Mapinduzi yetu na fikra mpya, vitu ambavyo haviepukiki kamwe

Na Ally Saleh

Kwa mara nyengine tena Zanzibar inapita katika sherehe za mapinduzi yake, ambaye kwa watetezi wake wakubwa huitwa matukufu, na hii ikiwa ni miaka 48 tokea tukio hilo la Januari 12, 1964. Mapinduzi hayo yalitokea chini ya mwezi mmoja tokea Zanzibar ilipopata uhuru wake hapo Disemba 10, 1963 na kuipa Zanzibar kiti katika Umoja wa Mataifa Disemba 18, 1963.

Kwa hivyo Uhuru wa Zanzibar na Mapinduzi ya Zanzibar ni matukio yaliopishana kwa mwezi mmoja tu, lakini kwa kiasi kikubwa imani iliopo hivi sasa na kwa miaka 48 kuwa hapakuwa na Uhuru wa wananchi, bali Mapinduzi ndio ambayo yamekuwa ni ya umma.

Hayo ya kipi halali na kipi haramu, kwa sababu pia kuna hoja kuwa Mapinduzi hayakuwa ya lazima mbali ya matendo ya ziada yaliokithiri, yasiwe ni mjadala wetu wa leo, lakini zaidi haja yetu ni kutizama mbele tuendeko.

Ila msimamo wangu uko wazi kwa umri wa utu uzima wangu ni kwamba siafikiani na baadhi ya sababu za kufanya Mapinduzi hasa ile ya kwamba uchaguzi wa mwisho ulikuwa haramu kwa maana ya kupendelewa ZNP wakati miaka kadhaa sasa mambo kama hayo yanafanywa na Serikali kukipendelea chama kilichowahi kukaa katika uognozi.

Maana pia hatutakuwa na haja ya kujadili juu ya madai kuwa kulikuwa na haja ya kuomba radhi au angalau kukiri juu ya hayo matendo ya ziada ya kufunga, kutesa, kuuawa kwa wananchi Mapinduzi yakiwa yameshapita, na bila hadi leo Serikali kutolewa tamko juu yake.

Ila sasa tukitaka tusitake, na ndipo ninapowaambia wengi ninaokutana nao, Mapinduzi sasa ni halali kwa maana ya tukio ambalo limepita, lipo na tutaendelea kuwa nalo, sio kwa maana ya tukio la mwaka 1964, lakini kadri ambavyo litaweza kubadilika kukidhi haja ya wakati.

Kwa hali hiyo, leo ikiwa ni miaka 48, bado kuna walio miongoni mwetu ambao hawaoni na kwa kweli wanapinga kabisa dhana ya kusherehekea Mapinduzi kwa maelezo ya kuwa yanawakumbusha dhulma zilizotokea na kwa hivyo wananasibisha Mapinduzi na uharamu kwa ujumla wake.

Binafsi ni katika wanaotofautiana na mtizamo huo, na inawezekana kunyooshewa kidole, lakini kwa fikra zangu Mapinduzi kama Mapinduzi ni lazima yakubalike kwa sababu kama ni malengo, au kama ni mtizamo wake, umeendelezwa kwa kiasi kikubwa kama ambavyo kuna upungufu na makosa kwa kiasi kikubwa pia.

Kwa maneno mengine, kama ingekuwapo Serikali iliyochaguliwa na wapiga kura ya Muhammes Shamte ya 1963 ingekuwa na malengo ya kujenga nchi kama ambavyo mfululizo wa Serikali toka Abeid Karume pia wanalengo lile lile.

Tofauti ya Uhuru na Mapinduzi kwa maana ya itikadi ndio ambayo imetawala nchi hii kwa muda mrefu na kugawa watu wake karibu kati na kati kwa muda mkubwa, tuseme kwa kiasi pia hadi hivi leo.
Kosa la Serikali ya Mapinduzi kutosuluhisha umma uliogawiwa kiitikadi mara baada ya Mapinduzi, na badala yake Serikali hiyo kujikita katika kujenga itikadi ya upande mmoja na kusahau kushirikisha karibu nusu nzima ya Wazanzibari, iliibakisha Zanzibar katika mgawiko ambao Mapinduzi ilikusudia kuuondoa.

Kwa muda mrefu baada ya Mapinduzi vitendo vya ubaguzi, na upendeleo kwa baadhi ya raia na kuwatenga raia wengineo. Pengo la kipato likajenga kuwa kubwa zaidi katika muda wa Mapinduzi kuliko kabla. Matumizi mabaya ya madaraka ndio yakaongezeka.

Baadhi ya Sera zilikuwa za kibaguzi na baadhi zilikuwa zina malengo ambayo hayangeweza kutekelezeka na baadhi kama ile ya kuchukua ardhi kutoka kwa waliokuwa na nyingi kuwapa wasiokuwa nayo haikuwa na maandalizi, kama pia ilivyokuwa Sera ya Elimu na Afya.

Kwa hivyo baada ya miaka 48 tumebadilika. Tumekiri  baadhi ya Sera kutotekelezeka na kumefanywa mabadiliko kwa mujibu wa mahitaji ya wakati na mitizamo mingi ya kubadilisha misimamo mikali ya Mapinduzi imefanywa, na kwa sasa Mapinduzi zaidi ni dhana kuliko ilivyokuwa hapo awali.

Na ndio hapa nikawa na fikra kuwa wanaoendelea kuyakataa Mapinduzi hadi sasa mimi sioni kuwa kuna Mapinduzi kwa maana halisi, ila ninachoona ni Serikali iliyobadilika kiasi cha kuwa imekwenda na wakati na jina tu ni la Mapinduzi.

Kuna mabadiliko makubwa ya Katiba, muundo wa Serikali, uendeshaji wa Serikali, uwajibikaji wa Serikali na kwa ujumla ukuzaji na ustawishaji wa demokrasia na utawala bora kiasi ambacho hapawezi tena kuwa na Serikali ya Mapinduzi zaidi ya jina tu.

Uhuru wa vyombo vya habari ulianza kwa shida sana lakini hatua iliyofikiwa sasa ni ya kupigwa mfano ingawa tunakiri kuwepo kwa vipingamizi lakini nia inaonyeshwa kubadili hayo, ijapo changamoto itabadi kwa wanasiasa na watendaji kutekeleza wajibu wao kwa waandishi wa habari.

Changamoto ambayo pia inaielekeza Serikali kuondosha sheria zenye kukandamiza uhuru wa uandishi ndani ya Zanzibar ambao unahitajika sana ili kuweza kuendeana na hali mpya ya kijamii, kisiasa na kisheria ndani ya nchi.

Tangu kuwepo kwa Mapinduzi tumekuwa na chaguzi kadhaa, na ingawa kumekuwa na malalamiko juu ya udhati na uwazi wake lakini ni wazi kuwa kumekuwa na maendeleo makubwa katika uendeshaji na usimamizi wake.

Tulianza katika wakati ambapo kulikuwa na uingiiliaji mkubwa, tukaaanza kuwa na Tume ya Uchaguzi iliyo huru zaidi na kufuata misingi ya kiuchaguzi yenye vigezo vya kimataifa hadi leo  mfumo wa uchaguzi umeimarika na kwa kiasi kikubwa unaelekea kutoa mshindi wa kweli anaechaguliwa na wapiga kura.

Na kila mtu ni shahidi kuwa Uchaguzi wa mwisho kufanyika nchini wa 2010 umeonyesha njia ambayo Zanzibar inaelekea kwa sababu uchaguzi huo ulitoa taswira kuwa Zanzibar inaweza kubadilika kwa sababu kinyume na chaguzi zote, huo hata nzi hakufinywa kudhirisha mabadiliko makbuwa yajayo.

Na kuwezekana kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni kitu ambacho kisingeweza kutarajiwa hata miaka miwili tu nyuma, na sasa tuna Serikali ambayo pamoja na kuiitwa ni ya Mapinduzi lakini ni pana kushirikisha Upinzani ndani yake.

Kwangu mimi hii ni hatua moja kubwa sana na kama kulikuwa na watu wana shaka kuwa hilo halingedumu, basi sasa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ina umri wa mwaka mmoja na inasonga mbele na kujifunza kutokana na changamoto inazozikabli, lakini kuundwa kwake kulikuwa ndio muhimu.

Kwa hivyo kwa fikra zangu kwa sasa kuwepo au kutokuwepo kwa Mapinduzi  au hata dhana yake si suala muhimu tena. Maana moja ya msimamo mkubwa wa Mapinduzi, kama ambavyo ilikuwa nia ya Uhuru ni kuleta umoja na masikilizano ndani ya nchi, ili Serikali iwe na nafasi ya kutimiza wajibu wake.

Hilo sasa linafanyika kwa umakini chini ya SUK, na kwa hivyo kama leo tusingekuwa au kwa kuwa na Mapinduzi, dhamira hiyo inatimizawa kikamilifu na kwa hivyo kwa kiasi tukiri kuwa tumefikishwa hapa na Mapinduzi ya 1964, kwa sababu wapo wanaoyaamini kama ambavyo wapo wanaoamini Uhuru wa 1963 la muhimu wote ni wamoja ndani ya nchi yao.

Kwa hivyo tusherehekea Mapinduzi kwa sababu pamoja na kuzama na kuzamuka, kwenda sawa na kutetereka ndio yaliotufikisha hapa leo, na leo kwa fahari kabisa tumeweza kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambao utamu wake ni kama Uhuru au Mapinduzi.

Hatuna sababu tena ya kukwama kimawazo kwa kushikilia vitu vya kiitikadi tu na ambavyo baada ya miaka 48 lazima tutakuwa na fikra mpya. Na fikra yetu mpya iwe kuijenga Zanzibar yetu kwa kuhakikisha kuwa SUK inasimama, maana tumeona tulivyokuwa tukiyumba 1964 hadi 2010.

Kamba hii ishikiliwe na kila mmoja wetu maana imeonyesha kila dalili ya kheri na maslahi ya Wazanzibari kwa ujumla wao, wa ndani na wa nje.

Advertisements

7 responses to “Mapinduzi yetu na fikra mpya, vitu ambavyo haviepukiki kamwe

 1. tungelionyeshwa katiba iliotumika kipindi hicho 1963 ili tujuwe kuwa kweli ilikuwa ya kiubaguzi?
  Ally saelh msaada wako KAMA KWAIDA YAKO JUU MSAADA MITHILI YA HAYA

 2. JAMANI HUU SI WAKATI WA KUSHEREHEKA ZNZ BALI NI KUHUDHUNIKA KWANI 26-4-1964 RASMI ZANZIBAR ILITAWALIWA NA WAKOLONI WA TANGANYIKA HADI SASA. Yaarab tunakuomba utusaidie kupata uhuru wa ZANZIBAR. Nchi zote duniani zimeshapata uhuru bado sisi tu zanzibar.

 3. He! mungu tumekukosea nini sisi wazanzibar mpaka ukatupelekea kutawaliwa na TANGANYIKA? Mungu tusamehe tuliyokosea ili tupate uhuru wa zanzibar.

 4. shukran @ ally saleh kwa msaada wako mkubwa ktk kutoa taaluma sahihi kwa wazanzibari.
  Sio kama mzee moyo ambae haoni haya kukidanganya kizazi cha sasa.

 5. JAMANI WATANGANYIKA WAMETUDHARAU SANA MPAKA KUFIKIA HATUA ZANZIBAR KUIFANYA WIZARA NA RAISI WA ZANZIBAR KUWA WAZIRI ASIYEKUA NA VIZARA MAALUM. Haya yote yanasababishwa na kuepo kwa viongozi wasio na elimi katika smz kufikia hatua ya kuibadilisha bendera ya smz na kuwa bendera ya wizara ya TANZANIA. Ukitaka ushahidi kuwa bendera ya smz ni bendera ya wizara ya TANZANIA angalia bendera zote za wizara za TANZANIA utagundua kuwa kuna kipendera kidogo cha muungano juu yake kama ilivyo bendera ya zanzibar. Kibendera hicho cha muungano katika bendera za wizara za muungano ikiwemo zazanzibar inaashiria WIZARA ZA SEREKALI YA TANZANIA.

 6. Haya, Mi sioni sababu ya kusheherekea mapinduzi kama ilivyo maana yake, kwa maana naweza sema wazi kua zanzibar mpaka sasa bado hakuna Rais, hii ni kua kila mzanzibari alie fikia umri ni lazima awe na kitambulisho cha mzanzibar mkaanzi, labda iwe kimebadilishwa jana maana sipo sasa Zanzibar. ila ni kua kitambulisho hicho ndicho kilicho muezesha Dk.Shein kupiga kura kama mzanzibari, kumbe nae pia ni mkaazi tu wa zanzibar, hapaswi kua Rais wa zanzibar kwanza, pili wala tusiendembali , kitambulisho hicho hicho kimeandikwa …. Nationality/uraia. Tanzanian, na hapa kila mtu anajua kua Rais wa Tanzania ni Mh,Kikwete. kwa maana Dk. Ali Mohammed Shein, ni mkaazi wa tu zanzibar, na kama Raia wa Tanzania Rais wake ni Mh. Jakaya Kikwete.
  Sasa jamani hebu tuelezeni vizuri hizo sherehe za mapinduzi zina maana gani kwa zanzibar, kwa kua wanzaibari wote ni raia wa Tanzania na rais wa Tz kila Mtu anamjua?….

 7. Ahsante, ukweli ni huo lakini ukweli hasa ni ZANZIBAR NI KWAMBA ZANZIBAR NI WIZARA YA TANZANIA KWA MUJIBU WA BENDERA YA ZANZHBAR ILIVYO (yaan bendera ya smz inafanana na bendera zote za wizara za TZ kuna kibendera kidogo cha TZ kinachoashiria wizara za TZ) HICHI NDICHO KITU KILICHOMPELEKEA SHEIN KUAPA KUWA WAZIRI ASIYEKUWA NA WIZARA MAALUM TANZANIA.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s