Serikali kuchunguza ukosefu wa mafuta

Kaimu Waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini akiongea na waandishi wa habari katika wizara ya fedha

SAKATA la kuwapo kwa uhaba wa mafuta katika Mji wa Zanzibar, limeishtua serikali na imetangaza kuendesha uchunguzi ili kubaini tatizo hilo limetokeaje kwa vile haliko katika mazingira ya kawaida. Mji wa Zanzibar kwa kipindi cha wiki mbili sasa ulikumbwa na tatizo la uhaba wa mafuta aina ya petroli na kusababishwa bidhaa hiyo kuuzwa kwa shilingi 6000 kutoka shilingi 2000 kwa lita moja.

Hali hiyo ilisababisha wananchi wengi kupatwa na wakati mgumu wa kupata huduma hiyo, kwa kulazimika kuinunua bidhaa hiyo kwa njia ya magendo baada ya baadhi ya watu kutembeza biashara hiyo ikiwa katika vidumu, huku vituo vya kuuza mafuta kuonekana kuwepo misongomano ya watu.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Kaimu Waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame, alisema wameamua kuanzisha uchunguzi huo kutokana na kilichotokea kutokuwa katika hali ya kawaida.

Alisema uchunguzi huo wanalazimika kuufanya kutokana na uhaba uliojitokeza kuwa ni mkubwa kutowahi kutokea kiasi ambacho umeathiri shughuli za uchumi wa Zanzibar na kuisababishia jamii usumbufu wa kutumia muda mwingi kusaka nishati hiyo.

“Kwa sasa serikali itakamilisha uchunguzi wake kujua sababu halisi zilizosababisha upungufu huo ili kuona kama kuna hatua za ziada zitazopaswa kuchukuliwa, likiwemo dhidi ya Makampuni ya uingizaji wa mafuta ambayo yana dhima maalum kwa mujibu wa sheriaAlisema Waziri huyo.

Sambamba na hatua hizo Waziri huyo alisema serikali pia italiangalia suala la kupata njia mbadala na za muda mrefu za kulimaliza kabisa tatizo hilo ili kuweza kuleta manufaa kwa nchi.

Alisema serikali katika kulifanyia kazi suala hilo tayari imeshakutana na wadau wa sekta ya uuzaji na usambazaji wa nishati hapa nchini na kusikiliza madai yao juu ya kuwapo kwa hali hiyo.

Waziri huyo, alisema katika vikao hivyo kumejionesha kuwapo kwa mkanganyiko kati ya wafanyabiashara na mamlaka iliyopewa kazi ya kusambaza mafuta nchini badala ya kuondolewa kwa utaratibu wa kuzipa uwezo kampuni za kuuza mafuta kuingiza bidhaa hiyo kwa kutumia usafiri wao wenyewe.

Alisema utaratibu wa sasa unayataka makampuni ya mafuta ya Tanzania, kununua bidhaa hiyo kwa wakala mmoja aliyepewa kazi ya kusambaza mafuta Tanzania bara, jambo ambalo huyataka makampuni mengine kulazimika kukunua nishati hiyo kutoka kwao.

Kutokana na hali hiyo, Waziri huyo, alisema wafanyabishara wa Zanzibar na Wasambazaji wa mafuta hayo chini ya makampuni matatu likiwemo la Zanzibar Petrolium, United Petrolium na Gapco nayo yamekumbwa na utaratibu huo ambapo huwalazimu kununu bidhaa hiyo Tanzania bara.

“Tatizo la msingi kuwa upatikanaji wa mafuta hayo, wengi walikuwa wanategemea kuyanunua kutoka Tanzania Bara, ambako sasa, serikali ya Jamhuri ya Muungano imeanzisha utaratibu wa mafuta yote kuingizwa na kampuni moja tu nchini ambayo baadae huyauza makampuni mengine yenye vituo” Alisema Waziri huyo.

Akiendelea alisema kutokana na hali hiyo Waziri huyo alidai kuwa makampuni hayo yamelalamikia utaratibu huyo kwa kudai kuwa wanaathirika kutokana na kutegemea makampuni kuagiza mafuta yake.

Sababu nyengine ambayo Waziri huyo anaitaja juu ya sakata hilo ni kuibaini kuwapo marufuku ya serikali inayoyakataza makampuni ya kusambaza mafuta kuacha mchezo wa kuuziana mafuta baharini na kuhaulisha kutoka meli moja kwenda nyengine.

Alisema serikali imepiga marufuku juu ya uuzaji wa nishati ya mafuta kwa mtindo huo kutokana na kuweza kuhatarisha usalama huku taarifa za kiupelelezi zikionesha mfumo huo wanaoutumia wafanya biashara hiyo kuwa ni moja ya chanzo kikuu cha kuwapo kwa tatizo la magendo ya mafuta.

Alisema taarifa hizo zimeonesha suala la magendo ya mafuta hadi kufikia Febuari 24, mwaka huu kuna lita 80,783 za aina tofauti za mafuta zimeshakamatwa wakati zikiingizwa kwa magendo kwa kutumia madumu ya lita 20 na mapipa.

“Serikali inaendelea kufuatilia kwa undani zaidi iwapo sababu hizi zilizotajwa ndio pekee zilizosababisha uchelewaji wa kuingizwa kwa mafuta ambao unasababisha hali iliyojitokeza na usumbufu kwa wananchi” Alisema Waziri huyo.

Alieleza kuwa lengo la serikali kufuatilia suala hilo ni kuweza kupata suluhu ya kudumu itayoweza kuliondoa tatizo hilo ambalo limeonekana kujirejea katika miaka ya hivi karibuni.

Kuhusu madai juu ya serikali kudaiwa kushindwa kuchukua hatua ya kurudisha huduma hiyo kwa haraka Waziri huyo alisema sio kweli kwani biashara ya mafuta haiku mikononi mwa serikali.

Hata hivyo alisema serikali baada ya kubaini kuwapo kwa tatizo hilo ilifanya mazungumzo na Makampuni ya mafuta ili kuweza kupata ufumbuzi ikiwa pamoja na kuyasaidia makampuni hayo kupendelewa kupewa nafasi kupata nishati hiyo.

Akifafanua kauli hiyo Waziri huyo, alisema Makampuni ya Zanzibar yalipangiwa kupewa mafuta yakiwa ni ya tano katika foleni za makampuni ya Tanzania bara, lakini baadaSerikali ya Zanzibar kuzungumza na serikali ya Muungano, waliweza kupewa upendeleo maalum kupata huduma hiyo.

Hatua nyengine akiitaja Waziri huyo kuchukuliwa na serikali alisema ni pamoja na kufanya ziara katika eneo la kuhifadhia mafuta Mtoni Depot na vituo mbali mbali ambapo Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi alizungumza na Watendaji wa Makampuni hayo.

Kutokana na ziara hiyo Waziri huyo alisema ndio iliyochangia kuanza kurudi hali ya kawaida katika soko la jamii bidhaa hiyo, lakini hata hivyo, tayari kumekuwa na taarifa za kutoonekana na mafuta ya aina ya dizeli.

Akifafanua zaidi alisema hivi sasa mafuta aina ya petroli yalioingizwa nchini na kampuni ya United Petroleum ni tani 1,102 ambayo ni sawa na lita 1,451,000 kiwango ambacho kinatosha kwa mahitaji ya watu wa Zanzibar kwa kipindi cha wiki tatu ambacho kitawezesha kutoa muda wa kuingizwa mafuta mengine.

Kutokana na hali hiyo Waziri huyo alisema serikali inatoa pole kwa wananchi wote waliopata usumbufu kutokana na kukosekana kwa huduma hiyo jambo ambalo limeweza kudumisha amani ya nchi.

Alisema wananchi wanastahiki kupewa pongezi kwa kuweza kudumisha amani ya nchi huku wakifanya shughuli zao kama kawaida kwa vile hakuna aliyesitisha utoaji wa huduma na uzalishaji mali.

Wakati waziri huyo akitoa tamko hilo baadhi ya vituo vya kuuzia mafuta hayo hadi mchana wa jana baadi yake vilionekana kuwa shwari huku vyengine vikiwa na msongomano kutokana na tatizo hilo kurukia katika mafuta ya dizeli.

Na Mwantanga Ame

Advertisements

2 responses to “Serikali kuchunguza ukosefu wa mafuta

  1. WAZANZIBAR HATUUTAKI MUUNGANO NA MAKAFIRI WA TANGANYIKA. Znz bila ya kupata UHURU kutoka kwa wakoloni wa TANGANYIKA basi znz haiwezi kuendelea milele.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s