Tibaijuka akabidhi nyumba ya Wakfu

 

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka

Prof. Anna Tibaijuka afanya yaliyomshinda Mwinyi, Mkapa

*Akabidhi nyumba za Wakfu Kariakoo *Sheikh Bassaleh ampa salamu za Kikwete

Profesa Anna Tibaijuka amefanya yaliyoshindikana katika uongozi wa Alhaji Alli Hassan Mwinyi na Benjamin Willium Mkapa. Amefanikisha kurejeshwa nyumba za Wakfu za Waislamu zilizokuwa zimeporwa na akina Pius.

Katika kipindi cha Mzee Mwinyi na Mkapa, katika baadhi ya wakati, Waislamu waliishia kupigwa mabomu na kuwekwa ndani walipokuwa wakidai nyumba hizo za Wakfu zilizokuwa zimeporwa.

Lakini hatimaye nyumba hizo zimepatikana na Waziri mwenyewe Prof. Anna Tibaijuka kuchukua taabu ya kwenda kuwakabidhi Waislamu hati ya nyumba hizo zilizokuwa zimeporwa baada ya kuzipigania kwa zaidi ya miaka 21.

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka, akiwa ameandamana na Kamishna wa Ardhi Bi. Anna Mdemwa na Mdhibiti wa Hati Bi. Subira Sinde, juzi Desemba 14 baada ya swala ya Adhuhuri waliwasili katika eneo zilizopo nyumba hizo zilizokuwa zimeporwa mtaa wa Somali Kariakoo na kuwakabidhi Waislamu hati za nyumba hizo.

Imam wa Masjid Mwinyi, Sheikh Maulid Kambaya, ndiye aliyewapokea na kupokea hati hiyo kwa niaba ya wadhamini wa msikiti huo.

Akikabidhi hati ya nyumba hizo zilizopo kiwanja Plot No. 33 Block 77 Kariakoo jijini Dar es Salaam, Prof. Tibaijuka alisema anafarijika sana kuona kwamba amefanikiwa kuwapatia Waislamu haki yao hiyo na kulitatua tatizo kabla ya kwisha mwaka huu.

Alisema, awali walikuja Masheikh ofisini kwake na kumtaka awahakikishie kwamba atalishugulikia tatizo hilo la Waislamu kikamilifu ili haki ipatikane kwani ni muda mrefu sasa umepita bila kuonekana dalili za Waislamu kupatiwa nyumba hizo zilizokuwa zimetolewa wakfu kwa Waislamu na Hajat Aziza bint Omar mwaka 1991.

Kabla hajakabidhi hati ya nyumba hizo, Prof. Tibaijuka alieleza kuwa tatizo lililochochea Waislamu kuporwa nyumba hizo za Wakfu ni ucheleweshwaji wa kumilikishwa Wakfu huo kwa walengwa ambao ni Msikiti wa Mwinyi, mara baada ya mwenye nyumba kutoa wakfu huo, jambo ambalo liliwapa mwanya wajanja kutumia fursa hiyo kudhulumu.

Alisema, tatizo hilo limekuwa sugu na limekuwa likitokea mara kwa mara hasa kwa nyumba au viwanja vinavyotolewa na watu kwa ajili ya taasisi za dini hususan misikiti na makanisa, ambapo watu wenye tamaa na wahalifu hutumia ujanja kujimilikisha nyumba hizo.

Alisema kuwa kutokana na kukithiri kwa uhalifu wa aina hiyo hasa katika maeneo ya miji, ni vyema taasisi za dini zinapopata sadaka za wakfu, kuchukua hatua za haraka kuzimiliki ili kuziba nafasi kwa wale wenye uchu kudhulumu.

Ndugu zangu, kuweni macho na mali hizi zinazotolewa kwa ajili ya taasisi za dini, zinapotolewa wakfu kusaidia taasisi hizi hasa misikiti na makanisa, wajanja hapo hutokea na kujimilikisha kwa mbinu”, alitahadharisha Prof. Anna Tibaijuka.

Akizungumzia kuhusu nyumba nyingine ya wakfu iliyotolewa na Hajat Aziza bint Omar iliyopo jirani na msikiti wa Mtoro ambayo nayo imeporwa, Prof. Tibaijuka alisema tatizo hilo analishughulikia na yuko karibu kukamilisha utatuzi wake na kuahidi kuwa atakapokamilisha utatuzi wake atawakabidhi wakfu huo Waislamu.

Aliwapongeza Waislamu kwa kuvumilia na kuwa na subra katika kipindi chote hicho walichohangaika kupata haki yao na kuwaahidi kushirikiana nao kila watakapopata tatizo kama hilo.

Akizungumza baada ya makabidhiano ya hati ya nyumba hizo za wakfu, Maalim Ali Bassaleh ambaye naye alikuwa miongoni mwa viongozi wa dini waliohudhuria hafla hiyo, alisema tatizo la kuporwa nyumba za wakfu lisingekuwepo iwapo serikali ingeridhia kuwepo kwa Mahakama ya Kadhi nchini.

Alimweleza Prof. Tibaijuka kuwa kama kungekuwepo na Mahakama ya Kadhi nchini, wakfu ungesajiliwa na Kadhi na baadae kuwasilisha vielelezo vyake Wizara ya Ardhi na maendeleo ya makazi na hapo kazi ingekuwa rahisi kwa serikali na kwa wenye wakfu na migogoro isingekuwepo.

Hivyo alimtaka Prof. Tibaijuka kumfikishia ujumbe wake serikalini kwamba Mahakama ya Kadhi ina nafasi kubwa ya kuirahisishia serikali kazi na kupunguza migogoro mingi ya ardhi na majengo yanayohusiana na taasisi za kidini.

Pia alitumia fursa hiyo kumshukuru Waziri Tibaijuka kwa uadilifu aliouonyesha katika kutatua tatizo hilo la Waislamu na kusema kuwa kwa mwenendo huo, Waislamu sasa wanaona kuwa wapo watu waadilifu serikalini ambao wanaweza kuwapatia haki yao.

Nyumba zilizopo katika kiwanja No. 33 Block 77 Kariakoo jijini Dar es Salaam zilitolewa wakfu na Marehemu Hajat Aziza bint Omar kwa Msikiti wa Mwinyi ulioko Kariakoo mwaka 1991.

Hata hivyo baadae waliibuka watu waliotambuliwa kwa majina ya Pius Kipengele na Zakaria waliodai kuwa nyumba hizo ni mali yao na kuzipora.

Kufuatia uporaji huo, Wadhamini wa Masjidi Mwinyi walifungua kesi katika Mahakama ya Kisutu kudai haki ya Waislamu dhidi ya waporaji.

Kutokana na kudorora kwa kesi hiyo na Wadhamini wa Masjid Mwinyi kuelemewa kufuatia kesi hiyo kuchukua muda mrefu na kuhalalisha uporaji kwa waporaji, Waislamu kwa umoja wao waliamua kuingilia kati kupigania haki yao hiyo hadi pale itakapopatikana.

Sheikh Abraham Juma Kileo, Sheikh Ponda Issa Ponda, wanasheria Prof. Abdallah Safari, Yahya Njama na Benhaji Shaaban ambaye kwa sasa yupo nchini Uingereza, ni baadhi tu ya Waislamu waliojitolea kupigania haki hiyo ya Waislamu katika kesi hiyo.

 

 

Chanzo Gazeti la Annuur

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s