Siri ya mafanikio yetu ni umoja- Dk Shein

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein akiwapungia mkono wananchi waliofika kusherehekea miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliofanyika Januari 12 mwaka 1964 ambayo yaliuondoa utawala wa kifalme

Sherehe za miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizofanyika katika uwanja wa Amaan zimefana huku zikionesha umuhimu wa kuwepo kwa mshikamano mkubwa wa wananchi wa Unguja na Pemba. Sherehe hizo zinafanyika huku Wazanzibari wakiunganishwa na Serikali ya umoja wa kitaifa inayotokana na maridhiano ya kisiasa ambayo lengo lake kuondosha siasa za chuki na uhasama.

Mbwembwe za viongozi wa kitaifa wakati wakiingia katika uwanja wa amaan pamoja na gwaride la vikosi vya ulinzi ni miongoni mwa matukio muhimu ambayo yalifanikisha na kuzipamba sherehe za miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizofanyika katika uwanja wa Amaan.

Wananchi waliwashangilia viongozi wakuu wa kitaifa akiwemo rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Sheni ambaye aliingia uwanjani hapo akisindikizwa na mapikipiki ya askari wa polisi yapatayo 10.

Lakini kiongozi aliyevutia mara baada ya kuingia katika uwanja wa Amaan ni rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jakaya Kikwete ambapo kwa kawaida wanajeshi humsalimia kwa kupiga wimbo wa taifa.

Akilihutubia taifa katika kilele cha maadhimisho ya miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar; Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Sheni amesema malengo ya Mapinduzi ya mwaka 1964 yataendelea kutekelezwa ikiwemo kuwapatia wananchi wote huduma muhimu za jamii na maendeleo bila ya ubaguzi na kudumisha umoja.

Dk Shein alisisitiza suala la umoja na mshikamano wa wananchi wote wa Unguja na Pemba, na kusema ndiyo siri na mafanikio yote ikiwemo utulivu wa kisiasa.

Aliwataka wananchi wote wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao katika mchakato wa Tume ya marekebisho ya katiba wakati ukifika.

‘Wazanzibari wana haki ya kutoa maoni katika mchakato wa katiba mpya…..toweni maoni yenu kwa uhuru bila ya jazba ‘alisema na kuungwa mkono na wananchi kwa kusherehekea.

Alisema utaratibu huo wa kidemokrasia ndiyo njia pekee ambayo utawawezesha Watanzania kupata katiba itakayokidhi matakwa ya wote.

Aidha hakusita kugusia suala la kuimarishwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kupatiwa ufumbuzi wa kero za Muungano kupitia kamati ya pamoja chini ya makamo wa rais Dk Mohammed Gharib Bilali ni muhimu.

Dk Shein alisema malengo ya Mapinduzi ni muhimu kutekelezwa na kusimamiwa kikamilifu kwani ndiyo yaliyopelekea wananchi wa Zanzibar kufanya Mapinduzi na kuuondoa utawala wa kikoloni.

Alisema huduma za maji safi na salama, elimu kwa watoto wote wenye uwezo wa kwenda shule pamoja na huduma za afya na kutunza wazee wasiojiweze zitaendelea kutolewa.

‘Malengo ya Mapinduzi ya mwaka 1964 yataendelea kutekelezwa na kusimamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya umoja wa kitaifa…..tutawapatia wananchi huduma muhimu bila ya ubaguzi’ alisisitiza Dk Sheni.

Akifafanua kuhusu hali ya uchumi na changamoto zinazoikabili Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Sheni alisema hali ya uchumi pamoja na mfumko wa bei za vyakula mbali mbali na uharamia unaondelea kufanyika umechangia kusababisha hali ngumu ya maisha.

‘Mfumuko wa bei ni changamoto kubwa inayotukabili katika uchumi wa Zanzibar huku bei za vyakula zikipanda na kusababisha ugumu wa maisha’ alisema.

Akitoa mfano kasi ya ukuaji wa uchumi alisema imefikiya 6.5 ukilinganisha na ukuaji wa asilimia 6.7 katika mwaka 2009 na kutaja ukuaji mdogo wa sekta ya viwanda na huduma ambapo kwa mwaka 2010 ukuaji wa huduma ulifikiya asilimia 8.7.

Kwa upande wa mfumko wa bei alisema ni tatizo kubwa ambapo umekua kwa asilimia 6.6 kwa miezo ya Januari mwaka 2010 na katika mwaka 2011 hadi kufikiya asilimia 18.7.

Hata hivyo alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukuwa hatua mbali mbali kukabiliana na matatizo hayo ikiwemo kupunguza ushuru kwa bidhaa muhimu za vyakula ikiwemo mchele pamoja na unga wa ngano.

Rais huyo alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa sasa inaendelea kutekeleza sera na Mapinduzi ya kilimo katika uzalishaji wa chakula na kupunguza kutegemea kuagiza bidhaa muhimu ikiwemo mchele kutoka nje ya nchi.

Alisema Mapinduzi ya Kilimo yatafanikiwa kama wakulima watalima kilimo cha kisasa ikiwemo cha umwagiliaji maji cha mpunga kwa kutumia mbinu za kisasa na ushauri kutoka kwa wataalamu.

Dk.Sheni alisema Serikali inakusudia kuimarisha mabonde ya mpunga yaliopo Cheju kwa kuweka miundo mbinu ya kisasa ya umwagiliaji maji pamoja na kupeleka huduma za umeme.

‘Tayari tumepeleka umeme katika bonde la mpunga liliopo Cheju wilaya ya kati Unguja huku tukijitayarisha kuimarisha miundo mbinu ikiwemo ya barabara kwa ajili ya kurahisisha shunguli za wakulima; alisema Dk.Sheni na kushangiriwa na wengi.

Alisema mikakati ya kuleta mapinduzi ya kilimo itakwenda sambamba na kuimarisha chuo cha kilimo kiliopo Kizimbani, ambacho sasa tayari kimeanza kutambuliwa katika masomo yake.

Katika hotuba yake iliyochukuwa takriban saa moja na nusu Dk Sheni alitumia nafasi hiyo kuyataja mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar na huduma muhimu za jamii na maendeleo zinazopelekwa kwa wananchi.

Aliitaja sekta ya miundo mbinu ya barabara, kwamba imeleta mapinduzi makubwa ya uchumi ambapo hivi sasa barabara nyingi za vijijini zipo katika hali nzuri zikijengwa kwa kiwango cha lami.

Aidha Serikali itahakikisha inajenga kwa kiwango cha lami barabara zote muhimu zikiwemo zinazokwenda vijijini kwa ajili ya kuchochea maendeleo na kupunguza umasikini alisema.

Alizitaja barabara sita za mkoa wa kusini Pemba ambazo zimefunguliwa katika shamra shamra za miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar kama ni ushahidi tosha wa kuimarisha miundo mbinu ya sekta hiyo vijijini.

‘Tumedhamiria kujenga barabara zote muhimu zikiwemo zinazokwenda vijijini kwa ajili ya kuleta maendeleo na kupunguza umasikini wa wananchi wetu’ alisema Dk Sheni na kuipongeza Serikali ya Norway ambayo imefadhili mradi huo wa ujenzi wa barabara sita.

‘Ni sherehe ambazo zinatakiwa kuendelea kusherehekewa kwa lengo la vizazi vijavyo viweze kujuwa na kutambuwa kwamba tunatoka wapi na tunakwenda wapi’ alisema mmoja wa waasisi wa Mapinduzi Mzee Hassan Nassor Moyo wakati akizungumza na baadhi ya waandishi wa habari mara baada ya kumaliza sherehe hizo.

Moyo alisema kauli hiyo kufuatia baadhi ya watu wakipinga kufanyika kwa sherehe hizo ambazo hutumia fedha nyingi,huku wananchi wakihitaji huduma muhimu ambazo hazipatikani.

Aidha wananchi walijitokeza mapema na kuingia katika uwanja wa Amaan katika majira ya saa moja asubuhi na hawakujali na jua kali lililokuwa likitoka katika kipindi hichi cha kiangazi.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na wananchi wengi kutoka katika kisiwa cha Pemba ambapo walifika hapa kwa kutumia usafiri wa boti za kisasa pamoja na meli.

Awali Dk Sheni baada ya kuingia katika uwanja wa Amaan alipokea salamu ya heshima kutoka kwa vikosi vya ulinzi vya jeshi la Wananchi wa Tanzania pamoja na kukaguwa gwaride ambalo lilipita mbele wa wageni wa kitaifa kwa mwendo wa pole na haraka.

Aidha maandamano wa wananchi wa mikoa mitano ya Unguja na Pemba na wafanyakazi wa taasisi mbali mbali za wizara za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar walipita mbele ya wageni wa kitaifa wakionesha ushiriki wao na kuyaunga mkono Mapinduzi ya mwaka 1964.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Makamo wa Rais Dk Mohamed Gharib Biali, Waziri Mkuu Mizengo Pinda pamoja na Marais wastaafu akiwemo Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa.

Kwa upande wa Viongozi wa Zanzibar Makamu wa kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa pili, Balozi Seif Ali Iddi ni miongoni mwa waliohudhuria sherehe hizo pamoja na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, Waziri Kiongozi Mstaafu, Ramadhan Haji na mawaziri mbali mbali wa serikali ya Tanganyika na wale wa Zanzibar.

Aidha viongozi na wenyeviti wa chama cha mapinduzi wa mikoa yote ya Tanzania Bara walihudhuria sherehe hizo kwa lengo la kuimarisha uhusiano uliopo kati ya pande mbili za muungano.

Advertisements

2 responses to “Siri ya mafanikio yetu ni umoja- Dk Shein

  1. Nakubaliana na wote wanaosema kua sherehe kubwa za namna hii ni kupoteza mamilioni ya fedha ambazo zingetumika katika shughuli nyingi za huduma muhimu za jamii. Kama fedha hizi zingetumika kujenga kituo cha afya au shule nadhani ingekua na manufaa zaidi na sherehe ikawa ni ufunguzi wa hilo jengo

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s