Polisi watoe ufafanuzi, nani magaidi

Farouq Khalil Muhammad (38) amemfunguliwa mashitaka katika mahakama moja ya New York. Farouq anatuhumiwa kufanya ugaidi dhidi ya Marekani

Na Omar Msangi

Wiki iliyopita Desemba 10, 2011 kitengo cha ukachero cha Marekani, Federal Bureau of Investigation (FBI), wametoa taarifa kuwa wamemfungulia mashitaka Farouq Khalil Muhammad (38) katika mahakama moja ya New York. Farouq ambaye hivi sasa anaishi Canada, ni raia wa Iraq na anatuhumiwa kufanya ugaidi dhidi ya Marekani.
Katika maelezo ya mashitaka inadaiwa kuwa Farouq alikula njama na kusaidia vitendo vya kigaidi vilivopelekea kuuliwa askari 5 wa Marekani mwaka 2008 katika mji wa Mosul, Iraq. Labda tusimame kidogo hapa tufafanue na tupate maana ya shitaka hili. Mosul ni mji katika nchi ya Iraq. Iraq ndio nyumbani kwao Farouq Khalil Muhammad. Askari wa Marekani waliokuwa Mosul ni wavamizi. Ni jeshi la uvamizi lililokuwa limevamia Iraq likiuwa wananchi wasio na hatia kwa yale madai ya urongo kwamba Saddam Hussein alikuwa na silaha za maangamizi.

Kwa hiyo alichokuwa anafanya Farouq na wananchi wenzake wa Iraq ni kujihami. Ni kupambana na jeshi la wavamizi. Wanachosema FBI hapa ni kuwa iwapo askari wa Marekani watavamia nchi, kwa mfano Tanzania, wananchi wakishika silaha kujihami, kama walivyofanya akina Mkwawa na wazee wetu katika Majimaji, basi hao kwa tafsiri ya FBI ni magaidi.

Kwa maana fupi, wewe ukivamiwa, wewe ukipigwa na Marekani, usitikisike wala kulalamika, ukae kimya kipigo kiingie sawasawa.
Labda ninukuu sehemu ya maelezo ya mashitaka hayo ili kuchambua vyema hoja ninayotaka kujenga. FBI wanasema kuwa Farouq “…expressed rage at the American invasion of Iraq and desire to take revenge on the United States.”

Wakichambua zaidi na kufafanua mashitaka FBI wanasema kuwa Oktoba 18, 2009 Farouq akiongea na mama yake alisema kuwa “like if enemy comes inside your country mother, there should not be anyone left out, big or small, everyone has to stand up and fight…it is everyone’s responsibility to fight that enemy.”

Ufupi wa maneno ni kuwa kilichoelezwa katika nukuu hii ambayo imetajwa kuwa ni mazungumzo ya simu yaliyonaswa na makachero, wanachosema waliokuwa wakiwasiliana na kuhimizana ni kuwa kama “nduli” akivamia nchi yenu wananchi wana wajibu wa kupambana naye hadi kumng’oa.

Tulidai hapa kwamba Iddi Amin alivamia nchi yetu na kwa sababu hiyo tukalazimika kumpiga. Kama ni kweli alivamia, tulikuwa na wajibu ule wa kumpiga na kila mwananchi alikuwa na wajibu wa kusaidia kwa namna yoyote kuhakikisha kuwa mvamizi anapigwa.
Sasa wanachosema Wamarekani ni kuwa wao wana haki ya kuvamia nchi yoyote na akitokea mtu wa kupinga na kuhamasisha wananchi kupambana na jeshi la wavamizi la Marekani ni gaidi!

Kabla ya “Crusade” iliyotangazwa na George W Bush, msamiati huu wa ugaidi kama ulikuwepo ulibakia katika makamusi. Lakini baada ya kulazimishwa kwamba na sisi tuwe na “Patriot Act”, yetu polisi wetu na hata baadhi ya wanasiasa nao wimbo huu wameukariri na unaonekana kuwanogea. Sasa ambalo pengine ni muhimu kujua, je, walipopewa wimbo huu walipewa na maana yake? Je, maana waliyopewa ndiyo hii hii wanayotupa FBI?

Labda sasa turudi hapa nyumbani Afrika. Ethiopia ilivamia Somalia na sio kama tulivyoingia Uganda kwa vile tulidai kuwa Idd Amin katuvamia. Zenawi hakudai kuwa Somalia imemvamia. Tunaowaita magaidi leo ni watu waliosimama kutetea nchi yao kutokana na uvamizi wa Ethiopia.

Kutokana na uvamizi na uharamia aliofanya Meles Zenawi Somalia, ndio kulikopelekea kuundwa kwa serikali inayoitwa ya mpito (TFG). Waliokuwa wameshika silaha kupinga uvamizi wa Ethiopia, wanasema kuwa TFG ni serikali ya vibaraka. Hawaitaki na wanaipiga vita. Hawa tuwaiteje? Je, ni magaidi wasio na sababu kama alivyo hasidi au watetezi wa nchi yao dhidi ya uvamizi?

Kinacholeta taabu ni kuwa tunavyowatizama Wasomali wanaopinga uvamizi wa Ethiopia na sasa uvamizi wa Kenya, ni sawa na ule msimamo wa FBI wanaomshitaki Farouq. Na hii ni kwa sababu hili si tatizo letu. Tunalazimishwa tuone kuwa tuna tatizo la magaidi, lakini kwa vile ukwlei ni kuwa hatuna tatizo la ugaidi, sasa tunaishia kubariki vitendo vya kiharamia vya Ethiopia na kuwapachika ugaidi wanaojitetea na wanaotetea nchi yao kama sisi tulivyoingia vitani kutetea nchi yetu ilipovamiwa na Idd Amin.

Hivi sasa Kenya ipo vitani ikidai kupambana na Al Shabaab. Al Shabaab nao wanasema kuwa watapambana na Kenya na watapeleka kilio hadi Nairobi. Hivi ikitokea Nairobi ikapigwa na waliopiga wakadai kuwa wanalipiza kisasi kwa Wasomali wanaouliwa kwa risasi za askari wa Kenya, nani wa kulaumiwa? Pamoja na utandawazi na hii hali ya kujikuta katika makucha ya ‘USA hegemony’, tuna haja ya kuwa makini kidogo juu ya hii vita ya ugaidi tunayosukumizwa kushiriki.

Kwa nini tuhofie magaidi?

Dr. Robert M. Bowman, ambaye ni kanali wa jeshi mstaafu wa jeshi la anga la Marekani, mwaka 2001 alimwandikia barua ya wazi Rais George W Bush. Katika barua hiyo, Dr. Robert alijibu swali moja tu: Kwa nini Marekani inachukiwa na kwa nini imekuwa shabaha ya magaidi. Alianza barua yake kwa kupinga kile alichokuwa akisema Bush kwamba magaidi wanaichukia Marekani kwa sababu ya demokrasia, uhuru na kujali kwake haki za binadamu.

“We are not hated because we practice democracy, freedom, and human rights. We are hated because our government denies these things to people in third world countries whose resources are coveted by our multinational corporations. And that hatred we have sown has come back to haunt us in the form of terrorism…”

Alisema Marekani inachukiwa kwa sababu serikali imekuwa ikifanya uharamia na ugaidi duniani kote na kufanya mauwaji huku ikipindua serikali za wananchi na kuweka vibaraka na magaidi walio tayari kuuza na kuwasaliti watu wao pamoja na mali za nchi zao.
Katika barua hiyo, Dr. Robert akataja msururu wa uvamizi, ugaidi na uharamia uliofanywa na Marekani katika nchi mbalimbali na kusababisha maafa makubwa.

Hoja anayoibua Dr. Robert ni kuwa Marekani inachukiwa kwa sababu ya uharamia na uovu wake inaofanya duniani kote na kama imekuwa shabaha ya magaidi, basi wanaoitwa magaidi wanaipiga kwa sababu Marekani yenyewe imekuwa gaidi namba moja.

Pamoja na Dr. Robert wapo raia wengine wa Marekani walioandika juu ya mada hii wakitaja mifano mbalimbali ya matendo ya serikali yao ambayo ndiyo yanafanywa Marekani ichukiwe. Katika jumla ya mifano inayotajwa ni mauwaji ya El Chorillo. Katika mauwaji haya, askari wa Marekani waliuwa takriban watu wasio na hatia wapatao 5,000 katika kijiji cha El Chorillo na kuwachoma moto wengine katika shimo.

Hiyo ilikuwa mwaka 1989 Marekani ilipovamia Panama kumwondoa Manuel Noriega ambaye ilimwona ashakuwa mzigo alipotaka kurejesha mfereji wa Panama katika miliki ya watu wa Panama. Kutokana na jinsi askari wa Marekani walivoangamiza watu na kuwachoma, kijiji kilikuja kubatizwa na kuitwa Hiroshima Ndogo (Little Hiroshima).

Kama ni dhambi, basi dhambi kubwa waliyofanya wale watu zaidi ya 5,000 wa El Chorillo hata kijiji chao kikaangamizwa kama kimepigwa bomu la nyukilia, ni ule msimamo wao wa kizalendo wa kutaka makampuni ya kibeberu ya Marekani yaondoke Panama.
Sasa, Marekani ikilia ugaidi, hii ndiyo sababu ya kuwa shabaha ya magaidi. Na kwa maana hiyo hiyo, kama hivi leo Kenya na Uganda zitalia kitisho cha ugaidi, sababu itakuwa kuwa wamevamia nchi ya watu. Ni wavamizi. Wameingia katika nchi ya watu na wanauwa.

Na kama Dr. Robert alivyomwambia Bush, njia ya uhakika ya kuepukana na kuwa shabaha ya ugaidi ni kufanya mambo mema na kuacha uovu. Watu wakifanyiana wema, ugaidi utatoweka. Hatuna sababu ya kuwaogopa Wasomali maadhali hatujavamia nchi yao na kuuwa watu wao. Vinginevyo, tutakuwa tunaimba ‘ushahidi’ wa kufundishwa na hii itakuwa ni kujidhalilisha.

Nchi yetu bado ni masikini, lakini tunazofursa za kupiga hatua kama dhamira itakuwepo na tukatumia vyema akili na rasilimali zilizopo. Kwa upande mwingine, hivi sasa tunakabiliwa na tatizo kubwa la nishati ya umeme. Zipo nchi na yapo makampuni ambayo yakipewa fursa, kwa muda mfupi kabisa yanaweza kufanya tatizo hili kuwa ni suala la kihistoria. Umeme wa kutosha ukapatikana, tena kwa bei chini ya nusu ya sasa, na tukawa na ziada ya kuuza nje ya nchi.

Ila tukienda na mtindo huu wa ‘ushahidi’ wa kufundishwa, hata zikitokea fursa za uwekezaji ambazo zitatunasua na umasikini na kufuta tatizo la umeme, si ajabu tukaambiwa tuache na tukaacha.

Chanzo Gazeti la Annuur

Advertisements

One response to “Polisi watoe ufafanuzi, nani magaidi

  1. Tunashukuru Mungu SWT kwa kuwa bado tunayo wadadisi wa siasa na maneno wanaofanya juhudi kubwa kuhakikisha dhulma isidumu. Shukran, Ndugu Omar Msangi kwa ufafanuzi wako huu bora kabisa.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s