Hatima ya Hamad Rashid katika CUF ni leo

Sakata lililokuwa likifukuta ndani ya Chama Cha Wananchi (CUF) linalomhusisha Hamad Rashid Mohammed na viongozi wenzake linatazamiwa leo kupatikana ufumbuzi wake kupitia kikao cha kamati ya nidhamu kinachoendelea leo hii huko Tanzania

Kizitto Noya

HATIMA ya uanachama ya Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed inatarajiwa kujulikana leo atakapojieleza mbele ya Kamati ya Nidhamu na Maadili ya chama hicho. Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila kuvuliwa uanachama na chama chake hicho kwa madai ya kukiuka maadili na katiba ya chama ambayo kwa kiasi kikubwa yanafanana na yale yanayomkabili Hamad.

Hamad hivi karibuni amejikuta katika mgogoro na baadhi ya viongozi wa makao makuu ya CUF baada ya kutangaza kuwania nafasi ya katibu mkuu wa chama inayoshikiliwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad na kuanza kupita kwenye matawi akigawa misaada, hatua ambayo ilisababisha vurugu katika matawi aliyopita huku tukio katika Tawi la Chechnya lililopo Manzese, likisababisha umwagaji damu baada ya wanachama wanaomuunga mkono kupambana na walinzi wa Blue Guard.

Baada ya vurugu hizo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema Hamad angeitwa mbele ya kamati hiyo na jana, taarifa ya CUF ilisema mbunge huyo leo atahojiwa na kamati hiyo kwa tuhuma za kuvunja katiba ya chama hicho.

Kwa mujibu wa Katiba ya CUF, adhabu ya kosa la kuvunja Katiba ya chama ni kupewa onyo kali, kusimamishwa au kufukuzwa uanachama.Hamad Rashid mwenyewe, alithibitisha kuitwa kwenye kikao hicho na wanachama wenzake 13 wanaomuunga mkono.“Ni kweli nimeitwa lakini tuko wengi kidogo. Wameniandikia barua kuniita kwenye Kamati ya Nidhamu na Maadili kesho (leo), ila nasikitika kwamba walianza kunihukumu kabla ya kunisikiliza,” alisema Hamad.

Kuhusu alichoitiwa Hamad alisema: “Wanasema nimevunja Katiba ya chama,” huku akirejea adhabu zilizoanishwa kikatiba juu ya kosa hilo.Lakini, akionekana kujua kitakachomtokea kwenye kikao hicho, Hamad alisema kuwa atakata rufaa kupinga uamuzi wa kufukuzwa uanachama.

“Mimi kuitwa nilitarajia lakini hofu yangu ni kwamba wameshanihukumu kabla ya kunisikiliza. Ila msimamo wangu bado uko palepale, nitakata rufaa kupinga adhabu ya kufukuzwa uanachama,” alisema.

Awali, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mkuu wa Idara ya Nidhamu na Maadili ya CUF, Abdul Kambaya alisema Hamad na wenzake hao 12 wanaitwa kwenye kikao hicho ili kusomewa tuhuma zinazowakabili na kuwapa fursa ya kujieleza.

“Tayari tumeshawapa barua za kuwaita kwenye Kamati ya Nidhamu ya Chama kuanzia 27 na 29 kwa mahojiano zaidi,” alisema Kambaya na kuongeza kuwa kuhojiwa kwa viongozi hao kuna baraka zote za chama.

Mbali na Hamad, Kambaya aliwataja watuhumiwa wengine walioitwa kwenye kamati hiyo kuwa ni Juma Saidi Saanan (Mjumbe wa Baraza Kuu Unguja) na Shoka Khamis Juma (Mjumbe wa Baraza Kuu kutoka Pemba). Wengine ni Doyo Hassan Doyo (Mjumbe wa Baraza Kuu Tanga), Yasini Mrotwa (Mjumbe wa Baraza Kuu Mbeya), Doni Waziri (Mwenyekiti wa Wilaya ya Ilala) na Mohamedi Massaga (Katibu wa Wilaya ya Ilala).

Wanachama wengine Albadawi (Mwenyekiti wa Wilaya ya Temeke), Amir Kilungi, Yusufu Mbungilo (Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi Wilaya ya Temeke) na Nanjase ambaye ni Mwenyekiti wa Wilaya ya Nachingwea.

Pia wamo Tamimu Omari (Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mkunduge, Kata ya Tandale) na Ahmed Issah kutoka Wilaya ya Morogoro Mjini.“Tumeamua kuwaita kwa malengo ya kujadiliana na kuangalia mustakabali wa chama kwa mujibu wa katiba ya chama chetu,” imesema taarifa hiyo na kuongeza:

“Tunawomba wanachama kuendeleza amani na utulivu hasa katika kipindi hiki ambacho chama kinakaa katika vikao vya uamuzi.”
Baadaye Kambaya alisema kwa simu kuwa kamati hiyo, haina mamlaka ya kuwapa adhabu watuhumiwa hao hata kama watabainika kuwa na makosa.

“Sisi kazi yetu ni kuwasomea tuhuma zao na watapewa muda wa kujieleza kisha tutapendekeza adhabu kwenye vikao vya uamuzi ambavyo ni Kamati ya Utendaji na Baraza Kuu la Uongozi.”

Alipoulizwa vikao hivyo vitakaa lini alisema: “Kamati ya Utendaji itaketi Desemba 30 na Baraza Kuu la Uongozi Desemba 31, mwaka huu.”
Hata hivyo, alieleza kuwa mtuhumiwa asiyekubaliana na uamuzi wa vikao hivyo anaweza kukata rufaa kwenye Mkutano Mkuu wa Taifa ambao katika suala hilo, utapangwa na Baraza la Uongozi.

Ingawa haijathibitika kama Hamad na wenzake hao watafukuzwa uanachama, CUF ina historia ya kufanya hivyo kwa wanachama wake. Kumbukumbu zinaonyesha kuwa waliowahi kukumbuwa na masahibu hayo ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, James Mapalala na aliyekuwa Mbunge, Naila Jidawi na Salum Msabaha.

Lakini Kambaya alisema katika taarifa hiyo kuwa: “Tunawaahidi wanachama na Watanzania kuwa hatutamuonea yeyote katika uamuzi utakaotolewa na vikao vyote.”

Mgogoro wa Hamad na Maalim Seif ulianza kuibuka baada ya Hamad kutangaza nia yake ya kuwania ukatibu mkuu wa CUF kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika 2014.

Mgororo huo ulipambana moto mwishoni mwa Novemba katika mkutano wa Hamad uliofanyika Manzese, Dar es Salaam ambako mabaunsa wa chama hicho walivamia mkutano huo na kusababisha mapigano baina yao na wanachama waliokuwa wamehudhuria.

Tangu hapo, Seif na Hamad wamekuwa wakizunguka kwa nyakati tofauti mikoani mbalimbali nchini na kutoa matamko kadhaa kuhusu ugomvi huo.Mara ya mwisho Seif akiwa Mwanza, alisema mgogoro huo utamalizwa katika vikao vya ndani vya chama hicho.

Kwa upande wake, Rashid akiwa mkoani Singida alisema hana hofu na vikao hivyo na kwamba anavisubiri kwa hamu ili akaseme kile alichokiita ukweli juu ya hatima ya chama hicho chini ya uongozi wa Maalim Seif.

CHANZO: MWANANCHI

Advertisements

3 responses to “Hatima ya Hamad Rashid katika CUF ni leo

  1. Hata kama watamfukuza huyo Hamad Rashid ni sawa tu kwani kashaanza kuonesha unafiki muda mrefu na sisi wanje tulikuwa hatujui lakini wenyewe wa CUF walisha mjua zamaani ndio maana akanyang’anywa uongozi wa kambi isiyokuwa rasmi bungeli.

    sisi wa nje hujifanya tunamtetea kumbe unda hasa hatuujui, nibora afukuzwe kwani cansa usipo itibu mapema na kupakata ilipoanzia mwishowe utakuja kuukata mguu mzima.

    Na yeyemwenyewae kasema Maal Seif kashakuwa mtumzima kwahiyo ilikuwa amuheshimu asimpakazie magazetini asubiri vikao vya chama amwambie akini yeye anataka kuonyesha ubabe na hajui kumbe anajidhalilisha mwenyewe na nimtu asiye na fadhila huyoanayempakazia ubaya ndiye aliyemtetea sasa hivi akapata ulaji na mdomo wa kumtangazia ubaya.

    Mnafik anapokujia huja na uso wa Abu Bakar lakini moyo wake ni wa Abu Jahal ndiye huyo mpwendwa wenu Hamad Rashid anataka kuwazubaisha Wazanzibar wamshuhulikie yeye waache kuishuhulikia nchi yao na kuitetea kwnye katiba mpya ili awe yeye ndio gumzo, lakini Wazanzibar washambaini na mtego wake alio tumwa kufanya kachelewa.

  2. Kwa nini afukuzwe? Kwani maalim Seif chama ni chake peke yake hata mwenzie wasigombee ukatibu mkuu? Kwa maoni yangu Hamad aachiwe agombee ukatibu mkuu, chama kitaamua kwa kura kama anafaa au laa. Ninachokiomba tu wasifanye chuki binafsi wakakifuruga chama. Wote wawili (Hamad na Maalim) kila mmoja ana udhaifu wake.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s