Hapatakuwa na NGO za ‘briefcases’ kama zitawezeshwa

Na Ally Saleh

Mwishoni mwa wiki Rais wa Zanzibar, Dk Ali Muhammed Shein alizindua Jumuia ya Kuzuia na Kukinya Maafa (DCPM) na kuzungumzia mambo mbali yanayohusu Asasi Zisizo za Kiserikali (NGO) hapa Zanzibar.Kwa hakika DCPM imekuja baada ya tukio la mwaka jana la Septemba 10 ambapo meli ya MV Spice Islander ilizama na kusababisha kupotea kwa maisha ya watu 1370 wakiwemo maiti zao zilizopatikana na wengine ambao Mwenye Enzi Mungu hakujaalia kuwa hivyo.

Kabla ya hapo Zanzibar imekuwa ikipata majanga mbali mbali ambapo fikra pia ya kuanzisha asasi kama hiyo ilikuwa ikija na kuondoka na hata Serikali yenyewe si zamani sana ilianzisha idara yake mahsusi kwa ajili ya kukabiliana na majanga.

Majanga ya upepo, moto na hata mafuriko baada ya mvua kubwa yamekuwa ni baadhi ya matukio yanayoitikisa Zanzbibar pale yanapojitokeza lakini hata wakati mwengine matukio ya miripuko mikubwa ya maradhi kama cholera pia hutikisa jamii ya Zanzibar na huhesabiwa ni majanga ya taifa.

Tukio la Septemba 10, 2012 limetoa mafunzo mengi juu ya haja ya kukinga na kukabili majanga ambapo pamoja na kufanyika juhudi kubwa lakini kumeonekana kuwepo na upungufu mkubwa pia wa zoezi hilo zima kuanzia meli ilipokuwa inazama hadi tulipokunja mabanda katika Uwanja wa Maisara.

Kwa hakika ni suala la kushuruku kuwa kila kitu kilienda, lakini wengi wengi tumekuwa na mawazo kuwa mambo yangeenda vyema zaidi kama tungekuwa na matayarisho mazuri lakini pia taasisi zilizoiva zaidi katika masuala ya kuokoa, kama ilivyohitajika katika suala la MV Spice Islander.

Lakini pia haja ilionekana katika suala zima la kukabili makovu ya majanga. Uhaba wa wataalamu wa saikolojia ulionekana wazi wazi na hadi leo athari ya tukio hilo inaendelea katika akili na mioyo ya watu wengi waliokuwemo katika ajali hiyo lakini pia jamaa zao na wale wote waliokuwa wakisaidia au kuona picha au kusikia sauti za waliokuwa wakitapatapa au waliona maiti nyingi kwa siku moja na zikiwa na mitizamo mbali pamoja na kuwa zikitoka damu saa kadhaa toka kufariki kwao.

Ndipo Zanzibar School of Health (ZSH) , taasisi mpya ya ufundishaji wa mambo ya afya ikaona kuwepo kwa haja ya kuanzisha somo la Counselling Psychology kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Tumaini kilichopo mjini Iringa.

ZSH inataraji kufanya kazi na Serikali na taasisi kama DCPM ili kuweza kutoa mafunzo kwa watu wengi zaidi katika fani hii ambayo inahitajika sana kwenye suala la kukabili na kuzuia majanga, ambayo peke yake ni taaluma kamilifu kwa kila hali.

Ni matarajio yetu kuwa Serikali itashirikiana kama vile ambavyo DCPM itatoa ushirikiano na Serikali katika kuandaa mbinu za kun’gamua ishara za majanga ili yaweze kukabiliwa na mapema lakini pia itakuwa na mbinu za kisasa zaidi za kukabiliana na majanga jambo ambalo linaonekana liko nyuma kwa upande wa Serikali.

DCPM bila ya shaka itafanya kazi karibu na wananchi kwa sababu ni kupitia wananchi ndipo ambapo kazi yao itafanikiwa zaidi kwa vile ni wao ndio walio katika maeneo ya majanga lakini pia ni wao ambao wana taarifa za eneo lao na hivyo kuweza kusaidia kwa mfano kwenye harakati za uokozi.

Maisha mengi ya wanadamu hupotea katika sehemu za majanga katika dakika tano za mwanzo. Ili kukabiliana na hili ni matumaini yetu DCPM itaendesha mafunzo ya kitaifa ya umma juu ya suala la Huduma ya Mwanzo (First Aid) ili sehemu kubwa ya umma iwe inaweza kujisaidia na kuokoa maisha wakati wakisubiri msaada mkubwa zaidi kutoka kwa wataalamu.

Katika hotuba yake kwenye ufunguzi wa DCPM, Dk Shein alitumia muda wake kuzungumzia juu ya suala zima la utendaji wa NGO hapa Zanzibar ambapo kwa sasa idadi yake ya kuandikishwa ni 963.

Dk. Shein alisema anasikitishwa na ule anaosema ni ukweli kuwa nyingi ya NGO hizo ni za mfukoni yaani kwa kimombo “briefcase” ambazo kwa maelezo yake hazina mchango katika jamii kama ambavyo madhumuni ya kuandikishwa kwake yalivyo.

Pia alizungumzia suala la utegemezi ambapo NGO nyingi zimekuwa zikiomba fedha kutoka kwa wafadhili badala ya kujenga au kutengeneza mazingira ya kupata fedha ndani ya michango ya wanachama wake lakini pia kujenga uaminifu wa kutumia fedha zinazopatikana kwa mambo yaliopangwa na sio kuingia mifukoni mwa wana jumuia.

Ningependa kuzungungumzia machache katika eneo hili ambapo nahisi Serikali ingefaa ijue zaidi yanayopita katika taasisi hizi ili mazingira ya kufanya nazo kazi yawe mazuri zaidi kuliko yalivyo hivi sasa.

Kwa fikra zangu hakuna NGO ya “briefcase”. Zote ziliopo zinataka sana kuwa na ofisi na kuonekana mbele ya umma lakini zinakabiliwa na changa moto kubwa sana ya mapato. Kwa sasa tukitaka tusitake watoaji fedha kwa asasi hizi ni Wazungu, kama vile Waafrika au sisi wenyewe ni mafukara au hatujui kutoa msaada.

Sisi tumekulia katika NGO na tunajua namna ambavyo Wazungu wanavyotoa masharti kwa misaada yao na tabaan wana malengo yao na hilo lazima tulikubali tukitaka tusitake. Na masharti haya inawezekana tuyapende au tusiyapende lazima tuyafuate kwa sababu Serikali yetu haina utaratibu wowote au mfumo wowote wa kusaidia asasi za ndani.

Naumia sana tukiiziita NGO zetu kuwa ni za “briefcase” wakati hatuzichangii chochote na kama inavyotegemea Serikali kwa Wazungu na ndivyo asasi hizo pia zinaomba huko huko, wakati naamini kuwa kwa sababu asasi hizi zinafanya kazi ndani ya jamii Serikali ina wajibu wa kuziunga mkono.

Ili dhana ya kuwa mchango wa Serikali ni kutengeneza mazingira mazuri inafaa ipitwe na wakati na Serikali ifunguke zaidi wenyewe au taasisi zake au isonge mbele zaidi na kuweka misingi ya kisheria kwa makampuni binafsi au watu wenye uwezo wawe ni rahisi zaidi kuchangia.

Kwa sasa kuna haja ya Serikali kuzielekeza taasisi kama Shirika la Bandari, Bima, Mfuko wa Barabara, ZSSF, PBZ, ZRB na nyengine kama hizo zijipange vyema ili ziwe na muelekeo wa kusaidai jamii ( corporate social responsibility) kwa kujenga utamaduni wa kusaidia NGO.

Lakini ilivyohivi sasa badala ya taasisi kama hizo kusaidia NGO, basi ni Serikali inayokuwa ya mbele kwenda mara kwa mara katika taasisi hizo kwa misaada hii na ile na kuziwacha taasisi zinazoisaidia jamii katika kupigana na umasikini zikaombe kwa Wazungu na wakiwa wanyonge tunawaita kuwa ni wana wa ‘briefcase”.

Lakini pia tunaweza kurekebisha sheria ili watu wenye uwezo wapunguziwe kodi iwapo watatoa msaada kwa taasisi kama hizi zenye kutumikia jamii ili iwe ni kivutio kwa na sio kwa Serikali hiyo kugombea fedha kwa kuwaendea matajiri wetu kwa haja mbali mbali.

Mie naamini kuwa Serikali inaweza kabisa kuweka kiasi cha asilimia 1 hadi 5 ya pato lake kwa mwaka kuzisaidia NGO, bila ya shaka zile ambazo zitaweza kufuata masharti yatakayowekwa kwa sababu mchango wa jumuia hizo ni mkubwa sana kwa jamii na Serikali huwa inapunguziwa mzigo mkubwa.

Kwa fikra zangu napenda kunukuu msemo wa Kiswahili Mnyonge Mnyongeni lakini Haki yake Mpeni. NGO za Zanzibar zinapita katika wakati mgumu kwa sababu mbali ya kutopata msaada wa Serikali, zina wakati mgumu wa kushindana na NGO kubwa zaidi za Dar es salaam na ambazo ziko karibu zaidi na Wazungu.

Dk. Shein wakati umefika wa kufanya mabadiliko. Tupitie tena Sheria ya Usajili wa NGO na tupitie tena Sera ya Asasi zisizo za Kiserikali ili tuende na wakati na kwa pamoja tuziondoshe hizo zinazoitwa NGO za “briefcase.”

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s