Tibaijuka amepotoka – Jussa

Ismail Jussa Ladhu, Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF)

Nimeona kuna haja ya kutoa maelezo mafupi kuhusiana na Hoja ya Kujadili Jambo la Dharura niliyoiwasilisha Baraza la Wawakilishi na kupitishwa na Baraza hilo tarehe 23 Januari, 2012 baada ya kuona kuna njama za makusudi za kujaribu kuipotosha kutoka upande wa Tanzania Bara, zikiongozwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makaazi, Prof. Anna Tibaijuka.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari ambao anaonekana alikurupuka (au sijui alikurupushwa) kuufanya tarehe 25 Januari, 2012, siku mbili baada ya Baraza la Wawakilishi kujadili na kupitisha hoja niliyoiwasilisha, alikuja na maelezo marefu ya kuthibitisha kwamba Zanzibar ilishiriki kikamilifu katika mchakato wote wa kutayarisha na hatimaye kuwasilisha Andiko Rasmi la kuomba Umoja wa Mataifa kuiongezea Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukanda wa bahari kuu (Exclusive Economic Zone) kwa ziada ya maili za baharini (nautical miles) 150 baada ya kuongezewa maili 200 za awali, eneo ambalo ni sawa na kilomita za mraba 61,000.

Inasikitisha kuona mtu mwenye dhamana ya Uwaziri tena akiwa Profesa anashindwa hata kujiridhisha juu ya undani na uhalisia wa lile analotaka kulitolea taarifa kwa umma. Kama angelifanya juhudi ndogo tu za kuwasiliana na Ofisi za Baraza la Wawakilishi na kuomba kupatiwa nakala ya Hoja niliyoiwasilisha, Prof. Tibaijuka asingepotoka kiasi ambacho alipotoka.

Hoja yangu haikugusia suala la kushirikishwa au kutoshirikishwa Zanzibar katika mchakato huo. Mimi si mjinga wa kiasi cha wale wanaokurupuka kuzungumzia mambo wasiyoyajua hata nishindwe kuona picha inayomuonesha ofisa wa Zanzibar akiwa na ujumbe wa Tanzania Bara uliokwenda kuwasilisha andiko hilo. Isitoshe, hata katika maelezo ya hoja yangu nilinukuu habari iliyochapishwa na gazeti la Nipashe la tarehe 17 Januari, 2012 ambalo liliripoti maelezo yake Prof. Tibaijuka akitaja ushiriki wa maofisa na wataalamu wa Zanzibar katika matayarisho ya andiko hilo. Ndiyo kusema, nilikuwa najua ninachokizungumzia kwa sababu mimi sina tabia wala mwenendo kama wa Prof. Tibaijuka wa kukurupuka kuzungumzia nisichokijua.

Kama angejipa nafasi ya kuitafuta na kuisoma Hoja yangu ambayo sasa si yangu tena maana imeshapitishwa na Baraza la Wawakilishi na hivyo ni Hoja ya Baraza la Wawakilishi angejua kwamba miongoni mwa mambo niliyoyahoji ni hilo la kwa nini Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Mhe. Ali Juma Shamuhuna, na maofisa wa Wizara yake walishiriki katika mchakato huo huku wakijua kwamba Baraza la Wawakilishi lishapitisha maamuzi tarehe 08 Aprili, 2009 ya kukataa ushirikiano katika suala la EEZ na kutaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imiliki na kusimamia wenyewe ukanda wake wa EEZ. Uamuzi huo unajulikana hata na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kutokana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Waziri Kiongozi wa wakati ule, Mhe. Shamsi Vuai Nahodha, kumuandikia Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda kumueleza maamuzi ya Zanzibar yaliyofanywa na Baraza la Wawakilishi.

Kwa upande mwengine, mimi na Wajumbe wengine saba (7) waliochangia hoja hiyo tulikosoa kitendo cha Waziri Shamuhuna kushiriki katika suala hilo bila ya kulitaarifu Baraza la Mapinduzi (ambalo kwa Zanzibar ndiyo Baraza la Mawaziri) ikiwa ni kwenda kinyume na Katiba ya Zanzibar, Ibara ya 43 (5) inayozungumzia uwajibikaji wa pamoja (collective responsibility).

Kitendo cha Prof. Tibaijuka kukurupuka na kujibu hoja isiyokuwepo ya ushiriki wa Zanzibar kinaonesha jinsi asivyo makini katika kazi zake na ndiyo maana akashindwa kupembua na kutofautisha mambo madogo kama haya. Nadhani Rais Jakaya Kikwete anapaswa kufikiria tena uteuzi wake kwa mama huyu ambaye ameonesha dhahiri hana uwezo wa kuchambua mambo.

Kwa upande mwengine, namuonea huruma Prof. Tibaijuka kwa kufanya jaribio la jambo lisilowezekana tena katika Zanzibar ya leo. Kitendo chake cha kuihusisha hoja niliyoiwasilisha na CUF kilikuwa na lengo la kuchochea mgawanyiko wa itikadi za kisiasa katika suala kubwa linalogusa maslahi ya Zanzibar kama hili. Bahati nzuri, angejipa nafasi ya kuwasikiliza Mhe. Hamza Hassan Juma, Mhe. Asha Bakari Makame, na Mhe. Ali Mzee Ali, wote wakiwa Wawakilishi wanaotoka CCM, angejua kuwa zama za kuwagawa Wazanzibari zimepiwa na wakati kwani wote walitahadharisha juu ya uwezekano wa upotoshaji kama ule aliokuja kuufanya Prof. Tibaijuka.

Mwisho, niseme nimesikitishwa na kitendo cha Mhariri wa gazeti la Mwananchi kupitia Tahriri ya gazeti lake la tarehe 26 Januari, 2012, kupotosha kile kilichopitishwa na Baraza la Wawakilishi hadi kufikia kusema kuwa kimetokana na ‘maneno ya mitaani’ huku akijaribu kukionesha kama ni jambo langu binafsi. Kutokana na upotoshaji huo, nimemuandikia Spika wa Baraza la Wawakilishi barua ambayo nitaifikisha Jumatatu ya tarehe 30 Januari, 2012 kumuomba atumie Kanuni ya 116 (2) (a) kumuita Mhariri huyo mbele ya Kamati ya Maadili na Kinga za Wajumbe na kumtaka ajieleze kwa nini asichukuliwe hatua kwa kutenda kosa la jinai chini ya Sheria ya Kinga, Haki na Fursa za Baraza la Wawakilishi (Sheria Nam. 4 ya 2007), kifungu cha 32 (1) (a).

Ismail Jussa
Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe
ZANZIBAR

Advertisements

10 responses to “Tibaijuka amepotoka – Jussa

  1. I’m sure this woudn’t be Zanzibar’s coffin.We have already SAY BIG NO to our partners through our very strong Baraza la Wawakilishi. This is mainly because letting oil and 200 miles of exclussive economic zone to the be a Union matter is tantamount to dump Zanzibaris hopes for the benefit of some few politicians in the Union government. Tanzania is a corruption free zone. Anyone can take anything and no one asks.Look at abundant natural resources. Do they serve Tanzanians,? NO they serve some political oligarchy and their families and the so called investors. We are afraid and this to happen to our precious resource.
    As to Ben Mk. we will never forgive till one day he is brought to justice for massive killings,rape,torture of Zanzibaris in 2001.We will not mind if Tanzanians will forgive him for all what he has done while in office as we know that in Tanzania anyone can do anything and no question. From Radar scam,buying and selling of government assets at cheaper price, going contrary to leadership ethics and sooo many.

  2. Hongera mh.Kwa kumfahamisha huyo prof wa kuchora watu kama hawa ndio wa kuwafahamisha wakaelewa majukumu yao na kuweza kupambanua mambo,wasikurupuke watakufa vinywa wazi kwa kuongea yasiyo wahusu mwambie arudi tena chuoni.

  3. Nakupongesza Mh. Jussa kwa jibu lako makini kabisa. Na na’am, huyu Mhariri anapaswa kuchukuliwa hatua iwe funzo kwa wengine kuwa hawawezi kutumia vyombo vyao kueneza uwongo.

  4. Daima nitakupongeza Mheshimiwa Jussa, Mheshimiwa Ali Mzee Ali, Mheshimiwa Asha Bakar Makame, Mheshimiwa Hamza, na Wazanzibari wote kwa jumla na wengineo ambao wanajali jitihada chanya zinazofanywa ili kuleta upepo wa usawa na haki kwa Zanzibar. Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Hivyo tuungane sote kwa manufaa yetu.

  5. Nikikumbuka kipindi kile cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 nilikua nikisikia ikikaririwa hivi:’Kiongozi Makini na Mwakilishi makini’,hili lilikua na maana ya kumpigia kampeni Mwakilishi wa sasa wa Mji Mkongwe Mh.Ismail Jussa Ladhu,kiukweli hili halikua na chembe ya kusingizia kwa mwakilishi huyo wa Mji Mkongwe,kiukweli huyu ni Mwakilishi na Mwanasiasa na mwanaharakati wa kweli kiutendaji kitu kinachoenda sawa na kauli mbiu tuliyokua tukiisikia ktk kampeni za uchaguzi za chama cha wananchi CUF.Pr.Anna Tibaijuka inampasa ajaribu kuziangalia michango ya kina Hamza na Asha ktk hoja hiyo ya Jussa ambayo sasa imekua ya Baraza na wananchi pia kwa sababu imeshapitishwa kisha ndio atapata jawabu kwamba hii hoja ya Jussa inahusiana na UCUF/UZANZIBARI?!Sidhani kama nina zaidi tena,ila nayapongeza majibu ya Jussa kama nilivyoipongeza hoja binafsi ya Jussa tangu awali.Nalizia kwa kurudia tena kwamba Mh.Jussa ni mwakilishi makini kwa sababu ni msomi na anatetea kwa wazi maslahi ya Zanzibar na wazanzibar!

  6. kumuweka wazi prof. anna kuwa wazanzibari sasa sio wale wa miaka ya nyuma wakawa vibaraka kama mh. shamuhuna. hongera mh. jussa kwa kuijali zanzibar na kutetea zanzibar.. tunawataka viongozi kama nyinyi na sio akina shamuhuna wapenda vingoraa na madaraka

  7. VIONGOZI WA SMZ WASHINDWA KUFAFANUA KUWA BENDERA YA ZANZIBAR INAASHIRIA KUWA ZNZ SI NCHI BALI NI WIZARA YA TANZANIA. Ewe mzanzibari hakikisha mwenyewe kwa kuangalia bendera zote za wizara za TZ kama vile bendera ya BUNGE LA TZ, BENDERA YA POLISI WA TZ, BENDERA YA JWTZ WA TZ NA BENDERA YA SMZ, utagundua kuwa kuna kibendera kidogo cha muungano juu yake. Kibendera hicho kinaashiria wizara ya TZ.

  8. Mimi nakuombea heri na baraka Mheshimiwa Jussa, Moka akulinde na maovu ya hao wasoitakia kheri znz. HONGERA HONGERA HONGERA JUSSA.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s