Ujamaa uliziunganisha Tanganyika na Zanzibar

Mbunge wa Jimbo la Wawi Pemba kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Hamad Rashid Mohammed, akijumuika na vijana wa Chama Cham Mapinduzi (CCM) akiwa na Msindai kucheza miondoko ya Taarab, ikiwa ni sehemu ya kusherehekea mkesha wa maadhimisho ya sherehe za miaka 50 ya Uhuru zilizofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo. Mgeni rasmi katika sherehe hizo alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal

Na Fidelis Butahe

JAMHURI ya Muungano wa Tanzania iliundwa Aprili 26, 1964 kwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Mkataba wa Muungano ulitiwa saini na aliyekuwa rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa rais wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, Aprili 22, 1964 huko Zanzibar. Mkataba huo ulithibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi, Aprili 26 hadi 27, 1964.
Jina la “Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar” lilibadilishwa Oktoba 28, 1964 na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia Sheria namba 61 ya mwaka 1964 ya Jamhuri ya Muungano.

Ilivyokuwa

Vyanzo mbalimbali vya habari vinaeleza kuwa Watanganyika kama ilivyokuwa kwa wananchi wa nchi nyingine za kiafrika, hawakukubaliana na utawala wa kikoloni. Tangu mwanzo waliwapinga huku upinzani mkubwa ukionyeshwa na kabila la Wasambaa wakiongozwa na Kimweri dhidi ya Wajerumani. Wahehe wakiongozwa na Mkwawa kupigana dhidi ya Wajerumani na wakati wa vita vya Maji Maji chini ya uongozi wa Kinjekitile, Mputa na Kibasila.

Kukosekana kwa umoja kati ya wapigania uhuru wa mwanzo na uimara wa majeshi ya wakoloni yaliyokuwa na silaha bora za moto, kulidhoofisha mapambano ya uhuru na kusababisha hasara kubwa na kupoteza maisha ya watu. Kama ilivyokuwa kwenye makoloni mengi ya kiafrika, hisia za utaifa ziliendelea kuimarika katika Tanganyika baada ya mwaka 1945. Alama za utaifa zilianza kuonekana mara baada ya vita kuu ya kwanza ya dunia, kwa kuanzishwa kwa vyama mbalimbali vya Waafrika kwa upande wa Tanganyika na Zanzibar.

Kwa upande wa Tanganyika, African Association kilianzishwa mwaka 1929 kama kikundi cha mijadala baina ya wasomi na ilipofika mwaka 1948 chama hiki kikawa Tanganyika African Association (TAA). Baada ya vita ya pili ya Dunia, wanachama wa Tanganyika African Association (TAA) waliendeleza wimbi la utaifa. Mwaka 1953 chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere, TAA ilitambuliwa kama chama cha siasa na kuelekea moja kwa moja kuanzishwa kwa TANU mwaka 1954, chama kilichotumika kama chombo cha kisiasa cha watu katika kutoa vilio vyao vya kudai uhuru.

Kuanzishwa kwa TANU mwaka 1954, ulikuwa ndio mwanzo wa mbio za kupigania uhuru. Baada ya miaka saba ya mapambano ya kisiasa, Tanganyika ilikuwa huru chini ya chama cha TANU, kilichoimarishwa na vyama vya wafanyakazi na vya ushirika.

Kwa upande wa Zanzibar

Kwa upande wa Zanzibar, chimbuko la Jumuiya ya Waafrika ilikuwa ni vilabu vya mpira wa miguu vilivyoanzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1930. Ilipofika mwaka 1934, Jumuiya ya Waafrika ilianzishwa rasmi na kupewa jina la African Association (AA). Baada ya vita ya pili ya dunia kama ilivyokuwa katika sehemu nyingine za dunia, kulikumbwa na uhaba mkubwa wa chakula, ubaguzi na mgawanyiko baina ya jamii.

Kutokana na matatizo hayo ya ubaguzi, kulianzishwa Jumuiya ya Washirazi (Shirazi Association) kwenye visiwa vya Unguja na Pemba, lengo likiwa ni kudai kupatiwa haki mbalimbali za kijamii na kulinda utambulisho wao. Kuundwa kwa chama cha ZNP (Zanzibar Nationalist Party) mwaka 1957, kulifanya viongozi wa Jumuiya ya Waafrika (African Association) na wale wa Shirazi Association waone umuhimu wa kushirikiana.

Waligundua kuwa Serikali ya kikoloni na chama cha ZNP walishirikiana kuendeleza dhuluma dhidi ya Waafrika. Viongozi hao waliona ulazima wa kuungana kuwa kitu kimoja kupigania uhuru. Katika kutekeleza azma hiyo, viongozi wa Jumuiya hizo walikutana na kukubaliana kuunganisha Shirazi Association na African Association mwaka 1957. Muunganiko huo ulisababisha kuundwa kwa chama cha Afro- Shirazi Union ambacho baadae kiliitwa Chama cha Afro-Shirazi chini ya uongozi wa Sheikh Abeid Amani Karume.

Vuguvugu la kisiasa

Kati ya mwaka 1957, mara baada ya uchaguzi mkuu wa kwanza na mwishoni mwa mwaka 1963, kabla ya mapinduzi ya mwaka 1964, Zanzibar ilitawaliwa na vuguvugu na mivutano mikali ya kisiasa. Mapambano haya ya kisiasa yalikuwa kati ya Chama cha Afro-Shirazi kilichoungwa mkono na Waafrika na kile cha ZNP kilichoungwa mkono na Wakoloni, Sultani pamoja na jamii ya Waarabu.

Chama cha ZNP baada ya kushindwa uchaguzi, kilianzisha kampeni za kushawishi wenye mashamba na mabepari wengine waliokuwa wakimiliki njia kuu za uchumi kuwafukuza kazi au kutowaajiri wafuasi wa ASP. Chama cha ZNP kiliwatafutia kazi na kuwabakisha mashambani waafrika wote waliokubali kukiunga mkono.

Wakati wa mvutano huo wa kisiasa kati ya ASP na ZNP ukipamba moto, kulijitokeza tofauti miongoni mwa viongozi wa ASP. Tofauti hizo zilichangiwa na uroho wa madaraka, ubinafsi na kutokuwa na msimamo imara miongoni mwa baadhi ya viongozi wa chama hicho.

Pia, Serikali ya Sultani nayo ilichochea migogoro hiyo ili ijinufaishe kisiasa. Migogoro hiyo ilisababisha kujitoa kwa baadhi ya viongozi wa ASP ambao walifanya mkutano na baadhi ya wanasiasa mashuhuri wa ASP huko Pemba, Novemba 1959 na walikubaliana kuanzisha Chama kipya cha siasa cha Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP).

Wakati vyama vya ASP, ZNP na ZPPP vikiwa katika malumbano makali ya kisiasa, serikali ya Kikoloni ilifanya matayarisho ya uchaguzi wa pili. Uchaguzi ulifanyika Januari 16, 1961 ambapo siku moja kabla ya uchaguzi huo, serikali ilitangaza kuwa chama kitakachoshinda kitaunda serikali na wizara zote zitakuwa chini yake. Katika uchaguzi huo ASP ilishinda kwa kupata viti 10, ZNP kilipata viti 9 na chama cha ZPPP kilipata viti 3. Kutokana na kuenea kwa chuki za kisiasa miongoni mwa Wazanzibari, Vyama vikuu vya kisiasa vilifikia muafaka wa kumaliza hali hiyo.

Hatahivyo, ASP haikufikisha zaidi ya nusu ya kura na hivyo haikuweza kuunda serikali. Njia pekee iliyobakia ilikuwa ni kuishauri ZPPP ichanganye viti vyake na chama kimoja kati ya ASP na ZNP. ZPPP na ZNP viliungana na iliamuliwa kuwa iundwe serikali ya muda na kusubiri uchaguzi mwingine uliopangwa kufanyika Juni, 1961. Waingereza walitoa uhuru kwa Serikali ya Mseto ya ZNP/ZPPP ya waziri mkuu, Muhammed Shamte.

Chini ya ushauri wa Waingereza, Shamte aliwatenga ndani ya Serikali yake baadhi ya viongozi wa ZNP wenye msimamo wa Kikomunisti wakiongozwa na Abdulrahaman Babu, na hivyo kutokea kutofautiana kwa baadhi ya viongozi wa ZNP na Serikali ya ZNP/ZPPP. Baada ya kutengwa na Serikali hiyo, ZNP walijitoa na kuanzisha chama cha umma. Chama hicho kilivunjwa mara tu baada ya mapinduzi ya mwaka 1964 huku viongozi na wafuasi wake wakijiunga na Serikali ya ASP chini ya uongozi wa Abeid Karume.

Zanzibar ilikuwa na wakati mgumu katika kupigania uhuru, Waingereza walijikita zaidi kwa madhumuni ya kibiashara na kwa nia ya kukomesha biashara ya utumwa, walifanya hivyo kwa sababu walitaka nguvukazi rahisi ambayo ilikuwa inapotea. Waingereza walifikia makubaliano na Sultani mwaka 1822 ili kukomesha biashara ya utumwa, lakini ilichukua zaidi ya miaka 50 hadi utumwa kutokomezwa.

Makubaliano ya Waingereza na Wajerumani ya mwaka 1890 yalifanya Zanzibar kuwa koloni la waingereza ambao walimshirikisha Sultani katika utawala wao. Waingereza waliainzisha ubaguzi wa rangi Zanzibar kwa wazungu na waarabu kupendelewa kuwa tabaka la juu na Waafrika la chini. Waingereza walifanya Zanzibar kuwa ni koloni la Waarabu na ilipofika Desemba 1963, Sultani alipewa mamlaka kamili ya kutawala Zanzibar.

Januari 12, 1964, aliyekuwa Sultani wa Zanzibar, Jamshid bin Abdulla, aling’olewa madarakani katika mapinduzi yaliyokuwa yameandaliwa kwa usiri, ustadi na ujasiri mkubwa wa wanamapinduzi wa ASP na Jamhuri ikatangazwa.

Muungano.

Muundo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa nchi ya Tanzania kama ulivyoelezwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, una vyombo viwili vyenye mamlaka ya utendaji ambavyo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Pia, ina vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki ambavyo ni Mahakama ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Pia kuna vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma ambavyo ni Bunge na Baraza la Wawakilishi. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inashughulikia mambo yote ya Muungano kama yalivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, na yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanzania Bara na serikali ya mapinduzi ya zanzibar inayoshughulikia mambo yote yasiyo ya muungano kwa upande wa Tanzania Zanzibar.

Muungano wa Tanzania ni tukio la nadharia iliyotafsiriwa katika vitendo, kwani kuunganisha Tanganyika na Zanzibar ilikuwa ni hatua ya watu walio wakweli. Ni ushahidi unaojitosheleza kuwa wananchi wa Tanganyika na Zanzibar wakiongozwa na viongozi wao wa mapambano ya kudai uhuru, walitoa kauli zilizokuwa zikimaanisha walichofikiri na kuazimia na sio kwa sababu ya kusombwa na jazba za kisiasa.

Sababu za Muungano

Sababu za Muungano huo ni pamoja na kuwepo kwa mahusiano ya karibu ya kihistoria baina ya Tanganyika na Zanzibar katika nyanja mbalimbali kama biashara, utamaduni, lugha na mahusiano ya karibu kisiasa ya TANU na ASP. Moyo wa kuwa na Muungano wa Afrika kwa kuanzia na Shirikisho la Afrika Mashariki ulianza hata kabla ya uhuru wa Tanganyika.
Mwalimu Nyerere pamoja na viongozi wengine waliokuwa wakipigania utaifa katika ukanda wa Afrika Mashariki walikuwa na matarajio ya kuwa na Muungano wa Afrika. Mwalimu Nyerere alipenda kuwepo Muungano wa Afrika kwa kuanzia na mashirikisho ya kikanda.

Baada ya kushauriana na viongozi mbalimbali wa iliyokuwa Jumuiya ya Wapigania Uhuru wa Afrika Mashariki na Kati (Pan- African Freedom Movement for East and Central Africa – PAFMECA) Mwalimu Nyerere alitoa tamko wakati wa mkutano wa nchi huru za Afrika uliofanyika Addis Ababa mwaka 1960.

Katika mkutano huo Nyerere alizungumza mambo mengi na baadhi yalinukuliwa katika gazeti la Tanganyika Standard, Novemba 1964). Alisema, ““Wengi wetu tunakubaliana bila kikwazo kwamba Shirikisho la Afrika Mashariki litakuwa ni jambo zuri. Tumesema na ni kweli kwamba mipaka inayotenganisha nchi zetu imewekwa na mabeberu na sio sisi wenyewe na kwamba tusikubali itumike dhidi ya umoja wetu…lazima tuzisumbue ofisi za wakoloni kwa nia si ya kudai uhuru wa Tanganyika, kisha Kenya, na Uganda halafu Zanzibar lakini kwa nia ya kutaka uhuru wa Afrika Mashariki kama Muungano mmoja wa Kisiasa”.

Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari, 1964 yalifanyika wakati Mwalimu Nyerere akiwa ameshachoshwa na kukatishwa tamaa na mazungumzo ya Shirikisho la Afrika Mashariki. Mapinduzi hayo yaliiweka madarakani serikali ya chama cha ASP kilichokuwa na mahusiano ya karibu na TANU kwa upande wa Tanganyika, mwaka 1977, TANU iliungana na ASP na kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

CHANZO: MWANANCHI

Advertisements

One response to “Ujamaa uliziunganisha Tanganyika na Zanzibar

 1. Butahe, maelezo yake kuhusu uasiliaya wa siasa za Tanganyika na Zanzibar hadi
  kuunganishwa kwa nchi mbili hizo na tukawa na TANZANIA YA LEO NI SAFI KABISA.

  Maelezo yake kishistoria ni sambamba na ukweli wenyewe ingawaje kwa ufupi tu.
  Muungano wa Tanzania ni muungano wenye nguvu za kijadi baina watu wa nchi mbili
  zinazohusiana kidamu,kiutamduni na ushirika wa Kihistoria kwa mambo mengi,taabu za
  kutawaliwa,kunyanyaswa na wageni wa Kutoka Ulaya na Asia Arabuni na BARAHINDI.

  Watanzania wote wanapaswa kujivunia sana kabisa na nchi yao waliyoipata kwa njia
  za ujasiri na mapambano dhidi ya maaduwi wa Umoja wa AFRIKA.

  Maaduwi wa Tanzania ya leo sio wa njee tu , bali tumekabiliwa na maadui walioko ndani
  ya nchi yetu,wananchi wenzetu lakini wana lengo la kutuvunjiya MUUNGANO WETU kwa
  vijisababu vya choko-choko wanavyochomezwa na kutumiliwa na maadui wetu wa njee.

  Uishi Muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar Milele – AMIN !!

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s