Mchele wa mapembe na bei iumizayo Z’bar

Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein akifuatana na Waziri wa Fedha,Uchumi na Maendeleo Omar Yussuf Mzee na Waziri wa kilimo na Maliasili Mansour Yusuf Himid,alipotembelea Bonde la Mpunga la Mziwanda,Wilaya ya Micheweni,Mkoa wa Kaskazini Pemba, akiwa katika ziara ya kutembelea Wilaya hiyo na kuona mambo mbali mbali ya kimaendeleo

HISIA za wananchi wa Zanzibar hazitofautiani sana na watu wa jamii nyinginezo, mara tu utajapo bei za vyakula. Lakini unapotaja bei ya mchele, sukari na unga wa ngano, ujue unagusa nyongo zao. Bei za bidhaa hizo kwao ni siasa kuu inayofanana na pale wanaposikia huduma ya maji, elimu na tiba.

Zaidi ya asilimia 90 ya watu Unguja na Pemba wanaamini katika kula wali kama chakula chao kikuu. Vyakula vingine kwao ni nyongeza tu.

Katika takwimu kama hii, ni dhahiri kupanda holela kwa bei za bidhaa hizi, ni siasa ingawa hapajawahi kutokea vurugu kwenye nyanja hii. Ni tofauti na ilivyowahi kutokea Zambia miaka ya 1990 serikali ilipopandisha bei ya unga wa sembe. Nchi ilitikisika kwa ghasia. Utamaduni wa Wazambia ni kula ugali tu, vyakula vingine ni nyongeza.

Bali sasa hali inakuwa ngumu kwa Wazanzibari. Kula wali inakuwa vigumu. Bei ya mchele imekuwa ikipanda sana kiasi cha watu kuanza kuzoea utamaduni mgeni – kula ugali.

Wazanzibari wanaokula ugali kama moja ya vyakula muhimu kwao, zaidi ni waliozoea kusafiri upande mwingine wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – kule ambako wanakuita Mrima au Bara au Tanganyika .

Mchele unasarifiwa kwa namna mbalimbali kimapishi; lakini chakula maarufu kinachopikwa kutokana nao ni wali. Mara chache pilau na biriani.

Mapenzi ya vyakula hivi kwa familia za Kizanzibari hayapimiki hata kwa kipimo gani. Ni makubwa, makubwa, makubwa.

Kwa sababu hiyo, bei ya mchele ni jambo kubwa kwao; jambo kubwa kwa maisha yao ya kila siku na naona bei ya mchele kwa Wazanzibari ni siasa.

Ukweli, katika miaka ya karibuni, hili limekuwa likijadiliwa sana . Mjadala umekua kwa sababu mbali na bei kupanda kwa kasi, watu wamebaini mchele wanaolazimika kuununua kwa fedha nyingi, ni ule ambao ubora wake unatiliwa shaka.

Mara nyingi wanauchukulia kama usiofaa kwa matumizi ya binadamu, pamoja na kuwa ni mara chache mno umetajwa kitaalamu katika sura hiyo baada ya kuchunguzwa katika maabara.

Mchele huu ulianza kuingizwa Zanzibar katika miaka ya mwisho ya 1990 na kuwa mchele mgeni machoni mwa watu waliozoea kula wali wenye harufu nzuri uliokuwa ukiletwa kwa gunia la uzito wa kilo 100; badala ya kilo 50 siku hizi.

Mchele wa uzito wa kilo 100 ulikuwa ukiagizwa na BIZANJE, shirika la serikali lililokuwa maarufu kwani likiagiza pia sukari, unga wa ngano na bidhaa nyingine zisizo za chakula.

Ukweli, mchele huu ni wa kiwango duni. Wapishi wanasema huwa hautoi wali mtamu kama ilivyokuwa ule uliozoeleka ukiingizwa na BIZANJE kutoka Thailand .

Mara kadhaa ubora wa mchele wa mapembe umepata kutiliwa shaka. Mara chache Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, imepata kuutangaza hivyo, ikiwemo tangazo lao lilipoleta tafrani baada ya waagiziaji kuvunja makufuli ya ghala ulipohifadhiwa kwa ajili ya kuharibiwa.

Wenyewe walifanikiwa kuutorosha na kuingizwa sokoni kisiwani Pemba na Tanga. Kashfa hii haikuwashikisha adabu watoroshaji wala viongozi wakuu wa wizara husika. Watumishi wa kati, ndio waliosokomezwa.

Imekuwa ikielezwa mitaani mara nyingi kuwa mchele wa mapembe unakutwa katika maghala nchini Pakistan au India ukisubiri kuharibiwa au kuuzwa kwa ajili ya kutengeneza chakula cha mifugo.

Lakini ndio mchele unaoingizwa kwa wingi miaka hii na kuuzwa kwa maelfu ya familia. Basi hata huu bei yake imekuwa kali kuliko matarajio ya wananchi.

Umetokea mgogoro baada ya kuingia kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). Katika kujaribu kutimiza matumaini ya wananchi ya unafuu wa gharama za maisha, serikali iliahidi kuangalia upya bei.

Haraka ikatoa msamaha wa kodi ya forodha kwa mchele, pamoja na sukari na unga wa ngano. Msamaha wa kwanza uliofuta kodi yote, ulitolewa Novemba 2010.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayesimamia Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee alisema katika barua yake ya tangazo la msamaha kuwa umelenga kuleta unafuu wa bei kwa walaji.

Katika tangazo lake, Waziri Mzee alisema mamlaka ya kusimamia utekelezaji wa uamuzi huo yameachiwa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko.

Hii inasimamiwa na Nassor Ahmed Mazrui, mfanyabiashara wa siku nyingi na mkandarasi wa shughuli za ujenzi. Kwa miaka mingi aliongoza jumuiya ya wafanyabiashara, wenye viwanda na kilimo Zanzibar (ZCCIA).

Alipoona sera zake zimegonga mwamba kutokana na ukaidi wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku wakimkwamisha kwa makusudi kuitumia sekta ya biashara kukuza sekta binafsi na kuipa nguvu serikali kuinua pato la taifa la nchi, akatoka.

Akaingia katika siasa, mchezo aliokuwa akipenda kuwaambia wasiri wake, wakiwemo waandishi wa habari weledi, kuwa aliingizwa kwa lazima kwa sababu walikuwa wakimsingizia kufadhili chinichini upinzani.

Mazrui ni kiongozi katika Chama cha Wananchi (CUF) na ni mwakilishi wa kuchaguliwa jimbo la Mtoni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar .

Kukabidhiwa dhamana ya kuongoza wizara inayohusu biashara ni jambo zuri na ilitarajiwa mambo mengi yatabadilika. Watu waliamini sekta ya biashara na viwanda itakua.

Wakati fulani alisikika akisema hadharani “Sasa mapembe basi.” Labda alimaanisha kuwa hataruhusu Wazanzibari kula mchele wa mapembe.

Mwaka mmoja sasa tangu serikali iundwe, mchele wa mapembe umeendelea kuingizwa kwa wingi nchini. Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia zaidi ya 80 ya mchele unaoingizwa Zanzibar ni huu.

Asilimia ilobaki ni mchele unaotoka Tanzania Bara na ule wa hadhi ya juu ambao kwa watu wa kipato cha kawaida, hasa wale masikini, huusikia tu au kuuona madukani au kwa jirani zao.

Kilo moja ya mchele wa hadhi hii huuzwa kwa hadi Sh. 4,000 wakati ule wa mapembe unauzwa kwa Sh. 1,400.

Nikasimuliwa kwamba ndani ya Baraza la Wawakilishi, Waziri Mazrui aliwahi kusema kuwa bei ya mchele wa mapembe ni Sh. 1,200; lakini tangazo lake hilo likaibua mjadala mrefu.

Tangazo hilo lilisukuma wananchi kufikiria upya ile ahadi aliyoitamka kabla – kwamba “sasa mchele wa mapembe bye bye.” Siku hizi watu wanasema hivi hivi, “yule Waziri alikusudia kuwa mapembe basi nyumbani kwake kwa vile ni waziri sasa.”

Mimi siamini hili. Ninataka kuamini kwa udhati wa moyo wake Waziri Mazrui alitaka kupeleka ujumbe kwa umma kuwa atahakikisha unaingizwa mchele wa hadhi na siyo wa mapembe. Kama ahadi hii haijatimia, hili linabaki kuwa swali kwake tutakapokutana.

Uchunguzi wangu umeonyesha wafanyabiashara wamehalifu makubaliano. Najiuliza wamepata wapi jeuri ya kuikaidi serikali, tena hii mpya ya umoja wa kitaifa?

Inakuaje serikali itoe msamaha wa kodi kwa bidhaa hizi, halafu wafanyabiashara wakaziuza kwa bei isiyotarajiwa? Hili haliwezi kufanyika bila kuhusisha kiongozi wa juu.

Advertisements

2 responses to “Mchele wa mapembe na bei iumizayo Z’bar

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s