Sheria ya kulinda watoto itekelezwe

Watoto wanahitaji kulindwa na kuheshimiwa katika makuzi yao hivyo kuna kila sababu ya kuwekewa misingi mizuri ya sheria kutokana na madhila wayapatayo kutoka kwa watu wanaowadhalilisha na kuwanyanyasa kutokana na utoto wao kwani tujuavyo mtoto huwa hana sauti mbele ya mtu mzima lakini jee ndio anyanyaswe?

Na Ally Saleh

Sasa ni miezi 6 tokea Dk. Ali Muhammed Shein, Rais wa Zanzibar amesaini sheria muhimu sana katika maisha, makuzi na maslahi ya mtoto wa Kizanzibari ambayo ni thamini kupita thamani yoyote ile. Sheria Namba 6, 2011 imekuja baada ya juhudi, vilio na misukumo mbali mbali ya wana harakati kutokana na madai mengi ya unyanyasaji wa watoto wa Kizanzibari hali ambayo ilikuwa inaelekea kiwango cha kutisha.

Lakini mbali ya vitendo vya udhalilishaji bali pia haja ilikuwa imeonekana ya kubadilisha sheria za zamani kama zile za kuasili watoto ambapo imewahi kutokea watoto wa Kizanzibari wakichukuliwa kiholela kwenda kujiuunga na familia za kigeni bila ya ridhaa ya wazee wa asili.

Pia shughuli nyingi zinazohusu watoto kama vile vituo vya kulelea watoto, shule za watoto na kwa kiasi kikubwa vyuo vyetu vinasomesha mafunzo muhimu ya Kur-an na suala zima la Uislamu.

Taarifa za utafiti zimeeleza kuwa kuna tatizo kubwa la unyansaji wa watoto hapa Zanzibar na taasisi hizo nilizozitaja hapo juu zinatajwa kuhusika kwa kiasi kikubwa na kwa hivyo kuwa tishio kwa maisha ya vijana ya baadae.

Hivi karibuni kwa kujua ukubwa wa tatizo ndipo Serikali ikaamua kuanzisha kituo kiliopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja kinachoitwa One Stop Centre na kutafsiriwa kwa Mkono kwa Mkono kwa ajili ya kuwa ni kituo cha kuhudumia kesi kama hizo chini ya paa pamoja.

Sheria hii ina vipengele kadhaa na sisi tutavipitia vile muhimu lakini hasa madhumuni ya makala haya ni kuhimiza kukamilishwa kwa taratibu kadhaa zilizotajwa ndani ya sheria hii ili sheria ichukue mkondo wake na kutekelezwa kikamilifu.

Ndani ya Sheria hii mtoto anatajwa kuwa ni yule ambaye yupo chini ya miaka 18 na ndie huyo ambae analindwa kutokana na unyansaji kwa kuwa yeye kama mtoto hana uwezo wa kujikinga mbele ya jamii yenye mazonge mengi mno, uwezo wa kipato na hali kama hizo.

Sheria inamlinda mtoto asifanyishwe kazi za kumvunja nguvu, asionyeshwe picha za kumtia utuuzimani mapema na kubwa zaidi inajaribu kumkinga mtoto asiingizwe katika biashara za kusafirishwa kama bidhaa na kuingizwa kwenye kazi ya kitumwa, kutiwa katika umalaya au kutolewa viungo vyake.

Vipengele vinataka mtoto asilazimishwe kupimwa Ukimwi, lakini linalotia moyo zaidi ni kujua kuwa ndani ya Sheria hii imeanzishwa Mahakama ya Watoto ambayo kuwepo kwake kutawezesha kesi za watoto zisikilizwe katika mazingira maalum na sio kama ilivyo hivi sasa, lakini pia ina maana kuwa kesi hizi zitaweza kusikilizwa kwa haraka zaidi.

Sehemu ya Pili ya Sheria ya Watoto ndio inayoweka msingi mzima wa Sheria hiyo ambapo inatandika kile kinachoitwa Maslahi Mema ya Mtoto ambapo ni kutokana na maslahi hayo ndipo mtizamo mzima wa sheria unavyoelekeza.

Maslahi hayo ni yale ya kimwili na kihisia lakini pia yanajumisha haki nyengine mbali mbali ambazo mtoto lazima awe nazo kimsingi na sio za kupewa kwa njia ya kugaiwa au kama hisani.

Hizo ni pamoja na kuwa na wazee au kuishi na walezi , kuwa na jina, kuwa na uraia, kuandikishwa kama raia, kutobaguliwa, kushiriki katika harakati za makuzi yake kwa mujibu wa umri na watu wa rika lake, kusikilizwa maoni yake, kuujua na kushiriki katika utamaduni wake na kushiriki katika michezo.

Kifungu cha 16 cha Sheria kinasimama kulinda mtoto anaeishi na ulemavu. Sheria inasema wazi kuwa mtu yoyote hataruhusika kumdharau au kumnyanyasa mtoto anaeishi na ulemavu na kuendelea kutoa tafsiri pana sana ya maana ya ulemavu ukiwamo wa viungo, akili, ngozi na haki ya kupata elimu bila ya kubaguliwa.

Kifungu cha 20 kinaweka ulazima au wajibu wa mtu au afisa anaeshughulika na watoto, lakini pia wakiwemo waalimu, madaktari na wanasheria kuripoti iwapo watakutana na kesi yoyote ya unyanyasaji wa mtoto wakati wa kufanya kazi zao.

Ripoti hio itolewe kwa Mkurugenzi wa Ustawi wa Jamii, Maafisa wa Ustawi, Kituo cha Polisi au Sheha ili moja ya taasisi hiyo ianze mchakato wa kulifuatilia tatizo hilo linalokabiliwa na mtoto.

Mtoto hapaswi kuumizwa zaidi ya alivyonyanyaswa na kwa hivyo chini ya Kifungu cha 33 kinakataza mtu yoyote kutoa taarifa au kuchapisha picha ambayo itapekekea kumtambulisha mtoto alie katika hali hiyo, bila ya amri ya Mahakama. Adhabu kubwa ya faini au kifungo inatolewa kwa kosa kama hilo.

Sheria inazungumzia pia jinsi ya kumkamata mtoto ambaye atakuwa amekosana na sheria. Inaweka utaratibu wa kumkamata, inaweka utaratibu wa kmufikisha kituoni lakini inaweka pia utaratibu wa kuarifiwa wazazi au walezi wake katika muda unaofaa ili haki zake ziweze kulindwa.

Sheria inataja kwa kina utaratibu wa kuwa na vituo vya watoto ambako huko nako kumetajwa katika utafiti kwamba ni sugu kwa uharibifu wa watoto na vyuo vya kuosmesha masomo ya dini.

Kutakuwa na fomu kadhaa za kujaza na viwango vya kuvitimiza ambavyo vinapaswa kutimizwa na upande wa Serikali lakini pia kwa upande wamiliki kama hao ambao wengi wao hadi sasa wamekuwa wakifanya mambo kwa mteremko na mazoea tu.

Sasa wajibu wa kuitekeleza Sheria hiyo uko kwa kila upande. Na ni kwa kila upande kutimiza wajibu wake ndipo itakuwa na maana na kupunguza machungu tunayo yaona hivi sasa.

Kwa Serikali ni kuhakikisha kuwa taratibu zote zilotajwa chini ya Sheria zinakamilika. Kuwepo na Mahakama haraka, kuwepo na Maafisa wa Jamii wa kutosha, kuwepo kwa Sheria ndogo na taratibu zilizotajwa chini ya Sheria ili kila kitu kiende kwa kasi itakiwayo na usahihi mkubwa.

Upande mwengine ni ule wa taasisi mbalimbali unaojihusisha na masuala ya watoto ambapo kila mmoja ajipange sio tu kujua sheria, lakini kuitekeleza na kubwa zaidi ni kutoa elimu juu ya Sheria hiyo kwa watoto wenyewe lakini hata watu wazima.

Upande wa Polisi nao ni muhimu. Tunajua sasa wana dawati la jinsia lakini pia kumekuwa na lawama nyingi kwa Polisi kujaribu kuua au kupatanisha kesi za jinai za kunyanyaswa wanawake, tunaomba haya yasitokee kwa kesi za watoto.

Na bila ya shaka upande wa waandishi ni muhimu. Hivi karibuni Baraza la Habari MCT liliendesha mafunzo ya siku tatu kuwafunza waandishi namna bora ya kuandika mambo ya unyanyasaji wa watoto na pia kuipitia Sheria hii.

Ni matumaini yangu waandishi ndio watakuwa chachu ya kuleta mabadiliko ili tuepuke kuwa na jamii yenye chuki na hasira kwa sababu ya maovu na ukatili waliofanyiwa wakiwa watoto.

Utafiti unasema ukatili unaofanywa kwa mtoto akiwa mtoto unaweza kubaki akili kwa miaka 15 ikiwa hakupata matibabu ya uhakika. Na kwa kweli hatujawa na uwezo wa matibabu kama hayo na kwa hivyo kila vitendo vikitokea tunazidi kujenga wimbi la vijana wenye hasira.

Na jee hasira hizo watazitoaje? Hatujui. Na ndio maana ni vyema kukinga leo na sio kungojea kutibu kesho.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s