Raza anavyochochea mabadiliko Uzini

Hatimae Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi imependekeza jina la Mfanyabiashara Maarufu wa Zanzibar, Mohammed Raza Daramshi, kuwania jimbo la uchaguzi Uzini wilaya ya kati Unguja

Kalamu ya Jabir Idrissa

SIKUSUDII kamwe kushinikiza Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufanya maamuzi kisiyoyaamini. Ila najua wakithubutu, wataumbuka. Nimependa tu leo kueleza hisia za wananchi wa jimbo la Uzini, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini, Unguja, walioamua kumsogeza karibu Mohamed Raza, mfanyabiashara mashuhuri na kada mkubwa wa chama hicho. Maelezo ya fitna, ubaguzi uliopitiliza, udhalilishaji dhidi ya wananchi wa jimbo hili na kampeni ya kijinga dhidi ya matakwa yao inayofanywa na baadhi ya watu ndio yaliyonipeleka huko. Chimbuko ni uchaguzi mdogo. Wapigakura wa jimbo hili wanajiandaa kumchagua mjumbe wa Baraza la Wawakilishi mwezi ujao.

Kiti kimekuwa wazi tangu pale Mussa Khamis Silima, aliyekuwa mwakilishi wao, alipofariki dunia kwa ajali ya gari mkoani Morogoro wakati akirudi kuhudhuria vikao vya bunge mjini Dodoma . Alikuwa mmoja wa wabunge watano watokanao na Baraza la Wawakilishi. Vyama vimeanza kutafuta wagombea kwa ajili ya uchaguzi huo.

Kila mpenda ukweli anajua jimbo hili ni moja ya majimbo ngome kuu za CCM. Mara zote tangu mfumo wa vyama vingi urudishwe mwaka 1992, CCM siyo tu hushinda, bali kinashinda kwa kura nyingi.

Rekodi zinaonesha hakijashuka asilimia 90 ya kura zilizopigwa katika uchaguzi wote uliowahi kufanyika. Katika uchaguzi wa 2005, Muhammed Seif Khatibu, aliyegombea ubunge – na mpaka sasa kuwa mbunge wa jimbo hili – alijitapa bungeni kwamba yeye ndo mbunge aliyepata kura nyingi zaidi katika wale waliochaguliwa majimboni. Alipata asilimia 94.

Kitu kibaya kwa jimbo hili linalotegemea zaidi shughuli za kilimo, ni kuwa miongoni mwa majimbo yenye maendeleo duni Zanzibar . Halina huduma nzuri za afya, vituo vingi vya afya ni vikongwe na havina madaktari wajuzi.

Sehemu kubwa ya watu wana kiwango kidogo cha elimu. Hata ile skuli ya Ndijani ambayo ni moja ya skuli kongwe wilayani, imezorota.

Skuli nyingi majengo yake yamechakaa. Hazina maabara na pale zilipo, hazina vifaa vya kutosha na vya kisasa.

Walimu wake wamechoka kwa kukosa motisha kama vile kozi za mara kwa mara na maslahi bora. Wengi wao wanaishi mbali na pale wanapofundisha na kila mwezi hulazimika kufuata mishahara yao wilayani.

Ingawa asilimia kubwa ya watu ni wakulima na wafugaji, huduma za elimu kwa wakulima na wafugaji zingali tatizo kubwa.

Mpaka sasa wakulima wa jimbo hili, kama ilivyo kwa majimbo mengine, wanalalamikia wimbi kubwa la wizi wa mazao mashambani. Mara kadhaa utasikia mkulima kaibiwa mazao yake wakati akijiandaa kuvuna.

Unaweza kuondoka shambani kwako jioni na kupanga kurudi kesho yake kukata ndizi zilizokomaa vizuri, unapigwa na butwaa kesho ile kukuta jamaa wamekutangulia. Ni hivyohivyo kwa muhogo, majimbi na hata nazi. Wezi wa mazao hawachagui cha kuiba; huiba kila wanachoona watakiuza kwa urahisi.

Hakuna jitihada za dhati za serikali kutatua tatizo hilo . Udhaifu huo umesababisha watu wengi kuuliwa kwa vipigo wanapokutwa wameiba mazao. Watu wanachukua sheria mikononi kwa sababu dola haijaona hilo ni janga.

Huduma ya maji safi ndio yenye afadhali. Karibu vijiji vyote vinapata maji haya na hivyo kupunguza harubu za kusaka maji mbali na wanapoishi. Lakini pia, kwa vile vijiji visivyo maji ya mifereji (Bara huitwa maji ya bomba), wanapata maji kutoka visima vilivyochimbwa miaka mingi iliyopita. Ingawa kiasili haya ni maji safi , lakini usalama wake kiafya unatiliwa shaka.

Ni juzi tu barabara kuu ya jimbo hili – Mitini mpaka Mchangani – imejengwa upya kwa kiwango cha lami. Hiyo ni baada ya karibu miaka 20 ikiwa mbovu. Lakini barabara ndogo zinazounganisha maeneo ya ndani ya vijiji, nyingi ni za udongo ambazo ni shida kupitika wakati wa mvua.

Hayo yanatosha kuonesha wanajimbo wanasakamwa na umasikini. Na yawezekana hali hiyo imeongeza tatizo la maendeleo duni ya elimu ya watoto wao.

Asilimia kubwa yao huishia kidato cha pili, kiwango cha elimu ya lazima kwa Zanzibar . Kiwango cha elimu ya lazima kilipokuwa kidato cha tatu, watoto watatu tu kati ya kumi, kwa wastani, ndio walivuka. Mimi nilivuka mwaka 1979.

Uthibitisho wa ukweli huu ni watendaji waliopo ofisi ya wilaya wengi wao wanatoka nje ya jimbo. Hata kwa CCM, wafanyakazi wengi wa nafasi za kitaaluma waliopo ofisi ya wilaya, ni wageni. Matatizo haya yanalalamikiwa sana na wanajimbo. Na hapana shaka yamechangia kuwasukuma kubadilisha mwelekeo katika kuchagua viongozi.

Watu wa jimbo hili wamekaa na matatizo yote hayo wakati viongozi wawakilishi wao wote ni wenyeji wa asili wa vijiji vya jimboni. Taja diwani wa wadi, mwakilishi na mbunge wa jimbo hili, wote wana asili ya vijiji vya jimbo la Uzini.

Kinachosikitisha sasa, na wanajimbo wenyewe wanasikitika, ni kule kuendelea kwao kuishi katika ufukara wa kiwango hicho wakati wamekuwa wakichagua ndugu zao na kuwapa dhamana ya kuwawakilisha kwenye vyombo vya maamuzi. Sasa, wameamua kuleta mabadiliko. Wapo tayari kumchagua mtu wanayejua fika ametoka mbali na jimbo lao. Raza anatoka Shakani, Wilaya ya Magharibi, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Ishara ya hamu ya mabadiliko inaonekana wazi. Raza amepewa kura nyingi wakati amegombea uteuzi na watu 10 wenyeji, akiwemo Othman Maulid, kijana aliyekuwa wa pili katika kura za maoni za CCM katika kutafuta mgombea uwakilishi uchaguzi wa 2010. Raza alipata kura 1,968 wakati Othman alipata kura 642 na Khalfan Salum Suleiman kura 535.

Haya ni mabadiliko makubwa. Lakini ni mabadiliko waliyoyajenga watu wenyewe wa jimbo. Siamini kuna mtu aliyewasukuma kutamani mabadiliko na kutoa ishara hasa kuwa wanataka mabadiliko hayo. Kama mchambuzi, naona dhahiri wameamua kwa sababu imekuja tu bahati ya Raza kuamua kuingia katika mbio za kutaka awe mwakilishi wao. Pengine Raza alijua, akipita tu CCM, ameingia barazani.

Kule tu kujiingiza kwake katika kinyang’anyiro ndani ya CCM, chama wanachokiamini zaidi, kumewajenga moyo wanajimbo wa kufanya maamuzi magumu. Maamuzi haya kumbe yamesononesha wengi, wakiwemo wageni wa jimbo. Wanajimbo wanajiuliza, “nini hasa kinachowaumiza roho hata kuchukia maamuzi yetu?” Wahenga walisema, “Pilipili usiyoila yakuwashiani.” Wao inawahusu nini na ugombeaji wa Raza wakati hatakuwa mwakilishi wao? Atakuwa mwakilishi wa Uzini.

Kwa wale wanajimbo, kwani uharamu wa Raza kama kada wa CCM, umeanza lini? Wamechapisha katika mtandao wa Mzalendo.net ambao wengi wa washiriki wake kwenye mijadala ni Wazanzibari wa kuzaliwa, maoni chini ya walichoita “Barua ya wazi kwa Mhe. Kikwete – Uwakilishi wa Raza waleta manung’uniko.”

Ni uchafu kuyaeleza maana yanaashiria ubaguzi, chuki za kijinga, udhalilishaji wanajimbo, na upotoshaji mambo. (Wiki ijayo nitauweka hadharani na kuuchambua). Wanamsema Raza na kumuita “Mhindi asiyestahiki kuwa mwakilishi wa Uzini.” Wanamshawishi Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, asikubali jina la Raza kupitishwa kugombea uwakilishi.

Mwenyekiti Kikwete atakuwa muongoza kikao cha Kamati Kuu wiki hii, kinachopitisha majina ya wagombea. Ni hawahawa waliochomeka hoja dhaifu katika vikao vya Kamati za Siasa za CCM wilaya na mkoa vilivyojadili majina ya waombaji baada ya kura ya maoni kupigwa. Leo wanajitia kuhoji jimbo hili kutoa mwakilishi kutoka nje badala ya vijana wenyeji. Mbona hawaulizi kwanini jimbo ni duni kimaendeleo wakati vipindi vyote wamechaguliwa wenyeji?

Baadhi yao wamefikia kuwa mawaziri lakini wameshindwa kusaidia vijana wanajimbo kutimiza ndoto zao za kusoma hadi kiwango cha chuo kikuu. Mbona hawajauliza na kuwauliza wawakilishi hao? Vijana ambao siku hizi ndio wapigakura wengi zaidi popote pale nchini, wameanza kampeni kuhakikisha Raza anachaguliwa dhidi ya mgombea mwingine yeyote atakayepambanishwa naye.

Langu jicho!

Advertisements

5 responses to “Raza anavyochochea mabadiliko Uzini

  1. Jaman wazanzibar 2natakiwa kuibadilisha zanzibar kuifanya kua zenj yenye maendeleo haya yatatokea pale 2 2tapo wachagua viongozi wenye kupenda maendeleo na sio maslahi yao wa2 wa uzin mna nafas ss ya kuchagua maendeleo au kurudisha maendeleo kwa kuchagua m2 imara kwa maendeleo yenu jamani fanyeni mambo cc 2lombali na zenj 2we na hamu ya kurudi kwe2 kwa kufanya kazi na kujenga taifa kazi kwenu wa2 wa uzin one chance one goal be care

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s