufuata silibas ya Masomo ya kiingereza na Kiarabu na Dini hapo hapo na waache kupeleka watoto school kwani wakijipanga vema wataweza kutoa wanafunzi wazuri na kwa haraka sana.

 

Maalim Idriss hatunaye tena

 

Na Mohammed Omar (Juda)

 

Maalim Mohammed Idriss Saleh Comorian amefariki akiwa na umri wa miaka 78. Innalillah wainnailaihir rajiun.

 

Mauti yalimkuta Maalim Idriss usiku wa tarehe 5 Machi, 2012 sawa na tarehe 11 Rabiu thani 1433 na kuzikwa Machi 6 katika makaburi ya Mwanakwerekwe baada ya kuswaliwa katika Msikiti Mkuu wa Mwembeshauri.

 

Alifariki akiwa katika hospitali ya Daktari Jidawi, Vuga baada ya kuuguwa kwa muda kiasi ingawa hakuwa amelazwa awali.

 

Miongoni mwa watu mashuhuri walioshiriki maziko yake ni pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais, Alhaji Maalim Seif Sharif Hamad, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi na Kadhi Mkuu Sheikh Khamis Haji.

 

Katika mengi atakayokumbukwa Sheikh Idriss ni kwamba yeye ni katika Maulamaa mashuhuri wa asili wa Afrika Mashariki na Kati akiungana na Sheikh Ahmed Bin Sumeit, Sayyid Burhan Mkelle, Sheikh Abdallah Saleh Farsy na wengineo wengi ambao Maalim Idriss alifanya kazi kubwa kuhifadhi kazi zao. Baadhi ya kazi hizo, Maalim Idriss aliandikia makala na kuchapishwa katika magazeti ya Dira na kisha An nuur.

 

Marehemu Maalim Idirisa jina lake hasa ni Mohammed Idriss Mohamed Saleh Comorian, akiwa amezaliwa katika mtaa wa Vikokotoni Zanzibar tarehe 17 Septemba, 1934. Baba yake akiitwa Sheikh Idriss Mohammed Saleh, ambae alikuwa Mwalimu wa School na Mama yake akiwa ni Bi. Mwanakheri binti Mzee Haji Ally.

 

Jina lake limefanana na la Al Imam Mohamed Bin Idriss Shafii na hii ilikuwa ni fakhari ya wazee wake kutoa jina linalofanana na watu wema.

 

Akiwa wa kwanza kuzaliwa katika wale nduguze wanane (8), wanaume 4 na wanawake 4, Maalim Idriss alikulia katika mtaa wa Mchangani mjini Unguja na Kikwajuni.

 

Kama kawaida ya watoto wa Kiislamu afikapo umri mdogo wa kuanza kusoma huanzishwa madrasa, naye alianza kusoma chuo kwa Sayyid Mohamed Alawi Jamalily hapo Mchangani.

 

Baadae wazee wake walimpeleka kujiendeleza katika masomo ya Dini kwa Masheikh mbali mbali wakiwemo Sheikh Kamus hapo msikiti wa Mbuyuni, Sayyid Alawi, maarufu Sharifu Mrefu, Msikiti Rajab Majesti Cinema, Sheikh Abdallah Muadhini na Maalim Himidi.

 

Baadae wazee wake wakampleka skuli na alisoma skuli Shimoni, Kengeja, Pemba na kisha Government Boys Sec. School (sasa ni Ben bella) ambapo alimaliza darasa la 8.

 

Mwaka 1950 alijiunga na Chuo cha Ualimu (Teacher Training College) katika masomo ya Ualimu na kuwa Mwalimu ambapo alisomesha katika skuli ya Dole na skuli nyingine mpaka alipostaafu.

 

Marehemu Maalim Idriss baada ya kustaafu, alitumia muda wake kusomesha watoto wa Madrasa, hapo msikiti wa Mambo Msiige katika mwaka 1985 ambapo alikuwa Imamu.

 

Kwa kipindi chote hicho Marehemu aliweza kuanzisha N.G.O ikitwa IMRO kirefu chake ni Islamic Madrasa Relief Organition ambayo kazi yake ni kuvisaidia vyuo vya Qur’an na kuwasaidia watoto yatima, kazi ambayo alifanikiwa na inaendelezwa mpaka sasa.

 

Lakini katika kazi kubwa na muhimu zaidi ambayo inamfanya Maalim Idiriss kuwa mwanazuoni wa kipekee Zanzibar na Afrika Mashariki, ni ile kazi kubwa aliyofanya ya kukusanya historia sahihi ya Zanzibar, historia ya watawala wa Zanzibar katika nyakati mbalimbali, historia ya Maulamaa wa Zanzibar pamoja na historia ya misikiti.

 

Alifungua Maktaba na Ilsamic Museum nyumbani kwake Shangani, ambapo amekusanya vitu mbalimbali vya kale zikiwemo sarafu, picha za watu mashuhuri wa kale, mashairi, nyaraka, historia ya Maulamaa mbali mbali wa Afrika Mashariki, Comoro, Oman mpaka Yemen na maandiko ya watu mbalimbali ya kale. Kwa hakika maktaba hiyo ni hazina ya historia na elimu ambapo wasomi na watafiti mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, hasa Ulaya na Marekani, wamekuwa wakifika kupata taarifa na kuchota elimu.

 

Marehemu Maalim Idriss alifanya safari nyingi za nje ya nchi kama Uarabuni na Ulaya katika juhudi ya kuisimamisha maktaba hiyo na kwa kualikwa na taasisi mbalimbali za kitaaluma kutoa mihadhara na mijadala katika masuala ya historia ya Zanzibar na Afrika Mashariki.

 

Katika kazi nyingine Marehemu alikuwa kiongozi wa Uradi wa Bausudani. Alishika makamo hayo hadi kufariki kwake.

Uradi huu alikabidhiwa kuusoma hapo msikiti Jibril kila siku ya Jumanne laasiri baada ya kufariki Sayyid Idarusi bin Hassan al Sheikh Abubakar bin Salim hapo 1971.

 

Marehemu atakumbukwa pia kwa mchango wake kwa vijana kwani alikuwa kiongozi wa vijana tokea mwaka 1971. Alikuwa katika kikundi cha Taj Mahal, kikundi ambacho kilikuwa na vijana kina Ali Khalil, Awadh Karama, Ali Majid na wengine ambao sasa ni wazee na aliwalea vyema. Kikundi hiki bado kipo na Marehemu alikuwa ni mlezi.

 

Kikundi kingine ni kikundi cha Mambo Msiige ambacho leo ndio wameandaa Kisomo cha Khitma kwa kumuombea Mzee wao Maalim Idriss, kina Edi Kalipso na Vijana wenzake.

 

Katika jumla ya vijana wake aliowalea ni pamoja na Dr. Nofal ambae ni Daktari Mkuu wa hospitali ya Mnazi moja na Zahor ambaye ni Naibu Mkurungenzi Mkuu Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi Bahari Kuu Tanzania.

 

 

Maalim pia alikuwa Mwenyekiti wa Mwinyi Baraka Foundation, Mlezi katika Madrasatul Munawar Malindi, Miongoni mwa Wazee wa Ukutani Zanzibar na mjumbe katika Kamati ya Maulidi ya Mbuyuni akiwa ni mmoja katika waanzilishi.

 

Marehemu pia alikuwa ni mshauri katika kujenga Uzio katika Makaburi ya Mwanakwerekwe akisaidiana na Bi Sania Mahmoud.

 

Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya ZOP inayoendesha kambi 40 za matibabu Unguja na Pemba ikiwemo MOBILE CLINIC. ZOP ina miradi mingine ikiwemo ile ya afya maskulini, Skuli ya Viziwi, Ukusanyaji wa misaada na kuisambaza na hivi karibuni imezindua mradi wa ‘scholarship’ kwa watoto waliopoteza wazazi wao katika ajali ya Mv Spice Islanders.

 

Niseme kuwa Maalim alikuwa akipenda kuona Vijana wanasonga mbele na maisha wakiwa na elimu bora.

 

Marehem Maalim Idriss atakumbukwa katika hadhara nyingi, zikiwemo Hauli za wanazuoni kwani alikuwa msomaji wa Naashid, lakini pia alikuwa akichukua juhudi za makusudi kwa kutoa historia za Maulamaa wa Zanzibar na kazi zao walizokuwa wakizifanya.

 

Kadhalika pia atakumbukwa sana hapo msikiti Gofu kwani kila ifikapo Ramadhani alikuwa akisoma khitma na utangulizi kabla ya kuanza kwa Darsa, kazi ambayo ilikuwa ikifanywa na masheikh na Wazee waliotangulia.

 

Marehemu Maalim Idiriss alikuwa ni mtu karimu akipenda watu wa rika zote, akipenda kushirikiana na watu, mcheshi, sio mtu mkali hata pale anapokerwa huonesha hasira lakini ni wa muda mfupi. Niseme alikuwa na Haiba yenye mvuto mkubwa.

 

Katika jumla ya mambo ya mwisho aliyofanya katika uhai wake, ilikuwa katika ile hafla ya Madrasa Munawar, Malindi mwezi wa Muharam 1433h ambapo alikuwa mgeni rasmi.

 

Katika nasaha zake aliwataka walimu wa Madrasa wabadilike na kuboresha madrasa ambapo pamoja na Qur’an na Maarifa ya Uislamu watafundisha hesabu, kusoma na kundika, Lugha ya Kiarabu na Kiingereza.

 

Marehemu alikuwa mpenzi wa Mtume Muhammad (s.a.w) kiasi kwamba pamoja na kuwa afya yake haikuwa nzuri, lakini alikuwa akichukua taklifu kubwa kuhudhuria Maulid Nnabii katika kipindi chote cha Mfungo Sita uliopita.

 

Mwisho nawaomba vijana wamuenzi marehemu Maalim Idiriss katika kumkumbuka na kuendeleza kazi aliyoanzisha ya kuwaunganisha vijana.

 

Mola amrehemu na amlaze mahali pema yeye na watu wema na wazee wetu wote na jamii ya Kiislamu. Inshallah amuingize Peponi na tuwe nae pamoja na Mtume Muhammad (s.a.w).

 

 

(Mimi Mohamed Omar Al Sheikh Juda ni miongoni mwa Vijana wake alionilea katika maadili mema na ndie alienishika mkono kunipeleka msikiti wa Mbuyuni kwa Sheikh Kamus. Huko nimepata mengi sana na kufaidi haya leo niliyonayo).

 

 

 

 

Advertisements

2 responses to “Maalim Idrissa afariki dunia

  1. Inna Lillahi Wainna Ilayhi Rajiun, Marehemu Sheikh Mohamed Idrissa, ni Maalim wangu ambaye alishika msikiti pale mambo msije,shangani. na akawa imamu wa msikiti tangu mwaka 1985, na akautengeneza na akanzisha darsa la usiku mwaka huo huo 1985, na mpaka akauendeleza akaufanya wa gorofa na vijana wengi wa shangani walifarijika na mchango wake wa kutoa elimu ya dini ya kiislamu na sehemu mbalimbali walikua wanakuja kama vile malindi , mchangani n.k

    kwahio mimi ni mwanafunzi wake wa karibu sana ilikua wakati huo na muasisi wa darsa lake la mwanzo la mwaka 1985, nakumbuka wanafunzi wa mwanzo mwaka 1985, walikua wakiishi malindi ni: mohamed maharouk, khalifa maharouk hivi sasa yupo nchini Qatar,amour na ndugu yake suleiaman,mbambato jina lake la sasa anaitwa msumari mwenye duka darajani na ndugu yake rashid au chidi hivi sasa yupo oman, Abeid na kaka yake Rashid,walikua wanao ishi shangani ni :jabir haidar jabir, Mahmoud haidar jabir,mahamoud haidar jabir, muhamed haidar jabir, Eddy Kanji, Sabri Kanji, Muhamed Abdullah Abuso, idarous, Khalfan,ALI Kidomo na kaka yake Rashid, marehemu Muchi, Rashid Chama, muhamed Gharibu umarufu wake China, na wengine nimewasahau majina yao

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s