Hutuba ya ZLSC

Wakili wa kujitegemea, Awadh Said Ali akitoa mada katika moja ya makongamano ya katiba

Mheshimiwa Mgeni Rasmi uzinduzi wa Siku Ya Sheria Zanzibar utabaki na deni endapo tutasahau kukumbuka na kutambua mchango mkubwa alioutoa Mwanasheria Msomi Mashuhuri wa Zanzibar Professor Haroub Othman ambaye katika uhai wake sio tu kuwa aliasisi fikra hii bali aliipigania sana Zanzibar iwe na Maadhimisho haya. Kwa kuwa leo hii tunaadhimisha maadhimisho ya mwanzo akiwa yeye hayupo nasi na ameshatangulia mbele ya haki tunamuomba Mweyenzi Mungu amuweke mahali pema peponi. Aamin

HOTUBA YA RAIS WA CHAMA CHA WANASHERIA ZANZIBAR KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA SHERIA ZANZIBAR TAREHE 07-02-2012 KATIKA VIWANJA VYA VICTORIA GARDEN, ZANZIBAR.

– Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
– Mheshimiwa Jaji Mkuu wa Zanzibar,
– Mheshimiwa Jaji Kiongozi wa Tanzania,
– Waheshimiwa Majaji wa Mahkama Kuu, Zanzibar,
– Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar,
-Mheshimiwa Spika wa Baraza La Wawakilishi, Zanzibar
– Mheshimiwa Kadhi Mkuu wa Zanzibar,
– Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar,
– Mheshimiwa Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar,
-Mheshimiwa Mkuu Wa Mkoa Wa Mjini Magharibi,
-Mheshimiwa Mrajis Wa Mahkama Kuu , Zanzibar
– Waheshimiwa Mahakimu na Makadhi wote mliohudhuria,
– Waheshimiwa Mawakili wote mliohudhuria, kutokea Afisi ya Mwanasheria Mkuu, Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Mawakili wa kujitegemea,
– Waheshimiwa wafanyakazi na watendaji wote wa Idara ya Mahkama mliohudhuria,
– Wageni waalikwa,
– Mabibi na Mabwana,
ASSALAM-ALEYKUM,
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyenzi Mungu, mwingi wa Rehma na ukarimu kwa kutujaalia sote uzima na afya njema na kutuwezesha kujumuika pamoja kwa furaha katika kuadhimisha siku hii adhimu, Siku ya Sheria Zanzibar, ikiwa ni maadhimisho ya kwanza katika Historia ya Zanzibar.
Mh. Mgeni rasmi, sisi Chama Cha Wanasheria Zanzibar tukiwa wadau katika maandalizi ya maadhimisho haya, tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwako wewe binafsi kwa kukubali mwaliko wa kuwa Mgeni Rasmi katika hafla hii. Mheshimiwa tunaelewa ukubwa na wingi wa majukumu yako, tena ya Kitaifa, lakini umetupa faraja na msukumo mkubwa kwa uamuzi wako wa kumega na kutukirimu muda wako adhimu na kuamua kushirikiana nasi katika maadhimisho haya.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, naomba pia nichukue fursa hii kumpongeza kwa dhati Mh. Jaji Mkuu wa Zanzibar kwa kuongoza, kwa umakini na bidii kubwa juhudi za pamoja zilizopelekea kufanikisha azma hii ya muda mrefu ya jamii ya wanasheria Zanzibar ya kuwa na maadhimisho ya siku ya Sheria Zanzibar. Maadhimisho ambayo hutoa fursa ya kuwakutanisha kwa pamoja wanasheria kutoka Taasisi Kuu za Sheria Zanzibar na kuweza kujumuika pamoja na kujadiliana mambo yanayohusiana na taaluma ya sheria kwa ujumla, kuangalia changamoto inazozikabili taaluma hii na kutafuta njia bora za kutatua changamoto hizo.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, ni kutokana na uongozi makini , uliojaa ubunifu na busara wa Mh. Jaji Mkuu wa Zanzibar ambapo ilimpendeza kutushirikisha sisi Chama Cha Wanasheria Zanzibar, Afisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na wadau wengine katika tasnia hii ya sheria katika maandalizi yote ya maadhimisho haya ambapo leo hii kwa majaaliwa ya Mwenyenzi Mungu Mtukufu azma ya muda mrefu imefanikiwa.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi uzinduzi wa Siku Ya Sheria Zanzibar utabaki na deni endapo tutasahau kukumbuka na kutambua mchango mkubwa alioutoa Mwanasheria Msomi Mashuhuri wa Zanzibar Professor Haroub Othman ambaye katika uhai wake sio tu kuwa aliasisi fikra hii bali aliipigania sana Zanzibar iwe na Maadhimisho haya. Kwa kuwa leo hii tunaadhimisha maadhimisho ya mwanzo akiwa yeye hayupo nasi na ameshatangulia mbele ya haki tunamuomba Mweyenzi Mungu amuweke mahali pema peponi. Aamin
Mh. Mgeni Rasmi, katika taaluma ya sheria mawakili wanajukumu kubwa la kuelekeza kwa njia ya ushawishi wa kitaaluma njia iliyo bora na sahihi ya kupita lakini uamuzi wa mwisho wa njia ipi ndio sahihi na bora ya kupita hubaki kwa waheshimiwa majaji wetu baada ya mazingatio ya kina ya mapendekezo ya mawakili. Wakati tunaadhimisha sherehe hii njia aliyoionesha Mh. Jaji Mkuu ya kuwa na ubunifu, kuongoza kwa umakini, bidii , busara na ushirikiano ni njia ambayo hatuna budi kuienzi na itoshe tu kusema kuwa hii ni “precedent” tosha ya kufuatwa katika uendeshaji wa shughuli zetu.
Mh. Mgeni Rasmi, kama unavyojua, kauli mbiu yetu katika maadhimisho haya inasema “Kupiga Vita Rushwa Katika Utoaji Haki”. Uchaguzi wa kauli mbiu hii haukuja kama sadfa. Kama inavyoeleweka, yapo matukio makubwa ya kisheria, kwa mfano mchakato wa uandaaji katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo yangetegemewa kwa wakati huu yawe na ushawishi mkubwa katika kuweka kauli mbiu ya maadhimisho kama haya. Hata hivyo baada ya kuzingatia kwa kina ukweli kwamba mfumo wetu wa utoaji haki haukunusurika na janga hili la maangamizi la rushwa, athari zake kwa jamii na Taifa letu kwa ujumla ndio ikaonekana haja ya kutoa umuhimu na kuzipa kipaumbele juhudi za kusafisha mfumo wetu wa utowaji haki.
Mh. Mgeni rasmi, kauli mbiu ya maadhimisho haya inakiri kuwa rushwa ipo katika mfumo wetu wa utoaji haki. Kauli mbiu hii haitoi fursa ya kujiuliza kama rushwa ipo au la. Ingetoa fursa hio ingekuwa ni kichekesho au kituko katika macho ya wanajamii ambapo kila mmoja anaelewa fika kuwa rushwa imejikita katika Taasisi zetu za utowaji haki.
Mheshimiwa Mgeni rasmi, umuhimu wa kutenda haki haustahiki kusisitizwa mno, ni wajibu wa msingi wa sote tuliotwishwa jukumu hili lililo nyeti mno katika ustawi wa jamii ya haki. Kwa kujikumbusha naomba ninukuu maneno ya Jaji Mkuu Oputa aliyekuwa Jaji Mkuu wa Mahkama Kuu Ya Nigeria aliyoyatoa mwaka 1981 kwenye Jarida la “The Law and the Twin Pillars of Justice” Oweri Government Printer uk 71 aliposema:
“[Justice] should be pure, visibly pure, and unadulterated. It should be fair, equitable and impartial. It should be no respecter of person, personalities, or establishments. It should not be commercialized, nor should it be bought and sold, for nothing is as hateful as venal justice. It should be quick, for delay is certain denial. Legal justice should as closely as possible, resemble the virtue whose name it bears – virtue by which we give to everyone his due.”
Mheshimiwa Mgeni rasmi, jukumu la kutenda haki bila kuangalia vishawishi vyovyote linadhihirishwa na nembo maarufu ya mwenye jukumu la utowaji haki akiwa ameshikilia mizani mkono mmoja na upanga upande wa pili na akiwa macho yake yamefungwa kitambaa ikimaanisha haja ya kutenda haki bila kuona vishawishi vya aina yoyote ambavyo vingeweza kukupelekea kuzongwa na upendeleo, woga, chuki, au vishawishi vyenginevyo.
Jukumu la utowaji haki ni jukumu takatifu, halitakiwi liwe na doa, shaka wala dosari yoyote. Ni jukumu linalobeba ujasiri mkubwa ndio maana msingi mkuu wa jukumu hili unasema “Haki itendeke, lolote naliwe” (Let Justice Be Done, though the heavens falls) Msingi huu umetokana na kisa mashuhuri katika simulizi za kisheria kinachojulikana kama Hukumu ya Piso. Piso alimhukumu askari mmoja adhabu ya kifo kwa kumuuwa mtu mmoja aliyeitwa Gaius. Akaamrishwa muuaji kutekeleza hukumu ile ya kifo. Mara tu kabla ya utekelezaji wa Hukumu hiyo Gaius akaibuka, yuhai na mzima. Mtekeleza Hukumu akazuia utekelezaji hukumu na akaenda kuripoti yaliyojiri kwa Piso – Mtoaji Hukumu. Piso akatoa Hukumu wote watatu sasa wauliwe. Askari lazima auliwe kwa vile tayari hukumu ya kifo juu yake ilishatolewa. Na mtekelezaji hukumu auliwe kwa kukhalif amri halali ya kuuwa iliyotolewa. Na Gaius auliwe kwa sababu ya kuwa chanzo kilichopelekea hao wawili kuuliwa. Mwishoni kwa msisitizo Piso akasema “Fiat justice, Ruat caelum” – Let Justice be Done, though the Heavens fall.
Mheshimiwa Mgeni rasmi, ni huzuni kubwa kuwa rushwa imezagaa katika jamii yetu. Imekuwa sehemu ya maisha yetu. Imeshaingia katika utamaduni wetu na kuifanya kama khulka ya kawaida . Lakini huzuni kubwa zaidi ni pale rushwa inapovamia mfumo wetu wa utoaji haki. Ile sehemu ambayo ni kimbilio la waliokosa haki zao, tena pengine kwa rushwa tu, nako kumeota rushwa. Hali hii ni hatari kubwa kwa ustawi wa Taifa lenye dhamira ya kujenga jamii ya usawa na haki.
Mfumo wa utowaji haki usipokuwa safi dhidi ya rushwa hata juhudi zote za Serikali na jamii kwa ujumla za kupiga vita rushwa hazitozaa matunda yanayotegemewa . Sana sana wala rushwa walio nje ya mfumo wa utoaji haki watalazimika kuongeza dau la rushwa ili kuweka kasma ya kwenda kutoa huko watakapopelekwa katika vyombo husika.
Vyombo vya utoaji haki vinapogubikwa na rushwa athari yake ni kubwa, jamii hupoteza imani na vyombo hivi na hivyo hulazimika kuangalia njia mbadala – na inapofika hapo ndipo ambapo rushwa huitumbukiza jamii katika maangamizi. Mfano wa haya ni pale tunavyoshuhudia kwa wenzetu jinsi nchi zinavyoingia katika maangamizi/mauwaji pale Taasisi za Utoaji Haki kama TUME ZA UCHAGUZI NA MAHKAMA zinaposhindwa kutimiza wajibu wao katika utoaji Haki hasa kwa Rushwa ya kisiasa au fedha.
Mheshimiwa Mgeni rasmi, hapa Zanzibar kwa uzoefu wa haraka rushwa za aina mbili ndizo kuu zilizojikita katika mfumo wetu. Ya kwanza ni rushwa ya fedha na ya pili ni rushwa ya kisiasa. Katika muktadha huu naomba ninukuu maneno ya Mheshimiwa Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mh. Omar O. Makungu aliyoyatoa katika Hotuba yake aliyoitoa katika Hafla ya kuwakubali wanasheria wapya 22 kuwa mawakili wa Mahkama Kuu ya Zanzibar tarehe 10-11-2011 ambapo alisema:
“Naomba nimalizie kwa kuwaomba kuwa tuienzi taaluma yetu ya Sheria na tusikubali ichafuliwe na wanasiasa kwa maslahi yao kwani siasa na uchu wa fedha ndio maadui wawili wakubwa wanaoiandama taaluma hii. Tujiepushe na kuweka siasa na fedha mbele.”
Mheshimiwa Mgeni rasmi, kwa hakika kama nilivyosema mwanzo kuwa suala la kuwepo rushwa katika Taasisi zetu za utoaji haki halina haja ya kutupotezea muda. Ni jambo lililo wazi, kwa lugha nyepesi ya kileo ni kuwa “hilo halitaki tochi.” Pia athari za rushwa kwa jamii inayojinasibisha na lengo la kujenga Taifa lililostaarabika ni nyingi mno na zenye matokeo ya kutisha. Kitu kilicho muhimu kuliko vyote ni kuangalia hatua gani zichukuliwe ili kuzisafisha Taasisi zetu hizi na mfumo mzima wa utoaji haki kutokana na janga hili la rushwa. Maoni yetu ni kuwa ziko njia nyingi zinazostahiki kuchukuliwa katika juhudi za kupambana na rushwa, baadhi ya hizo ni kama hizi zifuatazo:
Kwanza kabisa ni kuweka jitihada maalum katika kuhakikisha wote wanaokabidhiwa jukumu la kuongoza au kuwa sehemu ya Taasisi ya utoaji haki wanakuwa ni watu wanaotambulika katika kujiwekea rekodi iliyotukuka katika kuichukia rushwa. Uteuzi wa watu safi ndio mwanzo mwema na wa lazima katika mapambano dhidi ya vita hivi vya rushwa. Mheshimiwa Mgeni Rasmi, nchi yetu ni ndogo ikiwa na watu wachache na hivyo takriban wote tunajuana. Wenye rekodi isiyoridhisha wanajulikana. Wasio wala rushwa tunao na wanajulikana. Wanaotiliwa mashaka nao wapo na wanajulikana. Ni wajibu kuwaepuka wanaotiliwa mashaka kwani ni wazi bila ya kufanya hivyo wataharibu taswira nzima ya chombo husika.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi jukumu kubwa la mamlaka ya uteuzi (Appointing Authority) hutimizwa pale uteuzi sahihi unapofanyika. Uteuzi unapoelekezwa kwa mtu makini, mahiri, muadilifu, mtu wa haki na mchukivu wa rushwa hapo tutakuwa tumepunguza ugumu wa tatizo tunalopambana nalo kwa kiwango kikubwa sana. Hapa naomba ninukuu maneno ya Waziri Mkuu wa kwanza wa Singapore Mwanasheria Lee Kuan Yew katika kitabu chake maarufu cha From Third World To First uk. 245: aliposema
“Selecting the right man for a key constitutional position, like the Chief Justice………..is vital. A wrong choice could mean years of public embarrassments and endless problems”
Mheshimiwa, dhamira ya mamlaka ya uteuzi katika mapambano dhidi ya rushwa huonekana kwanza katika uteuzi. Katika hili, napenda nichukue fursa hii kwa niaba ya Chama Cha Wanasheria Zanzibar kukupongeza rasmi kwa kuonesha dhamira ya dhati ya kupambana na vita hii ambayo imejidhihirisha katika teuzi ulizofanya za wakuu wote wa Taasisi zote zilizokabidhiwa jukumu la kusimamia mfumo wetu wa utoaji Haki, kuanzia uteuzi wa Jaji Mkuu, Mwanasheria Mkuu na Mkurugenzi wa Mashtaka. Tunaamini katika teuzi hizi suala la mapambano dhidi ya rushwa ulilipa kipaumbele. Ni imani yetu kuwa wenzetu hawa waliokabidhiwa majukumu haya wataweka suala la kupiga vita rushwa kuwa Ajenda No 1 katika mikakati kazi wanayopanga. Haitoshi kuwa na kiongozi safi asie mla rushwa lakini anaongoza Taasisi iliyobobea rushwa.
Mheshimiwa Mgeni rasmi jengine ambalo hatuna budi kuliangalia kwa umakini katika mkakati wa mapambano haya ni maslahi ya watendaji wote wa Taasisi za utoaji haki. Mbali na ukweli kuwa baadhi ya watendaji hujiingiza katika rushwa kwa utashi wa tamaa zao binafsi za kujinufaisha zaidi lakini ni ukweli pia kuwa wengine hujitumbukiza katika rushwa sio kwa mapenzi yao ya tamaa bali ni kutokana na hali duni ya maslahi.
Mheshimiwa Mgeni rasmi, tunaelewa kuwa katika mambo uliyoyapa kipaumbele mara tu baada ya kushika madaraka ni pamoja na kuimarisha maslahi ya watendaji katika taasisi za utoaji haki hasa mahkamani . Ongezeko la maslahi lililofanywa katika kipindi cha karibuni ni la kupigiwa mfano na limeonesha kwa dhati dhamira njema ya Serikali ya kuleta mageuzi makubwa katika mfumo wetu wa utoaji haki. Hili ni moja katika juhudi maridhawa za kuhakikisha kuwa watendaji husika hawaingii katika vichocheo vya rushwa.Mheshimiwa Mgeni Rasmi; tunakupongeza kwa dhati kwa hatua hii muhimu mno na pia tunapendekeza utaratibu huu uendelee na pia uangalie watendaji wote kuanzia ngazi ya chini kabisa hadi ngazi ya juu kabisa.
Mh. Mgeni rasmi kiwango kikubwa cha shughuli ya utoaji haki hufanyika huko ngazi za chini za taasisi zetu, hivyo sambamba na kuangalia maslahi katika ngazi za juu bali pia maslahi yaimarishwe pia huko ngazi za chini . Kwa mfano ongezeko la mara hii limeacha kiwango cha unyonge kwa Mahakimu wa Mahkama za Mwanzo kwa vile halikuangalia usawia katika Mahkama zetu. Mheshimiwa Mgeni rasmi grafu yetu daima huonyesha wazi kuwa kila pale penye maslahi duni na vilio vya rushwa huwa vingi na vikubwa na pia kinyume chake.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi baada ya uboreshaji huu wa maslahi ya watendaji hatua ambayo ni wazi ina kila aina ya uhalali ni kuwa pasiwe na chembe ya uvumilivu pale penye tuhuma za rushwa. Tuache kuipiga vita rushwa kwa misamiati na maneno makali tu (rhetorics) kama vile “Rushwa ni adui wa haki” nk, tutoke kwenye maneno na sasa tuelekeze juhudi zetu katika kuonesha kuchukizwa na rushwa kwa vitendo. Tuondokane na tabia ya kulindana, kubebana, kupendeleana na kustiriana. Tuichukie rushwa kwa dhati na tupambane nayo kwa ukweli – bila huruma wala muhali. Endapo hatutoitokomeza rushwa ni wazi rushwa itatutokomeza na kutuangamiza kama jamii. Haki isiwe kwa wenye fedha tu au mamlaka HAKI itolewe kwa kila inayemstahikia bila ya kujali uwezo wake wa kifedha, mamlaka yake katika jamii, au nafasi yake katika uongozi.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi juhudi za Serikali yako kutunga sheria ya kuanzishwa mamlaka ya kupambana na rushwa, ambayo imepitishwa hivi karibuni na Baraza La Wawakilishi ni jambo la kupongezwa na linalotupa faraja sana katika muelekeo wa vita hivi dhidi ya rushwa .Hata hivyo mwanzo mwema huu hautozaa matunda yoyote kama hatutokuwa waangalifu na hatua zetu za baadae kama tunavyotanabahishwa:
“ it is easy to start off with high moral standards, strong convictions and determination to beat down corruption. But it is difficult to live up to these good intentions unless the leaders are strong and determined enough to deal with all transgressors and without exceptions.” pg 189 ( Lee Kuan Yew).
Mh. Jambo jengine ni msukumo katika utashi wa kisiasa katika kupiga vita rushwa- juhudi hizi hutegemea pia dhamira ya uongozi wa kisiasa kuhakikisha kuwa kuna mgawanyo sawia (equitable distributions) wa matunda ya nchi yetu. Sehemu moja ya jamii inapotumia nguvu ya sheria kujihalalishia maslahi na mustakbal mwema katika khatma zao ni wazi kuwa sehemu nyengine ya jamii nayo itaangalia njia zilizo nje ya sheria kujiwekea mazingira bora ya maslahi yao na khatma yao na hapa ndipo vichocheo vya rushwa vinapoanza kuibuka na katika mazingira haya wapambanaji wa kutokomeza rushwa hukosa uhalali wa kimaadili (moral authority) wa kupambana ipasavyo.
Mh. Mgeni rasmi pia jamii yetu kwa upana wake ielewe kuwa ndiyo yenye jukumu la kufichua vitendo vya rushwa na kusimamia, kwa kutumia vyombo husika, utokomezaji wa vitendo hivyo. Utolewe mwamko mkubwa kwa jamii juu ya jukumu hili na pia tutoe mwito kwa asasi za kiraia( non state actors) ambazo mchango wao mkubwa umezaa matunda katika maeneo muhimu kama vile haki za binadamu , utawala bora, demokrasia, ukimwi , mazingira na mengineyo. Sasa waelekeze nguvu zao katika juhudi hizi za kuondokana na janga la rushwa.

Mheshimiwa mgeni rasmi nimalizie kwa kukumbushana kuwa hakuna aliye juu ya sheria- sisi sote tuko chini ya sheria, awe wakili, awe hakimu, awe mwendesha mashtaka, awe Jaji – sote tuko chini ya sheria na katika jukumu la utoaji haki sote tuko chini ya Mamlaka Kuu Ya Haki iliyo juu yetu sote ambayo ipo siku tutaulizwa jinsi tulivyotenda haki katika utowaji haki.
Mheshimiwa mgeni rasmi, naomba nikiwa mwingi wa heshima , kuwasilisha na niwashukuru wote kwa kunisikiliza.
Awadh Ali Said
Rais Chama Cha Wanasheria Zanzibar (ZLSC)

Advertisements

One response to “Hutuba ya ZLSC

  1. Hotuba tumeipata ila nahoji tu, huyu ni Rais wa Chama cha Wanasheria (zls) au ni wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC) naona unapotosha wasomaji. ZLSC haina Rais.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s