Hizbu ut- Tahrir watathmini matokeo ya mitihani

Kongamano la chanzo ya kufutiwa matokeo ya mitihani ya kidato cha nne lililofanyika leo katika ukumbi wa Skuli ya Hailesselasie, lililotayarishwa na Hizbu ut Tahrir Afrika Mashariki, wlaiokuwepo mbele kutoka ni Mwalimu Chande Chande, Ali Amour Makame, Masoud Msellem Mwalimu Muhija Zubeir na Khamis Ali

 

Suluhisho la suala la muungano huu sio kuwa na serikali tatu, nne au tano, bali ni kuondosha msingi dhaifu wa kibepari katika kusimamia mambo yetu yote, yawe ni katika muungano, katiba, vyama, uchumi, jamii na mengineyo. Kwa sababu huu ndio msingi wa tatizo.

 

“CHANZO CHA KUFUTWA MITIHANI YA KIDATO CHA NNE

NA

SULUHISHO LAKE KIISLAMU”

 
Mada iliyowasilishwa katika
Kongamano Maalumu Kujadili Mgogoro wa Kufutwa Matokeo ya
Kidato cha Nne lililoandaliwa
na
Hizb ut-Tahrir Afrika Mashariki

 

Ukumbi wa Hailesselassie – Zanzibar

04/02/2012 – 11 Rabi thani 1433

 

 

 

بِِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

KUFUTWA MATOKEO YA MITIHANI- CHANZO CHAKE NA SULUHISHO LAKE KIISLAMU
Matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yaliyotangazwa mnamo tarehe 7 Februari mwaka huu yamesababisha majonzi, huzuni, malalamiko na masikitiko makubwa katika kila nyumba hususan kwa wakaazi wa Zanzibar na jamii ya Waislamu kwa ujumla. Kiasi cha kupelekea Kamati ya wazee wa wanafunzi waliosibiwa na qadhia hii ndani ya Zanzibar kutoa muda wa siku saba kwa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA )kurejea tena mtihani ili kuondoa manun’guniko na utata uliopo. (Zanzibar leo, 01 Machi, 2012)
Tukiangalia takwimu zinaonyesha kati ya watahiniwa 426,314 waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2011, ni wanafunzi 33,577 tu ndio waliopata daraja la kwanza mpaka la tatu (Division 1 – 3) ambao ni sawa na asilimia 9.8. Kwa upande wa waliopata daraja la nne ( Division 4) ni wanafunzi 146,639 sawa na asilimia 43.60, na waliofeli kabisa ni 156,089 sawa na asilimia 46.40. Kinacholeta simanzi na mfadhaiko mkubwa ni kwamba kuna wanafunzi wengine 3,301 waliofutiwa matokeo kwa kashfa za udanganyifu, ambao zaidi ya wanafunzi 1700 kati ya hao ni kutoka Zanzibar, hii si idadi ndogo hasa ukilinganisha na wanafunzi wote 27,502 waliofanya mtihani huo kutoka Zanzibar. Jambo hili limewaacha wanafunzi, wazazi, walimu, wadau mbali mbali na raia walio wengi kuelekeza moja kwa moja lawama na shutuma kali dhidi ya Baraza la Mitihani (NECTA) kwa kuendeleza dhulma kwa wanafunzi jumla wa kiislamu na kuibua upya kero ya muda mrefu ya kukandamizwa na kushushwa hadhi ya Zanzibar kwa makusudi ndani ya muungano. Aidha, kuna shutuma / dhana kwamba wanafunzi wa Zanzibar wamefelishwa makusudi ili kuwanyima fursa ya kupata elimu ya juu. Kwa kuwa mtazamo wa haraka wengi wa watendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa si Waislamu.
Kuhusiana na sakata lote hili Baraza la Mitihani liliweka wazi msimamo wake katika kikao chake cha 86 kilichofanyika tarehe 7/2/2012 kwa kutamka: “Baraza limeamua kuwa watahiniwa wote waliofutiwa matokeo yao kutokana na kujihusisha na udanganyifu au kuandika matusi kwenye karatasi za majibu hawataruhusiwa kufanya mtihani wa baraza kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu” alisema Dkt Joice Ndalichako. (Katibu mkuu wa Baraza la mitihani Tanzania) Aidha, Katibu Mkuu huyo alisisitiza pia kuwa Baraza halina taarifa yoyote ya uvujaji wa mitihani, bali kilichopo ni udanganyifu wa wanafunzi, waliofanya udanganyifu huo wanastahiki adhabu za kinidhamu.
Ni muhimu kuzingatia vipengele vifuatavyo juu ya songombingo hii iliyojiri ndani ya jamii yetu:
Kwanza, Suala la kubatilishwa matokeo ni la kihistoria na lilianza tangu kuasisiwa kwa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) mwaka 1974, ambapo mwaka mmoja tu baada ya kuasisiwa kwake (1975) kulianza kupatikana kashfa ya uvujaji wa mitihani, na wanafunzi 72 ndani ya mwaka huo huo walifutiwa matokeo yao. Hali iliendelea hivyo, na taarifa za kufutwa kwa matokeo kila miaka ikawa kama ifuatavyo:-
MWAKA    IDADI YA WANAFUNZI WALIOFUTIWA MATOKEO
1976     30
1977     454
1979    140
1980     154
1981    203
1982 138
1983 402
1984 327
1992 1563
www. jitokezedirectory.blogspot.com
Katika mwaka wa 1998 uvujaji ulifurutu ada na kuruka mipaka hadi NECTA ikaamua kufutilia mbali mitihani yote nchi nzima, na baadae kufanyika upya mapema mwaka 1999. Halkadhalika mwaka 2008 Baraza lilisema ni mtihani wa hisabati tu ndio uliovuja, na baadae kukazuka matamko makali kutoka wadau mbalimbali na baadhi ya wanasiasa kuwataka watendaji wa Baraza hilo kujiuzulu kutokana na uzembe huo. Janga hili la uvujaji wa mitihani si tu linaikabili Tanzania pekee bali inashuhudiwa katika nchi nyingi kama si zote za kidemokrasia/kibepari zikiwemo za Ukanda wa Afrika Mashariki. Kwa mfano, katika mitihani ya kitaifa ya darasa la nane nchini Kenya iliyofanyika mwaka 2011, wanafunzi takriban 8000 wa shule 335 za msingi walifutiwa matokeo, na Waziri wa Elimu wa Kenya (Profesa Sam Ongeri) alikaririwa akisema: ‘Suala la udanganyifu wa mitihani si suala la mtu mmoja bali ni mtandao mkubwa unaowahusisha wamiliki wa shule, wanafunzi, wazazi, watendaji wa baraza la mitihani la taifa (KNEC)  wakiwemo pia wasimamizi wakuu wa vituo mbali mbali ( Supervisors) na wakaguzi (invigilators’. http://www.all africa.com- exam leakages inkenya. Aidha, iliripotiwa katika mwaka huo huo ndani ya Kenya katika mitihani ya kidato cha nne shule kadhaa hasa Mjini Mombasa kupata nakala pungufu za mitihani ukilinganisha na idadi ya watahiniwa waliopo. Hali inayoashiria kuwepo kwa uvujaji wa mtihani huo. Na hivi majuzi Profesa Ongeri (Waziri wa elimu Kenya) ametangaza tena kufutiwa matokeo wanafunzi 2927 kutokana na udanganyifu.
Qadhia kama hii pia huripotiwa nchini Uganda, ambapo ndani ya mwaka 2006 baraza la mitihani ya nchi hiyo (UNEB) iliwafutia matokeo watahiniwa 2000 na baadhi ya walimu na watendaji kukamatwa. http://www.gbooza.com .
Chanzo cha yote haya ni kutokana na udhaifu wa kimaumbile wa mfumo wa kibepari ambao haungalii chochote zaidi ya maslahi katika vitendo. Kwa maana ya kwamba, kitendo katika mfumo huu hufanywa kwa gharama yoyote kikiwa na maslahi, na huachwa kikikosa maslahi. Mfumo wa Magharibi uliosukumwa kwa shinikizo katika nchi zetu. Mfumo huu umeathiri fikra za kila mtu ndani ya jamii. Ndio maana baadhi ya watendaji wa mabaraza ya mitihani kamwe hawajali zaidi ya maslahi na matumbo yao, walimu nao wametawaliwa na maslahi, wazee na wanafunzi nao ni vivyo hivyo. Kwa hivyo, tusishangae bali tutarajie chini ya mfumo huu batil kuona kashfa na aibu kama hizi kuongezeka siku hadi siku ndani ya jamii zetu. Kwani ulafi, uroho na tamaa ya kidunia ndio matunda ya mfumo wa ubepari/kidemokrasia.
Pili, Kwa kuwa mfumo wa kibepari haukujifunga juu ya kipimo cha halali na haramu, masuala ya udanganyifu, uwongo na kughushi ni suala la kawaida kama maji ya kunywa katika maisha ya kila siku. Na ndio maana tunaushuhudia kwenye kila nyanja, katika udakhili wa vyuo vikuu, shule za sekondari, ajira nk. Masuala ya kughushi vyeti, kuiba mitihani, rushwa za fedha na za ngono na kujuana, haya yamekuwa ni mtindo wa maisha kila uchao. Aidha, mfano mwengine mzuri ni katika mwaka wa 2009 tuliposhuhudia kashfa kubwa kwa baadhi ya wabunge na viongozi wa juu ndani ya serikali ya Tanzania kughushi vyeti vya vyuo vikuu katika fani mbalimbali, zikiwemo shahada za uzamili, udaktari n.k. Basi ikiwa hii ndio hali ya viongozi wa juu, je hali ya wanaoongozwa itakuaje? Kadhalika tukumbuke kwamba chini ya ubepari, udanganyifu si tu hutendwa na watu binafsi, bali hutendwa hata na dola takriban katika nchi zote ulimwenguni, si madola madogo wala dola zilizoendelea. Marekani kinara wa ubepari na demokrasia chini ya uongozi wa rais Bush ilitoa ushuhuda wa nyaraka za uwongo za kughushi kuthibitisha kuwepo kwa silaha za maangamizi ndani ya Iraq, kwa lengo la kujihalalishia kuivamia nchi hiyo mwaka 2003. Uvamizi uliopelekea kuangamiza maelfu ya Waislamu wasio na hatia. Na hadi hii leo hakuna hata kipande cha silaha ya maangamizi kilichopatikana. Bila ya kusahau kashfa ya udanganyifu iliyopelekea kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Karl – Theodor Zu Guttenberg mwaka 2011 baada ya chuo cha Bayreuth ndani ya Ujerumani alipochukuwa shahada yake ya uzamili (doctorate) kumvua shahada hiyo baada ya kugundua kushiriki katika udanganyifu wa mitihani.
Tatu, kuhusu suala kwamba Zanzibar na Waislamu jumla wakiwemo wa Tanganyika kufelishwa na kudhulumiwa kwa makusudi na Baraza la Mitihani, hapana shaka hali hiyo ni suala la kutarajiwa, kwa kuwa nidhamu ya kidemokrasia ni nidhamu ya kikafiri na huwa ni wajibu kwa nidhamu hiyo kuwapendelea makafiri wenzao, na kwa hivyo, haitarajiwi kamwe kuwapendelea Waislamu hata Waislamu wakijipendekeza namna gani kwa nidhamu hiyo ya kikafiri. Kwa upande wa malalamiko ya Zanzibar kuhusiana na dhulma inayotokamana na muungano wake na Tanganyika, kwa hili lazima tukumbuke kwamba fungamano lililojengewa muungano huu si fungamano sahihi la kiislamu, kwa kuwa muungano huu uliundwa na dola ya Uingereza kwa maslahi yake, na leo unaendelezwa pia na Marekani kwa maslahi yake. Muungano huu umeundwa juu ya msingi batili wa mfumo wa kibepari, na kamwe haukujengwa juu ya fungamano madhubuti la haki na uadilifu la kiislamu. Kwa hivyo, dhulma na kukosekana uadilifu ni hali ya kimaumbile katika muungano huu kutokana na kuasisiwa juu ya fungamano dhaifu, haramu na la kimakosa. Allah Ta’ala anatueleza matatizo ya kufungamana kwa fungamano dhaifu ambalo halikusimama kwenye nguzo imara ya Uislamu.

وَإِنَّ كَثِيرًا مِنْ الْخُلَطَاءِ لَيَبْغِي بَعْضُهُمْ عَلَى بَعْضٍ إِلاَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَقَلِيلٌ مَا هُمْ:).
“Hakika ya wa washirika wengi hudhulumiana wao kwa wao isipokuwa wale walioamini na wakatenda amali njema, nao ni wachache” 24
Kwa hivyo, chini ya muungano huu wa Tanganyika na Zanzibar na muungano mwengine wowote ambao hauna fungamano sahihi, hali ya kutoaminiana na kudhulumiana baina ya pande mbili ni jambo la kawaida na la kutarajiwa. Hili hudhihirika hata katika Muungano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Tanzania inaonekana kusuasua katika kuikubali mikataba kadhaa inayotaka kupitishwa na Muungano huo, ikikhofia Kenya inayoikodolea macho rasilimali zake hususan ardhi. Halkadhalika, katika Muungano wa Sarafu moja ndani ya Ulaya (Euro zone), Ufaransa na Ujerumani zinaonekana kuziburuza nchi nyengine ndogo ndogo za umoja huo kama Ugiriki kiasi cha hata kuzipangia bajeti nchi hizo.
Baadhi hulikabili suala la muungano baina ya Zanzibar na Tanganyika kimakosa kwa jazba na hulifanya daraja la hukuza hisia za kiaswabia/kiubaguzi baina ya wakaazi wa Bara na Visiwani. Jambo ambalo ni kinyume na Uislamu. Aidha, wengine hususan baadhi ya wanasiasa katika kujificha kushindwa kwao na kuwashughulisha watu wasikabiliane na tatizo msingi, huonesha kimakosa kwamba matatizo ndani ya muungano na muungano wenyewe ndio chanzo cha dhiki zote, badala ya kuonesha kiusahihi kwamba muungano ni tunda (product) linalotokamana na tatizo msingi. Kimsingi maumbile ya wanaadamu huwalazimu kutaka kuishi pamoja na kushirikiana katika muamalat/maingiliano na mambo yao ya kila siku, lakini tatizo huzuka juu ya msingi unaojengewa mahusiano baina ya watu hao. Na katika suala la muungano, tatizo ni msingi batil wa uliojengewa uhusiano huo. Msingi uliojengewa muungano huu unatokamana na nidhamu potofu na ya kikafiri ya kibepari/kidemokrasia. Vivo hivyo, tukumbuke pia kwamba vyama, chaguzi na michakato ya katiba zetu zote zimesimama juu ya msingi sawa na muungano, ambao ni msingi batil wa kidemokrasia ya kimagharibi. Kwa hivyo, kwa hakika ni kuchanganyikiwa kusikokuwa na mfano, upande mmoja kupinga muungano kwa kuwa unaidhulumu Zanzibar, na upande wa pili kuunga mkono vyama vya kidemokrasia na kuchangia mchakato wa katiba ya kidemokrasia, ilhali hivi vyote msingi wake ni mmoja wa kibepari na ndio uliotufikisha katika mashaka tuliyonayo. Suluhisho la suala la muungano huu sio kuwa na serikali tatu, nne au tano, bali ni kuondosha msingi dhaifu wa kibepari katika kusimamia mambo yetu yote, yawe ni katika muungano, katiba, vyama, uchumi, jamii na mengineyo. Kwa sababu huu ndio msingi wa tatizo.
Katika qadhia hii ya kubatilishwa matokeo ya mitihani ni vyema pia tukabainisha hatari inayotukabili na ufahamu wa kimakosa wa kuifungamanisha elimu ya kiskuli na rizki. Huu ni ufahamu wa hatari unaopingana na aqeeda ya kiislamu, unaowakosesha Waislamu utulivu na kuwajaza hangaiko lisilokuwa la lazima katika nafsi zao. Ufahamu huu licha ya kuwa ni wa kimakosa pia upo kinyume kabisa na uhalisia wa mambo yalivyo. Watu wangapi waliosoma na kufika elimu ya juu lakini humalizikia kuajiriwa na watu ambao hata hawakuiona milango ya shule? Leo kwa bahati mbaya baadhi ya Waislamu wameshikilia ufahamu huu mbovu kiasi cha kupelekea baadhi ya wanafunzi na wazazi kukata tamaa kabisa na maisha kwa kufutiwa matokeo ya mitihani, au wakati mwengine Waislamu huwa tunang’ang’ania elimu hii hata ikiwa katika maskuli wanayosoma watoto wetu tunadhuriwa imani yetu, kama kuzuiliwa ibada ya kuswali, kuvaa hijab nk.
SULUHISHO
Uislamu umeifanya elimu ya kuzijua hukmu za kisheria ndio elimu faradhi kwa kila Muislamu mukalaf/aliyebaleghe, na ukawajibisha kujifunza elimu hizo kwa mwanamme na mwanamke, na asiyejifunza hupata dhambi na atakuwa mas’ul mbele ya Allah Ta’ala. Aidha, Uislamu ukakataza kutenda kitendo chochote bila ya kuijua hukmu yake ya kisharia. Na ukalifanya lengo kuu la elimu hiyo ni kuijenga na kuifinyanga shakhsia/haiba ya kiislamu na si zaidi ya hilo. Kadhalika, ukahimiza kujifunza taaluma nyengine katika mambo ya fani na ufundi kama kemia, fizikia, udaktari, ufundi nk. kwa lengo la kuongeza maarifa, utafiti na kuzitumia katika maisha ya kila siku katika matumizi mbali mbali ya wanaadamu. Lakini ukaziweka elimu hizi katika daraja la ‘mubaha’ na sio faradhi. Kwa hivyo, asiyejifunza elimu hizi za kiskuli huwa hapati dhambi. Pamoja na hivyo dola ya kiislamu ya Khilafah itahakikisha kwa kadiri itakavyowezekana kwa kila raia anapata elimu zote mbili bila ya malipo yoyote. Kwa upande wa kukabiliana na ghushi na udanganyifu, Uislamu chini ya dola yake ya Khilafah kwanza, utaandaa mazingira mwanana ya kuwajenga raia wake maadili ya kiislamu. Maadili yatakayowafanya kuyafungamanisha maisha ya dunia hii na maisha yajayo, kiasi cha kumfanya mtu akhofu kutenda kitendo cha udanganyifu. Na lau mtu atafanya udanganyifu, adhabu kali ya taazir itamkabili. Hapana shaka hata katika mfumo wa kidemokrasia suala la udanganyifu huadhibiwa, lakini mfumo huu una migongano dhahir. Kwa upande mmoja kughushi na udanganyifu ni kosa, na kwa upande wa pili kipimo cha vitendo katika mfumo huo ni maslahi. Hiki ni kizungumkuti cha wazi ambacho ni dalili ya kutofaa mfumo huo. Katika Uislamu kila kitendo chenye sifa ya kughushi na udanganyifu kwa mujibu wa Uislamu huadhibiwa, lakini zaidi ya hilo kipimo cha vitendo ni halali na haramu, na kamwe si maslahi. Amma kwa upande wa kujenga mahusiano thabiti baina ya raia, dola ya kiislamu ya Khilafah itafutilia mbali aina zote za miungano batil ya kibepari na ya kikoloni kama muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Aidha, Khilafah itazirejesha tena ardhi zote za Waislamu zilizomegwa kama Sudani ya Kusini, Timori ya Mashariki nk. Na zaidi Khilafah itapambana vikali na harakati za kiaswabia zinazodhamiria kuzitenga ardhi za Waislamu, kama vile jaribio la kukitenga kisiwa cha Pemba, na vuguvugu la chama cha Mombasa Republican Council (MRC) kinachokusudia kuumega mwambao wa Kenya. Na badala yake dola ya Khilafah itawafungamanisha raia kwa msingi madhubuti wa aqeeda ya kiislamu. Msingi ambao hauwabagui raia kwa mujibu wa maeneo wanayotoka, rangi, kabila wala dini. Kama inavyong’ara tareekh yetu tukufu ya kiislamu namna dola ya Khilafah ilivyoweza kuwafungamanisha kitu kimoja raia wa maeneo mbali mbali, wakiwemo mafursi, mabarbara, maqibti, waturuki na wakaazi wa Ulaya Mashariki, na kuwatumikia wote kwa uadilifu na insafu.

 

 

Advertisements

One response to “Hizbu ut- Tahrir watathmini matokeo ya mitihani

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s