Athari za mafuriko waliokufa kufikia 41

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Bi. Monica Luis, Mkazi wa Jangwani aliyeathirika na mafuriko ya Mvua kubwa iliyonyesha jijini kuanzia majuzi, wakati makamu alipotembelea katika Kambi ya Shule ya Sekondari Azania jijini Dar es Salaam leo Desemba 23, kwa ajili ya kuwapa pole waathirika wa mafuriko hayo.

MIILI saba ya watu imeopolewa eneo la Jangwani na kuhifadhiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na kufanya idadi ya waliokufa kutokana na mvua kubwa zilizonyesha jijini Dar es Salaam kuanzia Desemba 20 na kuhifadhiwa hospitalini hapo, kufikia 22 hadi jana.Kadhalika maiti za watu wanne zimefikishwa katika hosipitali ya Mwananyamala na kusababisha chumba cha kuhifadhia maiti cha hosipitali hiyo kufurika hivyo kusitishwa kwa upokeaji wa maiti zaidi.

Kutokana na maiti 11 walioopatikana jana, idadi ya waliokufa imefikia 41 tangu kutokea kwa maafa hayo ambayo pia yaliwaacha maelfu ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam bila makazi.

Baadhi ya wananchi walionekana wakianza kufanya usafi katika nyumba zao tayari kurejea maisha yao katika makazi yao mabondeni, ikiwa ni siku moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kutoa amri ya kuwataka wahame.

Ofisa Uhusiano Msaidizi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Jezza Waziri alisema jana kuwa katika hospitali hiyo wamepokea maiti saba kati ya hizo wanaume sita na mwanamke mmoja na kwamba wote waliopolewa kutoka kwenye tope eneo la Jangwani.

Waziri alisema kati ya maiti hizo saba, wawili wametambulika ambao ni Juma Ibrahim (28)  na Abdallah Salum (22), wote wakazi wa Jangwani na kwamba watano hawakutambulika.

“Leo zimeongezeka maiti saba ambazo ni wanaume ni sita na mwanamke mmoja, waliotambuliwa wote wanatokea  Jangwani na imefanya idadi kufikia maiti 22 ambao wamekufa na mafuriko ya maji na kuletwa hapa,”alisema Waziri.

Kwa upande wa hospitali ya Mwananyama, imestisha kupokea maiti kutokana na uwezo wa chumba chake cha kuhifadhia miili kufika kikomo.

Katibu wa Afya wa hospitali hiyo,  Edwin Bisaka  alisema uwezo wa chumba cha kupolea maiti ni watu 15 ambao tayari wametimia tangu kuanza kwa mafuriko hayo Desemba 20.

Alifafanua kwamba, kutokana na hali hiyo miili yote itakayokuja kuanzia jana jioni ingepelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuongeza kwamba, jana pekee ilipokelewa miili minne.

Alisema maiti hao wanne, watatu waliokotwa eneo la Hananasifu na moja eneo la Kawe na kutaka watu waliopotelewa na ndugu zao wafike hospitalini hapo kwa ajili ya kuwatambua kwani majina yao hayajafahamika.

Mabondeni kubomolewa

Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, imeazimia  kubomoa nyumba zote zilizojengwa mabondeni, katika kipindi cha mwezi mmoja kuanzia sasa, ukiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Kikwete.

Juzi Rais Kikwete, alitembelea Shule ya Msingi Mchikichini kwa lengo la kuwapa pole watu walioathiriwa na mafuriko yaliyotokana na mvua zilizonyesha kwa kipindi cha siku tatu mfululizo na kuwataka wanaoishi mabondeni kuhama mara moja, ili kuepuka kupoteza maisha na mali zao.

Kufuatia agizo hilo, jana halmashauri hiyo ya manispaa ya Ilala, iliitisha kikao cha dharura cha Baraza la Madiwani, kutathmini athari zilizotokana na mafuriko na kutoa maazimio ya namna ya kubaliana na athari hizo katika siku zijazo.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Gabriel Fuime alisema halmashauri imeazimia kubomoa nyumba zote zilizojengwa mabondeni na kwamba utekelezaji wa mpango huo utakuwa ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kuanzia leo.

“Tumeazimia kuwa kuanzia kesho (leo) Kamati ya Mipango Miji ipite katika maeneo yote hatarishi na kubaini hatua za kuchukuliwa ili kuepusha maafa,”alisema Fuime. Fuime alisema halmashauri pia imeazimia kuwepo timu ya uokoaji itakayofanya shughuli hizo kila inapotokea.

Halmashauri hiyo imeshauri pia kuwe na Kamati ya Kudumu ya Maafa ya Mkoa, itakayokuwa na vifaa vya kisasa kwa ajili ya kusaidia shughuli za uokoaji.

Fuime ilitoa wito kwa taasisi na wananchi kuendelea kutoa misaada ya kibinadamu na miundombinu katika maeneo yote, yaliyoathirika na mafuriko. Kwa upande wake Meya wa halmashauri ya manispaa hiyo, Jerry Slaa alisema hatua hiyo ni utekelezwaji wa maagizo yaliyotolewa na Rais juzi.

Wajipanga kurudi

Wakati manispaa ikianza kutekeleza amri ya Rais,  jana baadhi ya wakazi wa Msimbazi na Jangwani, walisema licha ya agizo hilo hawawezi kuhama katika makazi yao kwa sababu hawana maeneo mengine ambayo wanaweza kwenda.

Athumani Mohamed Mkazi wa Msimbazi, alisema hata kama Serikali inawataka wahame katika maeneo hayo hawawezi kuhama mpaka watakapotafutiwa maeneo ya kwenda.

“Mimi nimepanga hapa Msimbazi kwa zaidi ya miaka 10, sasa leo ninapoambiwa nihame huku nikiwa sijui wapi nitakwenda, sitaweza kufanya hivyo zaidi ya kufanya usafi nyumbani kwangu na kuendelea kuishi na familia yangu,” alisema Mohamed.

Mohamed alisema watahama ikiwa Serikali itawatafutia maeneo ya kwenda. Mkazi wa Jangawani, Aisha Abdala alisema wanasubiri maeneo ambayo watapewa na Serikali ili waweze kuhama.

“Mimi sina hamu tena ya kukaa hapa lakini sijui nitakwenda wapi naiomba Serikali itusaidie kukutafutia maeneo ya kutupeleka kwa haraka ilitujue kitu cha kufanya,” alisema Mohamed.

Mwananchi ilishuhudia baadhi ya wakazi wa  eneo la Mchikichini bondeni, ambao nyumba zao hazikubomolewa na maji wakiwa wanafanya usafi kwa lengo la kuendelea kuishi katika nyumba hizo.

Mbuyu wafunga barabara

Katika mtaa wa Togo mwisho, eneo la Kinondoni B, hali ilikuwa mbaya baada ya mti mkubwa wa mbuyu uliodumu kwa zaidi ya miaka 70 kung’olewa na mvua na kuziba njia ya mtaa huo.

Akizungumza na Mwananchi , mkazi wa mtaa huo ambaye pia ni mwanafunzi  wa kidato cha pili shule ya Sekondari Benjamini Mkapa, aliyejitambulisha kwa jina la Raymond alisema  hakuna mtu mmoja aliyejeruhiwa kutokana na tukio hilo bali vibanada viwili vya biashara vilivyokuwa chini ya mbuyu huo vilibomoka.

Raymnond alisema  katika kipindi chote cha takribani miaka 20 aliyoishi Kinondoni, hakutegemea kuona mbuyu huo uking’oka.

“Kwakweli hakuna mtu aliyejeruhiwa au kupoteza maisha, bali hawa  wafanyabiashara wawili waliokuwa wamejenga vibanda  vya saluni na  duka la kuuza  vifaa vya simu ndio wameathirika kibiashra kama unavyoona,”alisema Raymond .

Chadema wataka tume

Katika hatua nyingine, Chama cha  Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetoa msaada wa Sh25 milioni kuchangia waatihirika, huku wakitaka iundwe tume ya serikali ya kutathimini kiwango cha athari za maafa hayo.

Chadema pia kimetangaza kwamba  kinatarajia kuunda mfuko wa maafa wenye lengo la kukusanya fedha na vitu mbalimbali kwa ajili ya waathirikika wa mafuriko katika miji ya Dar es Salaam, Mbeya na Dodoma.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitoa kauli hiyo jana alipofanya ziara ya kutembelea waathirika wa mafuriko katika jiji la Dar es Slaam.

Mbowe katika msafara huo aliongozana na Naibu katibu Mkuu wa chama hicho bara taifa, Zitto Kabwe, Mbunge wa Ubungo John Mnyika, Mwenyekiti wa Vijana Taifa (Bavicha), John Heche, wabunge wengine na maafisa mbalimbali wa chama hicho kutoka makao makuu ya chama hicho, Dar es Salaam.

“Nimeona mwenyewe kiwango cha uharibifu uliotokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika jiji la Dar es Salaam na maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Katika tukio hili wapo waliopoteza ndugu zao na wengine wamejeruhiwa na nyumba zao kubomoka, nitumie fursa hii kuwapa pole waathirika wote kwa niaba yangu na chama changu,katika hili sisi tuko pamoja nanyi mungu awasaidie”alisema Mbowe.

Mbowe alisema tatizo lilitokana na mafuriko ni  kubwa kuliko inavyochukuliwa na Serikali hivyo kutaka uchukue hatua kwa kulitanga kuwa janga la kitaifa.

“Waliothirika na mafuriko haya ni wengi, waliopoteza maisha si thelathini kama inavyotajwa na serikali,waliathirika si elfu nne pekee kama inavyodaiwa na serikali bali ni wengi zaidi ya hao”alisema Mbowe na kuongeza:

“Iundwe kamati maalumu itakayohusisha wadau wa ngazi ifanye tathimini ili kubaini kiwango halisi cha athari zilizotokana na mafuriko, hilo ndilo litakalotoa fursa ya kupata kiwango halisi cha uharibifu na namna ya kushughukia tatizo,”alisema Mbowe.

Katika ziara yake hiyo, Mbowe alielezea kusikitishwa kwake na taarifa za kuwapo kwa watu wasio waaminifu wanaodaiwa kuiba misaada iliyotolewa kwa waathirika.

Alisema kitendo hicho si cha kibinadamu na kuwataka wahusika kuacha kufanya hivyo, kwasababu ni kutakatisha tama watu wenye mapenzi mema kujitolea kuwasaidia waathirika.

“Juzi (jana) tumetoa misaada, lakini usiku tukapata taarifa kuwa kuna watu wanashirikiana na baadhi ya watendaji kuchakachua chakula cha misaada na kuuza, taarifa hizo siyo njema hata kidogo. Nitumie fursa hii kuwataka wahusika  waache sababu za kuwakatisha tamaa hata watu wengine wanaotoa misaada na wenye nia ya kusaidia,” alisema.

Mbowe alitoa angalizo, “Hiki si kipindi cha kulumbana,bali ni wakati wa kushirikiana kuwasaidia waathirika na baada ya hapa, serikali taasisi na wadau kukaa pamoja kunoa namna gani tunalitafutia ufumbuzi suala la waanachi kuishi maeneo yasiyo salama”alisema.

Mbowe pia alisema licha ya kuwa tukio hilo ni la kiasili bado kuna uzemba wa kibinadamu uliosababisha kiwango cha waathirika kuwa kikubwa.

Alitaja sababu hizo kuwa ni kitendo cha serikali kushindwa kupima maeneo na kuwapatia wananchi na wakati mwingine, inapopima ardhi imekuwa ikiwapora wananchi masikini na kuwauzia matajiri.

“Hili bado kunauzembe mahali,watu wote niliowatembelea humo Jangwani ukiwauliza wanakueleza walipimiwa maeneo na serikali katika maeneo ya Segerea lakini wahusika waliuza maeneo hayo kwa matajiri hali inayowalazimu kubaki mabondeni,”alisema Mbowe.

CUF waomboleza

Kwa upande wa Chama cha Wananchi (CUF), kimetoa pole kwa waathirika wa mafuriko hayo na kuitaka serikali kuwatafutia  hifadhi waathirika wote.
Chama hicho pia, kimeitaka serikali kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kutoa maelezo ya sababu zipi zilizowafanya  wananchi kuruhusiwa kujenga nyumba mabondeni hali iliyosababisha maafa kuwa makubwa.

Kwa mjibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na jana na kuasainiwa na Naibu  Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Uenezi, Amina Mwidau mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam na maeneo mengine zimesababisha maafa makubwa ikiwa ni pamoja na kupoteza uhai watanzania.

“Mvua hii inayoendelea kunyesha sehemu mbalimbali za nchi yetu imesababaisha athari kubwa,huku Dar es Salaam ikiwa imeathirika zaidi,wenzetu  zaidi ya 15 kwa Dar es Salaam wamepoteza maisha na pia wapo wasioa na makazi na kwa makioni madhara yake hayajafahamika,”alisema  Mwidau katika taarifa hiyo.

Aliongeza, “Tunawataka Watanzania wote waliopoteza ndugu na jamaa zao wawe wavumilivu katika kipindihiki kigumu na pia kwa wananchi wote ambao nyumba zao zilibomolewa.”  CUF inatoa wito kwa  kila mtu achukue hatua za tahadhari mapema kulingana na mazingira yake ili kukabiliana na madhara ya mvua zinazoendelea ili asiathirike sana ama asiathirike kabisa.

Habari hii imeandikwa na Geofrey Nyang’ro, Pamela Chilongola, Aidan Mhando, Nora Damian na Furaha Maugo. kutoka Gazeti la MWANANCHI

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s