Ushindi wa Raza, salamu za mabadiliko

Mohammed Raza ametangazwa mshindi katika Jimbo la Uzini baada ya chama chake cha CCM kupata kura, 5377, kikifuatiwa na Chadema 281, CUF 223, Tadea 14 na AFP 8 ambapo kura zote zilizopigwa ni 5903, zilizoharibika 28 makadirio ya kura 8755.

WANANCHI wa jimbo la Uzini wamekinusuru chama wakipendacho – Chama Cha Mapinduzi (CCM) dhidi ya anguko la kihistoria. Wamemchagua Mohamedraza Hassanali Mohamedali, kada wa CCM na mfanyabiashara maarufu Zanzibar , kuwa mwakilishi wao. Raza amechaguliwa kwa kura 5377, sawa na asilimia 91 ya kura 5903 zilizopigwa katika uchaguzi mdogo wa mjumbe wa baraza la wawakilishi uliofanyika 12 Februari. Uchaguzi huo ni wa kujaza kiti kilichokuwa wazi kufuatia kifo cha Mussa Khamis Silima, aliyekuwa mwakilishi.

Raza anasubiri kula kiapo (kuapishwa) katika mkutano ujao wa baraza utakaofanyika Aprili mwaka huu, ili kuanza rasmi kutumikia wananchi wa jimbo hilo .

Kwa kumchagua Raza, wananchi wa Uzini wamekilinda chama chao, wamempa ridhaa na wamethibitisha imani kwake kama kiongozi mwakilishi wa matatizo na matumaini yao .

Lakini pia, kwa kumchagua Raza; wananchi wa Uzini wamezishinda mbinu na kampeni za wanachama wenzao wachache walioeneza fitna juu yake mara tu baada ya kupata ridhaa ya wanachama wa CCM katika kura za maoni wakati chama hicho kikitafuta mgombea wake kwa ajili ya uchaguzi huo.

Hata hao walioendesha kampeni chafu dhidi ya Raza, sasa wanalazimika kuficha hisia zao na kumtilia nguvu ili afanikiwe kutimiza matumaini ya wananchi.

Inafurahisha kukuta kwamba Raza alianza mapema kutimiza ahadi zake kwa wananchi. Alipokuwa akipita katika vijiji vya jimbo hilo kabla ya kura za maoni, alisikiliza vilio na matatizo ya wananchi. Akatoa ahadi za kutatua matatizo aliyosimuliwa na kulalamikiwa.

Nilisema wakati ule kwamba wananchi wa Uzini hawakufanya kosa kuamua kumpa ridhaa Raza. Wanamjua alikotoka, masafa kutoka jimbo lao, lakini waliirukia bahati iliyotokea ya Raza kukimbilia kuchukua fomu ya kuomba chama chake kimpitishe kugombea uwakilishi hapo.

Walimtia moyo kwa kumpigia kura nyingi ili agombee. Kikao cha Kamati Kuu, baada ya kufanya uchambuzi mpana, hakikujiachia tu, kilifanya uamuzi wa haki kwa wananchi ambao walishaahidi kuwa huyo waliyempa kura za maoni, kati ya wana CCM 11, ndiye wanayemtaka.

Kamati Kuu ikawapa walichokitaka. Wananchi wakaahidi kuendelea kumpa moyo Raza. Wakamsikiliza wakati wa mikutano ya kampeni. Wakasikiliza na maneno ya wagombea washindani wake, wakijua kuwa walichokitaka wameshakipata.

Raza alishindana na Ali Mbarouk Mshimba kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye amepata kura 281 (asilimia 4.8); Salma Hussein Zarali wa Chama cha Wananchi (CUF) aliyepata kura 223 (asilimia 3.8); Khamis Khatib Vuai wa TADEA aliyepata kura 14 (asilimia 0.2) na Rashid Yussuf Mchenga wa AFP aliyepata kura 8 (asilimia 0.1).

Mpigakura mmoja anasema mara tu baada ya kupiga kura yake Jumapili: Nimeipiga kura yangu kwa ajili ya maendeleo yangu na wala sikufanya kosa katika uchaguzi huu. Nimechagua mgombea aliyetakiwa na wengi.
Nilipomuuliza ni mgombea gani huyo, akasema, “Hakuna mwingine isipokuwa Raza, yuleyule ambaye wabaya walimpigia kampeni chafu. Huyu ndiye atakuwa mwakilishi wetu mpya.”

Maneno hayo ni salamu muhimu kwa CCM na makada wake wale waliokuwa na mawazo tofauti na chaguo la wananchi wa Uzini.

Lakini matokeo ya uchaguzi mdogo wa uwakilishi jimbo la Uzini yameshtua wasiozifahamu vizuri siasa za jimbo. Wanasema walitarajia CHADEMA ingeshinda. Wengine walitarajia CUF ingeshika nafasi ya pili.

Waliokuwa na imani hiyo hawakufahamu maana ya wakati na mazingira mapya yaliyojengeka kwa wapigakura. Tena walibeza ukweli kwamba wapigakura wengi sasa ni vijana. Wapigakura wa kundi hili wana mtizamo mpya wa mambo tofauti kabisa na wazee wao.

Wapigakura vijana wanataka maendeleo ya kweli si lelemama na kampeni za maneno. Wanataka viongozi wanaoweza kuthubutu kutembea kwenye maneno yao . Viongozi wenye utashi wa kutimiza hadi zao. Hawajali tena viongozi wasemaji, wanaamini katika viongozi watendaji.

Wapigakura vijana wanajua wanakabiliwa na matatizo mengi yao binafsi kama vijana na maeneo yao . Wanatambua kwamba wakilala hawataamshwa na mtu. Wakilala watalala mpaka mwisho wa maisha yao kwa sababu, sasa wanajua wapo katika zama za kuwaona viongozi wakijali zaidi maslahi yao binafsi kuliko kutambua shida za wananchi.

Vijana wa Uzini ingawa wapo vijijini, wapo mjini, wapo Zanzibar, wapo Tanzania, wapo Afrika, wapo ulimwengu wa kileo. Wapo katika dunia inayokwenda kwa kasi kubwa katika kila nyanja ya maendeleo.

Ingawa wapo mbali na wanaofaidi maendeleo, wale vijana wenzao wa mataifa tajiri, wanajua hata wao wanaweza kuendelea na kuishi kama wenzao hao iwapo viongozi wao wataamua kuwasaidia. Katika wakati huu, hakuna linaloshindikana iwapo viongozi watatenda kwa bidii.

Vijana wa Uzini wanatokana na familia fukara ambazo zilishindwa kuwasaidia. Si katika elimu wala ajira. Wengi wao wameishia elimu ya lazima; kidato cha tatu kwa wale waliomaliza miaka ya 1990 na kidato cha pili kwa waliomaliza miaka ya karibuni.

Wale waliomaliza kidato cha nne wamekwama kupata ajira. Wameshindwa kujenga nguvu ya kiuchumi na kwa hivyo kuendelea kuishi na wazazi wao kwa kazi zenye kipato kisichotosheleza mahitaji ya lazima ya familia.

Matatizo kama hayo yamekosa kiongozi mwakilishi wa kuyafuatilia ili kuyapatia majibu. Hali imekuwa hivyo pamoja na wananchi wa Uzini kuendelea kuchagua ndugu na jamaa zao kutoka jimboni.

Na hizi ndio changamoto wanazomkabidhi Raza leo. Mwenyewe anajua maana ameelezwa yote haya alipofanya ziara ndefu ndani ya jimbo kabla ya kura ya maoni na wakati wa kampeni.

Wananchi wa Uzini wametoa funzo kubwa kisiasa. Ninaamini hawakuchagua CCM. Hawa wamechagua mtu aliyemtaka. Wamemchagua Raza, waliyeamini atawafaa, atatii matarajio na matakwa yao .

Hawakujali CCM, CHADEMA, CUF, TADEA wala AFP, bali walitafuta ni mgombea yupi mwenye sura ya imani kwao. Ndio maana zilipotokea chokochoko kwamba Raza ametoka mbali na jimbo na ni Mhindi asichaguliwe, walisema wazi watamchagua Ali Mbarouk Mshimba, mgombea wa CHADEMA.

Watu walitaka mtu wanayemuamini siyo chama. Chama kilipoingizwa katika kampeni chafu dhidi ya Raza, wakatoa indhari kuwa jina lake lisiporudishwa , wanajua nani wampe kura. Hakuwa mwalimu Salma ingawa wanampenda, hakuwa Khatib ambaye wanampenda, wala hakuwa Mchenga ambaye wanampenda. Walitaka mtu wa kuwatumikia.

Na hapo ndipo nisemapo sikushangaa CHADEMA kuchukua nafasi ya pili. Siasa zinabadilika kutokana na mambo mengi, mojawapo ni mazingira na wakati. Jimbo hili lina watu waliokuwa wakitafuta chama cha kukiegemea kwa kuwa hawakuona kama CUF kinawafaa, baada ya CCM.

Watu wa jimbo hili wenye asili ya Bara wameishi kwa vitisho kila wakati wa kampeni ulipofika. Walitishwa hata na viongozi wa CCM. Lakini waliamua kupenda CCM kwa sababu ni chama dola. Waliishi kwa nidhamu ya woga. Waliamua bora zimwi likujualo. Waliopenda CUF walifinyangwa.

Lakini sasa pepo za kisiasa zinabadilika. Kupenda siasa za upinzani Zanzibar inakuwa kawaida. Tena sasa CCM inasimangwa hivihivi mchana kweupe kuwa imeshindwa kuhudumia wananchi kimatarajio. Wanasema imechoka kama ambavyo viongozi wake wamechoka. Wanachagua mabadiliko.

2 responses to “Ushindi wa Raza, salamu za mabadiliko

  1. Raza umejibebesha jukumu! Mm si kulaumu ni saizi yako! Lkn umeahidi uadilifu kwa watu wako! Nawapongeza ndugu zangu wa uzini kwa kumchagua RaZA maana ndugu zangu rangi nyeupe kwenu ni uchafu 1964 mulizchoma moto. Nafurah mumetubu Allah atawasamehe! Sasa tuungane kuikomboa znz yetu! Nyinyi ni mashahidi kanisa lilivyonawiri huko! ALLAH AWAONGOZE HUENDA MUKAONA NJIA!

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s