Kilio cha Wazanzibari kisipuuzwe


Leo kumfanyika mjadala wa wazi wa wadau wote wa elimu wakitathmini matokeo ya mitihani ya kidato cha nne ambayo yameleta masikitiko makubwa miongoni mwa wazanzibari. Katika mjadala huo wa wazi umewashirikisha walimu, wazazi, na wanafunzi ambao umetayarishwa na Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA) kwa kushirikiana na wadau wa elimu Zanzibar umejadili kwa kina changamoto zilizojitokeza katika matokeo hayo ya mitihani ambapo wanafunzi 3303 wamefutiwa matokeo yao na Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania (NECTA). Gazeti la Anuur linalotoka kila Ijumaa limenadika kadhia ya mitihani hiyo na kusisitiza kwamba kilicho cha wazanzibari kisipuuzwe. 

Kuna jambo kubwa

Katoliki hawajasema

 

*Wapo wangapi Baraza la Mitihani?

*Kwa nini wanampa Nyerere ‘utakatifu’?

*Kilio cha Wazanzibari kisipuuzwe

 

 

Na Omar Msangi

Mwaka 1965 aliyekuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu-Tanzania Episcopal Conference (TEC), Father Robinson alitoa taarifa akikiri kwamba shule za Kanisa Katoliki zilikuwa zikitegemea fedha kutoka serikalini kwa asilimia 100. Kwa sababu hiyo akasema, kama serikali itasitisha utaratibu wake wa kuchota fedha kutoka Hazina ya kodi za ‘Watanganyika’ na kuwapa Wakatoliki, basi itabidi shule hizo zifungwe.

Kabla ya hapo tunaambiwa kuwa serikali ilikuwa ikizipa shule za Kanisa ruzuku iliyofikia asilimia 66% ya bajeti ya shule hizo. Ruzuku hiyo ikitoka katika Hazina ya taifa inayochangiwa kwa kodi za Waislamu, Wakristo na watu wa dini nyingine.

Hivyo ndivyo mambo yalivyokuwa. Huo ndio utaratibu wa mambo ulivyo katika nchi hii tunayotamba kwamba haina ubaguzi wala upendeleo wa kidini wala wa kikabila.

Hivi sasa Kanisa Katoliki lipo katika shamrashamra likitamba kuwa katika zile shule kumi bora katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yaliyotangazwa hivi karibuni, basi saba ni za Katoliki.

Katika kumi bora kidato cha nne, Wakatoliki wazoa 7”, limeandika gazeti la Tumaini Letu linalotolewa na Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

Katika idadi ya shule zilizoshika nafasi ya kumi bora kitaifa…shule saba zilizoshika nafasi hiyo zinaendeshwa na kumilikiwa na Kanisa Katoliki.”

Limefafanua gazeti hilo namba 00401 la Ijumaa Februari 10-16, 2012.

Tumaini Letu likazitaja shule hizo kuwa ni St. Francis iliyoshika nafasi ya kwanza, St. Joseph Millenium nafasi ya tatu, wakati shule ya wasichana ya Marian, ikishika nafasi ya nne.

Shule nyingine ni Seminari ya Don Bosco iliyoshika nafasi ya tano, Kasita seminari nafasi ya sita, St. Mary’s Mazinde Juu nafasi ya saba na shule ya Canosa iliyoshika nafasi ya nane.

Shule nyingine tatu katika kumi bora ni Feza Boys iliyoshika nafasi ya pili, Mzumbe nafasi ya tisa na shule ya sekondari Kibaha iliyoshika nafasi ya kumi.

Pamoja na kutupa taarifa hii kwamba katika zile shule kumi bora, saba ni za Katoliki, zipo taarifa nyingine muhimu na nyeti zaidi ambazo Wakatoliki hawajasema. Moja ni idadi yao katika Baraza la Mitihani la Taifa (Tanzania Examination Council). Na pili, idadi yao katika ile jumla ya Maofisa Elimu wa Wilaya na Mikoa (DEOs/REOs).

Katika shule kumi bora kwa kufaulisha, za Wakatoliki ni saba. Je, wakatoliki hawa katika Baraza la Mitihani wapo wangapi? Lakini si idadi yao tu katika Baraza, muhimu zaidi ni je, katika Idara na Vitengo muhimu na nyeti kwa shughuli za utungaji mitihani, usahihishaji, utoaji gredi na kuweka takwimu, Wakristo ni wangapi?

Katika kipindi hicho ambacho Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu akisema kuwa serikali ilikuwa ikilipa gharama zote za kuendesha shule za Kanisa Katoliki, kulikuwa na mgogoro katika wilaya ya Pare (sasa Mwanga) ambapo Wazee wa Kiislamu walitangaza kugoma kulipa kodi kwa kuona kuwa serikali ilikuwa inachukua kodi zao na kuwapa Wakristo kujenga na kuendesha shule, lakini nao walipoomba (kama ndio utaraibu, wakanyimwa). Lakini zaidi walikuwa wakizuiwa kuanzisha shule na kulazimishwa kupeleka watoto wao katika shule ya kanisa. Katika mgogoro huo ilibidi Mwalimu Nyerere kumtumwa (Marehemu) Rashid Mfaume Kawawa kuusuluhisha ambapo kikao kilifanyika Toloha. Wazee wanasimulia kuwa pamoja na kuwa waliandaa chakula kumkirimu mgeni, lakini walikubaliana kuwa kama Kawawa hatakuwa amekuja na jibu la kuwaridhisha, hawampi chakula chao.

Tunajua kuwa kwa maadili ya utumishi wa serikali, mtumishi anatakiwa kuwahudumia watu wote bila ya ubaguzi wala upendeleo. Lakini katika utaraibu huu (usio rasmi) aliotuambia Father Robinson, imani ya wananchi kuwa maadili ya utumishi wa umma yanafuatwa wanapokaa Wakatoliki/Wakristo watupu katika nafasi nyeti na muhimu kama Baraza la Mitihani, itatoka wapi?

Katika kitabu ‘Muslims and the State in Tanzania’ kimetajwa kisa cha Waislamu wa Mtwara mjini kuomba eneo la kujenga Msikiti katika barabara (mtaa) maarufu kuliko zote mjini hapo, TANU Road. Ni kando kando mwa barabara hii ambamo zipo ofisi za kiserikali na taasisi mbalimba muhimu za kijamii. Pamoja na kuwa inakisiwa kuwa Waislamu katika mkoa wa Mtwara ni zaidi ya asilimia 85, lakini kulikuwa hakuna hata Msikiti mmoja katika barabara hiyo, wakati kuna makanisa matano (wakati huo 1997) ambayo ni: Kanisa la Katoliki Magomeni, Kanisa la KKKT, Anglikana, Sabato na Catholic Parish Church.

Katika miaka ya nyuma, baina ya kanisa la KKKT na Anglikana, karibu na uwanja wa Mashujaa, palikuwa na eneo ambalo halijatumika lililokuwa likimilikiwa na Wizara ya Elimu na Utamaduni. Mwaka 1995 Wizara ya Elimu kupitia gazeti la serikali ilitangaza kuachia sehemu kubwa ya eneo hilo ili ipangiwe matumizi mengine.

Ni wakati huo Waislamu wa Mtwanra wakaona watumie fursa hiyo angalau nao wawe na Msikiti katika eneo hilo la mjini. Wakaandika barua rasmi tarehe 11 Septemba, 1997 kwa Manispaa kuomba eneo hilo.

Ilipofika tarehe 8 Desemba, 1997, Mipango Miji waliwaandikia barua Waislamu wakiwafahamisha kuwa maombi yao yamekubaliwa. Hiyo ilikuwa barua kumbukumbu namba MM/TC/L.VII/12/89.

Taarifa zinafahamisha kuwa viongozi wa makanisa walipojua kwamba Mipango Miji wameidhinisha Waislamu kupitia taasisi ya MIDECE (Mtwara Islamic Development Centre) wapewe eneo hilo, walikutana wakajadili na kisha kuwaambia waumini wao kuwa Waislamu wanahangaika bure, Wizara ya Ardhi haitawapa eneo hilo.

Haya ndiyo yaliyotamkwa pia na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Nsa Kaisi. Mkuu huyo wa Mkoa alimwambia Sheikh, Mzee Nasuma ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bakwata kwamba atahakikisha Waislamu hawapati eneo hilo. Alisema, labda afe au ahamishwe. Lakini muda wa kuwa yupo hai na ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Waislamu hawapati eneo hilo.

Kilichofuatia hapo ni mlolongo mrefu ambao makala hii haitoshelezi kuyaeleza yote. Lakini moja ya mambo yaliyokuwa yakifanyika, ni pamoja na watu wa Ardhi Mkoa kushirikiana na viongozi wa makanisa kujadili namna ya kukwamisha maombi ya Waislamu. Mfano kwa mara ya kwanza Waislamu walipowasilisha maombi yao kwa Ofisi ya Ardhi, walijibiwa kwa kifupi kuwa eneo hilo halikutengwa kwa ajili ya matumizi ya shughuli za ibada. Waislamu wakaridhika wakaondoka. Huku nyuma baadhi ya watumishi wa ofisi hiyo wakawasiliana na Kanisa la Assemblies of God wakaleta maombi harakaharaka na wakapewa eneo hilo walilokataliwa Waislamu kuwa sio kwa ajili ya Msikiti wala Kanisa. Hata hivyo baadae maofisa hao wa Ardhi walilazimika kuandika barua ya kuwasimamisha Assemblies of God kujenga kanisa katika eneo hilo baada ya Waislamu kuja juu.

Mfano wa pili, katika kuhangaikia suala hili, Waislamu walikuwa wakiwasiliana na Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) wakati huo akiwa Bwa. Mwakatobe. Ambacho Waislamu walikuja kujua baadae ni kuwa wakati Mwakatobe kila siku akiwapa kauli nzuri kwamba atawasaidia, wakiondoka hukutana na viongozi wa kanisa na kuwapa taarifa na kupanga mikakati ya pamoja. Moja ya mikakati aliyowapa ya kuwakwamisha Waislamu ni kuwa waende Dar es Salaam wakamwone Waziri wa Ardhi, wakati ule Gideon Cheyo wamwambie kuwa maombi yao ya kupewa eneo la kujenga kanisa yamekataliwa wakati ya Waislamu yamekubaliwa.

Viongozi wa makanisa Mtwara walifanya kama walivyoelekezwa na RAS wakaenda Dar es Salaam wakamwona Waziri wa Ardhi akawaahidi kwamba atahakikisha kuwa Waislamu hawapati eneo hilo. Lakini Waziri akawaelekeza waende na Wizara ya Elimu na Utamaduni wakamwone Dr. Ndagala ili naye asaidie katika kukwamisha kwa vile eneo linaloombwa awali lilikuwa likimilikiwa na Wizara ya Elimu. Viongozi wa makanisa walimwona Dr. Ndagala naye akaahidi kukwamisha maombi ya Waislamu.

Lakini Dr. V. K. Ndagala akawaambia kwamba, haisaidii sana kuwakwamisha tu Waislamu, yeye angependa baada ya kuwakwamisha Waislamu, basi Wakristo wapewe eneo hilo. Kwa hiyo akawaelekeza wakamwone Afisa mmoja Ikulu ili naye atumie msuli wa Ikulu kuhakikisha kuwa Wakristo wanapata eneo hilo. Taarifa zinafahamisha kuwa Afisa huyo wa Ikulu, aliahidi kutimiza wajibu wake kwa Kanisa. Kuwakwamisha Waislamu na kuwapendelea Wakristo wenzake.

Labda niongeze mfano mmoja, baada ya RAS, Bwana Mwakatobe kukamilisha kuweka mtandao wa kuwakwamisha Waislamu, aliandika barua na kuituma kwa EMS, kuwasilisha maombi ya Waislamu Wizara ya Ardhi, Dar es Salaam. Waislamu walimteua Sheikh Marijani kufuatilia majibu ya barua hiyo Wizarani. Hata hivyo, kila alivyokuwa akifika ofisi inayohusika aliambiwa kuwa hakuna barua iliyopokelewa kwa EMS kutoka Mtwara. Marijani aliamua kwenda ofisi za EMS (Expedited Mail Service) Dar es Salaam ambapo alionyeshwa kuwa barua yao ilichukuliwa na Afisa wa Wizara ya Ardhi anayeitwa Bwana Magambo ambaye ofisi yake ipo ghorofa ya 9 katika jumba la Wizara. Bahati mbaya siku hiyo Magambo hakuwepo kazini. Watu wengine ikabidi wapekuwe na kukuta barua hiyo ikiwa imewekwa katika lundo la makaratasi ya zamani (yanayongojea kuchomwa moto au kufungwa na kuwekwa stoo.)

Hadithi ya kisa hiki bado ni ndefu, lakini tutosheke na kipande hiki. Ila tu niseme kuwa kimiujiza, kwa nguvu za Mwenyezi Mungu, Waislamu walipata eneo lile.

Kama huu ndio mtandao wa Wakristo katika Wizara ya Ardhi, ofisi ya Wakuu wa Mikoa mpaka Ikulu, swali ni je, mtandao kama huu haupo katika Baraza la Mitihani? Ndio maana nikasema, kama ambavyo Kanisa Katoliki limetufahamisha kuwa wanashikilia asilimia 70 katika zile shule bora, ni muhimu pia wakatufahamisha katika Baraza la Mitihani wapo kwa asilimia ngapi?

Kama mtandao wa Wakristo unaweza kujipanga kutoka wilayani, Mkoa, Wizara mpaka Ikulu kiasi cha Mkuu wa Mkoa na Waziri kutamba kuwa atahakikisha kuwa atawakwamisha Waislamu kupata ardhi ya kujenga Msikiti, kwa nini kusiwe na wasiwasi kuwa katika Baraza la Mitihani kunaweza kuwa na mtandao ambao unahakikisha kuwa shule na watoto wa Kikristo ndio wanaoongoza kila mwaka?

Hapa lazima tujiulize, ile kada ya uongozi wa Baraza, Waratibu wa Masomo, Maofisa wa Elimu Wilaya/Mkoa na watu wote muhimu wanaohusika na mitihani pamoja na kuchagua wanafunzi wa kuingia kidato cha kwanza, tano na vyuo mbalimbali, Wakristo wapo wangapi na watu wa dini nyingine wangapi?

Katika hali kama hii ya kisa cha Mtwara, wasio kuwa Wakristo watakuwa vipi na imani na Baraza la Mitihani iwapo itaonekana kuwa nafasi zote nyeti zimeshikwa na Wakristo?

Baada ya kuwa walikuwa na Mkuu wa Mkoa aliyeapa kuwa muda wa kuwa yupo hai na ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, atahakikisha kuwa Waislamu hawapati ardhi TANU Road; sasa Mtwara wamepelekewa Mkuu wa Mkoa ambaye mwaka jana alipewa Nishani ya mtakatifu Gregory Daraja la kiraia kwa utumishi uliotukuka kwa Kanisa Katoliki Mkoa wa Kigoma. Nishani hiyo alipewa na Papa Benedikto wa 16. Na kazi yake imeanza kuonekana katika suala la kufukuzwa kwa wanafunzi wa Kiislamu wa kidato cha sita Ndanda.

Itakumbukwa kuwa Wizara ya Elimu ilitoa uamuzi kuwa wanafunzi Waislamu waliofukuzwa wakilalamika kuwa walikuwa wakinyanyaswa na Mkuu wa Shule, warudishwe shule na wafanye mtihani.

Hata hivyo baadae Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Bwana Joseph Simbakalia anadaiwa kutoa tamko mbadala akidai kuwa msimamo wa kuwafukuza wanafunzi hao uko pale pale na kwamba, vijana 15 kati yao wataruhusiwa tu kuingia katika chumba cha mtihani kama watahiniwa wa nje ya shule (private candidate). 

Aidha, Joseph Simbakalia alidaiwa kusema kuwa wanafunzi hao 15 watalazimika kwanza kukubali mashariti watakayopewa kabla ya kuingia katika chumba cha mtihani.

 

Katika hali hii ya kuwa na watumishi wa serikali ambao wanafikia kiwango cha hali ya juu cha kutumikia makanisa yao mpaka kupewa tuzo na wakuu wa dini zao, je, bado wasio kuwa Wakristo waamini kuwa watu hawa watawatumikia bila ya ubaguzi na upendeleo?

Hivi sasa Kanisa Katoliki lipo katika mchakato wa kumtangaza Mwalimu Nyerere kuwa ni mtakatifu. Hapana shaka hapewi heshma hii kutokana na jinsi alivyowatumikia Watanzania mpaka kuwafikisha mahali wanapanga foleni kutwa wakisubiri robo kilo ya unga wa njano au muhogo. Hawakumpa nishani hiyo kwa kuifikisha nchi hii ambapo kila bidhaa muhimu ikawa haipo, na rushwa kutawala, usemi “mnyonge hana haki” ukatawala kama alivyosema Padiri John Sivalon. ‘Utakatifu’ anapewa kutokana na jinsi alivyotekeleza ahadi yake ya kulipa kanisa katoliki “a better chance”. Na ni kutokana na “better chance” hiyo, leo Wakatoliki wanatamba.

Swali ni je, hali hii mpaka lini? Sifa gani ambazo zinahitajika kushika nafasi ya uongozi wa Baraza la Mitihani, ambazo watu wengine hawana ila Wakristo tu?

Wapo viongozi watendaji wa ngazi za juu kama Katibu Mtendaji wa Baraza na wasaidizi wake, wapo wakuu wa vitengo muhimu, wapo waratibu wa masomo n.k, je, Wakristo wangapi na Waislamu wangapi?

Kama nafasi hizo watakuwa wamehodhi Wakristo, tufahamishwe, sifa gani zinahitajika ambazo Waislamu hawana mpaka serikali ilazimike kuweka Wakristo watupu?

Malalamiko ya Wazanzibari yasipuuzwe

Wakati Wakatoliki wakisherehekea kwa shule zao kuchukua nafasi 7 katika zile kumi bora, Zanzibar ni kilio. Wanasiasa, walimu, wanafunzi na jamii kwa ujumla, wanajiuliza, imekuwaje idadi kubwa ya shule na wanafunzi waliofutiwa matokeo yao iwe kutoka Zanzibar? Inakuwaje matokeo yao kila mwaka yawe mabaya?

Inawezekana kuna uzembe mkubwa unafanyika katika shule za Unguja na Pemba kiasi cha kuwafanya wanafunzi kufanya vibaya. Labda walimu hawajitumi kusomesha kwa juhudi na wanafunzi hawajali masomo. Inawezekana pia kuna udanganyifu mkubwa na ukiukwaji wa kanuni za mitihani unaofanywa na walimu na wanafunzi wa Zanzibar.

Hata hivyo, kama Mkuu wa Mkoa, anaweza kuapa kwamba atatumia madaraka yake kukwamisha maombi ya Waislamu kupata ardhi, je, hatuoni kuwa watu wanaweza kuwa na wasiwasi kuwa huenda hata katika Baraza wakawepo wakuu ambao nao wanaapa kwamba watahakikisha kuwa hakuna Mzanzibari (Muislamu) anayeongoza katika mtihani wa kidato cha nne na sita?

Kama Waziri anaweza kukutana na viongozi wa makanisa wakala njama za kuwahujumu Waislamu, kwa nini kusiwe na wasiwasi kuwa viongozi hao wa makanisa wanaweza kukutana na walioshikilia nafasi nyeti katika Baraza na kula njama za kuhujumu watoto wa Kiislamu?

Katika kadhia ya MIDECE na viongozi wa serikali mkoani Mtwara, tumeona jinsi RAS, kinyume na maadili ya utumishi wa serikali, alivyokuwa akikutana na viongozi wa makanisa. Je, mahusiano kama haya hayawezi kutumika katika Baraza la Mitihani kuhujumu wasio Wakristo?

Mtu ambaye ana chuki, upendeleo na ubaguzi dhidi ya Waislamu kama wale waliojitokeza katika mtandao wa watumishi wa serikali katika kadhia ya MIDECE, je hata ikitokea kuwa wilaya au mkoa mmoja katika mikoa ya Zanzibar umeongoza kwa kiwango cha kufaulu, atathubutu kutangaza au ‘atachakachua’?

Labda nimalizie kwa swali, katika matokeo ya mwaka 2010, mkoa gani uliongoza kwa kiwango cha ufaulu?

Baadhi ya taarifa zinasema kuwa ulikuwa Unguja. Je, mkoa huo ulitajwa?

Kama haukutajwa kwa nini wakati tunaona fahari kutaja watoto wa Kikristo na shule za Kikristo zilizoongoza?

Mwaka huu je, Mkoa gani unaongoza kwa kiwango cha kufaulu? Kwa nini ‘data’ hiyo muhimu haikutajwa hadharani wakati wa kutangaza matokeo?

Haki inatakiwa itendeke na ionekane kwamba imetendeka. Katika mazingira kama haya ya kuwa na mtandao wa akina Mwakatobe, Gideon, Dr. Ndagala, wakihodhi ofisi za serikali, itakuwa kujidanganya kudhani na kuamini kwamba hakuna hujuma wanayofanyiwa wasio wa dini ya wale waliotupa barua ya MIDECE katika kapu la taka.

 

Advertisements

8 responses to “Kilio cha Wazanzibari kisipuuzwe

  1. Mawazo yangu tuachane na utegemezi huu wa elimu kwa Tanganyika. Wakati umefika sasa aidha tuwe na Baraza letu la mitihani au kama tunaona hatuwezi basi tujiunge na mifumo mengine ya elimu ambayo ni bora zaidi na ya kisasa duniani. Mfumo huu tayari umeshaanza kuonyesha kua haufai tena. Wasiojisomea ndio wanaopasi kwa kuvuja mitihani na wale wanaofanya vizuri wanaambiwa mtihani umevuja au wamekopiana. Unaposikia pahala mitihani inavuja basi jua hapo na elimu haipo tena.

  2. Sio matokeo bali chanzo cha elim yenyewe ndio matatizo hayo mengine baadae.bila ya marekibisho hayo hamna lolote hadi kiyama

    • Mtoa mada umezungumza kweli ” joyce ndalichako ni mkatolik na tumemsikia mara nyingi hata ktk seminar akitamka yesu asifiwe hili hatuzui hadi kiama! WAZANZIBAR tusishawishike na wanasiasa kwamba muungano una faida! Sasa muda umetimu muungano na uvunjwe kila mtu nchi yake! Hatutaki wagalatiya kwetu! Muungano huu una imarisha ukristo! TU!

  3. Suluhu ya matatizo kuanda maandamano ya kuta kuvunja muungano bila ya hivyo tutaendelea kulalamika kwani hawana vichwa vizuri peke yao wasingalipitwa na wazanzibar vyuoni

  4. Hello Webmaster, I noticed that http://zanzibaryetu.wordpress.com/2012/02/17/mnakaribishwa-katika-mjadala-wa-wazi-wa-elimu/ is ranking pretty low on Google and has a low Google PageRank. Now the Google PageRank is how Google is able to see how relevant your webpage is compared to all the other webpages online, if you cannot rank high at the top of Google, then you will NOT get the traffic you need. Now usually trying to get to the top of Google costs hundreds if not thousands of dollars and very highly optimized targeted marketing campaigns that takes a team of experts months to achieve. However, we can show you how to get to the top of Google with no out of pocket expenses (free traffic), no stupid ninja tricks, no silly mind control techniques, and this will be all white hat with no blackhat software or tactics that could possibly land you on bad terms with Google and put you in the dreaded “Google Sandbox”. We’ll show you how to easily capture all the targeted traffic you need, for free, multiple ways to land fast (not months) first-page rankings in Google and other major search engines (Bing, Yahoo, Ask, etc), even show you strategies on how to earn daily commissions just try Ranking Top of Google, please check out our 5 minute video.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s