Wazanzibari wana akili, na utamaduni wao

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein

Kalamu ya 14 Des 2011

KWA kuwa Rais Jakaya Kikwete ameshatia saini muswada wa sheria ya marekebisho ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , ni rahisi kuamini hatua zinazofuata zinaandaliwa. Hatua mojawapo ni ya kiongozi huyo kuunda tume itakayosimamia, pamoja na mambo mengine, ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu katiba mpya wanayoitaka.

Rais anatakiwa kuunda tume hii kwa ushirikiano na makubaliano na Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye ndiye Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa sasa. Awali, kabla ya muswada wa sheria hiyo kusomwa kwa mara ya pili bungeni, pale ulipofikishwa na kusomwa kwa mara ya kwanza na hatimaye kuondoshwa kujadiliwa, Rais wa Zanzibar alikuwa anatakwa ushauri tu.

Haikuwa lazima ushauri wake ukishapimwa kuwe na makubaliano kati yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania . Na haya ni miongoni mwa manufaa yaliyopatikana kwa Zanzibar , baada ya muswada huo kurudishwa bungeni.

Sheria ya marekebisho ya katiba inatoa mamlaka sawia kwa viongozi hawa wawili, marais. Sasa kwa kila hatua inayotakiwa kufuatwa, basi shurti Rais wa Jamhuri ashauriane na akubaliane na Rais wa Zanzibar .

Na hili likaleta shida kwa kambi rasmi ya upinzani, inayoongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kama ilivyoelezwa waziwazi katika hotuba ya kambi hiyo iliyowasilishwa bungeni na Msemaji wake katika masuala ya sheria na katiba, Tundu Lissu.

Basi mamlaka hayo “makubwa” yakatifua hasira na chuki. Zanzibar ikachukuliwa kama mzaha badala ya kupewa nafasi na hadhi yake ambayo tunaamini ni muhimu katika morali wa kuendeleza muungano.

Ni jambo la bahati mbaya sana kusikia kauli hii. Lakini ni jambo la bahati mbaya zaidi kubaini ukweli kwamba kauli hiyo imetokana na kutokuwepo kwa Tanganyika , kibayana.

Tanganyika, ndiye mshirika mkuu wa kuasisiwa kwa Muungano wa Tanzania . Ni kuchanganywa kwake na Zanzibar ndiko kulikozaa kiitwacho Jamhuri ya Muungano wa Tanzania . Laiti Tanganyika ingekuwepo bila kificho kama ilivyo tangu 1964, isingekuwa rahisi kuichukulia Zanzibar ni mshirika mwepesi.

Jamhuri ya Watu wa Zanzibar iliunganishwa na Jamhuri ya Tanganyika ndipo ilipozaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 26 Aprili, 1964.

Akili inayofikiri vizuri haraka inakamata kwamba kitendo cha kuificha Tanganyika , kilichofanywa kwa hila kwa sababu sivyo makubaliano yalivyoelekeza, kilitengeneza mapema kabisa mazingira ya muungano wenye utata.

Muda wote huu wa miaka 47 ya muungano, Zanzibar imekuwa ikijadiliana uhusiano wa kimuungano na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , zao lililotokana na jamhuri mbili zilizounganishwa. Kila moja ilikuwa na mamlaka na madaraka yake. Wala hayo hayakuzingatia ukubwa wa eneo au wingi wa watu wake.

Kumbe kilichotakiwa kilillahi tangu pale, ni kuitandua bayana Tanganyika baibui lililofunikwa ili viongozi wake ndio wakae upande mmoja na kujadiliana na Zanzibar watakaokuwa upande wa pili.

Huo ni muungano wenye mfumo wa serikali tatu. Unayo serikali pekee ya Zanzibar kama ulivyonayo serikali pekee ya Tanganyika , kisha unayo serikali ya ushirikiano – muungano – inayoshughulikia masuala yaliyounganisha jamhuri zile mbili.

Hakika kauli iliyotoka zama hizi za sasa ya kuwa Zanzibar imechukua mamlaka makubwa ya ushiriki hata watu wake kuwa na sehemu katika mchakato wa kutunga katiba kwa ajili ya yale mambo ambayo si ya muungano isingesikika.

Jambo zuri ni kwamba si juu ya viongozi wa mamlaka ya Zanzibar wala wananchi wenyewe wa Zanzibar kubeba lawama kwa mfumo huo.

Si juu yao , na kwa hakika hasa, si haki yao kwasababu hata wenyewe wamekuwa wakilalamika kuwa mfumo wa muungano wa serikali mbili umeleta matokeo hasi kwa nchi yao . Umeidhoofisha kwa namna mbalimbali.

Ndio maana mara kadhaa upande wa Zanzibar kumesikika kauli za kwamba kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haijaona umuhimu wa kuifichua Tanganyika ili ikasimamia maslahi yasiyokuwa ya kimuungano, basi ni wakati sasa Zanzibar ndiyo ivikwe joho la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kile kiitwacho Tanzania Bara ibaki peke yake.

Imekuwa ikiaminika Zanzibar kuwa kwa kufungiwa baibui la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Tanganyika imekua vizuri kimaamuzi, kiuchumi na kisiasa kuliko ilivyo kwa Zanzibar ambayo kwa mfano, hainufaiki ipasavyo na sera za kifedha za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ingawa yenyewe ilishiriki kuunda benki hiyo kwa kuchanga asilimia 11 ya hisa za kuanzishwa kwake.

Benki Kuu ya Tanzania ilianzishwa rasmi baada ya kusambaratika kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki (EACB) ambayo ilikuwa chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) iliyovunjika mwaka 1977 kutokana na misuguano ya kisiasa iliyokabili nchi wanachama – Tanzania , Kenya na Uganda .

Madai ya muungano kuwa wa mfumo wa serikali tatu si ya leo. Yaliibuka miaka mingi iliyopita, na hata kabla ya Tanzania kurudisha mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992.

Mzee Aboud Jumbe Mwinyi alipeleka waraka maalum kwenye vikao vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliokuwa na mapendekezo ya kufikia lengo hilo . Aliliwa njama, mpango wake ukabezwa na jamhuri ikamfukuza urais kwa kumtaka atie saini hati maalum iliyoandaliwa na Rais Mwalimu Julius Nyerere mjini Dodoma .

Mzee Jumbe, aliyekuwa mhitimu wa shahada Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda , alikuwa kiongozi aliyepewa ridhaa na wananchi wa Zanzibar ambao hawako Dodoma bali Unguja na Pemba . Lakini, aliuzuliwa wadhifa wake kimabavu mjini Dodoma .

Rai ya kuitandua baibui Tanganyika , ili iwepo bayana, ilikuja tena mwaka 1994. Kulijitokeza kilichojiita G-55, mjumuiko wa wabunge wa upande wa Tanganyika walioshinikiza bunge kuidhinisha mpango huo.

Mwalimu Nyerere, wakati huu akiwa kiongozi mstaafu, alikasirika sana na akalazimisha kuingia kwenye vikao ambako alikemea viongozi wawili wa ngazi ya juu kwa kile alichokiita “kutomshauri vizuri” aliyekuwa mrithi wake kimadaraka, Mzee Ali Hassan Mwinyi.

Viongozi waliovikwa gunia la lawama walikuwa John Malecela, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na kiongozi wa serikali bungeni, na Horace Kolimba, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM msimamiaji mkuu wa sera za chama hicho tawala.

Kama hayo hayakutosha kuwa adhabu kwao, Mwalimu aliwatungia Malecela na Kolimba, kitabu mahsusi – Hatima yetu na Uongozi wa Tanzania – kilichowapaka “unuko” huku akiwaapia Watanzania kuwa hao hawafai kuwa viongozi.

Yote hayo ni historia. Ila yameleta athari nyingi kihadhi ya watu hao na mwenendo wa siasa ndani ya mfumo wa muungano wa serikali mbili.

Leo, tunapozungumzia ujaji wa mchakato wa katiba mpya ya Watanzania, tunayakumbuka kama njia ya kufikia matarajio salama. Basi huu ndio wakati wa Watanzania kueleza ukweli wanaoutaka.

Ni wakati wao kueleza wanataka muungano wa mfumo gani – serikali mbili au tatu? Zanzibar imeshaamua kwamba inataka mfumo wa serikali tatu, wanaoamini ndio utaleta muungano endelevu unaozingatia uwazi na hali halisi iliyopo sasa.

Wazanzibari wamejengwa hivyo. Wanatumaini hivyo. Wanaamini hivyo. Huo ndio mwelekeo wao maana wamechoka kusimangwa kwa udogo wao. Labda watu hawajui, Zanzibar ni ndogo kieneo tu, bali watu wake wana akili na utamaduni wao.

2 responses to “Wazanzibari wana akili, na utamaduni wao

  1. Wazanzibar tunataka serikali 3 na kama haiwezekani basi tupo tayari kuvunja muungano kwa gharama yoyote ata kama wakituua tupo radhi lakini lazma jamhuri ya watu wa Zanzibar isimame

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s