SMT ilipuuzia maazimio halali ya BLW – Jussa

Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF) Ismail Jussa Ladhu leo amewasilisha hoja ya dharura katika kikao cha Baraza la Wawakilishi juu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwasilisha maombi ya kutaka eneo la ukanda wa Bahari ya Hindi

Katiba ya Zanzibar, Ibara ya 1 inaeleza, “Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake, ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar”
HOJA YA KUJADILI JAMBO LA DHARURA

(CHINI YA KANUNI YA 42 (1), (4), (5), (9) na (10) YA KANUNI ZA BARAZA LA WAWAKILISHI, TOLEO LA MWAKA 2011)

KUHUSIANA NA HATUA YA SERIKALI YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KUWASILISHA MAOMBI KWENYE UMOJA WA MATAIFA (UN) YA KUTAKA KUONGEZEWA UKANDA WA BAHARI KUU (EXTENDED CONTINENTAL SHELF) IKIWA NI NYONGEZA YA ENEO LA UKANDA WA UCHUMI BAHARINI (EXCLUSIVE ECONOMIC ZONE – EEZ) KWA ZIADA YA MAILI ZA BAHARINI (NAUTICAL MILES) 150 BILA YA KUZINGATIA MAAZIMIO YA BARAZA LA WAWAKILISHI YA MWAKA 2009

Mheshimiwa Spika,

Kwa kutumia Kanuni ya 42 (1), (4), (5), (9) na (10) ya Kanuni za Baraza la Wawakilishi, Toleo la mwaka 2011, na kufuatia ruhusa ulioitoa katika kikao cha tarehe 20 Januari, 2012, nina heshima kubwa kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar tunaowawakilisha hapa katika chombo chao hichi kitukufu kuwasilisha hoja hii ya kujadili jambo la dharura kuhusiana na hatua ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwasilisha maombi kwenye Umoja wa Mataifa ya kutaka iongezewe eneo la ukanda wa bahari kuu yaani (Extended Contintental Shelf) kwa ziada ya maili za baharini (nautical miles) 150 ikiwa ni nyongeza ya ziada ya eneo la maili za baharini (nautical miles) 200 za Exclusive Economic Zone (EEZ) zilizokwisha tolewa katika mwaka 1989.

Mheshimiwa Spika,

Kanuni ya 42, fasili ya (10), inaeleza kwamba, “Kwa madhumuni ya Kanuni hii jambo lolote litahesabiwa ni muhimu kwa Umma iwapo litagusia maslahi ya nchi au wananchi wake na utatuzi wake utategemea hatua zaidi kuliko zile za utekelezaji wa kiutawala peke yake.” Kwa maoni yangu na naamini maoni ya Waheshimiwa Wajumbe wengi wa Baraza hili tunaamini jambo hili linatimiza masharti hayo.

Mheshimiwa Spika,

Taarifa za kuwepo maombi haya tulizipata tarehe 16 Januari, 2012 pale Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makaazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Prof. Anna Tibaijuka, alipofanya mkutano na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam na kueleza dhamira hiyo. Likiandika taarifa za mkutano huo, gazeti la Nipashe la mjini Dar es Salaam la tarehe 17 Januari, 2012, lilieleza:

“Tanzania imetangaza kuwasilisha maombi Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN), jijini New York, nchini Marekani, kudai umiliki wa eneo la ziada nje ya maili 200 za Ukanda wa Kiuchumi Baharini (EEZ) katika Bahari Kuu ya Hindi, ili iweze kulifanyia utafiti zaidi kuhusu rasilimali zilizoko chini ya bahari kwa lengo la kuinua uchumi wa nchi.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, rasilimali hizo ni pamoja na mafuta, gesi na madini.
Eneo hilo linatokana na ongezeko lingine tena la maili 150 na hivyo kufanya jumla ya mpaka hadi maili 350, ambazo ni sawa na kilomita 560 kutoka kwenye ‘baseline’.
Waziri Tibaijuka alisema maombi hayo yanatarajiwa kupelekwa na jopo la wataalamu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar na wajumbe wawili kutoka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, litaongozwa na Waziri Tibaijuka.”

Mheshimiwa Spika,

Kwa mujibu wa Andiko la Kitaalamu lililowasilishwa Umoja wa Mataifa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuhusiana na maombi hayo na ambalo liliwasilishwa rasmi tarehe 18 Januari, 2012, na ambalo nimebahatika kupata nakala yake, eneo hilo la ziada lililoombwa litakuwa sawa na kilomita za mraba 61,000 katika ukanda wa bahari kuu. Aliyewasilisha si Waziri anayesimamia mambo ya Muungano kwani Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makaazi, vyote si mambo ya Muungano.

Mheshimiwa Spika,

Ukiangalia ramani ya eneo lililoombwa ambayo inapatikana kwenye ukurasa wa 13 wa Muhtasari (Executive Summary) ya Andiko hilo, na ambayo kwa faida ya wajumbe wa Baraza lako tukufu, nimeiambatanisha pamoja na maelezo ya hoja hii, utagundua kuwa sehemu kubwa mno iliyoombwa ni eneo la bahari kuu ambalo kimsingi liko upande wa mashariki wa visiwa vya Unguja na Pemba. Ndiyo kusema mwenye haki ya kuomba eneo hili na kufaidi rasilimali zilizomo (ikiwa zimo) ni nchi ya Zanzibar.

Mheshimiwa Spika,

Katiba ya Zanzibar, Ibara ya 1 inaeleza, “Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake, ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar”

Mheshimiwa Spika,

Baraza lako tukufu katika kikao chake cha tarehe 08 Aprili, 2009, (Baraza la Saba, Mkutano wa Kumi na Tano), lilikuwa na mjadala mzito wa siku tatu mfululizo kuhusu ‘Taarifa ya Mapendekezo ya Serikali kuhusu Ripoti ya Mshauri Muelekezi juu ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia’ ambapo kutokana na uzito wake, wajumbe 49 wakiwemo Waheshimiwa Mawaziri wengi wa wakati ule na pia Waheshimiwa Mawaziri wengi tulio nao sasa walichangia mjadala huo, tena kwa hisia kali za kizalendo na mapenzi ya kweli kwa nchi yetu tukufu. Baada ya mjadala huo, hatimaye wewe Mheshimiwa Spika uliingia katika historia kwa kuwahoji Wajumbe kuhusiana na maazimio matatu yaliyowasilishwa na Serikali. Azimio la tatu lilikuwa la aina yake na ili tujikumbushe hali ilivyokuwa naomba uniruhusu ninukuu moja kwa moja kutoka kwenye Taarifa Rasmi (Hansard) ya Baraza kwa siku hiyo ya tarehe 08 Aprili, 2009, ukurasa 71 – 72 kuhusu suala hilo kama ifuatavyo:

“Pendekezo la Tatu:
Waheshimiwa Wajumbe naomba niwahoji wale wanaokubaliana na pendekezo la EEZ sehemu ya Bahari Kuu, serikali inashauri kwamba Wajumbe wakubali kwamba suala hili liende kwa mashirikiano ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wale wanaokubali pendekezo hilo wanyanyue mikono.

Wanaokubali pendekezo hilo…
Wanaokubali pendekezo hilo…

(Hoja ilitolewa iamuliwe)
(Hoja iliamuliwa na kukataliwa)

Kwa hivyo pendekezo hili lisahihishwe na inavyoonekana kufuatana na michango ya WaheshimiwaWajumbe kwamba eneo hili pia liwe katika mikono ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Ni sawa ndio tunachokubali hicho.

Wajumbe: Sawa.

Mhe. Spika: Wanyanyue mikono basi Waheshimiwa Wajumbe, wale wanaokubali. Na wale wanaokataa.

Mhe. Waziri wa Utalii, Biashara na Uwekezaji: Mhe. Spika naafiki.

(Hoja ilitolewa iamuliwe)
(Hoja iliamuliwa na kuafikiwa)

Mhe. Spika: Kwa hivyo, pendekezo la eneo la Bahari Kuu katika suala zima la utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi liwe katika mikono ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hayo ndio mapendekezo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, yaliyopitishwa leo hii tarehe 08/04/2009 saa 7:00 mchana.”

Mheshimiwa Spika,

Nimekuomba ruhusa yako ninukuu sehemu hiyo ili Waheshimiwa Wajumbe tuelewe kilichoamuliwa na Baraza lako tukufu, na maamuzi hayo ni halali hadi wakati huu kwa sababu hakujatolewa azimio jengine la kuyafuta au kuyabadilisha.

Mheshimiwa Spika,

Inaeleweka kwamba baada ya Baraza kupitisha azimio hilo na yale mengine mawili yaliyolitangulia, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia kwa aliyekuwa Waziri Kiongozi wakati huo, Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha, iliiandikia rasmi Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda, kuiarifu juu ya msimamo wa Zanzibar na kutaka hatua zichukuliwe kuyaondoa masuala hayo katika orodha ya mambo ya Muungano. Hilo halijatekelezwa hadi sasa ingawa kutokutekelezwa kwake hakubatilishi maamuzi ya Baraza lako tukufu.

Mheshimiwa Spika,

Suala la kuihoji Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya hatua ilizofikia katika kusimamia utekelezaji wa maazimio hayo limekuwa likiibuliwa mara kwa mara katika mikutano ya Baraza lako hili. Mara ya mwisho wakati wa kikao cha Bajeti cha mwaka 2011, Serikali iliwataka Waheshimiwa Wajumbe wawe wavumilivu na kuliacha suala hilo lije litekelezwe wakati wa mjadala wa kupata Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika,

Kwa msingi huo ingetegemewa basi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano isichukue hatua zozote zitakazopelekea kuyafanya maazimio haya ya Baraza la Wawakilishi ambayo sasa ndiyo msimamo rasmi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yakawa hayana maana tena. Kitendo cha kupeleka maombi Umoja wa Mataifa kutaka kuongezewa ukanda wa bahari kuu ambao tayari Zanzibar imeamua kila upande isimamie wenyewe, ni kwenda kinyume na dhamira (spirit) hiyo na hakiashirii kuwepo kwa nia njema.

Mheshimiwa Spika,

Mimi binafsi na Waheshimiwa Wajumbe wenzangu, tumeshtushwa sana na kauli ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Mheshimiwa Ali Juma Shamuhuna, aliyoitoa kwenye Baraza hili siku ya Ijumaa ya tarehe 20 Januari, 2012 kwamba yeye hafahamu kuwepo kwa azimio hili, na kwamba yeye na Wizara yake imeshirikishwa na imeshiriki kikamilifu katika kuandaa Andiko lililofikishwa Umoja wa Mataifa. Bahati nzuri amekiri kwamba suala hilo amelifanya bila ya kulitaarifu Baraza la Mapinduzi ambalo kikatiba ndilo msimamizi mkuu wa maamuzi ya kisera kwa Zanzibar.

Mheshimiwa Spika,

Kiongozi wa Shughuli za Serikali katika Baraza la Wawakilishi ambaye ni Makamu wa Pili wa Rais, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, aliliomba Baraza kwamba suala hili ilivyokuwa halijafikishwa kwenye Baraza la Mapinduzi basi waachiwe Serikali wakalijadili na halafu wataleta taarifa mbele ya Baraza hili katika kikao kijacho. Kimsingi tulikubaliana na ombi hilo isipokuwa kutokana na uzito wa suala lenyewe na jinsi lilivyogusa hisia za wananchi wa Zanzibar ambao ndiyo tunaowawakilisha hapa, tukaomba tupewe nafasi ya kulijadili kupitia hoja hii ya kujadili jambo la dharura na kupata fursa ya kutoa mapendekezo yetu ambayo tungependa Baraza la Mapinduzi liyazingatie wakati wanatafakari hatua za kuchukua.

Mheshimiwa Spika,

Baada ya maelezo hayo, sasa basi nipendekeze kwa Baraza lako tukufu kwamba lilitake Baraza la Mapinduzi wakati wa kujadili suala hili lizingatie mambo yafuatayo:

1. Kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iiandikie rasmi Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuitaka isimamishe mchakato wote wa maombi ya kutaka kuongezewa eneo la ukanda wa bahari kuu yaani (Extended Contintental Shelf) kwa ziada ya maili za baharini (nautical miles) 150 ikiwa ni nyongeza ya ziada ya eneo la maili za baharini (nautical miles) 200 za Exclusive Economic Zone (EEZ) hadi hapo suala hilo litakapopatiwa ufumbuzi wakati wa mjadala wa Katiba Mpya.

2. Kwamba iwapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haitochukua hatua za kusimamisha mchakato huo, basi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipeleke ujumbe wake na barua rasmi Umoja wa Mataifa kuutaka usimamishe kushughulikia maombi hayo hadi hapo suala la mchakato wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano utakapomalizika na kukubaliana maeneo ya ushirikiano na maeneo ambayo kila upande utayasimamia wenyewe.

3. Kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iitake Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusitisha shughuli zote ambazo zinahusiana na kutumia rasilimali zilizomo eneo la ukanda wa bahari kuu (EEZ) hadi hapo suala hili litakapomalizwa baina ya pande mbili, na

4. Kwamba iwapo hatua hazitochukuliwa kuhusiana na mambo hayo, basi Zanzibar haitofungika na chochote kitakachoamuliwa kuhusiana na mambo hayo ambayo hayakushughulikiwa na Zanzibar yenyewe.

Mheshimiwa Spika,

Naomba kutoa hoja.

ISMAIL JUSSA LADHU
MJUMBE WA BARAZA LA WAWAKILISHI
JIMBO LA MJI MKONGWE

Advertisements

16 responses to “SMT ilipuuzia maazimio halali ya BLW – Jussa

 1. Hawa ndio Wawakilishi tunaowataka watutumikie. Sio wale wanaokwenda barazani kwa ajili ya maslahi yao na ya vyama vyao tu.Nna hakika fimbo ya Chama hapa itatumika kuwanyamzisha baadhi ya Waawakilishi au kulifanya suala hili lionekane ni la upande mmoja tu. Wazanzibari sasa tuamke na tuangalie nani yupo pale kwa maslahi yake na ya chama chake na nani yupo kwa maslahi ya Zanzibar na Wazanzibari kwa ujumla.Wakati wa kuamka ni sasa wenzetu wameanza kujikatia mapande bila hata kujali wenye nchi Kwani tulishaamua zamani juu ya suala hili tokea tarehe 8/4/2009 kua suala la bahari watuachie wenyewe.

  • tunaiyomba serekali kushughulikia jambo hili kwa haraka sana pia wajumbe wa baraza lawawaakilishi wazidi kushikamana ili kwa uwezo wa allah iwe sababu ya zanzibar kutoporwa eneo lake.Wazanzibari tupo pamoja na wao

 2. mimi nasema siku zote watanganyika hawajali utu wao wanajali mali tu,huuwana wenyewe kwa wenye mtu anaweza kummkata mwanawe kiongo na akaenda kumuuza ati albino ,,,, Mi nadhani muungano ufikie tamat tena tumechoka kuonekama mabaradhuli… huwezi ukafanya biashara na mtu anaekuendea kunyume , na mimi nasema hasa watanganyika wanataka kutumeza.. Naomba RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE atowe tamko kuhusu hili. jamani wazalendo jee tuna haja ya kuwa na muungano!!!!!!! mie nasema simsamehe mtu yeyote alienganisha visiwa hivi na maaduwi hawa wadhalim wakubwa. Inshallah Mwenyezi mungu hatolisimamisha hili ila kwa kweli hatuna imani na muungano wa aina yoyote labda EAC tu basi .

 3. what about we part ways guys…cuz’ most pple in the main land do not see any benefit of union..everyday noise..noise ..noise from your side …we can part ways and stay in peace…

 4. Kwanza mheshimiwa Jussa, lkn pia tunaitaka Serikali iiamuru SMT na sio kuiomba kusitisha maombi hayo na haraka SMZ itume wjumbe UN kwa lengo la kwenda kupinga maombi hayo haraka iwezekanavyo hatutaki mzaha ktk rasilimali ztu tena wakae mbali nazo haziwahusu waache wizi..

 5. ASALAM ALAYKUM!

  Jussa tutampongeza lakini tutamuomba achokoe zaidi, kwani hili ni mmoja kati ya mambo ambayo tunasema ni katika Kero za Muungano.

  kuna Mikataba ya Kaimataifa, Convention y akila namna amabayo Tanzania yameridhia lazima nayo hayo yapitiwe na vilevile kuna haja ya kupata Focal Point kwenye kila Mkataba na kuipitia na kujua hali ya Mikataba hiyo, kipi kwa faida ya Zanzibar.

  Mie nimehisi kua Jussa amefany akazi kubwa, lakini kwasasa kuna haja yeye na wenzake wagawane majukumu ya kuipitia Mikataba yote ya Kimataifa na kuangalia sehemu ya Zanzibar imefaidikaje na kama hakuna basi uandaliwe mkakati.

  Masuala kama haya yanataka hata NGO’s nao wapewe majukumu na wnaanchi wafahamishwe na hata suala hili kunahitajika wananchi wafahamishwe kwa lugha nyepesi na wananchi waweze kuelewa na wataalamu wetu wanapofika katika vyombo vya habari wajitahidi kama wawezavyo wazungumze kwa lugha inayofahamika na kila mtu.

  Jambo liloniosha tena kwa marashi ya wardi ni pale umoja ulipojitokeza katika kulijadidli suala hili na vilevile Spika kwa upande wake kulivalia njuga.

  Mwanzo wa Safari.

  Ngaridjo Onana

  Hamza Z. Rijal

  • Ah hawa watanganyika wapata kiburi chote hichi kwa kukalia kiti cha zanzibar UN kwa nn zanzibar ickidai kiti chake 2kaona kama wataomba bahari au uwanachama wa UN

 6. Assalam allaykum!!

  Kwa mtazamo, utaona wazi kua chimbuko la tatizo hili ambalo lililo ikumba zanzibar kwa sasa na lenye kutishia kwa kutoweka moja kwa moja kwa zanzibar ni Pale tulipo fanya Muungano wa Katiba. na Hii ni mbinu ya hali ya juu kuwa baada ya kusuasua kwa Raslimali za zanzibar ambazo sinasadikika kuepo (Mafuta, Gesi asili nk.) katika ukanda wa bahari. pande za zanzibar, na kukataliwa na wazanzibar kua mambo ya muungano. ndo Ikazalika mbinu hii na kua baadhi ya viongozi wetu waliikubali kwa maslahi yao binafsi. hii ni mbinu ya kuthibitisha kua Zanzibar si nchi kwa maandishi na kwa matendo. badala tu ya kuepo midomoni mwa viongozi wa tanganyika.
  Hali hii si ya kuifumbia macho kabisa ikiwa kama kweli bado wazanzibari tunataka tuwe na nchi yetu. (zanzibar). na tunawataka kua wasitishe maombi hayo kwamba wazanzibari hatujaridhika nayo.
  na ikiwa watakataa kusimamisha maombi yao, na kufanikiwa Umoja wa mataifa, basi nikubaliane na Mh.Jussa pamoja na Baraza la wawakilishi la Zanzibar. Kua Zanzibar haitofungika na chochote kitakachoamuliwa kuhusiana na maombo hayo ambayo hayakushughulikiwa na Zanzibar yenyewe. na Suluhu ya tatizo hili na mengineo (kero za muungano,zanzibar ni nchi, nk) ni KUUVUNJA MUUNGANO ambao ndio unaotoa fursa kubwa kwa viongozi wa tanzania kupata nafasi ya kutudhalilisha, kutudhulumu, na kuhujumu Uchumi wa nchi yetu.
  ZANZIBAR DAIMA!!.

  Abdallah Sulayman

  zanzibar

 7. wanzanzibar sasa tuamke tukilala tuu sisi hatutokuwa na tofauti na palestina walivyo sasa hapo tukifika tutakuja hubakia kutafuna vidole tuu. na watu kama hawa shamhuna inabidi washuhulikiwe ndio wasaliti wenyewe hawe waji……… wakumbwa hawa.

 8. 2kisema hawa c ndug ze2 co kosa maana ndugu humjali mwezake kinyume kumkandamiza mwezake ni uadui co wajitawale wao

 9. Asante sana. May I ask, if there is a short summary in English available, please, because my Kiswahili is not very advanced?

 10. NIKIWA KAMA MZANZIBARI IWEJE SISI TU TUFUNGIKE NA MUUNGANO WATANGANYIKA WAO WASIFUNGIKE? SMZ NAYO IVUNJE MUUNGANO KWANI WATANGANYIKA WAO WASHAUFUNJA TOKEA WALIPO MTANGAZA WAZIRI MKUU WA MWANZO JAMBO AMBALO HALIMO KTK MUUNGANO.

  SMZ AMKENI HAKUNA MZANZIBARI ANAETAKA MUUNGANO HATA ALIEKO TUMBONI

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s