Majumuisho ya mkutano wa Redet

Wajumbe wa mkutano wa kutathimini hali ya kisiasa uliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar

Washiriki walisisitiza kwamba mijadala yote ya sasa na ijayo juu ya uimarishaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar iendeshwe kwa kuzingatia ukweli kwamba uimara wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa unategemea zaidi na uwezo wake wa kutatua kero mbalimbali za wananchi. Kero zinazopaswa kupatiwa suluhu ni pamoja na huduma za msingi za kijamii hususan afya, elimu na maji, ajira kwa vijana, mfumuko wa bei na vitambulisho vya Uzanzibari. Washiriki walishauri kwamba wanachi nao wana wajibu wao wa kushirikiana na serikali kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayoisibu jamii ya Zanzibar

MAJUMUISHO NA MAPENDEKEZO YA MKUTANO WA PILI WA HALI YA SIASA ZANZIBAR

Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam uliandaa mkutano wa pili wa hali ya siasa Zanzibar uliofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 13 Februari hadi tarehe 14 Februari 2012, kwenye ukumbi wa Hoteli ya Bwawani. Mada kuu ya mkutano huo ilikuwa ni ‘Uimarishaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Mkutano huo ulihudhuriwa na zaidi ya washiriki 200 waliowakilisha makundi mbali mbali ya kijamii na kisiasa ndani na nje ya Zanzibar.

Mkutano ulifunguliwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad ambaye aliwapongeza waandaaji na washiriki kwa ujumla kwa uamuzi wao wa busara wa kukutana kwa lengo la kujadili kwa kina na kwa umakini juu ya haja na umuhimu wa kuimarisha utendaji na ufanisi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Kabla ya hotuba ya ufunguzi, Mwenyekiti mwenza wa REDET pamoja na Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walimkaribisha mgeni rasmi na kupitia kwake kuishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa namna walivyoanza vema kusimamia misingi ya serikali ya umoja wa kitaifa tangu kuundwa kwake mwaka 2010 baada ya uchaguzi mkuu hadi sasa.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Makamu wa Kwanza wa Rais alisisitiza kwamba dhana ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar imepokelewa vizuri na wazanzibari wengi, wawekezaji na Jumuiya ya kimataifa. Mheshimiwa Maalim Hamadi alikiri kwamba zipo changamoto mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kisiasa ambazo zimekuwa zikiathiri vibaya utendaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar tangu kuanzishwa kwake. Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni uwezo mdogo wa kifedha wa serikali unaokwaza serikali kukidhi matarajio ya wananchi waliowengi; kasi ndogo ya kurekebisha kasoro na kero zilizojitokeza katika uchaguzi wa 2010 hususan katika mfumo wa uandikishaji wa wapiga kura na utoaji wa Vitambulisho vya Uzanzibari; na kuwepo kwa watu wachache wasiofurahishwa na maridhiano yaliyofikiwa nchini Zanzibar. Aliwaeleza washiriki kwamba serikali inatambua uwepo wa changamoto hizo na kwamba hatua mbalimbali za kuzitafutia ufumbuzi zimekuwa zikichukuliwa. Aliwasihi Wazanzibari kutumia barabara na kwa umakini fursa iliyopo sasa ya kutunga katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili taifa letu liendelee kuimarisha zaidi karakati za miaka hamsini ya kujenga taifa huru na linalotawaliwa kwa misingi ya utu, umoja, mshikamano, usawa na haki.

Mada zilizojadiliwa katika mkutano huo ni ; Misingi ya Kikatiba ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar; Serikali ya Umoja wa Kitaifa na Masuala ya Ushirikishwaji; Uendeshaji wa Shughuli za Baraza la Wawakilishi Zanzibar; Mhimili wa Utendaji/ Baraza la Mapinduzi Zanzibar; Udumishaji wa Imani ya Wazanzibari katika Kuimarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na Nini Kifanyike katika Kuimarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Washiriki wa Mkutano walijadili na kukubaliana yafuatayo:
1. Washiriki waliwapongeza viongozi wote wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dokta Mohammed Shein kwa kuonyesha utashi wa kisiasa na ujasiri wa kusimamia maridhiano na misingi ya uundaji na uendeshaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar. Walikiri kwamba yapo matokeo mazuri yaliyopatika katika kipindi kifupi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar. Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuimarika kwa amani na usalama; kuongezeka kwa uhuru wa vyombo vya habari; ushiriki wa AZAKI katika kudai uwajibikaji wa serikali; kuwepo kwa mshikamano wa kitaifa wakati wa majanga hasa katika kipindi cha msiba wa kitaifa uliosababishwa na ajali ya meli ya Spice Islander; kuongezeka kwa kiwango cha uvumilivu wa kisiasa miongoni mwa viongozi wa kisiasa na wafuasi wa vyama vya siasa na kupungua kwa kiasi kikubwa uhasama wa kisiasa; kuongezeka kwa kiwango cha imani ya wafadhili na wawekezaji kwa serikali ya mapinduzi Zanzibar. Serikali ilishauriwa kwamba iendelea kuweka mazingira muafaka ya kisiasa ili kupanua wigo wa ushiriki wa wananchi katika masula ya uendeshaji na uimarishaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Swala la kuyapa fursa sawa makundi ya kijamii yaliyoachwa nyuma hususan akina mama na watu wenye ulemavu lilijadiliwa kwa kina na wajumbe wanaishauri serikali kulipa uzito unaostahili.

2. Washiriki walikubaliana kwamba Mgawanyo wa madaraka baina ya mihimili mikuu ya serikali na ushiriki wa wananchi katika masuala ya siasa ni kati ya mambo muhimu ya kuzingatiwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Walishauri kwamba katiba na sheria zilizopo viangaliwe upya ili kuwepo kwa ushiriki mkubwa wa wanachi na mgawanyo mzuri wa madaraka. Walisisitiza kwamba kuwepo kwa mgawanyo mzuri wa madaraka, uongozi unaoheshimu utawala wa kikatiba na ushiriki mkubwa wa wanachi kupitia vyombo vyao vya ushiriki vitaondoa hofu ya uwezekano wa kuyumba kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

3. Washiriki walikubaliana kwamba kuna haja na umuhimu wa kuwa na upinzani imara na makini ndani ya Baraza la Wawakilishi na ndani ya jamii ya Zanzibar kwa ujumla ili wananchi wapate fursa ya kuishauri na kuidhibiti barabara Serikali yao ya Umoja wa Kitaifa.Wajumbe walishauri kwamba ili mfumo wa vyama vingi uweze kufanya kazi kwa mujibu wa matarajio ya wanachi wengi, wadau mbalimbali wa siasa Zanzibar wanapaswa kuendelea kuunga mkono juhudi zilizopo za kuimarisha vyombo na taasisi zote za kidemokrasia. Nguvu na juhudi zaidi za kuimarisha utendaji wa vyombo vya habari, Asasi za Kiraia, vyama vya siasa, serikali za mitaa, Baraza la Wawakilishi, Bunge na Mahakama vinatakiwa kuongezwa na serikali inatakiwa kuunga mkono wadau wote wenye nia na uwezo wa kutoa michango katika eneo hili

4. Washiriki walisisitiza kwamba mijadala yote ya sasa na ijayo juu ya uimarishaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar iendeshwe kwa kuzingatia ukweli kwamba uimara wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa unategemea zaidi na uwezo wake wa kutatua kero mbalimbali za wananchi. Kero zinazopaswa kupatiwa suluhu ni pamoja na huduma za msingi za kijamii hususan afya, elimu na maji, ajira kwa vijana, mfumuko wa bei na vitambulisho vya Uzanzibari. Washiriki walishauri kwamba wanachi nao wana wajibu wao wa kushirikiana na serikali kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayoisibu jamii ya Zanzibar

5. Washiriki wa Mkutano walikubaliana kwamba fursa iliyopo sasa ya kutunga katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni ya kihistoria na inatakiwa kutumiwa vizuri na watanzania wote ili hatimaye taifa liweze kujenga mwafaka kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo masuala yanayohusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao umedumu kwa takriban miaka hamsini. Wajumbe walikubaliana pia kwamba pamoja na kuwepo na harakati za kuunda katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ipo haja pia ya Wazanzibari kuanza kufikiria namna ya kuboresha zaidi katiba ya Zanzibar. Ilisisitizwa pia kwamba wanachi ndiyo wenye mamlaka ya mwisho kuhusu uendeshaji wa nchi. Hivyo serikali zote (ya Muungano na ya Mapinduzi Zanzibar) zimetakiwa kuweka mazingira mwafaka ya kisiasa ili raia wote watumie haki na wajibu wao kuamua bila woga wala jazba juu ya aina ya katiba waitakayo.

6. Wajumbe walikubaliana kwamba utekelezaji wa program kadhaa za ujenzi wa uvumilivu wa kisiasa Zanzibar umekuwa na mafanikio makubwa kutokana na kuungwa mkono na wadau wote wa siasa Zanzibar wakiwemo viongozi wote wa vyama vya siasa, vyombo vya habari, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, AZAKI na wabia wa maendeleo. Miongoni mwa mafanikio ya program hizo ni kuwepo kwa amani na utulivu katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi mkuu wa 2010 na baada ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa. Wajumbe walikubaliana kwamba kazi iliyoko mbele yao ni kuunda na kutekeleza program nyingine kama hizo zenye lengo la kujenga imani ya kisiasa Zanzibar. Programu hizi zitaongeza mwangaza na uelewa kuhusu mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na faida zake.

7. Wajumbe wanaishauri serikali kuanza utekelezaji wa mapendekezo ya kamati ya watu sita kwani utekelezaji wake unaweza kuiimarisha zaidi serikali ya umoja wa kitaifa

Advertisements

2 responses to “Majumuisho ya mkutano wa Redet

  1. Pingback: Majumuisho ya mkutano wa Redet·

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s