‘Mapalala’ haweshi ndani ya CUF

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na wananchi wa Kilwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Magengeni Kilwa Kivinje katika ziara yake ya baadhi ya mikoa ya Tanzania Bara.

Kama CUF iliweza kukaa pamoja na CCM iliyodaiwa kutumia vyombo vya dola kuwafanyia ukatili, uovu na idhilali ya kutisha wanachama wake, hasa kila unapoingia uchaguzi mkuu, vipi ishindwe kutumia vikao vyake kusawazisha sintofahamu iliyo katika safu yake ya uongozi?

*Kama Seif aliweza kukaa na Kingunge wa CCM *Vipi ishindikane kuzungumza madai ya Hamad?

Na Omar Msangi
Mwaka 1994 aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi, CUF, James Mapalala aliitisha mkutano wa hadhara katika viwanja vya Malindi. Lakini kabla kufika siku ya mkutano, ukazagaa uvumi kwamba mkutano huo ulikuwa umeandaliwa na ‘Komandoo., Dr. Salmin Amour na kwamba agenda kuu ilikuwa kumtukana Maalim Seif Shariff Hamad na kutangaza mgogoro ndani ya CUF.
Habari hizo zilisambaa kwa kasi ikidaiwa kuwa Mapalala anatumiwa tu ili kukivuruga chama. Baada ya kutafakari habari hizo, viongozi wa CUF na wafuasi wao waliamua kutokufanya lolote kuzuiya mkutano ule. Wakahudhuria na kwa utulivu kabisa wakasikiliza kilichokuwa kikizungumzwa.

Naam, kama ilivyotarajiwa mada kuu ya Mapalala ilikuwa kumsema Maalim Seif na kutuhumu kwamba baadhi ya viongozi ndani ya CUF walikuwa na agenda ya kurejesha Uarabu na Usultani. Alidai chama kimetekwa nyara na watu wa Hizbu na kwamba lengo lao ni kumrejesha Sultan na Waarabu kutawala Zanzibar/Tanzania. Akiyasema hayo kulikuwa na kundi kubwa la vijana wakishangilia.

Hata hivyo, Unguja ndogo, vijana wale walitambulika kuwa ni vijana waliokusanywa kutoka maskani za CCM. Baada ya mkutano ule, haukupita muda, James Mapalala aling’oka yeye na kuwaacha aliodai kuwa wanataka kuleta Uarabu na Usultani.

Mambo hayakuishia hapo. Walifuatia akina Nyaruba, Tamwe Hiza, Shaybu Akwilombe, Wilfred Rwakatare na wengine kama hao.
Hivi sasa kunaonekana kufukuta mgogoro mwingine wenye sura ile ile ya ‘ki-Mapalala’ na ‘ki-Nyaruba nyaruba.’ Lakini kabla ya kuutizama kwa undani, turejee katika uchaguzi mkuu mwaka 2000 na yaliyojiri baada ya kutangazwa matokeo.

Rekodi zinaonyesha kuwa yalipotokea mauwaji Januari 26 na 27 mwaka 2001, Maalim Seif Shariff Hamad hakuwa nchini. Alikuwa nje ya nchi ambapo alikwenda muda mfupi baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi mkuu ambapo Mheshimiwa Aman Abeid Karume alitangazwa mshindi.

Kwa upande wa Hamad Rashid Mohammed, japo alikuwa nchini, hakushiriki maandamano hayo. Si kwa kuyaandaa wala kuhamasisha wananchi kushiriki. Alikuwa rumande baada ya komandoo Salmin kuwaacha ndani kwa muda mrefu akidai kuwa maadhali si mapapai kwamba yataoza, wakae tu. Kwa maana nyingine, maandamano hayo yalifanyika bila ya uongozi wa Maalim Seif Shariff Hamad wala Hamad Rashid Mohammed.

Serikali kwa upande wake ilitoa tangazao la kupiga marufuku maandamano yale. Hata hivyo CUF wakashikilia msimamo wao wakisema kuwa maandamano yao ni ya amani na haki yao ya kikatiba kuonesha kutoridhishwa kwao na matokeo ya uchaguzi. Kweli CUF wakaandamana. Lakini hata kabla ya maandamano, mauwaji yakaanza. Polisi wakavamia msikiti wa Mwembetanga mara baada ya swala ya Ijumaa wakauwa watu wawili.

Serikali badala ya kuwachukulia wanachama na wapenzi wa CUF kuwa ni wananchi na raia wa Tanzania waliopinga amri ya polisi ya kutokufanya maandamano, ikawaona kama magaidi hatari. Iliwatizama kama maharamia na wapiganaji wenye silaha waliovamia mitaa ya Pemba na Unguja. Kwa hiyo askari wakatoka kama wanakwenda vitani. Watu wengi wasio na hatia hata wale waliokuwa majumbani na kondeni wakauliwa, kutiwa vilema na kuharibiwa mali zao.

Yalitajwa pia matukio ya wanawake kubakwa, uporaji na utekaji nyara. Akina mama walivamiwa majumbani wakaporwa vidani na mikufu na mabinti wakatekwa na kufanyiwa ukatili wa kuwanajisi kwa siku kadhaa zilizofuatia mauwaji. Hali ilikuwa mbaya zaidi katika kisiwa cha Pemba ambapo inasemekana mamia ya watu waliuliwa japo serikali ilisema ni ishirini na saba (27) tu.

Kama nilivyotangulia kusema yote haya yalifanyika wakati Maalim Seif akiwa nje ya nchi. Wana-CUF waliandamana japo mwenye urais wake alikuwa hayupo ambapo kwa kawaida mgombea ndiye huwa mstari wa mbele akiwahamasisha na kuwaongoza wanachama na wafuasi wake kupinga matokeo.

Kwa hiyo japo walioandamana walimpigia kura Maalim Seif na japo walitamani na walitaka awe Rais, lakini lengo na agenda yao haikuwa Maalim kuwa Rais wa Zanzibar, vinginevyo walivyoona mwenyewe haupiganii wangekosa nguvu ya kuandamana. Lakini inavyoonesha, na ndio ukweli wenyewe, kwamba agenda yao ilikuwa kuondoa serikali ya CCM waliyoamini kwamba inawadhulumu, kuwahujumu na kudumaza maendeleo ya nchi. Ndio maana kutokuwepo Maalim Seif hakukuwazuiya kuandamana.

Wakati ule haikutangazwa wazi Maalim alikuwa nchi gani huko Ulaya na alikwenda kufanya nini. Alikwenda kimya kimya na hata aliporudi, alirudi kimya kimya. Haikutangazwa lini alirudi na alikuwa wapi. Wananchi walijua kuwa karudi siku walipomuona akiandamana na kada wa CCM Mzee Kingunge Ngombale Mwiru kwenda Pemba kutoa ubani kwa wafiwa.

Ni wazi kwamba Maalim baada ya kurudi alikaa na CCM wakajadili yaliyojiri Pemba na Unguja na wakaafikiana nini cha kufanya kutuliza hali. Wakati ule wananchi wa Mtambile, Micheweni na Pemba kwa ujumla, walikuwa wakiwaona CCM ni wauwaji. Na CCM ni watu, ni viongozi, sio kadi, bendera na ofisi au rangi za njano na kijani.

Kwa hiyo kama CCM walionekana wauwaji, akina Philip Mangula, Malecela, Kingunge, Benjamin Willium Mkapa, Amani Abeid Karume na timu yake, ndio walikuwa wauwaji wenyewe wakitumia vyombo vya dola. Wauwaji waliouwa wanachama wa CUF na wananchi wa Pemba. Wauwaji waliomuuwa Imam wa msikiti wa Mwembetanga.

Hata hivyo, pamoja na ukweli huo, na pamoja na ukweli kwamba bado jeraha lilikuwa bichi kwa maana kuwa bado hata wafiwa walikuwa hawajaondoa matanga, CUF waliweza kukaa na CCM wakapanga namna ya kuwafariji na kuwatulizwa wafiwa Pemba. Walikaa wakaona kuwa CCM lazima ijikoshe na mapema kwa kutoa ubani.

Kwa busara na uungwana wao (?), CUF wakakubali kuibeba CCM kwenda Pemba kutoa ubani. Maalim Seif Shariff Hamad akabebeshwa msalaba wa kuandamana na Mzee Kingunge Ngombale Mwiru. Hivi sasa zipo taarifa nyingi katika vyombo vya habari zikionesha kuparurana Maalim Seif Shariff Hamad na Hamad Rashid. Wote hawa, kila mmoja ana madai yake dhidi ya mwenzake na kila mmoja anajitahidi kujieleza ili mwenzake aonekane kuwa ndiye mbaya. Na katika kufanya hivi, kila mmoja anajitafutia wafuasi.

Wapo wanaomtuhumu Mheshimiwa Hamad, Mbunge wa Wawi, kwamba kanunuliwa na CCM amng’oe Maalim Seif katika nafasi ya u-Katibu Mkuu achukue nafasi hiyo yeye. Wanaodai hayo wanasema kuwa Hamad ameahidiwa kupewa Urais wa Zanzibar, na kwamba Maalim Seif hatakiwi kwa sababu ana agenda ya kuvunja muungano.

Kwa upande mwingine inadaiwa kuwa Hamad anamtuhumu Maalim Seif kwamba anakidumaza chama. Amewatelekeza Blue Guard na kwamba hana mpango wa kuimarisha CUF kwa upande wa Bara. Anaona CUF ni ya Unguja na Pemba. Inasemekana kuwa katika kikao kimoja cha ndani cha hivi karibuni kilichofanyika katika ofisi ya CUF Vuga, Zanzibar, ilitolewa taarifa na mmoja wa ‘makachero’ ambao awali walionekana watu wa Hamad wakajua siri na mpango mzima wa Hamad.

“Mimi namuachia Mungu, nani mkweli na nani anasema uwongo, itajulikana”, anadaiwa kusema Maalim baada ya kutolewa taarifa ile.
Inawezekana Maalim Seif kama ana madai dhidi ya Hamad Rashid akawa yupo sahihi, kwa maana kuwa anayosema juu ya Hamad ni kweli. Kwa upande mwingine, inawezekana Hamad Rashid akawa sahihi katika tuhuma anazomrushia Maalim Seif.

Kwa upande mwingine inawezekana mmoja wao ndiye akawa sahihi na mwingine kapotoka au wote wakawa wazushi tu. Lakini mimi nadhani kama ni kuzingatia masilahi ya chama na masilahi ya wanachama na wapenzi wa CUF waliokipa uhai chama hicho kwa kujitoa muhanga kwa hali na mali, muhimu hapa sio nani sahihi.

Swali ni je, kwa nini kama kuna tatizo viongozi wasikae wakazungumza na kufikia makubaliano badala yake wanaparurana na kushambuliana katika mikutano na katika vyombo vya habari? Kama CUF waliweza kukaa na CCM ambao kwa wakati ule walikuwa ‘wauwaji’ waliouwa wananchama wao mpaka wengine wakaamua kukimbilia uhamishoni na mpaka sasa wapo Somalia, kipi kinawashinda leo kukaa na kuzungumzia matatizo yaliyo ndani ya chama chao na kupata ufumbuzi ?

Kama CUF iliweza kukaa pamoja na CCM iliyodaiwa kutumia vyombo vya dola kuwafanyia ukatili, uovu na idhilali ya kutisha wanachama wake, hasa kila unapoingia uchaguzi mkuu, vipi ishindwe kutumia vikao vyake kusawazisha sintofahamu iliyo katika safu yake ya uongozi?

Wanachotakiwa kufahamu Maalim Seif Shariff na Hamad Rashid ni kuwa wale wanachama wa matawi ya Kossovo, Chechnya, Gaza na Kandahar, hawakuwa wakijitoa muhanga na kujitolea kuimarisha na kutetea chama kwa vile kuna sura ya Hamad Rashid na Maalim Seif katika CUF. Walifanya vile kwa sababu hata kabla ya CUF walikuwa na matatizo yao, walikuwa na agenda zao na matarajio yao.

Ilipoibuka CUF na kutangaza kuwa inapigania haki sawa kwa wote, ikasimama kama chama cha wananchi na cha kutetea wananchi, umma ukawa pamoja nacho. Wakati vyama vingine vikitoa posho na kukodi magari kwa ajili ya wanachama wao kwenda katika mikutano ya hadhara, CUF haikuwa na tatizo hilo. Watu walikuwa wakichangishana na kukodi magari, maelfu wakawa wanafurika katika mikutano. Mpaka hivi sasa hakuna chama kilichoweza kuvunja rekodi ya CUF ya kuwa na wanachama na wapenzi wenye kujitolea kwa hali na mali kukihami chama. Kwa hakika kilikuwa kweli chama cha wananchi.

Sasa kama imefika mahali Hamad na Maalim wameona muhimu ni u-Katibu Mkuu na hawawezi kukaa wakaongea katika vikao vyao vya ndani wakalimaliza, wajue kuwa wakiendelea kulumbana majukwaani, kwanza watakuwa wanajidhalilisha wenyewe, lakini pili watafanya wanachama wao wawadhanie vibaya.

Huko nyuma kulikuwa na wakina Nyaruba wakafuatiwa na akina Tamwe Hiza, Shwayb Akwilombe na Rwakatare. Uzoefu huo umewafanya wanachama wa CUF kubaki na wasiwasi kuwa chama chao kimejaa mamluki. Mapandikizi CCM B, vijana wa Nyerere waliotumwa kuwa wapinzani ambao kazi yao ni kuwapandisha joto wanachama wao na kulishusha.

Sasa kama ‘vijana hao wa Nyerere’ wapo katika CUF, itakapofika mahali kwamba CUF inatakiwa ifikie pale ilipofikia NCCR Mageuzi ya Agostino Lyatonga Mrema, vikao vya kichama havitasaidia kitu. Japo CUF waliweza kukaa na CCM na wakaweza kwenda pamoja kuhani wafiwa Pemba, itaonekana jambo lisilowezekana kukaa na kuzungumzia tofauti za Hamad Rashid na Maalim, wote Wapemba. Wataendelea kulumbana mpaka yatokee yale yaliyomsibu Mrema alipotofautiana na Mabere Marando.

Nani Mabere na nani Mrema katika mgogoro huu wa CUF ndicho wananchi wanasubiri kuona. Hata hivyo wanachotakiwa kufahamu Hamad Rashid na Maalim Seif ni kuwa CUF haikufika hapo ilipo kwa umahiri wa uongozi wa yeyote kati yao. Bali imefika hapo kwa nguvu ya wananchi ambao hivi sasa wanawasaliti kwa kuendeleza malumbano ya kugombea ukatibu.

Wale vijana wa Kosovo na Kandahar hawakuingia CUF kumfuata Profesa Lipumba, Maalim Seif wala Hamad Rashid. Kama walivyomfuata Marehemu Kighoma Ali Malima katika NRA wakiamini kwamba ataleta ukombozi, haki sawa kwa raia wote na maendeleo, ndivyo walivyoingia CUF baada ya Malima kufariki.

Wapo wazee wa Pemba na wanachama wa CUF ambao wamekuja na hoja ya kutaka Pemba ijitenge na kuwa nchi mbali na Unguja na mbali na Tanzania au angalau iwe na madaraka ya ndani. Waliibua hoja hii baada ya kuona kuwa siasa za CUF Vs CCM haziwafikishi kwenye malengo yao. Madai ni kuwa kisiwa cha Pemba kwa muda wote kimekuwa kikihujumiwa na serikali ya mapinduzi (SMZ), serikali ya CCM. Na hii ni katika ajira, nafasi za madaraka, miundombinu ya kiuchumi na kijamii, huduma mbalimbali za kijamii, elimu n.k

Sasa kuwa kwao Wapemba kwamba wengi wao ni wapinzani wa CCM, sio kwa vile Maalim Seif na Hamad Rashid ni Wapemba waliotoka CCM wakaunda CUF. Ni kwa sababu waliamini kwamba ni wakweli katika madai yao na madai ya chama chao, CUF, kwamba wanapigania haki sawa kwa wote. Na kama haki kwa wote itapatikana kupitia CUF, madhila na shida za Wapemba zitakuwa zimeondoka.
Labda sasa Maalim Seif na Hamad Rashid wajiulize, malumbano magazetini na majukwaani, yatajenga nguvu ya kutatua matatizo ya Wapemba na Wazanzibari kwa ujumla au itakuwa kuwagawa na kuwadhoofisha?

Kama waliweza kukaa na CCM na wakakubaliana hata kwenda pamoja Pemba kuhani katika mauwaji ya 2001, kipi kinawashinda kukaa, kuzungumza na kumaliza tofauti zao? Lakini nimalizie kwa kusema kuwa kama ni kweli kwamba Hamad Rashid kapewa agenda ya kuchukua u-Katibu Mkuu ili apewe u-Rais Zanzibar na akakubali, atakuwa amejidang’anya na sidhani kuwa atakuwa na ujinga huo.

Wanaomuahidi lazima watakuwa watu ambao wapo serikalini, serikali ya CCM, na anatajwa Waziri Mkuu Pinda. Kumpa Hamad u-Rais maana yake ni kuing’oa CCM madarakani. Je, inawezekana CCM wakaweka mpango na mkakati wa kujitoa madarakani? Kama wamemuahidi, wameongopa. Lengo si kumpa Hamad Rashid urais, bali kukivuruga chama kibaki takataka. Hivi leo NCCR-Mageuzi ya Mbatia sio ile ya Agostino Lyatonga Mrema na Mabere Nyaucho Marando.

Chanzo Gazeti la Annuur

One response to “‘Mapalala’ haweshi ndani ya CUF

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s