Siku ya Sheria Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein,akitoa hutuba yake wakati wa sherehe za siku ya Sheria,Zanzibar,(kulia) ni Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe.Omar Othman Makungu,Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.Abubakar Khamis,na Jaji Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Fakih Jundu,(kushoto) ambapo "kauli mbiu kuga vita Rushwa katika utowaji wa haki" ,sherehe hizo zilifanyika katika viwanja vya Victoria Garden Mjini Unguja.

Tunapozungumzia Utawala Bora, maana yake kubwa kwa jamii ni kuwepo utawala wa sheria ambao unampa kila mmoja wetu haki yake. Hili ndilo lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo imejenga misingi madhubuti ya masuala hayo. Kwanza tumeweka Mahakama iliyo huru; pili, tumeanzisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka; tatu, tuna chombo huru cha kutunga sheria, yaani Baraza la Wawakilishi; nne, tunaendesha mfumo wa demokrasia wa kuwa na uchaguzi kila baada ya muda, uliowekwa na Katiba na vyama vya siasa vinaendesha shughuli zao kwa mujibu wa sheria bila ya kuviingilia.

HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA
MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI,
MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN,
KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA SHERIA
ZANZIBAR, TAREHE 7 FEBRUARI, 2012

Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria,
Mheshimiwa Jaji Mkuu wa Zanzibar,
Mheshimiwa Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar,
Mheshimiwa Jaji Kiongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu,
Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu Zanzibar,
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai Zanzibar,
Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS),
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS),
Viongozi wa Serikali na Dini,
Ndugu Wanasheria,
Ndugu Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana,

Assalamu Alaykum,

Kwanza kabisa, sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu (S.W) kwa kutujaalia kufika siku hii ya leo kuiadhimisha siku ya Sheria Zanzibar tukiwa wenye afya njema na furaha tele huku tunaendelea na joto la kiangazi.

Pili, napenda niwapongeze waandaaji wa maadhimisho haya kwa uamuzi wao wa kuandaa maadhimisho haya kwa mara ya kwanza hapa Zanzibar. Hili ni jambo zuri na nawashukuru kwa dhati kwa kunialika ili niwe Mgeni Rasmi katika sherehe hii ya kihistoria nchini kwetu. Naipongeza zaidi Mahakama kwa kuiandaa na kuiongoza shughuli hii.

Tatu, nimefarajika sana leo kupata bahati hii ya kusimama mbele ya hadhara hii ya Majaji, Mahakimu na Wanasheria wasomi (learned friends) kutoka katika Taasisi mbali mbali za Serikali na binafsi. Katika maisha yangu ya kuitumikia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar niliwahi kuteuliwa na Rais Mstaafu Dk. Amani A. Karume kuwa Waziri wa Katiba na Utawala Bora katika Awamu ya Sita na kwa kipindi hicho ingawa kilikuwa kifupi nilipata bahati ya kufanya kazi na Wanasheria wenye ujuzi mkubwa akiwemo Mwanasheria Mkuu wa wakati huo Mheshimiwa Idi Pandu Hassan na Katibu Mkuu wa wakati huo Ndugu Othman Masoud ambae kwa sasa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kutoka kwao nilijifunza mambo mengi ya thamani yanayoweza kuufanya umma au wananchi kuwa na imani na Mahakama na vyombo vya sheria na kwa pamoja tuliweza kuyatekeleza majukumu yetu katika kuendeleza utawala bora. Hivi sasa nimepata fursa nyengine ya kufanya kazi na wataalamu na mabingwa wengine wa sheria na ninatarajia kwamba nitaendelea kujifunza kutoka kwao na kwa pamoja tutatekeleza wajibu wetu.
Serikali imeamua kwa makusudi kuliimarisha jengo, viwanja na historia ya jengo hilo ambalo ndio Baraza la Kutunga Sheria la mwanzo hapa Zanzibar.

Mabibi na Mabwana,
Waliotangulia kusema kabla yangu, ambao ni mabingwa wa sheria, wamezungumzia mambo kadhaa yanayohusu mada ya sheria nchini kwetu. Nawapongeza kwa maarifa waliyotupa. Mimi nataka kuchukua fursa hii leo ya siku ya sheria kuzungumzia zaidi uhusiano wa wananchi na sheria. Kwa sababu sheria ni jambo linalomhusu kila mtu, ingependeza sana siku hii iwe ni ya maadhimisho ya sheria kwa programu mbali mbali za kijamii. Jambo hili litawaleta wananchi kuwa karibu na wanasheria, wakiwemo majaji, mahakimu, waendeshaji mashtaka, mawakili na wengineo. Hili ni muhimu katika kujenga uhusiano bora kati ya watendaji wa sheria na wananchi. Miongoni mwa mambo ambayo yatapaswa yawemo kwenye programu hio ni kama vile maonesho, kuzikaririr na kuzipitia hotuba za wanasiasa na vipeperushi zitasaidia kutoa elimu ya wananchi kuitumia sheria ipasavyo.

Mabibi na Mabwana,
Tunapozungumzia Utawala Bora, maana yake kubwa kwa jamii ni kuwepo utawala wa sheria ambao unampa kila mmoja wetu haki yake. Hili ndilo lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo imejenga misingi madhubuti ya masuala hayo. Kwanza tumeweka Mahakama iliyo huru; pili, tumeanzisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka; tatu, tuna chombo huru cha kutunga sheria, yaani Baraza la Wawakilishi; nne, tunaendesha mfumo wa demokrasia wa kuwa na uchaguzi kila baada ya muda, uliowekwa na Katiba na vyama vya siasa vinaendesha shughuli zao kwa mujibu wa sheria bila ya kuviingilia.

Hayo ni baadhi ya maeneo ya utawala wa sheria ambao tunauenzi Zanzibar. Lakini, pamoja na hayo ni muhimu kwa jamii yote kwa jumla ihusishwe ipasavyo na sheria ambayo ina upana mkubwa.

Mabibi na Mabwana,
Yapo mambo ya msingi katika kutekeleza sheria ili turudishe imani ya wananchi kwa vyombo vya sheria ambavyo vinakuhusuni sana waheshimiwa mlliopo hapa. Mara nyingi tumekuwa tukizungumzia utekelezaji wa sheria. Jambi hili ni muhimu katika kuhakikisha nchi ina Utawala wa Sheria na Utawala Bora.

Utekelezaji wa sheria unatoa haki kwa watu na unaleta amani na utulivu ndani ya jamii na unajenga imani za watu kwa vyombo vya sheria na sheria zenyewe. Lazima tukubalini sote kwamba utekelezaji wa sheria usioridhisha ndio hatimae unaoleta madhara ndani ya jamii. Inapofikia hatua hio ndipo wananchi wanapoanza kutoa masikitiko yao dhidi ya vyombo vya sheria pale vinapokosa kutekeleza sheria. Matatizo kama ya rushwa mara nyingi yanatokana na jambo hili.

Mabibi na Mabwana,
Napenda kuchukua fursa hii leo kuzungumzia zaidi suala hili la utekelezaji wa sheria. Hili ni jambo linaloanzia kutoka kwenye jamii. Ni ukosefu wa utekelezaji sheria, pale ambapo watu wanavunja sheria kwa kujenga katika vianzio vya maji, unapofanyika ukataji wa miti ovyo na uharibifu wa mazingira kwa jumla. Vyombo vya sheria vinavyohusika na watendaji wake hawatilii mkazo utekelezaji wa sheria zinazohusu mambo hayo.

Kwa mfano, sote tunaelewa kwamba rushwa isipodhibitiwa inapelekea vyombo vya kutekeleza sheria kama vile mahakama, polisi, wakusanyaji mapato na kadhalika kutotekeleza wajibu wao ipasavyo. Mambo haya yanapotendeka mwananchi anaweza kunyimwa haki yake ya kisheria.

Kadhalika, ofisa aliyepewa dhamana ya kukusanya kodi asipotekeleza wajibu wake ipasavyo anapelekea kuikosesha Serikali mapato ambayo yangeiwezesha Serikali kutoa huduma bora za aina mbali mbali kwa wananchi.

Ajali za barabarani zinaongezeka kutokana na wingi wa vipando kutokuwepo utekelezaji wa sheria kikamilifu. Magari yasiyofaa kuwepo barabarani yanaendeshwa na madereva wasiokuwa na leseni wanaachiliwa, jambo ambalo husababisha matatizo makubwa na ongezeko la ajali.

Mabibi na Mabwana,
Haya ni baadhi ya mambo ambayo wengi wetu tunayajuwa na bila ya shaka yanatendeka katika jamii. Ni vyema siku ya sheria kama hii leo, tukajadili bila ya woga matatizo yanayotokana na kutotekeleza sheria na kufanya mambo yanayopaswa ili kuyapatia ufumbuzi.

Bila ya shaka elimu kwa jamii kuhusu kuwepo kwa sheria fulani kama vile ya mazingira na kuelimisha madhara ya kutoitekeleza sheria hio ni jambo litalonufaisha jamii. Naelewa kwamba Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaendesha vipindi juu ya sheria hasa zinazohusiana na siasa; na pia Idara ya Polisi inatoa baadhi vipindi. Hayo ni mambo mazuri lakini wakati umefika kwa vyombo vyetu vyote vya sheria kutilia mkazo elimu kwa jamii ipasavyo.

Mabibi na Mabwana,
Nimefarajika kuwa maadhimisho haya ya siku ya sheria yamewekewa kauli mbiu maalum ya “Piga Vita Rushwa katika Utoaji Haki”. Kauli mbiu hii ni muhimu sana na imekuja wakati mzuri. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeridhia mikataba mbali mbali ya kimataifa ya kupambana na rushwa kama vile Mkataba wa SADC wa mwaka 2001 (the SADC Protocol Against Corruption, 2001) ambao Tanzania umeuridhia mwaka 2003; Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Rushwa wa mwaka 2003 “the United Nations Convention against Corrption 2003” ulioridhiwa na Tanzania mwaka 2004, na Mkataba wa Umoja wa Afrika dhidi ya Rushwa wa mwaka 2003 “the Africa Union Convention on Preventing and Combating Corruption of 2003” ulioridhiwa na Tanzania mwaka 2004.

Baada ya kuridhia mikataba yote hiyo Tanzania tulitakiwa tutunge sheria itayounda taasisi ya kupambana na rushwa. Kwa bahati nzuri wenzetu wa Tanzania Bara walitekeleza mapema lengo la kutunga sheria hio kwa kuunda TAKUKURU, lakini Zanzibar tuliamua kulifanyia kazi suala hili kwa kwenda nalo hatua kwa hatua. Ninafuraha hapa kutamka kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hatimae iliwasilisha mswada wa sheria kwenye ya Baraza la Wawakilishi mwezi uliopita kwa ajili ya kuanzishwa Mamlaka ya Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar. Kama mlivyosikia mswada huo tayari umeshapitishwa na Baraza hilo na wakati wowote nikishairidhia itakuwa sheria kamili na nitafanya hivyo muda ukifika. Ili kuimarisha vita dhidi ya rushwa Serikali imeamua kuanzisha chombo kinachojitegemea na chenye jukumu sio tu la kuchunguza makosa ya rushwa, bali pia kuelimisha wananchi kuhusu matatizo, madhara na athari za rushwa katika jamii.

Mategemeo yangu kuwa chombo tutakachokiunda kitakuwa madhubuti na kitafanyakazi zake kwa uwezo na uadilifu mkubwa, lakini ili chombo hiki kifanye kazi zake vizuri kinahitaji kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi, kwani wao ndio waathirika wakubwa na tatizo hili la rushwa. Kwa hivyo, natoa wito kwa wananchi wote kuisaidia Serikali katika dhamira yake hii njema ya kupambana na adui rushwa. Kama wanavyosema Wahenga: ”Kidole kimoja hakivunji chawa”. Natarajia wananchi wote wa Zanzibar kutokana na kupenda nchi yao wataunga mkono na kutoa ushirikiano wao katika kulifanikisha jambo hili.

Mabibi na Mabwana,
Katika kuhakikisha kuwa sheria zinafuatwa na haki inatendeka, ni lazima wahusika wote, wakiwa ni watendaji katika vyombo vya sheria, mahakama, taasisi za kodi na taasisi za kutoa huduma mbali mbali, wawe ni watendaji wakweli na waadilifu.

Kwa upande wa mawakili na mahakimu naelewa fika kwamba kabla ya kuanza kazi mnakula kiapo ambacho kinatamka wazi kuwa mtafanya haki bila ya woga, chuki au upendeleo. Viapo kama hivi vipo kwa watendaji wengine. Nasisitiza kwamba ufuatiliaji wa muongozo huu wa kazi utasaidia kuhakikisha utoaji haki kwa watu. Suala hili ni la maadili ambalo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inalitilia mkazo mkubwa kwa watendaji wote wa serikali. Napenda kutahadharisha kwamba sasa baada ya kupitishwa kwa Sheria ya Utumishi wa Umma 2011 (Public Service Act) vitendo vya rushwa na vyengine vilivyo kinyume na maadili havitavumiliwa tena. Wito wangu kwa watu wote ni kwamba sasa tuwe macho na tuache ile tabia ya kuachilia au kufumbia macho uvunjaji wa sheria na maadili kutokana na woga au kumuonea mtu muhali.

Tumetakiwa tufanye kazi zetu kwa ukweli, uwazi na kwa uadilifu. Kuhusu uadilifu tujifunze kwenye Qur-an tukufu, Aya ya 135 ya Surat Annisaa isemayo:

“Enyi mlioamini kuweni wenye kusimamisha uadilifu mnapotoa ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ijapokuwa ni juu ya nafsi zenu, au wazazi wawili na jamaa zenu. Akiwa tajiri au masikini Mwenyezi Mungu anawastahikia zaidi. Basi msifuate matamanio, mkaacha kufanya uadilifu. Na mkiupotosha au mkajitenga nao basi Mwenyezi Mungu anayajua vyema mnayoyatenda.”

Hapa Mwenyezi Mungu anatueleza wazi kuwa matamanio ndiyo yanayompelekea mtu kumiliki nafsi yake upande mmoja, basi msiyafuate matamanio au dharau mkaacha kufanya uadilifu.

Maneno haya ya Mwenyezi Mungu yametiliwa mkazo na Ibara ya II ya Maadili ya Pakistan (code of conduct) ambayo inasema na naomba ninukuu kama ilivyo kwa Kiingereza;

“A judge should be God-fearing, law abiding, abstemious, truthful in tongue, wise in opinion, cautious and forbearing, blameless, untouched by greed. While dispensing justice, he should be strong without being rough, polite without being weak, awe-inspiring in his warnings and faithful to his work, always preserving calmness, balance and complete detachment, for the formation of correct conclusions in all matters coming before him.”

“Hakimu awe mtu mwenye kumuogopa Mungu, anayetii sheria, mwenye kujinyima nafsi, mkweli katika asemayo, mwenye busara katika maoni, ana hadhari na mstahamilivu, asiye na lawama, haongozwi na tamaa. Wakati anaamua anatumia haki, awe thabiti bila ya kukasirisha, mpole bila ya kuwa dhaifu, mwenye kuogopwa na mwenye kutoa nadhari na mwaminifu katika kazi yake, siku zote anazingatia upole, anayejali usawa na asiekuwa na upendeleo, kwa lengo la kutoa uamuzi sahihi kwa masuala yote anayoletewa.”

Huu ni mwongozo mzuri kwa Mahakama na watendaji wote wa vyombo vya sheria. Napenda kumalizia kwa kutilia mkazo juhudi za pamoja ili turudishe imani ya wananchi katika utekelezaji wa maadili ya wanasheria ili tuwe na Utawala Bora wenye kuheshimu haki.
Kuhusu mahakama zetu za mwanzo jambo hili tunalijua kama tunavyoyajua majina yetu, suala hilo tutalimaliza na tutawalipa malimbikizo yao yote.

Mabibi na Mabwana,
Sisi Serikalini tumezingatia kupambana na rushwa, kazi hii tuifanye kwa pamoja bila ya woga na wala kutishika pale tutakapotishwa, tusibabaike, tushirikiane, tusipambane na wala tusitishane katika kupinga wajibu wetu na tusaidiane katika kuwatumikia wananchi wa Zanzibar.
Kwa mara nyengine nawapongeza waandaaji wa shughuli hii na kuwataka waendelee na maadhimisho haya kila mwaka ikiwezekana Unguja na Pemba na kwa shughuli mbali mbali. Serikali kwa upande wake itatoa kila msaada utakaohitajika ili kufanikisha maadhimisho haya nijuulisheni mtakapokwama. Pia, itaangalia suala la bajeti ya Mahakama na lile la kuanzishwa kwa mfuko wa Mahakama ili muhimili huu uweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo nalo tutalifanyia kazi na tutalifanyia kazi katika kipindi kijacho.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.

Advertisements

5 responses to “Siku ya Sheria Zanzibar

  1. Ahsante dr. Shein hata kama watanganyika hawakutambui kuwa wewe rais lakini WAZANZIBAR WOTE tunakutambua kuwa wewe ni rais wa znz. Maadui zetu watanganyika linawauma hili.

  2. hotuba nzuri lakini kusema kitu kimoja na kutenda chengine hilo ndio lilokosekana na kama huko serikalini uaminifu umekosekana sijui nje utetekelezwa vipi kwa kuanzia hio serikali haijatokana na uadilifu kama ni hivyo haiwezekani kusonga mbele na chombo cha hadaa ahsanteni

  3. Mm nimeguswa zaidi na na quran Annisai:135 hii aya imewasimamia wenye imani kwanza ambao ni waislam wanamtambua kuwa Allah ni mmoja ndio huo uwadilifu. Nahisi hata rais anajua uadilifu nchini petu haupo tena nitatoa mifano iliyo hai 1. Iweje muislamu ukubali kulisaliti taifa lako ulilopewa dhamana na kudiriki kulimilikisha kwa lisiyemuhusu! 2.wewe kiongozi wa znz inafika hadi unasema si lazima rais wa muungano awe kwa zamu znz na tgnk 3. Kwanini raslimali za znz zisitumiwe na
    wazanzibari? Mwsho kama rais una uwadilifu ebu tuelezee uadilifu wa serikali ya SMT kwa wazanzibar. Naomba tutafakari!

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s