Tuache kulalamika, tuchukue hatua tunapoumizwa

Ismail Jussa Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe akiongea katika vikao vya baraza la wawakilishi vilivyomalizika hivi karibuni huko Mbweni Mjini Unguja

Na Ally Saleh

Hatuwezi kusema kabisa na tukaeleweka bila ya kukubali kuwa kiwango cha demokrasia kinakua ndani ya nchi hii. Kila dalili inaonyesha hivyo na hii ni kwa kila ngazi ya maisha yetu. Tanzania imechukua bidii kubwa kufikia hapa. Kazi ya kina imefanywa kuhakikisha kuwa kila wigo umepanuliwa na hiyo ni kuanzia kwenye shina hadi tawi na kwa kila Mtanzania. Wiki iliyopita nilivutiwa sana na kipindi cha Pima Joto cha ITV wakati kiliporusha mjadala juu ya suala la tabia ya Watanzania kulalamika. Kwa hakika nilivutiwa na wachangiaji wake wa kuu ambao walieleza wazi wazi kuwa bila ya raia kulalamika hakuna nchi ambayo itafika popote pale.

Lakini zaidi walisisitiza kuwa malalamiko hayo yafuatiwe na kuchukua hatua kuonesha kama umeguswa, umekasirishwa, umeumizwa badala ya malalamiko kuishia kama malalamiko tu.

Wakati umepitwa hivi sasa wa mtu akikukanyaga, alisema mchangiaji wake mmoja, kuwa uwe wewe wa kumuomba sana na kumtafadhalisha kuwa aondoe mguu wake na kwa kuwa wewe unaumia kwa kanyago yake. La chukua hatua ajue kuwa anakuumiza na aondoe mguu wake halan.

Lakini mfano mzuri kabisa wa kuagana na malamamiko umenoshwa na vyombo vyetu vya kutunga sheria vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia Baraza la Wawakilishi la Zanzibar katika vikao vyake hivi vya karibuni, ambapo kile cha Baraza la Wawakilishi kimemalizika wakati kile cha Bunge kinaendelea.

Wabunge na Wawakilishi wameonyesha raia wanaowawakilishi kuwa sasa nao wanataka mabadiliko ya kutaka kulalamika hadi kufikia kuchukua hatua ili wao ndio wawe mfano wa Watanzania.

Hii ni ishara muhimu maana ndio njia pekee ya kuizindua Serikali juu ya mipango, maamuzi, utendaji na utekelezaji wake la sivyo Serikali hiyo itajisahau kuwa ina wajibu kwa wananchi na chembilecho yule mchangiaji wa ITV itakuwa inakanyaga watu na yenyewe ikitaraji kuwa ndio iombwe radhi.

Hatua ya Baraza la Wawakilishi hivi karibuni kuukataa Muswada wa Serikali juu ya Mafao ya Viongozi wa Siasa na kuurudisha kwa mara ya pili ni muhimu kwa afya ya siasa na demokrasia katika nchi na kwa hivyo inafaa kupongezwa sana na kila Mzanzibari ambae anataraji kuwa atawakilishwa vyema na Muwakilishi wake.

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi bila ya kujali vyama vyao waliiambia Serikali kuwa inakanyaga wananchi na wanaumia kwa Muswada huo ambao mmoja alithubutu kusema kuwa unarudisha ufalme na wengine wakisema ni kinyume na dhana ya kujenga usawa na kiuchumi haukhalis kabisa.

Wawakilishi walisema wamefadhaishwa kwa Serikali kuupeleka tena Barazani Muswada huo bila ya kujali kufanyia kazi mapendekezo ya awali na kwa sababu hiyo basi walikataa kuujadili na Serikali ikapata piga na aibu ya Muswada kupanguliwa kwa mara ya pili.
Hiyo ilikuwa sababu nzuri ya kupinga muswada wa Serikali kwa sababu hoja ilikuwa ni kwa malsahiya nchi si ya kikundi cha watu, si ya chama kimoja.

Lakini pia Baraza la Wawakilishi pia likaiambia Serikali kwamba halikubali kukanyagwa na kwa hivyo wananchi hawakubali kukanyagwa na wanachukua hatua tu na sio kulalamika katika suala la Tanzania kuomba kuongezewa eneo la Bahari katika Umoja wa Mataifa.

Baraza lilisema linajua kuwa mipaka ni eneo la Tanzania, linajua kuwa ni Tanzania inayopaswa kuomba, linajua kuwa linaombwa kwa faida ya kiuchumi lakini pia linajua kuwa Serikali ya Zanzibar ilishiriki katika mchakato huo.

Lakini likamwambia Waziri wa Ardhi, Makazi na Nyumba Professa Anna Tibaijuka kuwa pamoja na yote hayo watu waliowatuma kwenda Baraza la Wawakilisi hawakubaliani na yote hayo na wanataka Serikali yao ya Zanzibar ianze upya mchakato huo ili kuhakikisha maslahi ya Zanzibar.

Kwa nini Wawakilishi wamefanya hivyo? Ni kwa sababu Zanzibar imekuwa ikikanyagwa mara nyingi na Jamhuri ya Muungano na Wazanzibari wakati wote wamekuwa wakilalamika tu kuwa wanaumizwa na kwa upande wa Serikali ya Muungano si mara nyingi imekiri kuwa inajua inaiumiza Zanzibar.

Itakumbukwa Zanzibar mwaka jana kwa kuonyesha kuwa inaumizwa na haitaki tena kulalamika bali inataka kuchukua hatua Serikali ya Zanzibar ikachukua hatua ya kuunda taasisi zake mbili ambazo ziliopo kwenye Jamhuri ya Muungano zinaikanyaga Zanzibar na hata zikipigwa kelele hakuna linalofanyika.

Taasisi hizo zilikuwa ni Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar na pia Bodi ya Viwango va Zanzibar, ikionyesha ishara kubwa kuwa sasa pengine itakuwa basi kulalamika tu lakini hatua itachukuliwa maana bila ya hivyo hakuna la maana.

Bunge nalo limechukua hatua kama hizo kwa kukataa mwaka jana Muswada wa Sheria ya Kukusanya Maoni ya Katiba lakini pia hivi karibuni ilikataa sheria ya mikopo ya wanafunzi kwa sababu sheria hiyo inakanyaga wanafunzi watoto wa wakulima na wafanyakazi ambao wamelalamika kwa kuandamana na kugoma, lakini Serikali hata haijui kuwa inakanyaga watu.

Na dalili za Serikali kutojua kuwa inakanyaga ni ile ya mgomo wa Madaktari ambapo katika akili ya kawaida Mtanzania yoyote angetaraji kuwa njia ya busara ni ya Serikali kutafuta kila njia kumaliza mgogoro ule, lakini ikaamua kushindana na matokeo yake waliokanyagwa ni wanyonge ambao hawana uwezo wa kwenda kwenye matibabu ya fedha na Muhimbili na hospitali za Serikali ndio kimbilio lao.

Inapendeza kuona kuwa katika hilila madaktari hata umma umejua, kwa maana propaganda ya Serikali kuwapiga chapa madaktari kama ni wabinafsi na wasiopenda wananchi haikufanya kazi na matokeo yake hata wagonjwa walio vitandani wameungana na madaktari kwa kujua kuwa ni mgomo ambao si wa kukurupaka na kutaka mali bali ni mgomo wa kuwapa nguvu ya angalau kuishi na kufanya kazi katika mazingira yanayowastahili.

Tumesikia Bungeni na Barazani wajumbe wakiona haja ya kupaza malalamikoyao na kuingia katika kuchukua hatua kueleweka kuwa wananchi wanakanyagwa kwa kutumia haki walonayo kupiga kura ya kutokuwa na imani na Rais, kama italazimu kufanya hivyo.

Bila ya shaka Serikali ya Tanzania imekuwa ikielea katika bahari ya kuwa Tanzania ni nchi ya amani na kwa hivyo hakuna kitachotokezea zaidi ya kulalamika na kupiga kelele. Lakini labda mgomo kidogo kisha watu wote watarudi makazini mwao na maisha yatakwenda kama kawaida.

Ndio maana bei za vitu zinapanda kama zinavyopanda, mali ya umma inaibiwa kama inavyoibiwa, rasilmali za taifa zinafujwa kama zinavyofujwa, umeme unapandishwa kama unavyopandishwa na kikubwa kinachotokea ni malalamiko na hakuna anaesema kwa dhati na kuonesha hasira kuwa ameumizwa. Hii ndio Tanzania yetu.

Hatari iliopo ni kuwa hata Serikali ikitukanyaga na kutufirigisa hatuna cha kufanya kimfumo kwa sababu mfumo uliopo hauruhusu kuwatoa madarakani walioshika mpini mpaka wakati wa uchaguzi mwengine ufike, na kama wewe unaeumizwa utafika wakati huo.

Wito wangu ni kuwa tukielekea katika mjadala wa Katiba lazima tujipange kuhakikisha kuwa tunaziba kila mwanya wa wenye mamlaka kutukanyaga bila ya sisi kuwa na fursa ya kulalamika na kuchukua hatua. Lakini pia tupiganie kuwa na vipengele kuwa ikiwa wenye mamlaka watatukanyaga na kuendelea kufanya hivyo bila kujali basi tuwe na fursa ya kuwaondoa madarakani.

Haiwezekani, nasema haiwezekani tuende kama tunavyoenda hivi sasa. Lazima yale matamshi ya kuwa mamlaka ya kuendesha nchi ni ya wananchi wenyewe yawe kwa vitendo na yapewa mamlaka ya kweli kisheria na kikatiba ili tusiendelee kukanyagana na isiwe Bunge tu au Baraza la Wawakiilishi wenye kuweza kulalamika na kuchukua hatua lakini hata umma, ambao kwa sasa upo upo tu, kama naweza kusema hivyo.

Advertisements

4 responses to “Tuache kulalamika, tuchukue hatua tunapoumizwa

  1. Ni makala nzuri, mchango wangu utajikita zaidi kwenye hili suala la katiba.
    Leo kwenye kikao cha bunge umepelekwa mswada wa katiba kwa ajili ya marekebisho. Marekebisho hayo yanatokana na mapendekezo kutoka kwa wadau mbali mbali, hususan vyama vya siasa. Hakika inatia moyo na kuleta matumaini kuwa katiba ijayo itakuwa ni ya wananchi wote.
    Ulipopitishwa mswada wa marekebisho ya katiba yaliibuka madai mengi kwa upande wa Zanzibar ya kwamba kuna matakwa yao hayajatimizwa, wadau mbali mbali wa Zanzibar wamekuwa wakohoji kuwa ‘Zanzibar imepeleka madai yake 13, yamekubaliwa 10 na yaliyobaki yamekataliwa’. Hivi katika mswada uliopelekwa leo Bungeni, Zanzibar wamewasilisha tena hayo madai yao yaliyokataliwa na labda kuongeza mengineyo?. Kwangu bado ni kitendawili na hujiuliza ni madai gani hayo?, je yana athari gani kwa mustakabali wa nchi ya Zanzibar?.
    Kwa hakika, binafsi nina wasiwasi mkubwa sana na mchakato huu mzima na hatima ya Zanzibar. Hii ni kwa sababu, kwanini tunajadili katiba ya muungano wakati mshiriki mmoja wapo wa muungano huo hayupo. Hivi Zanzibar haioni kama pana haja ya kuwasilisha azimio baraza la wawakilishi kuitaka Serikali ya Muungano kupitia bunge kwanza wapeleke mswada wa kuifufua (kuitoa mafichoni!!) Tanganyika. Itapofufuka Tanganyika ndio sasa Zanzibar itaweza kuzungumza na mwenzake na kuangalia jinsi gani ya kuupanga ama vinginevyo huo muungano pindipo ikionekana pana umuhimu wa kuwepo kulingana na matakwa ya wananchi wa nchi mbili; Zanzibar na Tanganyika.
    Hili ni jambo muhimu sana linalohitaji kufanyiwa kazi. Tanganyika irudi kwanza halafu mjadala wa muungano baadae, ima ikiwa ni katiba ama mkataba

  2. Hata mm ninawasi wasi, nchi hizo zilipounganishwa bila ya idhini, shahidi na ridhaa kulikuwepo na hiyo nchi inayoitwa tanganyika. Ambayo wimbo wake wa taifa ni huu isipokuwa penye tanganyika pamewekwa tanzania, pendera na katiba hadithi ni ile ile! Hii ni pili pili ya macho kwanini tusidai nchi yetu kwanza? Hayo mambo 10 yaliyokubaliwa ni yapi? Yanafaida gani ikiwa mlegwa mmoja hayupo! Tutafakari

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s