Tendwa, Werema wajichanganya

Msajili wa Vyama Vya Siasa Tanzania, John Tendwa amejichanganya kuhusu sakata la kufukuzwa uanachama Bw. Hamad Rashid Mohammed na wenzake

 

Na Ally Saleh
Katika hili nahisi tendwa amepotoka kisheria na halikadhalika Jaji Werema amepotoka.tuanze na Tendwa. hoja ya tendwa ni kuwa kufukuzwa kwa hamad rashid ni hasara kwa taifa kwa sababu kutalazimisha kuitishwa uchaguzi mdogo. na wakati wa kufukuzwa kwa kafulila wa NCCR  alinukuliwa akisema kuwa gharama za kuitisha uchaguzi mpya ni karibu 7bn.

lakini katiba ya nchi inaruhusu chama kumfukuza mbunge kwa maana ya kuwa mbunge hudhaminiwa na chama kuingia katika siasa na kwa hivyo chama kina mashiko kwake. kama tendwa anaona hili linatia gharama basi apendekeze kubadilishwa kwa sheria na kifungu kipya kiingizwe juu ya utaratibu mpya na mwepesi kupata mbunge mpya kujaza nafasi
ya mbunge aliyechukuliwa nguvu zake na chama.

lakini kuna suala la mwenyewe mbunge kujiuzulu kama vile rostam kama ambavyo pia kuna suala la mbunge kufariki na kwa matukio yote haya ambayo kwa sasa lazima uitishwe uchaguzi tendwa atwambie mbunge mpya apatikane vipi bila gharama.

kisha hoja ya pili ya tendwa ni kuwa chama kuchukua madaraka ya kumfukuza mbunge na hatimaye kuondoshwa nafasi hiyo kunawanyima wananchi na watu waliomchagua haki yao ya kuwakilishwa na mtu waliyempigia kura.

hoja hii pia ni dhaifu kwa sababu nyingi.

kwanza ni kuwa mbunge huchaguliwa kwa misingi na matakwa ya chama na hutakiwa kutekeleza maamrisho ya chama chake na chama lazima kiwe na mamlaka ya kuzima jeuri au majivuno ya mbunge iwapo atakiuka hayo. lakini pia chama kinawajibu wa kuhakikisha kuwa kila kitu kinakwenda kwa taratibu na katiba.

sasa iwapo tendwa anaona hili ni zito au gumu basi pia asikiliaumu chama kwa kufanya hivyo kwa sababu kama nccr na cuf wamefukuza wabunge wao basi hadi sasa wamo ndani ya katiba za vyama vyao na sheria ya nchi.

ila ikiwa tendwa anaona uchungu kwa nini basi asipendekeze njia nyengine kwa wananchi ambao wanakosa kupata huduma kutokana na mbunge wao anaehamia dodoma na dar es salaam, au hata akiwepo jimboni hana msaada wowote.

kwanini asipendekeze kuwepo kwa sheria ya kumpigia kura ya NO CONFIDENCE mbunge ambaye anashindwa kuwajibika au ku deliver kwa watu walionchagua? kisha mwanasheria mkuu werema anasema kuwa cuf wamevunaja katiba kukataa maagizo ya mahakama na kwa hivyo chama hicho kifutwe kwa kuwa kimekosa sifa ya kuendelea kuwa chama cha siasa kwa kuvunja katiba.

hivi kudharau amri ya mahakama ni kuvunja katiba au kuvunja sheria? Jee kuvnja sheria ni sawa na kuvunja katiba? na jee chama kikivunja katiba ADHABU YAKE ni kufutwa? jee ni wapi na vipi chama kinavunja katiba? jee chama hakina watendaji na jee haiwezekana watendaji wakapata adhabu ya kuvunja amri ya mahakama badala ya kukiadhibu chama kwa ujumla wake?

kwani si mwanasheria mkuu huyu huyu anaye nyamaza kimya katiba ikivunjwa na mawaziri wa serikali kwa kuiliibia taifa na kuwafanyia khiyana wananchi na bado hasemi kitu na kwa kweli anafumbia macho na hataki kuchukua hatua yoyote ile?

hayo ndio yangu

NI KWA KUDHARAU AMRI YA MAHAKAMA, ASEMA KOSA HILO LINAKIFANYA KIKOSE UHALALI WA KUWA CHAMA CHA SIASA
Kizitto Noya
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema amesema Chama Cha Wananchi (CUF) kitakuwa kimevunja Katiba, kama kweli kilipuuza amri halali ya Mahakama iliyokizuia kuendesha kikao kilichowajadili na kuwafukuza Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed na wanachama wake wengine wane.

Januari 4, mwaka huu Jaji Augustine Shangwa wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, alitoa hati ya pingamizi kuzuia kufanyika kwa mkutano wa Baraza Kuu la CUF, na hatua yoyote ya kuwajadili Hamad Rashid na wenzake, lakini CUF kiliendelea na mkutano huo ambao uliwafukuza uanachama makada hao ambao wote walikuwa ni wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi.

Jana, Jaji Werema akizungumza na Mwananchi kuhusu mgogoro unaoendelea kufukuta ndani ya CUF dhidi ya mbunge huyo wa Wawi, alisema “… Sina hakika kama amri hiyo ipo, lakini kama kweli kuna ‘court injuction’ iliyotolewa na Mahakama kuzuia Hamad Rashid na wenzake wasijadiliwe na Baraza la Uongozi na kuwafukuza, basi CUF imevunja Katiba,” alisema Jaji Werema na kuendelea:”…Tena hakiishii (CUF) kuvunja katiba tu, kosa hilo linaenda mbali zaidi na kukifanya chama hicho kikose uhalali wa kuendelea ku-exist (kuwepo).”

Pamoja na Hamad Rashid, wengine waliovuliwa uanachama na kikao hicho cha Baraza Kuu ni wajumbe wa baraza hilo na maeneo wanayotoka yakiwa kwenye mabano ni Doyo Hassan Doyo (Tanga), Shoka Hamis Khamis Juma (Pemba) na Juma Saanane (Unguja).Jaji Werema alisema katika mifumo ya utawala duniani, lazima kuna chombo cha mwisho cha uamuzi, ambacho kimsingi, kinapaswa kuheshimiwa na vyombo vingine vyote bila kuhojiwa na kwa hapa nchini, mahakama ndiyo yenye mamlaka hiyo.

“Lazima kuwe na mtu au chombo ambacho kikisema, wengine mnasikiliza sasa kama kweli CUF waliiona amri ya Mahakama na wakaendelea na walichotaka kufanya, huku ni kuvunja Katiba. Na chama cha siasa kikivunja Katiba, kinakosa uhalali wa kuendelea kuwepo,” alisisitiza Jaji Werema.Jaji Werema alisema ingawa CUF inaweza ikawa sahihi kabisa katika uumuzi wake huo, lakini kama kilikaidi amri halali ya Mahakama, kimekosea.

“Ni ngumu kusema CUF imekosea kumfukuza Hamad wala kupuuza madai ya Hamad dhidi ya CUF. Kikubwa hapa ni nidhamu. Nidhamu kwa pande zote mbili, na nidhamu hiyo iambatane na heshima kwa sheria za nchi,” alisema Jaji Werema.

…Aungana na Tendwa
Awali, Jaji Werema aliungana na kauli iliyotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini John Tendwa kutaka kufanyike marekebisho ya sheria ili vyama vya siasa visiwe na mamlaka ya mwisho kumfukuza mbunge akisema:

“Mimi naungana na Tendwa kwamba sasa ni wakati muafaka wa kurekebisha sheria hii. Mbunge ni wa wananchi, lakini kikatiba mbunge pia ni wa chama. Inaonekana sasa vyama vya siasa vimeanza ku-abuse dhamana tuliyowapa ya kuwadhamini wabunge na kuanza kuwafukuza ovyo.”

Aliendelea,” Nasema nakubaliana naye (Tendwa) sheria ibadilike na tutafute njia ambayo inaweza kuleta mwafaka zaidi. Hatuwezi kuendelea kuikalia kimya sheria hii. Zamani tulipotaka mbunge adhaminiwe na chama, tulikiamini sana chama, lakini siku hizi mambo yamebadilika. Ukosefu wa nidhamu uko pande zote, siasa siku hizi ni ubishi tu.”

Kwa mujibu wa Jaji Werema, ili kulinda demokrasia ya kweli, ni lazima sheria hiyo ibadilishwe ili vyama visiwe na mamlaka ya kumfukuza mbunge moja kwa moja.”Wito wangu kwa watanzania ni kwamba, tutumie fursa hii ya marekebisho ya Katiba kujadili suala hilo, iwe kabla au baada ya mchakato, lakini sheria hii haitufai,” alisisitiza.

Tendwa akizungumza na waandishi wa habari Ikulu wiki iliyopita, alipinga uamuzi huo wa CUF kumfukuza Hamad Rashid akisema ulikiuka maslahi na haki ya wapigakua waliomchagua, kwani umeangalia maslahi ya chama zaidi na kwamba ipo haja ya sheria kubadilishwa ili mbunge aliyechaguliwa asiweze kufukuzwa kabla ya muda.

Kauli ya Seif
Lakini, juzi Maalim Seif katika mkutano wake wa hadhara jijini Dar es Salaam, alisema CUF hakijapokea barua yeyote kutoka mahakama kuu kuhusu pingamizi na kuwa kama kuna pingamizi lilishachelewa kwani chama hicho kilishafanya uamuzi.Alisema kama mahakama ilitoa pingamizi hilo, basi walikuwa na sababu ya kupeleka katika Ofisi za CUF kabla ya chama hicho kukaa kikao ambacho kilitumia Sh30 Milioni kufanya uamuzi mgumu ya kufukuza wananchama wake.

“Mahakama zinajua Ofisi za CUF zilipo, lakini imeshindwa kuleta pingamizi hizo halafu Kibwetere (Hamad Rashid Mohamed) anasimama kwenye vyombo vya habari kuongelea pingamizi la mahakamani”Alisema kinachoongelewa ni Hamad Rashid ni kupitia vyombo vya habari na sio mahakama kuleta barua ofisi za CUF. Alisema kama mahakama itafanikisha mpango wake wa kumsaidia Hamad Rashid basi mbunge huyo atakuwa wa jimbo la Mahakama na sio jimbo la Wawi.

Maalim Seif alisema Spika wa Bunge Anne Makinda ameshapewa Barua ya kufukuzwa uanachama Hamadi kama ataamua kumlea ni hiari yake.Alisema Spika ni mwenye uamuzi wa kutangaza Hamad Rashid sio mbunge kwakuwa hana sifa ya kuwa mwakilishi wa wananchi wa jimbo la Wawi baada ya kupelekewa barua na chama na sio mahakama, na kumtahadharisha spika kuwa ukimya wake utampoza kutokana na kushindwa kufanya uamuzi wa kitaifa.

Dk Kashililah
Katibu wa Bunge Dk Thomas Kashililah jana alishindwa kuthibitisha wala kukanusha kauli ya Seif kwamba CUF imeshakabidhi barua kwa spika kumjulisha kuwa Hamad Rashid amevuliwa uanachama CUF hivyo sio mbunge wa chama hicho.

“Soma gazeti la jana naona wakusema hivyo CUF, sasa unataka nithibitishe nini tena, huamini kauli yao? alihoji Dk Kashililah katika ujumbe wa simu ya mkononi Akizungumzia hatua hiyo ya CUF kudharau amri ya mahakama juzi, Hamad Rashid alisema anachojua yeye bado ni mbunge na leo anaenda mahakamani kujua hatima yake baada ya CUF kukaidi amri ya Mahakama.

Awali Hamad aliwaambia waandishi wa habari siku moja baada ya uamuzi wa kufukuzwa kwake kuwa anasikitika kwamba Maalim Seif hajitambui kuwa ni nani katika jamii, kwani angelijua hilo, asingebishana na mahakama.”Huyo ndiye makamu wa kwanza wa rais anayepingana na mahakama. Atawezaje kuendelea kuwa kiongozi kama hatambui hata mipaka yake?” alihoji.

Advertisements

4 responses to “Tendwa, Werema wajichanganya

  1. Nyinyi tanganyika kama mshaichoka znz ya nini na haina faida kwenu mna uhakika wazanzibar hawataki muungano sasa mnaianza cuf hamtoiweza na wanasheria semi wabovu wababaishaji

  2. hoja zao hazina masiko kisheria ila hili suala yahitajika marekebisho maana KENYA katiba yao imeruhusu wananchi km hawatopebdezewa na mwendendo wa mbunge wao ni ruhusa kubadili na kuchagua mwingine
    na suali hili nililijua mwanzoni kuwa sabotage kwa waznz kunyamazishwa haki wanazo dai………na ndio mawazo ya wengi haya
    msisimamo ni huu watakapo futwa cuf na ndio mwisho wa muungano huu lile panga la kuvunjwa ndio hatamu yake itaanza hapo…..
    nawakilisha

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s